Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kesi ya Mahakamani Siwezi kujizuia kuonyesha uthamini wangu kwa ile makala “Wakristo Waikabili Tena Mahakama Kuu ya Yerusalemu.” (Novemba 8, 1994) Niliisoma mara kadhaa na nilisisimuliwa na kile kilichotukia. Kwa kuwa Ariel Feldman alichukua msimamo imara kwa kupendelea kilicho sawa, ushahidi mzuri ajabu ulitolewa.
A. I. B., Brazili
Betri Nafanya kazi ya kushughulika na betri ili kujiruzuku na ningependa kuwashukuru kwa ile habari “Betri Hatari” iliyokuwa katika “Kuutazama Ulimwengu.” (Agosti 22, 1994) Lakini kulikuwa na jambo moja la maana lililokosekana kutokana na maelekezo yaliyotolewa na gazeti Snow Country ya kuwasha gari kwa kutumia waya zilizounganishwa kwa betri ya gari jingine, nalo ni hili, waya nyeusi yapasa kuwa muunganisho wa mwisho kufanywa.
P. R., Kanada
Asante kwa dokezo hilo la usalama.—Mhariri.
Amkeni! Yaleta Faraja Nilisoma ile makala “Magazeti Yatoayo Faraja Inayotumika” (Januari 8, 1995), nami nimekuwa na matokeo katika kutoa matoleo ya zamani ya Amkeni! Kwa ujumla watu ni wenye shukrani kwa msaada wowote wanaoweza kupata kwa matatizo yao. Mwanamke mmoja aliniambia kwamba mwana wake alikuwa na Kasoro ya Upungufu Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi. Nilimwangushia lile toleo “Kuwaelewa Watoto Wagumu” (Novemba 22, 1994), naye akaomba nakala nyinginezo 30 za kushiriki na marafiki!
D. Q., Marekani
Baada ya kusoma makala “Magazeti Yatoayo Faraja Inayotumika,” nilitafuta magazeti yangu ya zamani ili nione ikiwa ningeweza kupata mengine ili kuwapa wataalamu. Kufikia wakati huu nimezuru vitovu vya utunzaji wa afya, makao kadhaa ya kuhifadhia maiti, makao ya kufungia vijana, na baraza la elimu la Manispaa. Mara moja nilimaliza magazeti yangu!
D. R., Marekani
Useja Asanteni kwa makala “Maoni ya Biblia: Wakati Useja Ni Zawadi.” (Februari 8, 1995) Mahali ninapoishi, ndoa ni jambo kubwa; ndugu na dada Wakristo wanakusukuma kuoa. Sikufikiria sana kuhusu ndoa hadi nilipokuwa na umri wa miaka 30. Ndipo nikaanza kuhisi uhitaji wa mwandamani. Namshukuru Yehova kwa kuandaa makala hiyo wakati nilipohisi kwamba singeweza kuendelea kuvumilia.
E. M. A., Marekani
Miaka miwili iliyopita nilikuwa painia, mweneza-evanjeli wa wakati wote, na kadiri wakati zaidi upitavyo, ndivyo nizidivyo kutambua jinsi inavyotosheleza kumtumikia Yehova “bila kukengeushwa.” Niliamua kubaki mseja—makala hiyo ilifika barabara wakati ufaao.
G. V., Italia
Mitindo Katika makala yenu “Vijana Huuliza . . . Mitindo—Je, Nifuate Halaiki?” (Desemba 8, 1994), mlitaja kuchanja chale. Nilishangaa kwamba hamkurejezea ile amri kwenye Mambo ya Walawi 19:28: “Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu.”
L. D., Marekani
Maneno hayo kwa kweli yatoa kiasi fulani cha ufahamu wenye kina katika mawazo ya Mungu kuhusu jambo hili. Bila shaka, Wakristo hawako chini ya Sheria ya Kimusa. (Wakolosai 2:14) Hata hivyo, watu mmoja-mmoja watafanya vema kufikiria andiko hili wanapoamua kile watakachofanya kuhusiana na jambo hili. Hatari za afya zilizoripotiwa na mtazamo ambao kuchanja chale utatoa kwa wengine ni mambo ya ziada ambayo Mkristo apaswa kufikiria kwa uzito sana.—Mhariri.
Miezi sita iliyopita nilifuata halaiki katika mitindo na kumalizikia na chale katika kisigino changu. Kila wakati nitazamapo kisigino changu, nakumbushwa uamuzi wangu. Najiuliza tu mashaka ambayo wengine huenda wakawa nayo sasa kuhusu mwenendo wangu. Nina wasiwasi pia ikiwa huenda nikawa kisababishi cha kukwaza wengine kutanikoni. Nitafikiria kwa uzito zaidi wakati ujao mtindo wa halaiki utakapokuwa wenye kupendwa sana.
S. C., Marekani