Furahia Kukimbia-Kimbia—Lakini Chunga Hatari!
MVULANA mwenye umri wa miaka 18 alihitaji “miendo ya umbali zaidi na zaidi ili kuridhisha tamaa yake ya kukimbia,” laripoti gazeti la Kijerumani Süddeutsche Zeitung. Saa 8:00 usiku na tena saa 12:00 asubuhi, angekimbia “kilometa 24 kabla ya kurudi kulala, akiwa ametulia na kuridhika.” Hiki si kisa cha pekee, kwani wanasayansi watafiti katika mabara mengi wakati huu wanashughulika na wanaokimbia-kimbia walio waraibu wa endorphin. Uraibu kama huo waweza kusitawije?
Watafiti wamevumbua kwamba kujikakamua kwa kuendelea na kwenye kujisulubu kimwili, endorphin hufanyizwa katika neva za misuli. Endorphin hutokezwa (hutokana na) opiates ambavyo hutokeza hisia nzuri ajabu—nyakati nyingine ukiandaa usisimukaji kwa washupavu wa kukimbia-kimbia. Adai Wildor Hollmann, msimamizi wa shirika la kimataifa la kuchunguza dawa ya michezo: “Kama mofini hizi zaweza kuongoza katika uraibu au la kwa muda mrefu kimekuwa kibishanio fulani. Sasa ni uhakika uliothibitishwa.” Hivyo basi, inaonekana kuwa hatari kukimbia au kukimbia-kimbia kwa miendo mirefu na, bila shaka, katika kufanya utendaji wowote ule uhusishao kujikakamua kupita kiasi.
Je, huenda kukawa na madhara mengine ya kiafya yashirikishwayo na utendaji wa hali ya juu wa kimichezo? Ndiyo. Huenda ukakumbuka hadithi ya mjumbe Mgiriki aliyekimbia kutoka Marathon hadi Athene karibu miaka 2,500 iliyopita. Kulingana na hadithi hiyo, alianguka kwa kupoteza fahamu na kufa papo hapo baada ya kufikisha habari Athene za ushindi wa Ugiriki dhidi ya Waajemi. Watafiti huona katika hadithi hiyo kielelezo cha endorphins kwenye misuli. Wao wasema kwamba vipindi virefu vya utendaji wenye kujikakamua vyaweza kuongoza kwenye kifo kutokana na kusimama kwa muda kwa mpingo wa moyo kwani endorphins hupunguza kuhisi maumivu. Kwa kielelezo, chini ya hali za kawaida maumivu makali ya kifua hufanya mkimbiaji aache kukimbia, ambayo kulingana na wastadi, katika visa vilivyo vingi huruhusu moyo udumishe tena mdundo wake wa kawaida. Lakini wakati wa kujikakamua kabisa kimwili, endorphins hupunguza kuhisi maumivu, ikifanya viashirio vipitishwavyo na mwili kutohisiwa na mkimbiaji. Hilo laweza kuwa na matokeo yenye kudhuru.
Kwa upande mwingine, mazoezi ya kimwili yenye usawaziko ni yenye kujenga, na endorphins inayotoka kwenye nyakati kama hizo huonekana kuwa na matokeo chanya. Mwanamke mmoja ambaye kwa ukawaida hukimbia-kimbia aeleza hivi: “Mbeleni nilitumia dawa, bali sasa ninapokuwa katika hali ya tabia-moyo mbaya, mimi hukimbia.” Kutembea haraka au kukimbia kwa kweli huenda kukasaidia kuondoa au angalau kukabiliana na kushuka moyo. Endorphins yaonekana huchangia vizuri katika visa kama hivyo. Mazoezi ya kimwili huwa hatari tu yafanywapo kupita kiasi.—Linganisha 1 Timotheo 4:8.