Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Je, Ni Hadaa ya Kisayansi? Makala yenu ya majuzi “Wanasayansi Wahadaa Umma” (Januari 8, 1994) niliweza kuisoma. Wanasayansi waliohusika waonekana kuwa walifanya kosa sahili walilolisahihisha baadaye. Hivi ndivyo sayansi hutarajiwa kufanya kazi, lakini kichwa cha makala yenu chadokeza kwamba walifanya kosa la aina fulani. Ile kuba ya fuvu la kichwa iliyotajwa huenda ilikuja kugunduliwa ni ya punda, lakini uhakika huo hauhusiani kamwe na uasilia wa magunduzi mengine kama gofu maarufu la mwili liitwalo “Lucy.” Sisi twajua viumbe hawa walikuwako.
M. P., Marekani
Hatukuwa tukionyesha kwamba wanasayansi waliohusika katika ugunduzi hususa huu walikosa kufuata haki kimakusudi. Kwa kweli, tulimnukuu Dakt. Moyà mwenyewe na kutaja unyoofu wake. Kisa hicho kilitumiwa kutoa kielezi cha jinsi kweli ya kisayansi imedhabihiwa mara nyingi kwa faida ya kibinafsi, ya kisiasa, na ya utaifa. Kweli, vielezo vya visukuku vimepatikana. Lakini hakuna uthibitisho wowote ule kwamba viumbe hawa kwa kweli walikuwa mababu wa kale wa wanadamu. Kwa kielelezo, “Lucy” alikuwa na ubongo wenye ukubwa wa theluthi moja ya ule wa mwanadamu. Kwa wazi hiyo ilikuwa spishi fulani tu ya sokwe ambaye sasa amekwisha kutoweka wala si zaidi ya hilo.—Mhariri.
Uzoelevu Asanteni sana kwa ule mfululizo “Uzoelevu—Ni Nini Huusababisha?” (Aprili 22, 1994) Nilisoma makala hizo kutoka mwanzo hadi mwisho mara mbili. Ni kwamba, mimi nina kasoro ya ulaji. Mimi hujihisi nafuu kidogo nikipata matibabu katika kliniki, lakini bado huwa natatizika sana nyakati fulani. Makala hiyo iliimarisha azimio langu.
T. S., Ujerumani
Mimi nilikuwa mraibu wa dawa za kulevya na alkoholi hapo zamani. Ushauri mtoao wafaa kwelikweli. Nilihamasishwa pia kwa kutambua kwamba uraibu ni kipingamizi cha kiroho, kwa kuwa mraibu hawezi kuwa safi kabisa machoni pa Muumba wetu.
M. G., Ufaransa
Miaka sita na nusu iliyopita, nilifiwa na mwanangu kutokana na uraibu wa kokeni. Nikiisha kuhisi maumivu hayo na kufaulu kuyavumilia, nilikuwa tayari kushughulika na uraibu wangu mwenyewe wa chakula. Kwa kukulia katika familia yenye uzoelevu wa alkoholi, nilikuwa nimejifunza kutumia chakula kujifariji na kuepuka maumivu. Nilijaribu lishe mbalimbali, lakini wapi. Hata hivyo, kuuonja zaidi upendo wa Yehova baada ya miaka 20 ya kuwa Mkristo kumenisaidia sana. Asanteni, tena sana kwa makala hizo.
S. E., Marekani
Mhalifu Aliyerekebishwa Nataka kuwashukuru sana sana kwa ile makala “Utoro Wangu Kuelekea Kweli.” (Februari 8, 1994) Nina umri wa miaka 24, na nimo katika Gereza la Jimbo la Washington nikingoja kuuawa. Makala hii ilinilenga barabara nami nataka kufanya yaliyo sawa machoni pa Yehova. Brian Garner hakika aliugusa moyo wangu.
J. B., Marekani
Mimi ni mfungwa wa gereza moja la urekebisha-tabia la Missouri na nilichochewa na uamuzi wa Bw. Garner wa kujisalimisha kwa wenye mamlaka baada ya kujifunza ile kweli. Hii yaonyesha tokeo ambalo tengenezo lenu laweza kuwa nalo juu ya watu wenye akili iliyofunguka na moyo mwema. Ni rahisi kuona kwamba uhuru wa kweli huja kwa kujizoeza tu imani katika Mungu.
W. B., Marekani
Mwaka mmoja uliopita nilikuwa nikiiba-iba fedha kutoka kwa mashirika niliyofanyia kazi. Niliiba mamia ya maelfu ya yeni, jambo ambalo hakuna mtu angaliwaza msichana wa miaka 20 alikuwa akifanya! Hata hivyo, nilikuwa nikijifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, na dhamiri yangu ikaanza kunihukumu. Kwa hiyo nilirudisha fedha hizo na kuungama kwa wenye madaraka. Na ingawa maneno fulani makali yalisemwa, hakuna hatua zaidi iliyochukuliwa. Nashukuru sana kwa makala hii, kwa maana imenisaidia nitambue kwa mara nyingine tena jinsi rehema ya Yehova ilivyo kubwa sana.
S. M., Japani