Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 10/8 kur. 11-15
  • Baba Yangu ‘Aliondolewa Gerezani na Kombora la Atomi’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Baba Yangu ‘Aliondolewa Gerezani na Kombora la Atomi’
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutafuta Kusudi
  • Kupata Kusudi Maishani
  • Maisha Wakiwa Wahudumu wa Wakati Wote
  • Wazazi Wangu Wakamatwa
  • Kombora Lilipoanguka
  • Imani Yake Bado Ni Yenye Nguvu
  • Mwaminifu Hadi Mwisho
  • Miongo ya Utumishi Wenye Kuendelea
  • Yehova Haachi Watumishi Wake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Kuacha Ibada ya Maliki na Kuanza Ibada ya Kweli
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu
    Amkeni!—1993
  • Nilisaidiwa Kuacha Kuwa Mwenye Haya
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 10/8 kur. 11-15

Baba Yangu ‘Aliondolewa Gerezani na Kombora la Atomi’

SAA 2:15 asubuhi ya Agosti 6, 1945 kombora la atomi lililipuka juu ya Hiroshima, Japani, likiacha jiji ukiwa na kufutilia mbali makumi ya maelfu ya wakaaji walo. Baba yangu alikuwa amekataa kumwabudu maliki na kuunga mkono uanajeshi wa Japani, kwa hiyo wakati huo alikuwa mfungwa katika gereza la Hiroshima.

BABA alieleza mara nyingi lililotukia asubuhi hiyo ya kukumbukika. “Nuru ilimweka katika dari la kijumba changu gerezani,” akasema. “Ndipo nikasikia mngurumo mkubwa wa kuogofya kama kwamba milima yote ilikuwa imeporomoka kwa dakika moja. Papo hapo kijumba hicho cha gereza kilifunikwa na giza nene. Nilisukuma kichwa changu chini ya godoro ili niepuke kile kilichoonekana kama gesi nyeusi.

“Baada ya dakika saba au nane, niliinua kichwa changu kutoka chini ya godoro nikakuta kwamba ile ‘gesi’ ilikuwa imemalizika. Kulikuwa kweupe tena. Vitu kutoka kwenye rafu pamoja na vumbi jingi vilikuwa vimeanguka, mambo yakaborongeka kwelikweli. Kwa sababu ya ule ukuta mrefu uliozunguka gereza, hakuna moto uliokuwa umeingia kutoka nje.

“Nilitazama kupitia lile dirisha jeusi nikaduwaa weee! Vyumba vya kutengenezea vitu gerezani na yale majengo ya mbao yalikuwa yameangushwa yakatandazika kabisa. Halafu nikatazama kupitia lile dirisha dogo la mbele. Vijumba vya lile jengo jingine mkabala vilikuwa vimechanwa-chanwa. Wafungwa waliookoka walikuwa wakililia msaada. Kulikuwa na hofu na babaiko—tamasha ya vurumai na ogofyo tupu.”

Nikiwa mvulana nilisisimka kumsikiliza baba akisimulia kile alichokiita “kuondolewa gerezani na kombora la atomi.” Alisimulia kisa hicho bila hisia za hatia, kwa sababu alikuwa ametiwa gerezani isivyo haki. Kabla sijasimulia mashtaka yaliyofanywa dhidi ya baba na jinsi alivyotendewa katika miaka yake ya kuzuiliwa, acheni nieleze jinsi wazazi wangu walivyokuja kushirikiana na Todaisha, kama vile Watch Tower Bible and Tract Society ilivyokuwa ikiitwa katika Japani wakati huo.

Kutafuta Kusudi

Baba alikuwa mpenda vitabu sana, na mapema maishani alitafuta kujiboresha. Alipokuwa bado katika darasa la tano la shule ya msingi, alitoroka nyumbani kwake katika Ishinomori kaskazini-mashariki mwa Japani. Akiwa na fedha za kutosha tikiti ya safari ya kwenda tu, alipanda gari-moshi kuelekea Tokyo, ambako alikuwa amepiga moyo konde awe mfanyakazi wa nyumbani wa Shigenobu Okuma, aliyekuwa amekuwa waziri mkuu wa Japani mara mbili. Lakini mvulana huyu wa mashambani aliyevalia vitambara alipotokea nyumbani kwa Bw. Okuma, ombi lake la kazi lilikataliwa. Baadaye baba alijipatia kazi ya kuajiriwa na kukaa katika duka la maziwa.

Akiwa tineja bado, baba yangu alianza kuhudhuria mihadhara ya wanasiasa na wanachuo. Katika mhadhara mmoja Biblia ilitajwa kuwa kitabu cha maana sana. Kwa hiyo baba akajipatia Biblia, ikiwa kamili na marejezo-mlinganisho na atlasi ya Biblia. Alivutiwa sana na aliyosoma na kusukumwa kutaka kufanya kazi ambayo ingenufaisha wanadamu wote.

Hatimaye baba alirudi nyumbani, na katika Aprili 1931, alipokuwa na miaka 24, alioa Hagino mwenye miaka 17. Muda mfupi baada ya baba kuoa, mtu wa ukoo alimpelekea fasihi iliyochapishwa na Todaisha. Kwa kuvutiwa na aliyosoma, baba aliandikia Todaisha katika Tokyo. Katika Juni 1931 mhudumu wa wakati wote kutoka Sendai kwa jina Matsue Ishii alimtembelea katika Ishinomori.a Baba alikubali muunganisho wa vitabu kutoka kwake uliotia ndani The Harp of God, Creation, na Government.

Kupata Kusudi Maishani

Karibu hapo hapo baba alifahamu kwamba mafundisho mbalimbali ya kanisa, kama lile la mwanadamu kuwa na nafsi isiyoweza kufa, waovu kuchomeka milele katika moto wa mateso, na Muumba kuwa Mungu-utatu, yalikuwa ya bandia. (Mhubiri 9:5, 10; Ezekieli 18:4; Yohana 14:28) Pia aling’amua kwamba ulimwengu huu ungekwisha. (1 Yohana 2:17) Kwa kuwa alitaka kujua alilopaswa kufanya, alipasha habari mwakilishi mwekwa wa Todaisha aliyemtembelea Agosti 1931, na kutokana na mazungumzo yao baba akabatizwa na kuamua kuwa mhudumu wa wakati wote wa Yehova.

Baada ya mazungumzo marefu mama pia akasadikishwa kwamba aliyokuwa amejifunza kutokana na Biblia yalikuwa kweli. Aliweka maisha yake wakfu kwa Yehova na kubatizwa Oktoba 1931. Baba yangu alipotoa mali yake ipigwe mnada, watu wa ukoo wake walifikiri alikuwa amerukwa na akili.

Maisha Wakiwa Wahudumu wa Wakati Wote

Baba alimwachia mama yake fedha zote alizopokea kutokana na mnada huo, naye na mama wakaenda Tokyo katika Novemba 1931. Ingawa hawakuwa wamepokea maagizo yoyote juu ya jinsi ya kuongea na wengine juu ya habari njema za Ufalme, walianza kuhubiri siku iliyofuata kuwasili kwao huko.—Mathayo 24:14.

Maisha yao hayakuwa rahisi. Hasa mambo yalikuwa magumu kwa mama yangu aliyekuwa na miaka 17 tu wakati huo. Hakukuwa na Mashahidi wenzi, hakukuwa na mikutano, na hakukuwa na kutaniko—ni ratiba ya kila siku tu ya kugawanya fasihi ya Biblia kutoka nyumba kwa nyumba kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 alasiri.

Katika 1933 mgawo wao wa kuhubiri ulibadilishwa kutoka Tokyo hadi Kobe. Mimi nilizaliwa huko Februari 9, 1934. Mama yangu alifanya kazi kwa bidii katika huduma mpaka mwezi mmoja kabla ya kuzaliwa kwangu. Baadaye wazazi wangu walihamia Yamaguchi, Ube, Kure, na hatimaye Hiroshima, wakihubiri kila mahali kwa karibu mwaka mmoja.

Wazazi Wangu Wakamatwa

Roho ya uanajeshi ya Japani ilipokuwa ikiongezeka, vichapo vya Watch Tower Society vilipigwa marufuku na Mashahidi wakawekwa chini ya ukaguo mkali na Idara ya Makachero Maalumu. Halafu, katika Juni 21, 1939, wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova wakazingirwa Japani yote. Baba na mama walikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa. Mimi nilikabidhiwa katika utunzaji wa nyanya yangu aliyeishi katika Ishinomori. Baada ya kuzuiliwa kwa miezi minane, mama aliachiliwa na kuwekwa chini ya muda wa kuangaliwa, na hatimaye, katika 1942, mimi nikaweza kujiunga naye katika Sendai.

Kwa sasa, baba, pamoja na Mashahidi wengine, alihojiwa na makachero kwenye kituo cha polisi cha Hiroshima. Kwa sababu Mashahidi walikataa kumwabudu maliki au kuunga mkono roho ya uanajeshi ya Japani, walipigwa vikali. Mwenye kuhoji hangeweza kumbandua baba aache kumwabudu Yehova.

Baada ya muda wa zaidi ya miaka miwili akiwa kizuizini, baba alifanyiwa kesi. Katika kikao kimoja, hakimu aliuliza hivi: “Miura, wamwonaje Mwadhamu, Maliki?”

“Mwadhamu, Maliki, yeye pia ni mzao wa Adamu na ni mwanadamu asiyekamilika, awezaye kufa,” baba akajibu. Taarifa hiyo iligutusha sana karani wa mahakama hata akashindwa kuiandika. Waona, wakati huo Wajapani walio wengi waliamini maliki alikuwa mungu. Baba alipokea hukumu ya miaka mitano gerezani, na hakimu akamwambia kwamba kama hangeacha imani yake, angekuwa gerezani maisha yake yote.

Upesi baadaye, katika Desemba 1941, Japani ilishambulia Marekani kwenye Bandari ya Pearl, Hawaii. Chakula gerezani kikawa haba, na katika miezi ya majira ya baridi, baba alikaa nyakati nyingi za usiku akiwa mwenye baridi na kukosa usingizi kwa kukosa mavazi. Ingawa alikuwa amekatiziwa ushirika wote wa kiroho, aliweza kuwa na Biblia katika maktaba ya gereza, na kwa kuisoma tena na tena, alidumisha nguvu za kiroho.

Kombora Lilipoanguka

Mapema asubuhi ya Agosti 6, 1945, mfungwa mmoja alitaka kubadilishana vitabu na baba. Hii ilikuwa haramu, lakini kwa kuwa mfungwa huyo alikuwa tayari ametelezesha kitabu chake kikavuka lile pito la katikati ya kuta kikaingia katika kijumba cha baba, yeye alitelezesha kitabu chake kikaingia katika kijumba cha mfungwa yule mwingine. Kwa hiyo asubuhi hiyo badala ya baba kufuata ratiba yake ambayo kwa kawaida haikubadilikana, baba alikuwa akisoma wakati lile kombora lilipoanguka. Kwa kawaida angalikuwa akitumia choo katika kijumba chake cha gereza wakati huo wa asubuhi. Baada ya ule mlipuko, baba aliona kwamba eneo la chooni lilikuwa limeharibiwa na vifusi vyenye kuanguka.

Ndipo baba alipopelekwa kwenye gereza la hapo karibu la Iwakuni. Muda mfupi baada ya hapo, Japani ilisalimu amri ya Majeshi ya Muungano, naye akaachiliwa gerezani katikati ya vurugu la baada ya vita. Alirudi nyumbani Ishinomori katika Desemba 1945. Afya yake ilikuwa imeharibiwa kabisa. Alikuwa na miaka 38, lakini alionekana kama kizee. Kwanza singeweza kuamini alikuwa baba yangu.

Imani Yake Bado Ni Yenye Nguvu

Japani ilikuwa katika vurugu, nasi hatukujua wale Mashahidi wachache waaminifu walikuwa wametawanywa kwenda wapi. Wala hatukuwa na fasihi yoyote ya Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, baba alinifundisha moja kwa moja kutoka katika Biblia ile kweli juu ya Ufalme wa Yehova, ulimwengu mpya, na pigano linalokaribia la Har–Magedoni.—Zaburi 37:9-11, 29; Isaya 9:6, 7; 11:6-9; 65:17, 21-24; Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10.

Baadaye, nilipofundishwa nadharia ya mageuzi katika shule ya sekondari na kuanza kutia shaka juu ya kuwako kwa Mungu, baba yangu alijaribu kunisadikisha juu ya kuwako kwa Mungu. Nilipositasita kuamini, hatimaye alisema: “Walio wengi kati ya watu wa ulimwengu waliiunga mkono vita wakawa na hatia ya kumwaga damu. Mimi, kwa upande wangu, nilishikamana na kweli ya Biblia na sikuunga mkono kamwe roho ya uanajeshi, ibada ya maliki, wala ile vita. Kwa hiyo fikiri kwa uangalifu wewe mwenyewe uone ni ipi iliyo njia ya kweli ya maisha upaswayo kutembea ndani yayo.”

Kwa kujua mambo aliyofundisha baba yangu na kuishi kulingana nayo na kuyalinganisha na yale niliyokuwa nikijifunza shuleni, ningeweza kuona kwamba nadharia ya mageuzi haingeweza kuwa njia timamu ya kufikiri. Ingawa hakuna mwanamageuzi yeyote aliyekuwa amehatarisha uhai wake kwa ajili ya imani zake, baba yangu alikuwa tayari kufia zile zake.

Siku moja katika Machi 1951, zaidi ya miaka mitano baada ya vita kumalizika, baba alikuwa akisoma gazeti Asahi. Kwa ghafula akapaaza sauti hivi: “Lo, kumbe walikuja, kumbe walikuja!” Alinionyesha gazeti hilo. Ilikuwa makala juu ya wamishonari watano wa Mashahidi wa Yehova waliokuwa wamewasili Osaka. Akiruka kwa shangwe, baba alipashana habari na gazeti hilo akajua kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wameanzisha ofisi ya tawi katika Tokyo. Alijipatia anwani na kulitembelea tawi, hivyo akirudisha upashanaji wa habari pamoja na tengenezo la Yehova.

Mwaminifu Hadi Mwisho

Katika 1952 familia yetu ilihamia Sendai. Wamishonari wa Watch Tower Society Donald na Mabel Haslett walihamia huko mwaka huohuo na kukodi nyumba ya kufanyia Funzo la Mnara wa Mlinzi. Ni watu wanne tu waliohudhuria mkutano wa kwanza huo—akina Haslett, baba yangu, na mimi. Baadaye, Shinichi na Masako Tohara, Adeline Nako, na Lillian Samson walijiunga na akina Haslett wakiwa wamishonari katika Sendai.

Kupitia ushirika na wamishonari hawa, familia yetu ilifanya maendeleo katika ujuzi wa Neno la Mungu na tengenezo. Mama, ambaye imani yake ilikuwa imetikiswa na mambo yaliyokuwa yametukia wakati wa ile vita, alijiunga nasi baada ya muda mfupi kwenda mikutanoni na kushiriki katika huduma ya shambani. Mimi nilisukumwa kuweka maisha yangu wakfu kumtumikia Yehova Mungu nikabatizwa Aprili 18, 1953.

Baada ya ile vita baba alifanyia shirika moja la bima kazi ya mwuzaji. Ajapokuwa na athari za kifungo chake, zilizokuwa ni kutia ndani kasoro ya figo na msongo mwingi wa damu, alikuwa na tamaa yenye nguvu kurudia huduma ya wakati wote akiwa painia. Alifanya hivyo karibu na wakati uleule nilipobatizwa. Hata ingawa afya mbaya ilimzuia kuendelea akiwa painia kwa muda mrefu sana, bidii yake kwa huduma ilinisukuma kuacha chuo kikuu nilichokuwa nikihudhuria na kuchukua huduma ya wakati wote ikiwa kazi-maisha.

Isamu Sugiura, kijana mzuri wa kutoka Nagoya, aliwekwa awe mfanyakazi mwenzangu. Siku ya Mei 1, 1955, tulianza huduma yetu tukiwa mapainia wa pekee katika Beppu katika Kisiwa cha Kyushu. Kulikuwa na Mashahidi wachache tu katika kisiwa kizima wakati huo. Sasa, zaidi ya miaka 39 baadaye, tuna mizunguko 15 inayositawi kiroho kukiwa na Mashahidi zaidi ya 18,000 katika kisiwa hicho. Na katika Japani yote, sasa kuna Mashahidi karibu 200,000.

Katika masika ya 1956, Isamu na mimi tulipokea mialiko ya kuhudhuria Watch Tower Bible School of Gilead katika Marekani. Tuliona shangwe ya ajabu. Hata hivyo, nilipochunguzwa mwili kwa kujitayarisha kufunga safari, madaktari walipata kwamba nilikuwa na kifua kikuu. Nilirudi nyumbani Sendai nikiwa nimetamauka sana.

Kufikia wakati huo afya ya kimwili ya baba ilikuwa imekuwa mbaya zaidi, naye alikuwa akipumzika nyumbani kitandani. Nyumba yetu ya kukodi ilikuwa ya chumba kimoja tu cha meta 10 za mraba chenye sakafu ya majamvi. Baba yangu na mimi tulilala kando kwa kando. Kwa kuwa baba hangeweza kufanya kazi, mama alitatizika sana kutunza mahitaji yetu ya kifedha.

Katika Januari 1957, Frederick W. Franz, aliyekuwa msimamizi-msaidizi wa Watch Tower Society wakati huo, alizuru Japani, na mkusanyiko wa pekee ukapangwa kufanywa katika Kyoto. Baba alihimiza mama yangu ahudhurie. Ingawa hakuwa na nia ya kutuacha tukiwa katika hali yetu ya ugonjwa, yeye alimtii baba na kwenda mkusanyikoni.

Upesi baada ya hapo hali ya baba ilianza kuwa mbaya zaidi siku kwa siku. Tulipolala kando kwa kando, nilianza kufanya wasiwasi, nikamwuliza tungejitegemezaje. Alijibu hivi: “Sisi tumemtumikia Yehova Mungu, hata kuhatarisha uhai wetu, naye ndiye Mungu mweza yote. Mbona una wasiwasi? Yehova pasipo shaka ataandaa tuhitajicho.” Kisha akanionya kwa upole mwanana sana, akisema: “Sitawisha ndani yako mwenyewe imani yenye nguvu zaidi.”

Siku ya Machi 24, 1957, baba alivuta pumzi yake ya mwisho kwa utulivu. Baada ya maziko yake nilizuru kampuni ya bima aliyokuwa ameifanyia kazi ili nikamalize mambo nao. Nilipokuwa nikiondoka, meneja wa tawi alinipa mfuko wa karatasi akasema: “Huu ni wa baba yako.”

Niliporudi nyumbani niligundua donge kubwa la fedha humo ndani. Nilipomwuliza meneja juu yalo baadaye, alieleza kwamba fedha hizo zilitokana na faida za bima zilizokuwa zimekatwa kwenye mshahara wa baba kila mwezi bila yeye kujua. Hivyo maneno ya baba, “Yehova pasipo shaka ataandaa tuhitajicho,” yalitimia. Hii iliitia nguvu sana imani yangu katika utunzaji wa Yehova wenye himaya.

Miongo ya Utumishi Wenye Kuendelea

Usaidizi wa kimwili ulioandaliwa na fedha hizo ulinisaidia kukaza fikira juu ya kupata nafuu nikiwa nyumbani. Mwaka mmoja baadaye, katika 1958, mama na mimi tuliwekwa kuwa mapainia wa pekee. Baadaye, nilitumikia nikiwa mwangalizi anayesafiri katika Japani, halafu katika 1961, nikawa na pendeleo la kuhudhuria mtaala wa miezi kumi wa Shule ya Gileadi kwenye makao makuu ya ulimwengu ya Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York.

Niliporudi Japani, nilianza tena kutumikia makutaniko nikiwa mwangalizi anayesafiri. Halafu, katika 1963, nikamwoa Yasuko Haba, aliyekuwa akifanya kazi kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Tokyo. Alijiunga nami katika kazi ya kusafiri mpaka 1965, wakati ambao tulialikwa tukatumikie kwenye ofisi ya tawi katika Tokyo. Tangu wakati huo tumetumikia pamoja—kwanza kwenye tawi katika Tokyo, kisha katika Numazu, na sasa katika Ebina.

Mama alibaki akiwa mhudumu painia wa pekee mpaka 1965. Tangu wakati huo amefuliza kuwa mtendaji akisaidia watu wengi kukubali kweli za Biblia. Sasa ana miaka 79 lakini ana afya nzuri kwa kulinganisha na umri wake. Twafurahi kwamba yeye huishi karibu na aweza kuhudhuria kutaniko lilelile tuhudhurialo karibu na ofisi ya tawi ya Ebina.

Twamshukuru Yehova Mungu kwelikweli kwamba baba yangu aliokoka ule mlipuko wa kombora la atomi juu ya Hiroshima. Alidumisha imani yake, na tamaa yangu ni kumkaribisha arudipo katika ulimwengu mpya na kumsimulia jinsi tulivyokombolewa kutoka Har–Magedoni, pigano alilotaka sana kuliona. (Ufunuo 16:14, 16; 21:3, 4)—Kama ilivyosimuliwa na Tsutomu Miura.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa hadithi ya maisha ya Matsue Ishii, tafadhali ona Mnara wa Mlinzi la Mei 1, 1988, kurasa 21-5.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Katsuo na Hagino Miura, pamoja na Tsutomu mwana wao

[Picha katika ukurasa wa 15]

Tsutomu Miura akifanya kazi katika ofisi ya tawi ya Japani

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Hiroshima Peace and Culture Foundation kutokana na vitu vilivyorudishwa na United States Armed Forces Inistitute of Pathology

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki