Watoto Waliopotea—Ni Msiba Ulioenea Kadiri Gani?
‘MTOTO WANGU AMEPOTEA!’
Ni mambo machache ambayo yangeweza kusababishia wazazi walio wengi hangaiko kama kulazimika kutamka maneno hayo. Ingawa hakuna tarakimu hususa ulimwenguni inayoweza kuwekwa kuhusu idadi ya watoto waliopotea kutoka nyumbani kwao, twaweza kusoma msiba huu ulivyoenea kupitia ripoti zilizochapishwa katika mabara mengi.
KATIKA Marekani, kutoka watoto 500,000 hadi zaidi ya 1,000,000, ikitegemea jinsi wanavyobainishwa, kila mwaka wameorodheshwa kuwa waliopotea kutoka nyumbani kwao. Huenda wakawa wamepotea kwa pindi fupi ya wakati ama wakapotea daima. Uingereza huripoti kwamba karibu watoto 100,000 hutoweka kila mwaka, ingawa wengine husema idadi yao ni kubwa zaidi. Ule uliokuwa Muungano wa Sovieti ulisema kuwa makumi ya maelfu ya watoto walipotea huko. Katika Afrika Kusini idadi hiyo inasemwa kuwa zaidi ya 10,000. Na katika Amerika ya Latini, mamilioni ya watoto hukabili msiba huu.
Msemaji fulani wa Wizara ya Italia ya Mambo ya Ndani alionyesha kiwango cha tatizo hilo huko alipoandika katika L’Indipendente hivi: “Wao huondoka nyumbani kila siku kama siku nyingineyo yote. Wao huenda shuleni au kucheza, lakini hawarudi. Hutoweka, hutokomea kana kwamba hawakuwepo. Washiriki wa familia huwatafuta bila tumaini, lakini kunakuwa na dalili hafifu, fununu zisizotosha—na washuhudiaji wachache—tena wasio na hakika.”
Uchunguzi fulani wa majuzi katika Marekani kuhusu kiwango cha tatizo hili ulifunua kwamba kile kichwa “watoto waliopotea,” kwa uhalisi hutia ndani aina kadhaa. Aina moja ni watoto watekwa-nyara na watu wasiojulikana. Nyingine ni watoto waliotekwa nyara na mzazi, kama vile katika kesi ya ni nani mwenye haki ya kutunza mtoto. Kisha wale waliotupwa, watoto wasiotakiwa na wazazi au watunzaji. Pia kuna watorokaji, aina nyingine kubwa. Na kuna wale waliopotea njia au waliotegwa kutoka kwa familia yao kwa saa chache tu au kwa siku moja au mbili—walio wengi wakiwa watoto waliopitisha wakati uliokubaliwa au watoto ambao wazazi walikosa kuelewa madhumuni yao. Wachache mno wa hawa hupotea daima.
Hata hivyo, ni nini hutokea kwa watoto waliopotea katika aina zilizo mbaya zaidi? Kwa nini msiba huu watokea? Toleo hili la Amkeni! lachunguza sehemu mbalimbali za msiba huo na lajibu lile swali, Utakwisha lini?