Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 11/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Onyo Dhidi ya Upofu
  • Makelele ya Mjini Dhidi ya Ndoto za Kufurahisha
  • Je, Usifu Akili au Jitihada?
  • Mchomaji Makusudi wa Angani
  • Ni Hatari Kuwa na Silaha
  • “Barabara Kuu ya Kasa”
  • Watoto Walio Askari-Jeshi Waongezeka
  • Wazee Wanatumia Internet
  • UKIMWI—“Maradhi ya Kuambukiza Yanayoua Watu Wengi Zaidi”
  • Akina Mama Wenye Mkazo—Watoto Wenye Mkazo
  • Glakoma Ugonjwa Unaosababisha Upofu
    Amkeni!—2004
  • UKIMWI—Matokeo Yenye Msiba Mkubwa kwa Watoto
    Amkeni!—1992
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • UKIMWI—Je! Nimo Hatarini?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 11/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Onyo Dhidi ya Upofu

“Zaidi ya Wakanada 200,000 wana ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na ni nusu tu kati yao wanaofahamu jambo hilo,” lasema gazeti The Prince George Citizen. Ukiwa ndio kisababishi kikuu cha upofu, ugonjwa unaotanua mboni ya jicho huua chembe za neva zilizo sehemu ya nyuma ya jicho pole kwa pole. Tokeo huwa kwamba mtu hukosa kuona hatua kwa hatua kwenye pembezoni mwa jicho, huku akiweza kuona kwa sehemu ya kati ya jicho hadi hatua za mwisho za maradhi hayo. Wengi walio na maradhi hayo hawatafuti matibabu kwa sababu hawahisi maumivu yoyote na bado wanaweza kuendesha gari, kusoma, na kufanya kazi nyingi. Kulingana na shirika la Glaucoma Research Society of Canada, wale wanaokabili hatari kubwa zaidi wanatia ndani wazee-wazee, ambao washiriki wa familia yao waliwahi kupatwa na maradhi hayo, watu weusi wenye umri unaozidi miaka 40, na watu ambao wana msongo mkubwa ndani ya jicho. “Ikiwa tunaweza kuwafanya wanaokabili hatari kubwa zaidi wamwone daktari, hiyo itakuwa hatua ya maana sana ya kuzuia upofu unaosababishwa na maradhi yanayotanua mboni ya jicho,” akasema Dakt. Neeru Gupta, mkurugenzi wa chumba cha ugonjwa unaotanua mboni ya jicho katika Hospitali ya St. Michael, huko Toronto. “Jambo muhimu ni kwamba ugonjwa huo unapogunduliwa mapema na kutibiwa, mtu aweza kuepuka upofu.”

Makelele ya Mjini Dhidi ya Ndoto za Kufurahisha

Wakati wa mchana, zaidi ya Waitalia milioni 40—takriban asilimia 72 ya idadi ya watu—wanakabili kelele nyingi sana, kulingana na Wizara ya Mazingira ya Italia. Miongoni mwa madhara yanayoweza kutokea kwa kukabili kelele kwa muda mrefu ni kuongezeka kwa mpigo wa moyo, mabadiliko katika msongo wa ateri na uwezo wa kupumua, uvimbe wa tumbo, na kichefuchefu, laripoti Corriere della Sera. Katika majiji makubwa kelele za magari huvuruga usingizi wa kawaida. Kelele za usiku mjini zaweza kuzidi vizio 70 vya kiwango cha sauti, jambo ambalo huzidisha hatari ya kupunguza usingizi mzito na ndoto. Mkurugenzi wa sayansi wa shirika la kimazingira la Italia Legambiente, Lucia Venturi asema: ‘Inakadiriwa kwamba watu milioni 18 wanaoishi katika miji mikubwa hupoteza usingizi kwa muda wa dakika 30 kila usiku. Hizo hujumlika kuwa siku 22 bila usingizi kwa kila mtu kila mwaka.’

Je, Usifu Akili au Jitihada?

Wazazi wengi wanaamini kwamba ni jambo zuri kusifu akili ya watoto. Hata hivyo, utafiti mpya waonyesha kwamba sifa za namna hiyo kwa kweli zaweza kudhoofisha kichocheo chao na utendaji wao wa wakati ujao, laripoti Columbia Magazine, la Chuo Kikuu cha Columbia huko New York. Kulingana na Profesa Carol Dweck, ni afadhali zaidi kusifu watoto kwa ajili ya kazi yao yenye bidii, jambo ambalo huimarisha uwezo wao wa kukabiliana na magumu ya maisha. “Watoto wanaosifiwa kwa sababu ya akili yao wanahangaikia zaidi jinsi wanavyoonekana kuwa wenye akili na mara nyingi watapoteza fursa ya kujifunza jambo fulani la maana ili watambuliwe,” asema Dweck. Kwa upande mwingine, ripoti hiyo ilisema kwamba wale waliosifiwa kwa jitihada yao na uvumilivu wao wanaelekea zaidi kukazia fikira kujifunza na kukabili hali ya kutofaulu. “Kwa hiyo watoto hao watakosa fursa ya kuonekana kuwa wenye akili kusudi wajifunze,” asema Dweck. “Na hawavunjiki moyo wala kuhisi wamekataliwa wanapokosa kufaulu.”

Mchomaji Makusudi wa Angani

Kunguru-mdogo wanatuhumiwa kuwa walianzisha mioto miwili huko Kamaishi, Japani. Katika kisa cha kwanza, wazima-moto walioenda kuzima moto wa nyasi karibu na eneo la makaburi walipata uthibitisho wa kuhusika kwa kunguru-mdogo. Gazeti Nihon Keizai Shimbun laeleza: “Kunguru-mdogo hao waliokota keki zilizokuwa zimewekwa kaburini, na mara moja baada ya hapo, moto ulianza upande walikoelekea. Baadhi ya vijiti vya kufukizia uvumba, vilivyokuwa vimeachwa vikiteketea, havikuwako pia, na mishumaa, ambayo yaelekea iliangushwa na kunguru-mdogo, ilipatikana mahali kulipozuka moto.” Mwaka mmoja baada ya hapo, liliripoti gazeti Daily Yomiuri, moto ulizuka upande wa mlima katika eneo hilohilo. Katika eneo hilo, mzima-moto mmoja aliona kunguru-mdogo akibeba mdomoni kadibodi iliyokuwa ikiwaka na kuiangusha kwenye mto uliokuwa karibu. Wazima-moto walipata sanduku jingine lililokuwa limechomeka karibu na mahali moto huo ulipoanzia. Wakati huu, kunguru-mdogo walikuwa wamepata wapi mienge yao? Ilitukia kwamba mkazi mmoja wa karibu alikuwa akichoma makatoni matupu ya viazi kwenye jiko la makaa.

Ni Hatari Kuwa na Silaha

“Watu wenye magari wanaotekwa nyara na ambao hubeba bunduki huelekea kupigwa risasi mara nne kuliko wale wasiobeba,” lasema gazeti la Afrika Kusini The Natal Witness. Ripoti hiyo yaongezea kwamba “watu wenye silaha walielekea kuibiwa silaha zao mara nne zaidi ya walivyoweza kuzitumia.” Uchunguzi wa muhtasari wa kituo cha polisi ulionyesha kwamba washambuliaji waliwapiga risasi wahasiriwa katika visa 12 vya utekaji nyara. Hata hivyo, tarakimu hiyo iliongezeka na kufikia asilimia 73 wakati makafara walipotoa silaha ili kujilinda. Mtafiti Antony Altbeker alimalizia: “Ingawa huenda ukahisi kuwa salama zaidi unapokuwa na bunduki, hiyo haitokezi usalama halisi.”

“Barabara Kuu ya Kasa”

Mnamo Desemba kila mwaka, kasa 10,000 wa rangi ya kijani kibichi hurudi kwenye kisiwa kidogo cha Ascension Island kwenye Bahari ya Atlantiki ili kuzaana. Wakitumia setilaiti ili kufuatilia njia hiyo, wanasayansi Waingereza na Waitalia hivi karibuni wamegundua “barabara kuu ya kasa” kati ya kisiwa hicho na malisho ya wanyama hao kandokando ya jiji la pwani la Brazili, Recife, lasema The Times la London. Mwishoni mwa msimu wao wa miezi saba ya kuatamia, kasa wote hufuata njia ileile na kurudi hadi Brazili kwa kilometa 300 za kwanza. Kisha wanaacha njia hiyo kidogo na kuelekea kwenye malisho yaliyo sehemu tofauti-tofauti. Lakini vipi juu ya makinda, ambayo hayana nguvu za kutosha kuogelea mwendo wa kilometa 2,000 kurudi Brazili? Hao huelea kwenye mkondo wa bahari kotekote katika Atlantiki na Karibea, huku wakila yavuyavu na planktoni. Inadhaniwa kwamba baada ya miaka mitano au sita, kila mmoja hurudi kivyake hadi malishoni huko Brazili. Kisha, wanapofikisha miaka 20 hivi, wanajiunga na kundi kubwa mno linalohama na kurudi Ascension Island ili kuzaana.

Watoto Walio Askari-Jeshi Waongezeka

“Idadi ya watoto wanaotumiwa vitani imeongezeka kutoka kadirio lipatalo 250,000 miaka miwili hadi mitatu iliyopita kufikia 300,000 leo,” charipoti kichapo Go Between cha Shirika la Umoja wa Mataifa Lisilo la Kiserikali la Huduma za Upatanisho. Watoto ambao ni askari-jeshi—wengine wakiwa na umri wa miaka minane—kwa sasa wanahusika katika mapambano zaidi ya 30 ulimwenguni pote. Kulingana na Olara Otunnu, Mwakilishi wa Pekee wa katibu mkuu wa UM wa Watoto na Mapambano ya Kijeshi, “watoto wamelazimishwa kuwa vifaa vya vita, wanaandikishwa au kutekwa ili wawe askari-jeshi, hivyo wakilazimishwa watende kijeuri kama watu wazima wenye chuki.” Ili kuzuia ongezeko la idadi ya watoto wanaoingizwa jeshini, shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Watoto linaunga mkono pendekezo “litakaloongeza kiwango cha umri wa kuandikishwa jeshini kuwa miaka 18 na kusihi kwamba mtu anapoandikishwa jeshini akiwa na umri unaopungua miaka hiyo kuonwe kuwa kuhalifu sheria ya vita,” chasema kichapo Facts & Figures 1998.

Wazee Wanatumia Internet

“Uchunguzi mpya zaidi wa demografia katika Internet wadokeza kwamba wazee [umri wa miaka 50 na zaidi] wanatumia Internet kwa wingi zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali,” aripoti mwandishi wa habari Maria Seminerio wa shirika la ZDNet. Kulingana na Tim Cobb, msimamizi wa shirika lililofanya uchunguzi huo, “huo ni uthibitisho kwamba Internet inazidi kuwa na washiriki wengi na si uwanja tu wa watu walioerevuka kitekinolojia tena.” Kwa mfano, angalau asilimia 40 ya watu wazima wenye umri unaozidi miaka 50 huko Marekani sasa wana kompyuta nyumbani mwao, na asilimia 70 kati yao wanaripotiwa kuwa wanatumia Internet.

UKIMWI—“Maradhi ya Kuambukiza Yanayoua Watu Wengi Zaidi”

“Sasa UKIMWI ndio maradhi ya kuambukiza [pekee] yanayoua watu wengi zaidi ulimwenguni,” asema Peter Piot, mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la UKIMWI. Gazeti Science laripoti kwamba mnamo 1997, UKIMWI ulikuwa namba saba kati ya maradhi yanayoua watu wengi zaidi ulimwenguni. Lakini katika mwaka wa 1998 ulishinda maradhi mengine yote isipokuwa maradhi ya moyo ya ischemic, maradhi yanayohusisha mishipa ya damu ya ubongo-mbele, na maradhi ya kupumua, ambayo si maradhi ya kuambukia. Pia UKIMWI ulikuwa namba moja kwa kuua watu katika Afrika, ukishinda hata maradhi yasiyo ya kuambukia. Katika Afrika peke yake, UKIMWI uliua takriban watu 1,830,000 mwaka jana—mara mbili zaidi ya waliokufa kutokana na malaria, ugonjwa ambao ndio namba mbili kwa kuua watu katika bara hilo.

Akina Mama Wenye Mkazo—Watoto Wenye Mkazo

Mama mjamzito anapoishi akiwa na mkazo wa daima, huenda ukuzi wa mtoto wake ambaye hajazaliwa ukaathiriwa sana, laripoti gazeti National Post la Kanada. Kulingana na Pathik Wadhwa, wa Chuo Kikuu cha Kentucky College of Medicine, huko Lexington, Kentucky, mazingira ya tumbo la uzazi “huathiri ukuzi wa mtoto, na mkazo mwingi kwa upande wa mama waweza kuwafanya watoto wakabili hatari kubwa ya mapema ya kupatwa na maradhi.” Akina mama wenye mkazo pia “waelekea zaidi kuzaa watoto kabla ya wakati,” yasema ripoti hiyo. Watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Clemson, South Carolina, wanadokeza kwamba “mazoezi ya kustarehesha yanaweza kusaidia wanawake wajawazito walio na mkazo wapunguze msongo wao wa damu, na kuandaa mazingira yenye afya zaidi ndani ya tumbo la uzazi.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki