Kuutazama Ulimwengu
Gharama za Uhalifu
Kulingana na The Washington Post, Marekani hutumia au hupoteza dola bilioni 163 kila mwaka kutokana na uhalifu. Gazeti hilo laripoti kwamba hata baada ya kujirekebisha kulingana na infleshoni, jumla hii ni mara nne hivi ya kiasi kilichotumiwa katika 1965. Gazeti hilo laongezea kwamba hasara ya uhalifu yatia ndani “zaidi ya dola bilioni 31.8 za kiwango cha kitaifa na kijimbo kuhusu polisi, dola bilioni 24.9 kwa kurekebisha tabia za watu, dola bilioni 36.9 katika hasara ndogo-ndogo, dola bilioni 20 katika upunjaji wa bima, na dola bilioni 17.6 kwa hasara za mali moja-moja na gharama za kitiba. Na bado dola bilioni 15 zaidi zatumiwa kwa usalama wa watu binafsi, dola bilioni 9.3 kuhusu gharama za mahakama na dola bilioni 7.2 kuhusu kufanya daawa ya wahalifu na kutetea umma.” Mathalani, katika kisa kimoja cha kawaida ya kufyatua bunduki katika eneo la Washington, D.C., Post lasema kwamba kumtibu mjeruhiwa hugharimu wastani wa dola 7,000 muda wa saa chache za kwanza baada ya ule mfyatuo wa bunduki. Mjeruhiwa akiokoka, gharama ni karibu dola 22,000. Serikali ikijitia katika gharama ya kumsaka na kumshtaki mkosaji, hapo gharama za kumfungia huwa karibu dola 22,000 kwa mwaka.
Damu Isiyo Salama Katika Filipino
Katika Filipino, huduma za kutiwa damu mishipani ‘si salama, hazina matokeo na ni za utapanyaji,’ wakata shauri uchunguzi mpya uliofanywa na kikoa cha madaktari Wafilipino. Katika matokeo ambayo waziri wa afya wa nchini, Juan Flavier, aliyaita “ya kugutusha sana,” uchunguzi huo ulionyesha kwamba chache kuliko nusu ya benki za damu nchini zilikuwa na wafanyakazi wawezao kufanya uchunguzi wa viini vya UKIMWI, kaswende, mchochota-ini B, na malaria. Zaidi ya hilo, uchunguzi huo ulipima sampuli 136 za damu kutoka benki za damu ukapata kwamba hata kati ya damu iliyokuwa imechunguzwa viini, asilimia 4 hivi ilikuwa na viini.
Takataka Katika Njia Kuu Bora ya Habari
Njia kuu bora ya habari, mfumo wa miunganisho ya kompyuta uandaao ubadilishano wa habari miongoni mwa watumizi wa kompyuta, imesifiwa mahali pengi kuwa ajabu ya tekinolojia. Lakini pia ina vizuizi. Katika Globe and Mail la Kanada, mwanajarida Sean Silcoff aliandika juu ya ile miezi miwili aliyotumia “njia kuu” hiyo kwa makusudi ya utafiti. Alikata shauri kwamba ni “ovyo” na “imefujwa kotekote kwa takataka za utamaduni wa Magharibi.” Alisema kwamba kulikuwa na “vikundi vya mazungumzo” 3,500 katika mfumo alioutumia, vingi vikiwa na habari kama porojo juu ya mabingwa wa michezo na utumbuizo, mizaha yenye uchukizo usio na adabu, na vijambo vihusuvyo maonyesho ya televisheni yapendwayo na wengi. Moja hata lilikazia njia za kujiua. Silcoff alitamka hivi: “Kifaa kiwezacho kutimiza mengi ajabu kinatapanywa na jamii ionekanayo kuwa imejaa wagonjwa tele wa akili.”
Asali kwa Vidonda?
Akiandika katika Medical Post la Kanada, Dakt. Basil J. S. Grogono adai kwamba yule nyuki-asali duni huenda akaweza kuwafanyia mengi zaidi wale wasumbuliwao na vidonda vya tumboni kuliko hata vile madaktari wangeweza kufanya miongo iliyopita walipokuwa wakikimbilia-kimbilia kufanya upasuaji mkubwa. Asema kwamba wastadi zaidi wamekuja kutambua fungu litimizwalo na kijiumbe fulani, Helicobacter pylori, katika vidonda vya tumboni. Ingawa wengine wamependekeza kutumia dawa ili kupambana na kijiumbe-maradhi hiki, Grogono asema kwamba dawa hizi zina athari za kando zisizopendeza na kwamba huenda vijiumbe-maradhi vikasitawisha ukinzani kwazo. Kwa upande ule mwingine, yeye ataja uchunguzi mmoja wa majuzi uliochapishwa katika Journal of the Royal Society of Medicine ambamo nguvu za asali za kupambana na bakteria zilipimwa. Namna moja, iliyotoka kwenye nyuki wa New Zealand waliolishwa mmea uitwao manuka, ilikuwa na matokeo ya kupigana na kile kijiumbe-maradhi kinachosababisha vidonda.
Risasi na Divai
Wanasayansi katika Ubelgiji na Ufaransa wametambua kitu kiwezacho kuwa tisho katika divai fulani za Kifaransa—risasi (ledi). Risasi itokayo katika mitungi-fuwele ya kumimina divai na kutokana na karatasi za kufungia vitu zilizofanyizwa kwa risasi yaweza kuponyoka iingie katika divai. Lakini uchunguzi mpya huo, ulioripotiwa katika Science News, ulipata kwamba petroli yenye risasi ndiyo iliyokuwa chanzo cha michanganyo yenye risasi nyingi katika vikundi fulani vya divai za Kifaransa. Iwapo mashamba ya mizabibu yalikulia kando ya njia kuu zenye kupitiwa-pitiwa na magari mengi, risasi iliyotoka katika vibomba vya moshi wa gari iliingia katika zile zabibu. Kiasi cha michanganyo-risasi ya kikaboni katika divai hizo kilikuwa juu kuanzia mara 10 hadi 100 kuliko kile kilichopatikana katika maji ya kunywa. Richard Lobinski, wa Chuo Kikuu cha Antwerp katika Ubelgiji, apendekeza kuepuka vikundi vya divai zile tu za kati ya miaka ya 1975 na 1980, kwa kuwa utumizi wa petroli yenye risasi katika Ufaransa ulipungua katika miaka ya mwishoni mwa 1970. Hata hivyo, yeye asema pia kwamba petroli yenye risasi ingali ikitumiwa, hasa katika Ulaya ya Kati na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Adai kwamba michanganyo-kaboni yenye risasi ni hatari kuliko risasi ya kawaida kwa sababu ‘yaweza kufyonzwa kwa urahisi, hasa na ubongo.’
Watoto Katika Kisiwa Bila Televisheni
St. Helena, kisiwa kidogo kilicho karibu theluthi moja ya mwendo wa kutoka Afrika Magharibi hadi Amerika Kusini, chajisifia kuwa na watoto walio “miongoni mwa waliosawazika vema zaidi ulimwenguni,” lasema The Times la London, likitaja ripoti moja katika Support for Learning, jarida maarufu la kielimu. Mwandishi wa ripoti hiyo, Dakt. Tony Charlton, alipata kwamba ni asilimia 3.4 tu ya watoto wa kisiwa hicho walio na miaka kati ya 9 na 12 wenye matatizo mazito ya kitabia. The Times lasema kwamba kiasi hiki ndicho “cha chini zaidi kilichopata kutiwa katika kumbukumbu kwa umri wowote mahali popote ulimwenguni.” Ni nini sababu ya kuwako kwa watoto hao waliosawazika vema? Uwezekano mmoja ni ubora wa juu na kupatikana vyepesi kwa elimu ya watoto hao. Lakini Charlton apanga kuchunguza jambo jingine liwezekanalo kuwa kisababishi. Mpaka majuzi, wakati kiungo cha satelaiti kilipoanzishwa, kisiwa hicho hakikuwa kimepata kamwe kuwa na televisheni iliyotangazwa hewani. Yatarajiwa kwamba katika muda wa miaka mitatu, nyumba 1,300 kati ya zile 1,500 za kisiwa hicho zitakuwa na televisheni. Karibuni Charlton ataanza kuchunguza mabadiliko yoyote yatakayotokea baada ya hapo katika watoto wa kisiwa hicho.
Kutoruzuku Watoto, Kutopata Leseni
Jimbo la Maine, Marekani, limechukua msimamo thabiti kuhusu wazazi wakataao kulipa riziki ya watoto iliyoagizwa na mahakama. Imeondoa uhalali wa leseni za udereva za mababa wanane wasiotii kwa njia hiyo. Kulingana na The New York Times, Jane Sheehan, kamishna wa Huduma za Kibinadamu za Maine, asema kwamba mababa wanane hao walikuwa na deni la jumla ya dola 150,000 na kila mmoja wao alikuwa amepokea onyo la kutosha kwamba alikuwa katika hatari ya kupoteza leseni yake. “Hili halipasi kushangaza mtu yeyote,” Times lamnukuu akisema hivyo. “Sisi tumekuwa tukiwaonya watu tangu Agosti uliopita kwamba siku hii ingefika.” Ofisi yake imewapelekea maonyo kama hayo wazazi 17,400 ambao wamechelewa kwa zaidi ya siku 90 kutoa malipo ya kuruzuku watoto. Kufikia sasa, malipo ya kama dola milioni 11.5 yameingia kama tokeo.
Wakulima Werevu, Kunguru Wajanja
Katika Japani, kuna ushindani unaoendelea juu ya nani avune mazao ya kilimo. Kunguru na wakulima wanapambana daima, huku kunguru hao waliojanjaruka wakizigundua upesi mbinu zivumbuliwazo na wakulima. Ingawa hivyo, sasa wakulima wenye maarifa katika Wilaya ya Nagano wanatumia silika zilizo mbaya zaidi za ndege hao ili kuwatega, lasema Asahi Evening News. Walisimamisha kizimba cha meta tisa za mraba chenye kimo cha meta tatu karibu na mazao yao na kuingiza humo kunguru wa kutoka eneo jingine. Kunguru wenyeji wenye pupa, kwa kukasirishwa sana na wavamizi hawa wa eneo lao, huruka kuingia katika kizimba hicho kuwashambulia kunguru hao “wa kigeni,” kumbe wananaswa wao wenyewe. Je, ni mafanikio hatimaye? Mmoja wa wakulima hao asema: “Kwa kweli, kunguru walio wengi wapumbazwao na kizimba hicho ni wale wazururaji. Wale walio wenyeji ni werevu sana hivi kwamba sasa watupumbaza sisi na kurukia mbali.” Hivyo basi ushindani waendelea.
Zaidi ya Wavutaji Sigareti Bilioni Moja
Kulingana na tarakimu za majuzi kutoka WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), idadi ya watu wavutao sigareti ulimwenguni pote ni bilioni 1.1. Elekeo la sasa likiendelea, laonya WHO, “karibu nusu ya watu bilioni moja walio hai sasa watauawa na tumbaku, na karibu nusu ya hao, watu milioni 250, watakufa wakiwa na umri wa makamo.” Tangu miaka ya 1980, uvutaji wa sigareti umepungua kidogo katika mataifa yenye viwanda, lakini kumekuwa na ongezeko katika nchi zinazositawi. Hivyo, uvutaji wa ulimwengu wabaki kwenye sigareti 1,650 kwa kila mtu mzima kwa mwaka. Asema hivi Hans Emblad, mkurugenzi wa Programu ya WHO Kuhusu Utumizi Mbaya wa Dutu: “Kufikia sasa, tokeo halisi la mafanikio ya kuuza tumbaku katika nchi zinazositawi limekuwa ni kuhamisha maeneo ya utumizi ulioongezeka wa tumbaku yatoke nchi zilizositawi yawe katika nchi zinazositawi. Ule utumizi mwingi wa tumbaku haujaweza bado kudhibitiwa duniani pote.”
Vizuizi vya Usemi Visivyo na Madhara
Kwenye kongamano moja katika Darmstadt, Ujerumani, washirika wa Shirika la Uzoezano wa Tiba ya Kigugumizi walionya wazazi dhidi ya kuhangaishwa mno na vizuizi vya usemi visivyo na madhara vya watoto wao wachanga. “Wanne kati ya kila watoto watano walio kati ya umri wa miaka minne na sita wana vizuizi vidogo vya usemi visikikavyo kama kugugumiza maneno lakini ambavyo kwa kawaida hujimaliza vyenyewe,” laripoti gazeti Süddeutsche Zeitung. Wazazi wapaswa kuitikiaje wakati mtoto mchanga ajikwaapo kusema maneno? “Ili kutomnyima mtoto uhuru wake wa kiasili wa kutozuiliwa usemi,” laeleza gazeti hilo, “wazazi wapaswa waepuke kumsonga mtoto afanye vema, wapaswa kumruhusu wakati mwingi, na wapaswa kuijenga hali yake ya kujitumaini.”