Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 11/22 kur. 6-11
  • Kulea Mtoto Aliye Mgumu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kulea Mtoto Aliye Mgumu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuchanganua na Kuingilia
  • Watoto Wenye Mikazo
  • Punguza Ule Msuguano
  • Kudhibiti Tabia
  • Sifu, Usihukumu
  • Ono la Baba na Greg
  • Kulikabili Hilo Tatizo
    Amkeni!—1997
  • “Kaa Tuli na Ukaze Fikira!”
    Amkeni!—1997
  • Ubora wa Kutia Adabu katika Upendo
    Kufanya Maisha ya Jamaa Yako Yawe Yenye Furaha
  • Zoeza Mtoto Wako Tangu Utoto Mchanga Sana
    Siri ya Furaha ya Familia
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 11/22 kur. 6-11

Kulea Mtoto Aliye Mgumu

“ULIKUWA na siku njema?” Susan auliza mwanaye Jimmy aparamiapo kuingia garini mama ajapo kumchukua shuleni. Kwa kukunja uso, ampuuza mama. “Aha, haikosi ulikuwa na siku mbaya,” mama asema kwa huruma. “Unataka kulizungumzia?”

“Niache,” ajibu kwa kununa.

“Ninakuhangaikia tu. Waonekana huna furaha. Nataka kukusaidia.”

“Sitaki msaada wako!” mtoto apiga kelele. “Niache! Sikupendi. Natamani ningekuwa mfu!”

“Jimmy!” Susan atweta, “usiongee nami hivyo au—au nikugote! Nilikuwa tu najaribu kuwa mzuri. Sielewi ni nini unacho. Hakuna lolote nisemalo wala kutenda likupendezalo.”

Akiwa amevurugika na kuchoka kwa kazi yake ya siku, Susan ajipindapinda kati ya magari akistaajabia aliwezaje kupata mtoto kama huyo. Ajihisi kuvurugika, hoi, na mwenye hasira, pia mwenye uchukizo kumwelekea mwanaye, na hisia za hatia zamsumbua. Susan hajihisi kumpeleka nyumbani—mtoto wake mwenyewe. Hataki kabisa kujua yaliyotokea leo shuleni. Bila shaka mwalimu angepiga simu tena. Nyakati fulani Susan hushindwa na la kufanya.

Matukio yaonekanayo kuwa sahili hulipuka kuwa mauguo makali ya kihisia yenye kuhangaisha. Watoto walio na ADD/ADHD, ama wanaobandikwa “wagumu,” kwa ujumla wakabilipo matatizo, wao huitikia kwa ukali. Wao huchemka kwa haraka, wakiwaacha wazazi wakiwa na hasira, wamevurugika, na hatimaye kuchoka kabisa.

Kuchanganua na Kuingilia

Kihalisi, watoto hawa ni werevu, wabuni, na wenye hisia nyepesi sana. Ni muhimu kung’amua kwamba wao ni watoto wenye afya walio na mahitaji yasiyo ya kawaida, hivyo basi wakihitaji ufahamu wenye kina cha kipekee. Zifuatazo ni baadhi ya kanuni na maoni ambayo wazazi wa watoto kama hao wamepata kwamba ni zenye mafanikio.

Kwanza, ni vizuri kujifunza kutambua hali na vichochezi vinavyomkasirisha mtoto huyo. (Linganisha Mithali 20:5.) Inahitajika kwa mzazi kutazama zile ishara za mtoto zinazotangulia migongano ya kihisia-moyo na aingilie bila kukawia. Kiashiria kikuu ni wonyesho wa usoni unaoangaza kiwango kinachoongezeka cha kuvurugika hisia na kutoweza kudhibiti hali. Kutoa vikumbusha vya fadhili kwa mdomo kwamba mtoto huyo anahitaji kujidhibiti au, ikihitajika, kumwondoa katika hali hiyo huenda kusaidie. Mapumziko, kwa kielelezo, yana matokeo, si sana ikiwa aina ya adhabu bali ikiwa njia ya kumpa mtoto pamoja na mzazi fursa ya kutulia upya, na kisha kuendelea kwa kuafikiana.

Katika kielezi kilichotolewa, Jimmy aliitikia kupita kiasi kwa maswali sahili. Hii ni kawaida katika tabia ya kila siku ya Jimmy. Ingawa ni rahisi kwa mzazi kufikiri hasira na chuki hii ilielekezwa kwake binafsi, inahitajika kung’amua kwamba kwa kawaida fahamu huwatoka (usababu) watoto hawa mara wafikiapo kilele chao cha kuvumilia mbano. Hivyo basi, ni muhimu kutenda kwa ufahamu. (Mithali 19:11) Katika kisa cha Jimmy, Susan angeweza kufyonza hali hiyo kwa kunyamaza na kwa kukipa kivulana chake wakati wa kujidhibiti, na labda baadaye wangeweza kuzungumza matukio ya siku hiyo.

Watoto Wenye Mikazo

Familia ya kibinadamu haijapata kamwe kukabiliwa na matatizo makubwa, misongo, na mahangaiko kama yale yanayotaabisha ulimwengu wa kisasa. Nyakati hizi ni tofauti, madai ni mengi zaidi, na mengi zaidi yahitajiwa kutoka kwa watoto. Kuhusu suala hili, kile kitabu Good Kids, Bad Behavior husimulia hivi: “Mengi ya matatizo yanayoonwa kuwapata watoto huenda ama yanasababishwa ama kuchochewa na matazamio yenye kubadilika ya kijamii.” Kwa watoto walio na ADD/ADHD, shule yaweza kuwa mzigo mkubwa. Wang’ang’anapo ili kukabili mapungukio yao, wanalazimika kubadilika ili kufaa mlipuko wa maendeleo ya kitekinolojia yanayozidi kubadilika haraka katika mazingira yanayoonekana makali na hatari pia, yakiongezea hangaiko lao. Kihisia-moyo, watoto ni wachanga sana kushughulikia matatizo haya yote. Wanahitaji msaada wa wazazi wao.

Punguza Ule Msuguano

Ili uwe na watoto wenye furaha zaidi, wenye afya zaidi, ni muhimu kuandaa mazingira yenye utaratibu na usalama. Mpango unaofaa wa kupunguza msuguano katika nyumba huenda ukaanza na njia iliyorahisishwa ya kimaisha. Kwa sababu watoto hawa ni wenye kusisimuka, wakengeufu, na watendaji kupita kiasi, inahitajika kupunguza athari hasi ya kuwachochea kupita kiasi. Punguza kiasi cha vichezeo ambavyo watoto kama hao wanaruhusiwa kucheza navyo kwa wakati mmoja. Jaribu jambo moja ama mradi mmoja kwa wakati hadi umekamilika. Kwa sababu watoto hawa kwa ukawaida hawana utaratibu wao wenyewe, utaratibu hupunguza kuvurugika hisia. Kadiri vichezeo vitakavyokuwa vichache zaidi na karibu zaidi, ndivyo ilivyo rahisi zaidi kushughulikia kilicho cha maana.

Njia nyingine yenye matokeo ya kupunguza mkazo katika nyumba ni kutekeleza utaratibu, usio mgumu, unaowaandalia watoto hisi ya usalama. Ratiba ya wakati isiwe yenye kusongamana, kwa mpangilio wa matukio yapaswavyo kutukia. Hili laweza kufikiwa kwa kutumia madokezo yatumikayo kama yafuatayo. Andaa lishe ifaayo yenye mlo kamili na kumbwe mara kwa mara. Vifanye vipindi vya kwenda kulala viwe vyenye uchangamshi, upendo, na vyenye kupumzisha. Safari za kununua vitu zaweza kuwasisimua kupita kiasi sana watoto watendaji, basi panga kimbele na ujaribu kutoenda katika maduka mengi sana. Na mkiwa katika safari za nje, eleza aina ya tabia unayotazamia. Kawaida za kudumu husaidia mtoto aliye na mahitaji ya kipekee kudhibiti tabia yake ya usisimkaji. Zaidi ya hayo, husaidia kusitawisha kutabirika kwa maitikio ya mzazi.

Pamoja na nia ya kujenga, kubuni mfumo wa kanuni na kutia ndani matokeo ya kuzivunja bila kubadilika ni yenye faida. Kanuni wazi zinazopatana, na pia zenye kuafikika kwa wenzi wote wawili, huweka mipaka ya tabia yenye kukubalika kwa watoto—na pia hufunza utozwaji. Bandika orodha ya kanuni mahali panapofikika kwa ukawaida, ikiwa yahitajiwa (kwa wazazi ili wakumbuke, pamoja na mtoto). Upatano ndio ufunguo wa usalama wa kihisia-moyo.

Kufahamu machaguo ya mtoto, mapendezi yake na yasiyompendeza, na kubadilika kulingana nayo kwaweza kupunguza zaidi mikazo isiyo ya lazima katika nyumba. Kwa sababu asili ya kipekee ya watoto hawa kwa kawaida ni ya kubadilika-badilika na kusisimuka, kuingiliana kwao na watoto wale wengine katika utendaji kwaweza kuwa ono gumu sana. Kushiriki, hasa vichezeo, huenda hasa kukawa jambo la mizozano, hivyo wazazi waweza kuwaruhusu watoto kama hao wachague bidhaa wazipendazo ambazo waweza kushiriki na wengine. Zaidi, kuelekeza kiwango chao cha msisimuko kwa kuwaandalia kikundi kidogo cha wachezaji wenzi na kubuni utendaji ambao hautawasisimua kupita kiasi kwaweza kusaidia pia kudhibiti usisimkaji wao wa haraka.

Ni muhimu kwa wazazi kuruhusu kila mtoto akue katika njia yake mwenyewe na kuepuka kumfinya au kumfinyanga mtoto ili ajipatanishe isivyo lazima na mtindo. Ikiwa mtoto hapendi chakula fulani au vazi, liondoe. Michukizo hii midogo hata haifai kutokeza mzozano. Kwa msingi, usijaribu kudhibiti kila kitu. Uwe na usawaziko, lakini maamuzi yafanywapo juu ya linalokubaliwa kwa familia ya Kikristo, shikamana nayo.

Kudhibiti Tabia

Watoto wasiotabirika huhitaji hali ya juu ya udhibiti. Kama tokeo, wazazi wengi wanakumbwa na hisi ya hatia ikiwa wanalazimika kutoa nidhamu kila mara. Hata hivyo, ni muhimu kutambua, tofauti kati ya nidhamu na kuwatenda vibaya. Kulingana na kile kitabu A Fine Line—When Discipline Becomes Child Abuse, kwa kuripotiwa asilimia 21 ya kutendwa vibaya kimwili kote hutokea wakati watoto waonyeshapo tabia za ukali. Basi, machunguzo hukata mkataa kwamba watoto walio na ADD/ADHD wako katika “hatari kubwa zaidi ya kutendwa vibaya kimwili na kupuuzwa.” Bila shaka, kulea wachanga walio na mahitaji ya kipekee kwaweza kuwa kwenye mkazo, lakini utunzi wao lazima uwe wenye afya na usawaziko. Kwa kuwa watoto hawa kwa ukawaida ni wenye akili sana na wabuni sana, wao hutokeza tatizo kwa wazazi washughulikiapo hali ambazo zahitaji usababu. Watoto kama hao kwa kawaida huwa na njia ya kutambua kasoro katika usababu wenye akili wa wazazi. Usiwaruhusu! Baki na mamlaka ukiwa mzazi.

Kwa njia ya urafiki, lakini imara, yafanye maelezo kuwa mafupi; kwa maneno mengine, usieleze sana, na usiridhie kanuni zisizo za kuridhia. Acha “ndiyo” yako iwe ndiyo na “la” yako iwe la. (Linganisha Mathayo 5:37.) Watoto si waungwana; kama tokeo, kuridhiana pamoja nao huongoza kwenye mabishano, hasira, na kuvurugika hisia na hata kwaweza kuzidi kuwa kelele na fujo. (Waefeso 4:31) Vivyo hivyo, epuka kukanya mno. Nidhamu ikihitajiwa, yapasa kutolewa bila kukawia. Kile kitabu Raising Positive Kids in a Negative World hushauri hivi: “Tulivu, hakika, na imara—hivyo ndivyo mamlaka ilivyo.” Zaidi, ona dokezo hili bora katika The German Tribune: “Sikuzote ongea na mtoto kwa njia ya kuvuta uangalifu wake: tumia jina lake kwa ukawaida, sitawisha uhusiano wa macho na tumia lugha sahili.”

Kutenda vibaya hutokea wazazi waachapo kujidhibiti. Ikiwa mzazi anapiga kelele, tayari amekosa kujidhibiti. Mithali sura 15 huzungumzia habari ya kulea watoto na kutoa nidhamu. Kwa kielelezo, mstari 4 hutaarifu hivi: “Ulimi upozao ni mti wa uhai: lakini ushupavu katika ulimi ni uvundifu wa roho”; mstari 18: “Mtu mkali hutibua utesi: lakini yeye aliye mvumilivu wa hasira hutuliza mashindano”; na, mwishowe, mstari 28: “Moyo wa mwenyi haki hujizungumza atakavyojibu.” (The Old Testament in Swahili [Mombasa], italiki ni zetu.) Basi, ni muhimu kung’amua si tu lile tunalosema bali jinsi tunavyolisema, pia.

Sifu, Usihukumu

Kwa sababu watoto walio wagumu kulea hufanya mambo yaliyo ya ubuni, mageni, hata ya wehu, ni rahisi kwa wazazi kuanza kutafuta makosa, kudhihaki, kukemea, na kushambulia kwa hasira. Hata hivyo, kulingana na Habari Njema kwa Watu Wote, Biblia katika Waefeso 6:4 huwashauri wazazi kuwalea watoto katika “Nidhamu na mafundisho ya Kikristo.” Yesu alitoaje nidhamu kwa waliokosa? Yesu alitoa nidhamu yenye mafundisho iliyozoeza na kufunza watu, akishughulika nao ifaavyo na kwa imara. Nidhamu ni utaratibu, mbinu ya kuagiza, ambayo, unaposhughulika na watoto, kwa kawaida lazima ifanyike tena na tena.—Ona ile makala “Maoni ya Biblia . . . ‘Fimbo ya Nidhamu,—Je, Ni ya Kizamani?,” katika Amkeni! ya Septemba 8, 1992, (Kiingereza).

Kutoa nidhamu kwa njia yenye kufaa hutokeza mazingira ya kutumainiana, uchangamfu, na usalama; hivyo basi, nidhamu inapohitajika, inapaswa kutolewa pamoja na maelezo. Hakuna masuluhisho ya mara moja unapozoeza watoto, kwani watoto hujifunza polepole, baada ya muda. Huhitaji kujali kwingi na upendo, wakati mwingi na kazi, ili kulea ifaavyo mtoto yeyote, hasa mtoto mgumu kulea. Msemo mfupi ufuatao waweza kusaidia kukumbuka: “Sema umaanishalo, maanisha usemalo, na fanya usemalo utafanya.”

Moja ya sehemu zenye kuvuruga hisia sana ya tatizo la kushughulika na watoto walio na tabia ya kufadhaisha ni tamaa yao nyingi mno ya kukaziwa fikira. Kwa kawaida uangalifu wanaopata ni hasi badala ya chanya. Hata hivyo, uwe mwepesi kuona, kusifu, ama kuthawabisha tabia nzuri ama kazi iliyofanywa vizuri. Hili ni lenye kutia moyo sana kwa mtoto. Mwanzoni jitihada zako huenda zikaonekana kuwa za kuzidi mno, lakini zastahili matokeo hayo. Watoto huhitaji zawadi ndogo lakini za papohapo.

Ono la Baba na Greg

“Mwana wetu Greg alipatwa kuwa ana ADHD katika umri wa miaka mitano akiwa katika shule ya watoto wadogo. Wakati huo tulimwona tabibu wa ukuzi kuhusu watoto aliyehakikisha kwamba Greg bila shaka alikuwa na ADHD. Alituambia: ‘Si kosa lake, wala lenu. Hawezi kubadili hali, lakini nyinyi mwaweza.’“Sisi hufikiria maneno hayo kwa ukawaida, kwa sababu hutukumbusha kwamba tukiwa wazazi tuna daraka kubwa ili kusaidia mwana wetu kukabiliana na ADHD yake. Siku hiyo daktari huyo alitupa fasihi ya kusoma tufikapo nyumbani, na tunaamini ujuzi tulioupata katika miaka mitatu iliyopita umekuwa na umuhimu sana katika kutimiza madaraka yetu ya kimzazi kumwelekea Greg.

“Ni muhimu sana katika kulea mtoto aliye na ADHD kuimarisha tabia zifaazo na kuandaa maonyo na, ikihitajika, kumwadhibu kwa kukosa tabia. Kadiri uwezavyo kuwa mwenye utaratibu na upatani zaidi, ndivyo utakavyoyaona matokeo bora zaidi. Mitajo hii sahili huenda ikawa kisababishi kikuu katika kulea mtoto aliye na ADHD. Hata hivyo, kwa sababu unahitaji kuifanya mara nyingi sana kwa siku, ni rahisi kuisema kuliko kuifanya.

“Mbinu ambayo tumeipata kuwa yenye matokeo sana ni pumziko. Kila mara tutumiapo pumziko ili kubadili kukosa tabia, pia tunaanzisha programu ya kuimarisha ili kutia moyo tabia chanya zaidi. Kiimarishi hiki chaweza kuwa neno la ukubali, kumbatio, ama hata tuzo ama pendeleo. Tulienda dukani na kununua chati ya vibandiko. Tuliweka juu tabia iliyo nzuri. Kila tumwonapo Greg katika tabia inayofaa, tulimpa kibandiko ili aweke katika chati yake. Wakati chati inapojaa, kwa mfano vibandiko 20, anapata thawabu. Hiki kwa kawaida ni kitu anachofurahia kukifanya, kama vile kwenda kwenye mbuga. Inasaidia kwa sababu inamhamasisha kufanya vema. Huweka vibandiko na anaweza kuona anavyofanya na jinsi anavyokaribia kupata zawadi.

“Mbinu nyingine tuliyoipata kuwa yenye matokeo ni kumpa Greg machaguo. Badala ya amri ya moja kwa moja, tunampa uchaguzi. Ama anaweza kuwa na tabia inayofaa ama anaweza kupata matokeo ya kutenda kinyume. Hili hufunza daraka na kufanya maamuzi yanayofaa. Ikiwa ni kitu ambacho ni tatizo la kuendelea, kama vile kukosa tabia katika duka ama mkahawa, tunaweza kutumia chati ya vibandiko pamoja na zawadi. Hivyo yeye huona manufaa yaliyo katika tabia inayofaa, na tunamwonyesha ung’amuzi wetu wa maendeleo yake.

“Watu walio wengi hawana habari kwamba ADHD huathiri uwezo wa mtoto wa kutendesha tabia na miitikio. Watu wengi huamini kwamba watoto hawa wangeweza kudhibiti muda wao wa makini na tabia yao, ikiwa wangejaribu zaidi, na washindwapo, wazazi ndio wa kulaumiwa.

“Kihalisi haiwezekani kwa mtoto aliye na ADHD kukaa kitako kwa saa mbili katika mikutano ya kutaniko kwenye Jumba la Ufalme. Hatutasahau kamwe jinsi Greg katika ule umri wa miaka mitano tu alivyokuwa akilia kabla ya kila mkutano na kutuuliza, ‘Je, huu ni mkutano mrefu au mkutano mfupi?’ Angelia sana mkutano ulipokuwa wa saa mbili kwa sababu alijua hangeweza kukaa kitako kwa muda huo wote. Lazima uruhusu nafasi kwa mvurugo na mipaka uletao. Twajua kwamba Yehova afahamu mvurugo vizuri kuliko yeyote, na hilo ni chanzo cha faraja. Sasa Greg hatumii dawa na ameweza kufikia gredi yake ya masomo.

“Kufanya Yehova kuwa tumaini letu na kuweka macho yetu kwa kukaza kwenye ulimwengu mpya hututegemeza. Tumaini letu tayari lamaanisha zaidi kwa Greg. Yeye husisimuka hakika, hata hutokwa na machozi anapofikiria jinsi Yehova atakavyofutilia mbali ADHD katika dunia-Paradiso.”

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Thawabu ziwezekanazo kwa tabia nzuri:

1. SIFU—kusifu kwa mdomo kwa kazi iliyofanywa vizuri; uthamini wenye kuonyeshwa kwa tabia nzuri, ukiambatana na upendo, makumbatio, na uchangamfu katika maonyesho ya uso.

2. MFUMO WA CHATI—ukionyesha wazi, kwa vibandiko vya kuvutia ama nyota ili kutia moyo tabia nzuri.

3. ORODHA YA VITU VIZURI—ya matimizo yenye kukubalika na kusifika. Kila wakati mtoto huyo anapofanya jambo vizuri, hata liwe dogo kadiri gani mwanzoni, liandike, ulisome kwa mshiriki wa familia.

4. KIASHIRIA TABIA—ikitegemea umri wa mtoto, mtoto afanyapo kitu vizuri ongezea peremende au biskuti (kiimarishi halisi cha tabia). Lengo ni kusitawisha mfumo wa alama wa kutuza zawadi ambao huenda ukatia ndani kitu ambacho familia ilikuwa ifanye, kama vile kwenda kutazama filamu, kuteleza barafuni, ama kula mkahawani. Badala ya kukazia mtoto: “Ikiwa hautakuwa na tabia, hatutaenda,” jaribu: “Ikiwa utakuwa na tabia, tutaenda.” Jambo kuu ni kubadili kufikiri hasi kuwe kufikiri chanya, huku ukiruhusu wakati wa kutosha ili kubadilika.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wakati fulani mazungumzo yaweza kuwasha hisia-moyo

[Picha katika ukurasa wa 8]

Maamuzi yanapofanywa, yaeleze, na ushikamane nayo

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kwa kujisikia aongezea kibandiko kipya kwenye chati yake

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki