“Kaa Tuli na Ukaze Fikira!”
Kuishi na Tatizo la Upungufu wa Makini Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi
“Kwa muda wote, Jim alikuwa amesema kwamba Cal alikuwa tu mtoto aliyedekezwa na kwamba ikiwa tungemtolea—yaani ikiwa mimi ningemtolea—nidhamu ifaayo, angerekebika. Sasa daktari alikuwa akituambia kwamba halikuwa kosa langu, halikuwa kosa letu, halikuwa kosa la walimu wa Cal: kulikuwa na tatizo kweli na mwana wetu mdogo.”
CAL ana Tatizo la Upungufu wa Makini Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi (ADHD), hali ambayo hutambulishwa na ukosefu wa kuwa makini, mwenendo wa kutenda kutokana na msukumo wa ghafula, na utendaji wa kupita kiasi. Tatizo hilo hukadiriwa kuathiri kuanzia asilimia 3 hadi 5 ya watoto wote wenye umri wa kwenda shuleni. “Akili zao ni kama viteua-stesheni vyenye kasoro vya televisheni,” asema mtaalamu wa kujifunza Priscilla L. Vail. “Wazo moja huongoza kwa jingine, bila muundo wala utaratibu.”
Acheni tuzungumzie kifupi dalili tatu kuu za ADHD.
Ukosefu wa makini: Mtoto aliye na ADHD hawezi kupuuza mambo yasiyo na maana na kukazia fikira jambo moja. Hivyo, anakengeushwa fikira kwa urahisi na mambo anayoona, sauti, na harufu zilizopo. Yeye anakaza fikira, lakini hakuna jambo fulani hususa katika mazingira yake ambalo linashika uangalifu wake. Hawezi kupambanua ni jambo gani analostahili kulikazia fikira hasa.
Mwenendo wa msukumo wa ghafula: Mtoto aliye na ADHD hutenda kabla ya kufikiri, bila kufikiria matokeo. Yeye hudhihirisha upangaji na uamuzi wa hali ya chini, na nyakati fulani matendo yake ni hatari. “Yeye hukimbia barabarani, kupanda ushi, kisha kupanda mtini,” aandika Dakt. Paul Wender. “Likiwa tokeo yeye hupata mikato, majeraha, mikwaruzo, na ziara nyingi za kwenda kwa daktari isivyo lazima.”
Utendaji wa kupita kiasi: Watoto wenye utendaji wa kupita kiasi huhangaika daima. Hawawezi kukaa tuli. “Hata wakiwa na umri mkubwa zaidi,” aandika Dakt. Gordon Serfontein katika kitabu chake The Hidden Handicap, “mtu akichunguza kwa makini atagundua kwamba kuna namna ya msogeo wenye kuendelea unaohusisha miguu, wayo, mikono, midomo au ulimi.”
Hata hivyo, watoto fulani wanaokosa makini na wenye kutenda kwa msukumo wa ghafula si watendaji kupita kiasi. Tatizo lao nyakati fulani hurejezewa kuwa tu Kasoro ya Upungufu wa Makini, au ADD. Dakt. Ronald Goldberg aeleza kwamba ADD “yaweza kutokea bila utendaji wowote wa kupita kiasi. Au yaweza kutokea kwa kiwango chochote cha utendaji wa kupita kiasi—kuanzia usioonekana sana, kufikia wenye kuchukiza, hadi wenye kulemaza kabisa.”
Ni Nini Kisababishacho ADHD?
Kwa miaka ambayo imepita, matatizo ya kuwa makini yamelaumiwa kwa kila kitu toka ulezi mbaya hadi nuru memetevu. Sasa yafikiriwa kwamba ADHD inahusiana na vurugu katika kazi fulani za ubongo. Katika 1990 Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Kiakili ilichunguza watu wazima 25 wenye dalili za ADHD na kupata kwamba walimeng’enyusha glukosi polepole sana katika sehemu za ubongo ambazo ndizo huongoza misogeo na ukazaji fikira. Katika asilimia 40 ya visa vya ADHD, yaonekana mfanyizo wa mtu wa kijeni huchangia. Kulingana na The Hyperactive Child Book, mambo mengine yawezayo kuhusianishwa na ADHD ni utumizi wa alkoholi au dawa za kulevya na mama wakati wa ujauzito, kusumishwa kutokana na madini ya risasi, na katika visa fulani, ulaji.
Wabalehe na Watu Wazima Walio na ADHD
Katika miaka ya majuzi madaktari wamepata kwamba ADHD si hali ya utotoni tu. “Kwa kawaida,” asema Dakt. Larry Silver, “wazazi watamleta mtoto kutibiwa na kusema, ‘nilikuwa vivyo hivyo nilipokuwa mtoto.’ Kisha watakiri kwamba bado wana matatizo kungoja katika foleni, kukaa tuli wakati wa mikutano, kumaliza kazi.” Inaaminiwa sasa kwamba nusu hivi ya watoto wote wenye ADHD huingia katika ubalehe na utu mzima wakiwa na angalau baadhi ya dalili zao.
Wakati wa ubalehe, wale walio na ADHD huenda wakaacha tabia ya hatari na kuwa wakosaji. “Nilikuwa nikipatwa na wasiwasi kwamba hataingia chuoni,” asema mama mmoja wa balehe aliye na ADHD. “Sasa nasali kwamba asiingie jela.” Kwamba hofu hizo zaweza kuwa halali yaonyeshwa na uchunguzi uliolinganisha vijana 103 wenye utendaji wa kupita kiasi na kikundi cha watoto 100 wasio na tatizo hilo. “Kufikia miaka yao ya mapema ya 20,” laripoti Newsweek, “watoto katika kikundi cha walio na utendaji kupita kiasi walielekea kuwa na rekodi za kufungwa maradufu, walielekea mara tano kushtakiwa kwa makosa makubwa na kufungwa gerezani mara tisa kuliko wale wengine.”
Kwa mtu mzima, ADHD hutokeza matatizo ya kipekee. Dakt. Edna Copeland asema: “Mtoto mwenye utendaji kupita kiasi aweza kuwa mtu mzima ambaye hubadili kazi mara nyingi, kufutwa kazi mara nyingi sana, kutumia wakati katika utendaji usio na maana siku nzima na asiyeweza kutulia.” Visababishi visipofahamika, dalili hizi zaweza kuwekea ndoa mkazo. “Katika mazungumzo sahili,” asema mke wa mwanamume mmoja aliye na ADHD, “hata anaweza kukosa kusikia kila kitu nilichosema. Ni kana kwamba alikuwa mahali kwingine.”
Bila shaka, vitabia hivi ni vya kawaida kwa watu wengi—angalau kwa kiwango fulani. “Ni lazima uulize ikiwa dalili hizo zimekuwapo sikuzote,” asema Dakt. George Dorry. Kwa kielelezo, yeye ataja kwamba ikiwa mwanamume amekuwa msahaulifu tangu apoteze kazi yake au tangu mke wake azae, hiyo si kasoro. Zaidi ya hayo, ikiwa mtu kwa kweli ana ADHD, dalili huenea—yaani, huathiri karibu kila sehemu ya maisha ya mtu. Ndivyo ilivyokuwa na Gary mwenye umri wa miaka 38, mwanamume mwenye akili sana, mwenye nishati nyingi ambaye alionekana kwamba hangeweza kumaliza kazi hata moja bila kukengeushwa. Tayari ameandikwa kazi zaidi ya mara 120. “Nilikuwa nimekubali tu kwamba singeweza kufaulu kabisa,” yeye akasema. Lakini Gary na wengine wengi—watoto, wabalehe, na watu wazima wengi—wamesaidiwa kukabiliana na ADHD. Jinsi gani?