Kuutazama Ulimwengu
Lile Ongezeko la Takataka
Askari walinda zamu katika mpaka wa Poland wako macho kwa aina mpya ya mvamio siku hizi—takataka za kigeni. Kulingana na The Washington Post, katika 1992, mamlaka za Poland zilisimamisha masafirisho 1,332 yasiyotakwa ya takataka kutoka Ulaya Magharibi pekee. Katika nusu ya kwanza ya 1993, idadi ya masafirisho hayo iliongezeka kwa asilimia 35. Katika mabara mengi ya Magharibi, takataka zilizo hatari zimekuwa ghali sana kuzitupa hivi kwamba kuzisafirisha hadi mabara yasiyositawi sana ambamo sheria za kimazingira huenda ikawa vigumu zaidi limekuwa chaguo lenye mapato. Kwa kielelezo, kampuni mbili za metali za Marekani zilipatwa na hatia ya kuchanganya tani 1,000 za uvumbi wenye sumu kutoka kwa kiyeyushi kuingia ndani ya usafirishaji wa mbolea iliyopelekwa Bangladesh. Baadhi ya takataka hiyo husingiziwa kuwa msaada kwa wahitaji. Maofisa wa forodhani katika Poland waripoti kwamba kwa ukawaida wao hupokea bidhaa zinazoonyesha kuwa msaada wa kitiba kutoka Australia, Ulaya, na Marekani ambazo hutokea kuwa masazo ya sirinji, mavazi ya ndani, na vifaa vya choo—vyote vikiwa vimetumiwa na kuchafuliwa.
Gazeti la Talaka
Kwa kupata nafasi ya kujifaidi katika kiwango cha talaka kinachoongezeka, mchapishaji wa gazeti katika Ufaransa ameanzisha jarida la kawaida liitwalo Divorce. Mwanasafu kwa Bulletin ya Sydney, Australia, aeleza kwamba gazeti hilo hutokeza “safu za shauri kutoka kwa wanasheria na wanasaikolojia, madokezo kwa wanawake wanaojaribu kutafuta kazi ya kwanza baada ya ndoa, na—kwa walio hodari—jinsi ya kurudia ule mchezo wa kupeana miadi ya kijinsia.” Ingawa hivyo, mojapo ya habari ambazo gazeti hilo kwa wazi halishughulikii ni mapatano ya kindoa. Mwanasafu huyo aonelea hivi: “Yeyote anayetafuta shauri kuhusu jinsi ya kuunganisha uhusiano unaoyumba-yumba apaswa kuutafuta kwingineko.” Naam, tafuta shauri kutoka kwa Neno la Mungu lisilokosea, Biblia.
Ndege Mvumi wa Venezuela Hatarini
Spishi 28 tofauti za ndege wavumi katika Venezuela wako katika hatari ya kutoweka. Baadhi ya hizi hazipatikani penginepo ulimwenguni. Ndege mvumi ni wenyeji wa zile Amerika, akienea kutoka Alaska hadi Argentina na Chile. Ana uzani wa kati ya gramu 2 na 9, aliye mdogo zaidi akiwa ni ndege nyuki mvumi, aliye na kipimo cha karibu sentimeta 5, na mkubwa zaidi akiwa ni ndege mvumi jitu, ambaye ana kipimo cha sentimeta 21. Ni nini kinachofyeka ndege huyo mvumi katika Venezuela? Ni maradhi ama mnyafuzi? La. Carta Ecológica, barua-habari iliyochapishwa na kampuni ya mafuta ya Lagovén, yafunua hatia iko kwa ufyekaji misitu—ule utaratibu wa kuharibu mazingira ya ndege. Kiumbe mdogo huyu, avutiaye, mwenye urangirangi ni mmojapo tu wa waliohatarishwa na uharibifu wa misitu-mvua usio na huruma wa mwanadamu.
Zoea Lenye Madhara Lavunjwa
Serikali ya Pakistan imeamuru kwamba paketi za tambuu lazima ziwe na tahadhari ya afya sawa na ile iliyo katika paketi za sigareti, laripoti gazeti la Asiaweek. Gazeti hilo laeleza kwamba mamilioni ya watu katika kusini mwa Asia wana uraibu wa pan masala, mchanganyo wa tambuu na aina tofauti-tofauti za mafuta na viungo vingine vilivyofungwa katika majani ya tambuu. Hizi zimekusudiwa kutafunwa. India tayari iliweka maonyo katika paketi za tambuu kwa sababu ya uhusiano ulioripotiwa wa kansa ya mdomo. Na watoto wamepata kunyongwa hadi kifo na tambuu. Sheria mpya ya Pakistan itakataza uuzaji wa tambuu kwa watoto walio na umri ulio chini ya miaka mitano.
Fungu la Mababu na Manyanya Laongezeka
Machunguzo katika Marekani yaonyesha kwamba mababu na manyanya, hasa manyanya, wanachukua fungu lenye kuongezeka katika maisha ya wajukuu wao. Uchunguzi unaoendelezwa na Taasisi ya Kitaifa Kuhusu Uzee umepata kwamba asilimia 69 ya wale waliozaliwa kati ya 1931 na 1941 ni mababu na manyanya; kama asilimia 44 yao hutumia zaidi ya saa 100 kwa mwaka wakitunza mjukuu wao mmoja ama zaidi. Kwa wastani, mababu na manyanya hawa hutumia saa 659 pamoja na watoto, sawia ya siku 82 za muda wa saa nane, laeleza The Wall Street Journal. Uchunguzi ulipata, wanawake, hutumia wastani wa saa 15 hadi 20 kwa juma kuwatunza wajukuu na wana uwezekano wa mara 2.5 zaidi kuwa watunzaji kuliko wanaume.
Mababa Waadimika
Kama ilivyo katika sehemu nyingine za ulimwengu, vibano vya familia katika Japani haviko vile vilivyokuwa. The Daily Yomiuri liliripoti majuzi kwamba wanaume Wajapani wapatao 481,000, kwa sababu ya kuhamishwa kikazi walilazimika kuishi mbali na famillia zao. Tarakimu hiyo ni asilimia 15 juu zaidi ya miaka mitano iliyotangulia na ilitarajiwa kupanda tena zaidi kadiri matatizo katika kutafuta makao na shule yazidipo kuongezeka. Katika suala hilohilo, gazeti hilo liliripoti uchunguzi wa wanafunzi juu ya shule ya msingi na wa mwanzo wa sekondari ambayo asilimia 43 ya vijana walisema kwamba kamwe hawaongei na baba zao. Idadi kubwa, asilimia 18.4, walisema kwamba huwa hawana mazungumzo pamoja na mama zao.
Mabadiliko ya Kifamilia Katika Argentina
Uchunguzi wa majuzi ulifunua mabadiliko yaliyo makubwa kwenye muundo na mfumo wa kitabia wa maisha ya familia ya Kiargentina, kulingana na gazeti Clarín la Buenos Aires. Likieleza juu ya familia ya kiolezo—moja iliyo kubwa, iliyoungamanika, na wakati wa siku za mapumziko ama usiku ilayo pamoja–gazeti hilo lilisema hivi: “Wengi leo wangesema kwamba familia kama hizo za kiolezo ni taswira ya kale tu, ukale wa kuwazia unaoangazwa kwa picha.” Tarakimu katika kile kitabu La familia en la Argentina (Familia Katika Argentina), na Susana Torrado, zilionyesha kwamba katika mwongo uliopita, familia za mzazi mmoja, sasa zikiidadika kuwa 1,200,000, zimeongezeka katika Argentina kwa kukadiria asilimia 60 hadi 80. Watoto waliozaliwa nje ya ndoa sasa wafikia zaidi asilimia 36 ya uzaaji wote—ongezeko la karibu asilimia 30 tangu 1960. Zaidi ya hilo, mahoji yameonyesha kwamba thuluthi ya wale walio na umri wa kati ya 20 na 34 hawaamini kwamba kifungo cha ndoa ni cha maisha.
Msamiati wa Watoto
Watoto huenda wajue zaidi kuhusu mambo halisi yasiyopendeza ya ulimwengu wa kisasa kuliko vile watu wazima wangewadhania, uchunguzi katika Italia ulifunua. Kikoa kutoka Kitovu cha Utafiti cha Kitaifa cha Italia kilichunguza zaidi ya insha 5,000 zilizoandikwa na watoto wa shule wenye umri wa miaka sita hadi kumi. Kulingana na ile karatasi habari La Repubblica, ulinganisho wa msamiati wao wa maneno 6,000 na habari za kusomwa na watoto zilizoandikwa na watu wazima ulifunua kwamba “ulimwengu mtulivu kama usio halisi, bila matatizo” uonyeshwao kwa watoto ‘hauwadanganyi.’ Karatasi hilo laongezea hivi: “Wanajua hakika kinachomaanishwa na ‘dawa za kulevya,’ ‘UKIMWI’ na ‘kulalwa kinguvu.’” Watafiti hao walisema kwamba “ulimwengu wa maandishi ya watoto waonekana kuwa ulioendelea na uliopiga hatua zaidi pamoja na nyakati kuliko vichapo wanavyovisoma” vilivyoandikwa na watu wazima, aonelea Corriere della Sera.
Kuweka Chambo Katika Ndoano
Kanisa fulani la kievanjeli katika Maryland, Marekani, lilipata njia mpya ya kushawishi watu waliingie. Jumapili ya majuzi, watu 125 wa kwanza kuwasili kanisani walipatiwa kila mmoja dola 10. Lililotakiwa kwao ni kukaa tu muda wote wa ile ibada ya dakika 75, ambayo ilihusisha kiigizo na kuimba kwa kutegemezwa na bendi ya “roki-nyepesi.” Kulingana na shirika la habari la Associated Press, mkurugenzi msaidizi wa huduma za kanisa hilo alisema: “Watu wengi hulalamika hawaendi kanisani kwa sababu siku zote makanisa hutaka fedha. Tulifikiri, ‘Kwa nini tusiwe na ujasiri na tuwape fedha?’” Watu walio wengi, ripoti hiyo ilisema, walikubali fedha hizo, ingawa wengi walidai walizirudisha baadaye. Thelathini na wawili walibaki na fedha hizo.
Mapipa Makuukuu Yatumika
Badala ya kutupa mapipa makubwa ya kusafirisha kama takataka nyingi za metali, kampuni ya kusafirishia katika Afrika Kusini imepata njia za kuyatumia kwa maarifa yawapo yameisha mno kuweza kusafirishia bidhaa nzito tena. Mawili ya miundo hiyo mikubwa ya metali, iunganishwapo pamoja, hufanya kiasi kizuri cha darasa la shule. Kwa kawaida, upande mmoja wa kila pipa lazima utolewe, na madirisha na milango lazima ziongezewe upande uliosalia. Mapipa makuukuu yaweza pia kutumiwa kama makao, maduka, kliniki, na maktaba. Katika kisa kimoja, kulingana na lile gazeti African Panorama, “mapipa 16 yaliyogeuzwa huandaa madarasa 8 yaliyo na nafasi ya kutosha kwa wanafunzi zaidi ya 1,000.” Hivyo basi, zaidi ya mapipa 1,000 yametolewa yawe ya jumuiya zenye uhitaji za Afrika Kusini. Lakini kampuni inayohusika inaishiwa na mapipa makuukuu na inaomba msaada wa kampuni zile nyingine za kimataifa za usafirishaji zilizo na mapipa makuukuu ya ziada.
Kunyong’onyea kwa Ubongo
Kumeza alkoholi nyingi na mafuta kwa miaka hakuongezi uteketeke tu bali hudidimiza ubongo, kulingana na uchunguzi wa kikundi cha watafiti cha Koleji ya Kitiba ya Chuo Kikuu cha Akita katika Japani. Kwa zaidi ya miaka saba iliyopita, kikundi hicho kilifanya uchunguzi wa watu 960, kikitumia MRI (Taswira Sumaku za Mvumo wa Ubongo), na kikapata kwamba asilimia 58 ya wale wategemeao alkoholi walikuwa wamepata mnyong’onyeo wa ubongo. Miongoni mwa wale walio hipalipemia, kiwango cha juu cha vifanyiza mafuta katika damu, asilimia 41 ya wale walio katika umri wa miaka ya 40 na ya 50 na asilimia 55 ya wale walio na miaka zaidi ya 60 walionyesha mnyong’onyeo kama huo. Kinyume kabisa na hilo, ni asilimia 4 tu ya wale wasio na tegemeo la alkoholi wala hipalipemia walionyesha mnyong’onyeo. Ishara za kupunguka kiakili zilionekana miongoni mwa asilimia 80 ya wale walio na mnyong’onyeo, laripoti gazeti Yomiuri Shimbun. Profesa msaidizi Ikuo Naemura wa kikundi hicho cha utafiti ashauri hivi: “Mnyong’onyeo wa ubongo husitawi polepole lakini kwa hakika. Ni muhimu kuepuka kunywa sana alkoholi na kula mno chakula chenye mafuta.”