Vijana Huuliza...
Mitindo—Je, Nifuate Halaiki?
‘HIYO ni shwari aisee!’ ‘Hiyo ni kwao!’ Huenda pongezi zikavuma hivyo wakati marika wako waonapo unafuata mtindo wa karibuni zaidi. Ndiyo, mitindo ina uwezo wa kuvuta fikira na kuamsha maitikio yenye nguvu.
Hata hivyo, pia mitindo hubadilika kama halihewa na ni ya muda mfupi ajabu. Kulingana na uchunguzi mmoja wa mauzo, mtindo hutia mizizi kwanza miongoni mwa vikundi vidogo vya vijana wajasiri, wasiofuata desturi. Uanzapo kuenea, watengeneza bidhaa na watangazaji huuendeleza kwa njia ya matangazo ya magazeti, televisheni, na ya redio. Wanamuziki na watu maarufu hulipwa kuupa ustahifu na fahari kwa kuuidhinisha. Vijana wenyewe huenda wakauendeleza kwa kuufuata juu-chini. Ukipamba moto, waweza kuwa mtindo wenye kuvuma miongoni mwa “matineja walio wengi zaidi.”
Ingawa hivyo, hatimaye mtindo hupoa ukatokomea. (American Demographics) Lakini ingawa mtindo, dansi, au kifaa fulani kipya chavuma sana, huenda wewe ukahisi ukiwa chini ya msongo mkali kujipatanisha. Wengi huhisi kama Kim mwenye miaka 15: “Wafanywa uhisi ukiwa kama mkataliwa uwapo tofauti.”
Kurukia mitindo ya halaiki kwaweza kuwa shughuli yenye gharama. Kwa kielelezo, chukua ule mtindo wa pini uliofoka miongoni mwa vijana Wafaransa miaka michache iliyopita. Kulingana na makala moja ya 1991 katika The New York Times, “ni sharti la kifashoni kwamba kikofia chako cha mchezo wa besiboli au mashavu ya koti lako yajazwe pini za kuchomeka za enameli, zenye rangi za kupendeza zilizo na vidoadoa vilinganavyo na vile vya mchezo wa domino.” Mtindo huo ulionekana usio na madhara kamwe—lakini ilikuwa lazima ulipe donge la dola 12 kwa kila pini ya mbuni maarufu.
Huenda pia kijana akapata kwamba kuwa “shwari” humaanisha zaidi ya kutumia fedha nyingi. Kwa kielelezo, katika maeneo fulani ambako ni fashoni nzuri kuvaa kikofia cha mchezo wa besiboli, ni lazima uchague kikofia chenye rangi ifaayo, kinachowakilisha timu ifaayo, na sehemu ya mtindo wenyewe ni jinsi uvaavyo kikofia hicho.
Kwa vijana wengi hayo ni makubwa. Wao huona kwamba kufuata mitindo fulani ndio ufunguo wa kupata fahari au ukubali. Hata hivyo, tutaona kwamba kurukia kujiunga na halaiki si werevu sikuzote.
Kufikiria Hatua Zako
Biblia haishutumu kwa jumla mitindo yenyewe hasa. Huenda ikawa utendaji fulani fulani upendwao na wengi wafaa ujapokuwa wa kimitindo. Kwa kielelezo, mbio ya polepole ilionwa na watu fulani kuwa mtindo wakati ilipopata kupendwa na wengi miaka michache iliyopita. Lakini ni nani awezaye kukanusha manufaa za mazoezi ya kiasi, yafaayo?—Linganisha 1 Timotheo 4:8.Hata hivyo, mitindo fulani hutofautiana kuanzia ile ya kijinga hadi iliyo hatari kabisa. Hivyo onyo la mithali moja ya kale lafaa: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” (Mithali 14:15) Mtu mwenye busara ni mwenye hekima, mwenye utambuzi. Hafuati elekeo jipya kwa upofu eti kwa sababu tu lapendwa na wengi. Kwa hekima, yeye hupima uzito wa matokeo ya matendo yake.
Huenda gharama likawa jambo moja la kufikiria. Gazeti moja la Kanada laeleza juu ya msichana tineja afanyaye kazi katika mkahawa uuzao vyakula vya kutayarishwa haraka. Zaidi ya nusu ya fedha zake achumazo kwa jasho hutumika kununua mitindo ya karibuni zaidi ya mavazi. “Feza [“fedha,” UV] ni ulinzi,” yasema Biblia, yaani, ni chombo kihitajiwacho, chenye mafaa. (Mhubiri 7:12, Zaire Swahili Bible) Je, waweza kuthubutu kuzitumia kwa vitu ambavyo, kama atamkavyo mwandikaji mmoja, ‘vilikusudiwa kuwa vikuukuu mnamo majira mamoja au mawili’?
Huenda hatari ya kimwili ikawa jambo jingine la kufikiria sana. Kucheza breki dansi kulipendwa na wengi si muda mrefu sana uliopita. Lakini kulitokeza maumizo mengi ya mgongo. Namna gani leo? Makala moja katika gazeti Rolling Stone laongea juu ya mbinu za fujo kwenye vilabu vya dansi na tamasha za roki, kama vile “kupiga mbizi jukwaani” (kuruka kutoka jukwaani hadi mikononi mwa mashabiki wanaoshangilia), “kudundana,” na “kumoshiana”—utendaji wa “dansi” ambao kidogo ni zaidi ya jeuri iliyopangiliwa mipigo ya muziki. “Kitu hiki kimeruka mipaka mno. Namaanisha, kabisa,” alalamika kijana mmoja. Msichana huyo aeleza jinsi “wanamosha” ‘hujitamba kwenye sakafu ya dansi na kukatika chakachaka, wakiyongayonga kama chamchela yenye kupanuka daima, wakimgonga kiholela yeyote yule mwenye fursa mbaya ya kusimama karibu nao.’ Huenda mwenendo huo ukavutia wengine wa marika wako. Lakini je, kuwa mahali kama hapo au kufanya mambo kama hayo kutakupatia upendeleo wa Mungu, aamuruye Wakristo ‘wakatae katakata kukosa kuogopa Mungu na tamaa za kilimwengu na kuishi kwa utimamu wa akili’?—Tito 2:12, NW.
Namna gani hatari za afya za kutoboa mwili na kuuchanja chale—ambako pia kunapata kupendwa na wengi miongoni mwa vijana? Madaktari husema kwamba kuchanja chale kwaweza kuleta hatari za kitiba, kama vile mchochota wa ini na labda UKIMWI, ikiwa kanuni za usafi hazifuatwi. Halafu kuna lile tazamio la kubaki na michanjo-chanjo hiyo baada ya mtindo huo kutokomea mbali. Ni kweli, chanjo za chale fulani zaweza kufutiliwa mbali na kiangazia-nuru. Lakini matibabu ya kiangazia-nuru huhusisha vipindi kadhaa vya maumivu, ambavyo kila kimoja hugharimu mamia ya dola.
Yaliyo hatari kupita yote ni madhara ya kiroho yawezayo kutokea kwa kufuata mitindo fulani. Mengi yayo hutegemea watu maarufu—waigiza-sinema, wanariadha, wanamuziki, na kadhalika. Huwa jambo “shwari” kuvalia na kutenda kama yeyote yule aliye kivumisho wakati wa sasa. Lakini Yehova Mungu huionaje ibada hiyo ya majabali wenye sifa? Kama namna ya ibada ya sanamu. Hivyo Biblia huonya: “Ikimbieni ibada ya sanamu.” (1 Wakorintho 10:14) Watu wengi maarufu hawajali kamwe viwango vya kiadili vya Biblia. (1 Wakorintho 6:9-11) Kwa kuwa iko hivyo, je, kweli Mungu angeweza kufurahi ukitenda au kuvalia kwa njia ambazo hakika ni kama kuwasujudia watu hao?
Wazo Uwapalo Wengine
Pia Biblia huamuru vijana wawaheshimu wazazi wao. (Waefeso 6:2) Je, haingewavunjia heshima kama ungekuja nyumbani umejazana vito vya mwili au umechanjwa-chanjwa chale? Namna gani wengine, kama vile wanadarasa wenzako? Ikiwa wewe ni Mkristo, je, wangeona ni vigumu kukuchukua kwa uzito ikiwa ungejaribu baadaye kushiriki nao imani yako?—Linganisha 2 Wakorintho 6:3.
Hilohilo lingeweza kusemwa juu ya kuvalia baadhi ya mitindo ambayo wasanifu wa rapu hufanya ipendeze watu wengi. Ni kweli, kikofia cha mchezo wa besiboli ni kifuniko cha kichwa tu katika maeneo mengi. Lakini katika ujirani fulani wa mijini, “sasa siasa zahusika sana katika kupendwa kwa kofia fulani fulani.” (Entertainment Weekly) Je, kuvalia vikofia fulani, makoti, snika, au vifaa vingine vya hipu-hopu kungeweza kutoa wazo la kwamba wewe washikamana na mtindo-maisha wa rapu? Kumbuka, upendo wa Kikristo haujiendeshi ‘kwa kukosa kuwa na adabu’ wala kwa namna ya kushtua.—1 Wakorintho 13:5.
Fikiria lililopata kikundi kimoja cha wasichana matineja ambao, kulingana na gazeti People, waliwaonyesha ufidhuli wenyeji wa mji wenye kujali sana maungwana na wasiorukia mabadiliko mapya kwa kwenda shuleni wakiwa wamevalia “mavazi ya mtindo wa hipu-hopu.” Msichana mmoja alieleza hivi: “Sisi huona mavazi haya katika MTV [kituo cha televisheni kionyeshacho video za muziki]. Mimi nilifikiri yalionekana vizuri.” Hata hivyo, mavazi hayo ya kufuata maelekeo ya halaiki yaliwasha ubishi—na jeuri kati ya watu wa jamii mbalimbali.
Kwa hiyo sisi Wakristo twataka ‘kujiremba wenyewe pamoja na kiasi na utimamu wa akili.’ (1 Timotheo 2:9, NW) Hii yahusisha kufikiria hisia na mitazamo ya wengine na kutosisitiza juu ya upendelevu wa mtu binafsi. Yamaanisha pia kuepuka mitindo ya mavazi na mwenendo ambao wengine huona kuwa wa kupita kiasi.
Uhitaji wa Tahadhari
Bila shaka, kila mtindo ni lazima upimwe una uzito gani kulingana na ustahili wao wenyewe. Ingawa hivyo, kumbuka kwamba Shetani Ibilisi ndiye mtawala wa ulimwengu huu na mradi wake ni ‘kumeza mtu.’ (1 Petro 5:8; Yohana 12:31; 1 Yohana 5:19) Bila shaka mitindo fulani ipendwayo na wengi imetumiwa na Shetani kukengeusha fikira za vijana na kuwaongoza watoke kwa Mungu. Hivyo yafaa kuwa na tahadhari.
Kwa kawaida si jambo la hekima kuwa miongoni mwa walio wa kwanza kufuata elekeo au mtindo mpya wowote; ni salama zaidi kuegemea kutorukia upesi kufuata mabadiliko mapya. Kwa upande mwingine, pia Biblia hutahadharisha dhidi ya kuwa ‘mwadilifu kupita kiasi.’ (Mhubiri 7:16, NW) Hakika si lazima ukinze mabadiliko ya mtindo kufikia kuonekana mzamani hoi, mwanaajabu, au mzuzuaji.
Wakati mtindo uvunjapo waziwazi kanuni za Biblia au yastahikiyo, basi hapo yafaa kuuepuka kabisa. Ni kweli, si rahisi kuwa tofauti na marika wako. Lakini katika kitabu chake How to Say No and Keep Your Friends, mwandikaji Sharon Scott auliza: “Je, wewe una marafiki walio werevu sana na wakujuao vema sana hata iwapase wao kukufanyia maamuzi yako? Labda sivyo!” Je, haingekuwa afadhali kuongozwa na matakwa ya wazazi wako na dhamiri yako iliyozoezwa na Biblia? Huenda kufanya hivyo kusikuletee kibali cha marika wako, lakini kutaleta kibali cha Yehova, ambacho, tofauti na mtindo fulani wenye kupita mbio-mbio, chaweza kudumu milele!—Zaburi 41:12; Mithali 12:2.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Wazazi wako wataitikiaje ukikubali kufuata mtindo fulani?