Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Watoto Walio Wagumu Ilikuwa kwa shukrani zenye kuhisiwa moyoni kwamba nilisoma makala za Novemba 22, 1994, “Kuwaelewa Watoto Wagumu.” Mwana wangu ana ADHD (Kasoro ya Upungufu Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi). Kwa miaka mingi nilikuwa nikijiuliza makosa niliyokuwa nikifanya yaliyotokeza kuwa na mtoto mgumu mno kiasi hicho. Nilijifunza Biblia naye na kushughulikia mahitaji yake yote, lakini kila siku nilihofia kumwamsha asubuhi na baadaye kumchukua kutoka shuleni. Natumaini hiyo habari itasaidia wale wote wanaoshughulika na watoto ambao wana ADHD.
E. W., Marekani
Nina mwana wa umri wa miaka kumi aliye mgumu sana. Nyakati fulani nimehisi nikiwa nimedhoofika, nimeshuka moyo, peke yangu, na kueleweka vibaya. Asanteni sana kwa kunipa tumaini—na madokezo mengi yenye kutumika.
H. S., Afrika Kusini
Nililia mno nikisoma hizo makala. Mwana wangu ana ADD (Kasoro ya Upungufu wa Makini). Njia ya maisha ni ngumu mno kwa watoto hawa. Hata hivyo, wanastahiki na kustahili heshima na zaidi ya yote, upendo.
B. W., Marekani
Tuligundua miezi sita iliyopita kwamba mwana wetu ana ADHD. Akiwa na umri wa miaka miwili, yeye ni kimbunga halisi, hawezi kukaa tuli kwenye mikutano ya Kikristo, husukuma wengine, kukimbia huku na huku, na sikuzote yeye hujiumiza. Wengine wamejitenga nasi, na hata marafiki wema hawajizuii kutoa maelezo yenye kuumiza nyakati fulani. Asanteni kwa kufafanua hayo matatizo katika njia yenye kufahamika jinsi hiyo.
R. F., Ujerumani
Nina umri wa miaka 15 na nina ADHD. Ni jambo lenye kufariji sana kujua kwamba Yehova hutuelewa na aweza kutusaidia. Natumia dawa kwa ukawaida, na yanisaidia sana. Naweza kukaza fikira vizuri zaidi kwenye kazi yangu ya shule, ya nyumbani na funzo la Biblia. Nathamini sana hizo makala kwa sababu mlionyesha wengine kwamba tatizo hili ni jambo halisi na si mtindo fulani.
S. K., Marekani
Makala hizi zimesaidia sote wawili kuondoa hisia zetu za kutotimiza daraka tukiwa wazazi. Marafiki wenye nia njema wametaja kwamba mwana wangu, anayeugua ADHD, ameharibika au “anahitaji tu kuzabwa makofi.” Hizo makala zaweza kusaidia watu kama hao wafahamu shida ambayo wazazi wengi mno wamo ndani yayo.
T. G., Marekani
Kubuni Kazi Asanteni kwa ile makala “Kubuni Kazi Katika Nchi Zinazositawi.” (Oktoba 22, 1994) Wakati huuhuu ninahudhuria shule na napanga kuwa painia (mweneza-evanjeli wa wakati wote) nitakapofuzu. Tatizo kubwa mno litakuwa kupata kazi. Hadi wakati huu nilikuwa mimetaka kazi ya kukaa kitako ambapo singehitaji kujitahidi kimwili, lakini nilihisi kuaibika nilipojua jinsi ndugu zangu wa Kikristo katika nchi zinazositawi wanafanya kazi yoyote wanayoweza. Sasa nitafanya kazi yoyote inayoniwezesha kupainia.
Y. T., Japani
1914 Nimetoka tu kusoma makala zenu “1914—Mipigo ya Bunduki Ambayo Ingali Inatikisa Ulimwengu Wetu.” (Novemba 8, 1994) Ningependa kusema kwamba sijapata kusoma habari iliyokuwa wazi na sahili jinsi hiyo juu ya mada yenye kubishaniwa kama hiyo. Shule katika nchi yangu hazitoi masomo ya kina kuhusu historia za vita vya ulimwengu, lakini kupata uelewevu wa habari hii ni kwa manufaa makubwa katika kufahamu matukio ya ulimwengu.
W. S., Venezuela