Matreshka—Ni Mwanasesere Alioje!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA URUSI
MARA watalii wazuruo wanaponiona, wengi wao huonekana kuazimia kunichukua nyumbani kwao, wakiwa tayari kutumia fedha nyingi ili kufanya hivyo. Hakika sijui ni nini huwavutia kwangu. Vyovyote vile, wanajua machache mno kunihusu. Pengine ni jambo walifanyalo kwa kufuatisha mtindo. Lakini acha nijitambulishe. Jina langu ni Matreshka, nami natoka—lakini acha tuanze mwanzo.
Hakika, hakuna mtu anayejua nilitoka wapi ama wazazi wangu hasa walikuwa akina nani. Hadithi yenyewe ina fasiri mbili. Wengine hudai kwamba nilitoka kwenye kisiwa cha Honshu cha Japani nikiwa kichezeo kilichokuwa na sehemu kadhaa zilizohusiana. Wanasema kwamba nililetwa Urusi kutoka Honshu mwishoni mwa karne ya 19 na mke wa kabaila fulani Mrusi aliyeitwa Savva I. Mamontov (1841-1918). Kwa upande ule mwingine, kulingana na Mjapani fulani, alikuwa ni mtawa wa kiume fulani Mrusi aliyeleta mara ya kwanza wazo la kunitengeneza kuwa mwanasesere asiye na kifani. Lakini viwavyo vyote, wahunzi wa Kirusi walipendezwa na wazo hilo, naye Matreshka akatokea.
Mwishoni mwa miaka ya 1880, Urusi ilikuwa ikisitawisha uchumi na utamaduni wayo. Wakati uleule, Warusi walipendezwa sana katika kuhifadhi mapokeo yao waliyoyapenda. Wakiwa na nia ya kuhuisha utamaduni wa Warusi, wasanii mahiri Warusi walianza kukutana katika Mamontov, kutia ndani wapaka rangi mashuhuri kama vile Ilya Repin, Viktor Vasnetsov, na Mikhail Vrubel. Ili kuhifadhi kumbukumbu la ukulima wa Warusi, chumba cha sanaa kilijengwa karibu na Moscow. Huko, bidhaa za kikale, vichezeo, na wanasesere walikusanywa kutoka sehemu zote nchini.
Mwanasanaa mtaalamu aliyeitwa Sergei Maltyutin alifanya michoro ya kwanza yangu, lakini nilionekana tofauti kidogo wakati huo. Nilinuiwa kuonyesha msichana wa mkulima mwenye uso wa mviringo na macho mangavu. Nilivaa sarafan (vazi lisilo na mikono lililoshikiliwa na mishipi miwili), na nilikuwa na nywele zilizolainishwa vizuri, nyororo na zimetazo zilizofichika chini ya kitambaa chenye urangi. Wanasesere wengine, wadogo kuliko wale wa awali, waliwekwa ndani yangu. Walivaa kosovorotkas (blausi za Kirusi zenye kola iliyofungiwa upande mmoja), shati, poddyovkas (makoti ya wanaume yenye kiuno kirefu), na aproni. Kama ilivyofunuliwa na michoro ya Malyutin, hivyo ndivyo nilivyoonekana wakati nilipotengenezwa katika Moscow karibu 1891.
Mara nyingi mimi hushangaa kuhusu jina langu. Nilijua kwamba kwenye mwisho wa karne ya 19, Matrena (udogo wake ni Matreshka) lilikuwa mojapo la majina mashuhuri ya wanawake katika Urusi. Likiwa limetokana na shina la Kilatini matrona, lamaanisha “mama,” “mwanamke aliyestahiwa” ama “mama wa familia.” Kuweka mwanasesere mmoja ndani ya mwingine pia ilikuwa ishara ya uzazi na ubuni.
Si Rahisi Kunifanyiza
Katika jaribio la kunifanyiza, watu wamejulikana kutumia vifaa vingi na hatimaye kuacha kwa kushindwa. Si ajabu, kwani mpaka majuzi, kujua jinsi ya kunifanyiza kulikuwa siri. Hivyo ni wachache waliweza kunihodhi. Lakini sasa nitashiriki nawe siri hiyo.
Kazi inayohusika katika kunifanyiza huhitaji ustadi kwelikweli. Kwanza, ni muhimu kuchagua aina inayofaa ya mti. Kwa sababu ya ulaini wawo, kwa ujumla limewood huchaguliwa, mara chache sana alder ama birch. Baada ya miti kukatwa, kwa kawaida mapema katika masika, huondolewa maganda yake, kwa kuacha yanayotosha tu ili kuzuia mti usiatuke unapokauka. Kisha magogo huachwa yakiwa yamewekwa kwa miaka kadhaa ili kwamba yaweze kufurahia mzunguko ufaao wa hewa yakaukapo.
Kukatwa kwa miti hiyo huhitaji kufanywa kwa wakati ufaao, wakati haijakauka sana wala kuwa na unyevu mwingi. Ni stadi tu anayeweza kuamua wakati unaofaa. Kila kipande cha mti hupitia mifululizo ya utendaji mwingi kufikia 15. Mwanasesere aliye mdogo kwenye mfululizo—mmoja asiyeweza kugawanyika tena—anatengenezwa kwanza. Nyakati nyingine ni mdogo mno hivi kwamba ni lazima ukaze macho yako ama hata kutumia lenzi kuzi ili kumwona vizuri.
Mara mwanasesere mdogo anapokuwa ametengenezwa, mhunzi huanza mwanasesere wa pili ambaye ndani yake mwanasesere wa kwanza atatoshea. Kipande cha mti hutengenezwa vizuri kwa kimo kinachohitajika na kinakatwa sehemu ya juu na chini. Sehemu ya chini ya mwanasesere hutengenezwa kwanza. Kisha kibao huondolewa kutoka sehemu zote mbili za ndani za mwanasesere wa pili ili kwamba mwanasesere mdogo zaidi aingie vizuri ndani. Mhunzi stadi, kwa kushangaza, huwa hashughuliki kuchukua vipimo bali hutegemea tu uzoefu. Baadaye, yeye hurudia taratibu hiyo, kwa kutengeneza mwanasesere aliye mkubwa kidogo ambaye ndani yake wale wawili wa awali watatoshea.
Idadi ya wanasesere wanaokuwa ndani ya mmoja hutofautiana kutoka 2 hadi 60. Mwanasesere aliye mkubwa huenda awe mrefu kama mtu! Wakati kila mwanasesere anapokamilika, anafunikwa kwa gundi ya uwanga ambayo hujaza mwanya wowote kwenye umbo la nje. Kukausha kwa mwisho kunaanza, na mwanasesere anasuguliwa ili kulainisha umbo la nje kumwezesha mpaka rangi atandaze rangi kwa uwiano. Kisha mwanasesere anapata ubora usio na kifani.
Wakati Umetokeza Mabadiliko
Watu hubadilika kadiri wanavyokuwa wazee zaidi, na hilo laweza kusemwa kunihusu. Uhunzi wa kutengeneza Matreshka ulienea polepole kutoka Moscow hadi majiji na miji mingine, kutia ndani Semenov, Polkhovskii Maidan, Vyatka, and Tver.a Kila eneo lilisitawisha mtindo na njia yalo ya kurembesha. Kupoteza utambulisho wangu wa kweli kulikuwa kwenye kuvuruga, lakini mimi sikulalamika. Wakati wa sherehe ya kuadhimisha Vita ya 1812, mtu fulani aliagiza jozi ya wanasesere itengenezwe wakiwakilisha jenerali wa Kirusi Mikhail Kutuzov na jenerali wa Kifaransa Napoléon Bonaparte. Jenerali hawa wawili walikuwa ndio wanasesere wawili waliokuwa wakubwa zaidi na jenerali waliohusika kwenye nyanja za vita walitengenezwa wakiwa wadogo ili kutoshea ndani ya makamanda wao.
Kwa muda mrefu, ufanyizaji na uuzaji wa aina hii ya wanasesere ulidhibitiwa kabisa. Lakini mabadiliko ya kisiasa mwishoni mwa miaka ya 1980 yaliwapa wasanii uwezekano na uhuru mpya. Sasa wangeweza kutengeneza na kuuza bidhaa zao bila hofu.
Mpaka-rangi kwa jina Sikorskii alikuwa mmoja wa wale wa kwanza ambaye wanasesere wake walikuwa maarufu kwa umma. Wanasesere wake huhitaji bei ya juu, jozi moja ikigharimu dola nyingi kufikia 3,000. Mafanikio yake yalihamasisha wasanii wengine, na wakati wa miaka sita iliyopita, utengenezaji wa Matreshka umepata kichocheo fulani.
Jina langu, Matreshka, sasa limekuja kutumika kwa wanasesere wote wanaofanyizwa ili mmoja aingie ndani ya mwingine. Mada tofauti tofauti zinatokezwa: maua, makanisa, sanamu takatifu, hadithi za kale, mada za familia, hata viongozi wa kidini na kisiasa. Unamna mwingi unaopatikana sasa husaidia niwe na bei nafuu.
Nikiwa nimesimama kama kawaida katika duka la mauzo wakati wa kiangazi cha 1993 katika Moscow, mara nilisikia sauti ya kikundi fulani cha watalii wa kigeni waliokuwa wakija. Niliwasikia kwa mbali wakisema jambo fulani kuhusu mkusanyiko wa Mashahidi wa Yehova waliokuwa wakihudhuria na kwamba kila mmoja wao, kama kumbukumbu la tukio hilo la ajabu, alitaka kunipeleka nyumbani. Nikishangaa kwa nini, niliwatazama na macho mangavu. Kana kwamba anajibu, mmoja wao alisema: “Ni zaidi ya ukumbusho. Nataka marafiki wangu wakaone macho yake. Mimi huona ndani yao misemo ileile niliyoiona kwenye macho ya Warusi niliozungumza nao kuhusu Ufalme na jina la Mungu kama lipatikanavyo katika Biblia.”
Mashahidi wa Yehova? Ufalme? Jina la Mungu? Biblia? Macho yangu yakawa manene kadiri niliposikiliza, na moyo wangu ulipiga kwa kasi kidogo kwa sababu ya matazamio ya kupelekwa hadi maeneo ya mbali na baadhi ya watu hawa walioonekana wakiwa wenye kupendeza. Labda ningeweza kujifunza zaidi kuhusu sababu ya msingi ya wao kuzuru Urusi. Nina uhakika ni lazima iwe ni zaidi ya kukutana nami, mwanasesere aitwaye Matreshka.
[Maelezo ya Chini]
a Wakati wa miaka ya 1930, Vyatka ilikuja kujulikana kuwa Kirov na Tver ikawa Kalinin. Tangu kuvunjika kwa Muungano wa Sovieti, majina ya asili yamerudishwa.