Kuutazama Ulimwengu
‘Mfumo wa Mwisho Wenye Kushikilia Mamlaka Kamili’
“Kutoridhika katika Kanisa Katoliki la Ujerumani kuelekea mtazamo wa kudumisha kile kilichositawishwa na Vatikani kunaongezeka,” laripoti gazeti la Rome La Repubblica baada ya kuwekwa rasmi hivi majuzi kwa makadinali wapya 30 na John Paul 2. Mwanatheolojia asiyeridhika ajulikanaye sana Hans Küng anathibitisha kwamba ili kuchagua papa afuataye, kuna “uhitaji muhimu kwa kikundi cha wanaochagua kiwe ambacho kinawakilisha kikweli Kanisa Katoliki lote.” Küng aamini kwamba “papa kwa wazi amepoteza tumaini la sehemu kubwa ya washiriki waumini.” Küng aendelea hivi: “Haiwezi kupuuzwa kwamba, baada ya kuanguka kwa ufuatiaji wa kanuni za Stalin, mfumo wa Katoliki ya Roma ndio mfumo wa mwisho wa ukamili unaobaki katika ulimwengu wa Magharibi.”
Zuia Kuzeeka kwa Mapema
“Watu hurekebisha nyumba ili zifae watoto. Kwa nini wasizirekebishe kwa ajili ya watu waliozeeka?” auliza mtaalamu wa matatizo ya kuzeeka Wilson Jacob Filho wa Chuo Kikuu cha São Paulo. Licha ya nyumba zilizo salama zaidi kwa ajili ya wazee-wazee, yeye anadokeza kwamba wazee-wazee wafanye mazoezi ili kutia nguvu mfumo wa misuli ili kupunguza hatari ya kuanguka. Ni nini maadui wakubwa kuliko wote wa kuishi muda mrefu? Kulingana na daktari wa upasuaji wa plastiki Rogério Izar Neves, pia wa Chuo Kikuu cha São Paulo, maadui ni “njia ya maisha ya kukaa mahali pamoja, lishe isiyosawazika (hasa ulaji ulio na shahamu nyingi), uvutaji-sigareti, utumizi wa kupita kiasi wa vinywaji vya kialkoholi, mkazo, ukosefu wa usingizi.” Jornal da Tarde laeleza kwamba mkazo wa kupita kiasi hudhoofisha mfumo wa kinga, “ambao unahusiana kwa ukaribu na magonjwa mbalimbali na pia umri wa uzee.” Dakt. Neves aendelea kudai hivi: “Ukosefu wa upendezi katika maisha ndio kisababishi kikuu cha kuzeeka kwa mapema.”
Hatari ya Kiafya ya Utoboaji-Mwili
“Watu wanaacha sehemu za miili yao zitobolewe ambazo hazikutobolewa miaka kadhaa iliyopita,” asema John Pelton, mkurugenzi wa afya ya kimazingira wa Calgary Health Services katika Kanada. Kulingana na ripoti katika The Vancouver Sun, hii yatia ndani nyushi za macho, midomo, ndimi, na vitovu. Hofu kwamba mtindo huu unaozidi kukua ungeweza kupitisha UKIMWI na mchochota wa ini B na C zimefanya Utumishi wa Afya ya Kimazingira katika Alberta Health utokeze miongozo ya kudhibiti utoboaji mwili. “Viwango vipya hatimaye vitadhibiti mweneo wote wa utumishi wa kibinafsi usiozuiwa, kama vile utiaji-alama, kutolewa kwa nywele za mwilini kwa nta moto, uchanjaji-chale, kuharibu viini vya nywele kwa kutumia mkondo wa nguvu za umeme na unyimwaji wa hisi zote,” na muhtasari wa maagizo haya utapitiwa na maofisa wa afya ya umma na vikundi vya miradi ya kiutendaji, yaongeza hiyo ripoti. Kuhusu utumizi wa zana za utoboaji-sikio ili kutoboa mwili, mtu anayefanya taratibu hiyo akiri hivi: “Tumeona watu wakienda hospitali wakiwa na maambukizo. Kwa kweli inaogopesha kwelikweli.”
Dini Katika Upotezo wa Cheo
Dini kubwa kuliko zote ya Kiprotestanti ya Kanada, United Church of Canada, “ina ushirika unaozeeka na kudhoofika kwa haraka mno, na viongozi na waparishi wayo hawaafikiani juu ya vipaumbele vyao vyapaswa kuwa nini,” lasema The Toronto Star. Huku zaidi ya watu 3,000,000 wakidhania wana umoja na hilo kanisa, ni 750,000 tu walio katika orodha ya usajili ya kanisa. Wengi wa waungaji-mkono wayo bora zaidi wana umri wa zaidi ya miaka 55, ilhali watoto na wajukuu wa washiriki hawavutiwi nalo. Hilo kanisa lilionywa kwamba lazima lichukue hatua ya mara moja ya kurekebisha namna yalo ya kujiendesha au life. Washiriki wanataka kipaumbele kipewe ibada na hali ya kiroho, ilhali viongozi wa hilo kanisa wanataka kutoa uangalifu zaidi kwa masuala ya kijamii na ya kitufe. Kanisa likianguka, “itamaanisha pia kwamba kile ambacho kimekuwa cha maana kwa United Church hakijakuwa cha maana kwa Wakanada,” aonya mwanasosholojia wa Alberta Reginald Bibby. “Kile ambacho kanisa lashikilia kuwa cha maana hakijastahiki wakati, fedha au uangalifu wa Wakanada.”
Urithi wa Vita
Askari-jeshi elfu saba wenye uzoefu wa shambulio la Muungano wa Ulaya, miaka 51 iliyopita, walirudi kwenye fuo za Normandy Juni 1994. Lakini kumbukumbu zilikuwa nyingi mno kwa mamia yao ambao walilazimika kupewa msaada wa kiakili ili kukabiliana na hangaiko lililoletwa na hiyo sherehe. “Baadhi yao walikuja kusumbuka sana baada ya shambulio la majeshi yaliyoungana dhidi ya Ufaransa Juni 6, 1944,” akaeleza Dakt. Graham Lucas, akizungumza kwa niaba ya Combat Stress, shirika la kutoa msaada lisaidialo waliokuwa wanajeshi hapo mbeleni. “Walikuwa na hisia za hatia, kwamba hawakustahili kuachwa hai huku wengine wakiwa wamekufa, na walikuwa wakipata ndoto zenye kuogofya na usingizi uliokatizwa-katizwa.” Hisia hizo zilizokandamizwa kwa miaka mingi zimesababisha vidonda vya tumbo, pumu, na magonjwa ya ngozi, laripoti The Sunday Times la London. Mwanajeshi mmoja mzee, ambaye kumbukumbu zake bado humpa ndoto zenye kuogofya, alisema hivi: “Unaweza kufanya kupita kiasi miadhimisho hii. Watu ambao hawakuwa huko hawawezi kuelewa jinsi mambo yalivyokuwa.”
Samaki Mdusia
Candiru ni samaki mdusia ambaye huzaana katika mito ya majaruba ya Amazon. Kiumbe hiki chenye kupenyezeka nuru kifananacho na mkunga, chenye urefu wa sentimeta 2.5, kwa kawaida hupatikana katika mashavu ya samaki wakubwa zaidi, ambapo hujilisha kwa damu yao. Samaki huyu anaweza pia kuingia ndani ya vitundu vya binadamu na kusababisha uvimbe, kuvuja damu, na nyakati fulani kifo cha mwenye kuingiwa nayo. Hivi majuzi aina ndogo na yenye kulafua zaidi ya samaki huyu, yenye nusu ya urefu wa ile aina ya kawaida, imevumbuliwa katika Brazili. Ina meno mawili yaliyo na umbo la ndoana nyuma ya kinywa chake ambayo humpa mshiko wenye nguvu, ikifanya iwe vigumu kupukuswa. Kwa “jamii zikaazo kando ya mito, zilizo na vifaa vichache vya kitiba au bila, yaweza kuongoza kwenye maambukizo mabaya,” laripoti New Scientist.
Vyuo Vikuu Taabani
“Vyuo vikuu vya Afrika vilivyopuuzwa viko katika hatari ya kuanguka,” laripoti WeekendStar la Johannesburg. Kwa sababu ya ukosefu wa fedha, kuna kompyuta chache, na katika visa fulani simu zimekatwa. Chuo kikuu kimoja kina wanafunzi waliosajiliwa 35,000, lakini mwanzoni kilibuniwa kwa ajili ya wanafunzi 5,000 tu. Ni nusu tu ya vyeo vya uhadhiri vilivyo na watu kwenye chuo kikuu kimoja kilichokuwa mashuhuri katika Uganda. Mshahara wa mhadhiri kwenye chuo hiki kwa wazi ni dola 19 kwa mwezi. Vyuo vikuu fulani vimefungwa kwa miezi kadhaa kama tokeo la kugoma kwa wahadhiri au wanafunzi. Profesa fulani wa Kenya alitoa maelezo hivi: “Kujiangamiza kwa kielimu katika Afrika kunaendelea kuwa kubaya zaidi.”
Ni Nani Afanyaye Kazi ya Nyumbani?
“Ingeweza kuonekana kwamba usawa [kati ya wanaume na wanawake] haujaingia bado katika mazingira ya familia,” lasema Corriere della Sera, likiripoti juu ya uchunguzi wa utumizi wa wakati wa familia za Kiitalia uliofanywa na Central Statistics Institute. Awe na kazi ya nje au sivyo, bado ni mwanamke ambaye anapaswa “kuchukua mzigo wa kupanga familia,” akitoa—ikiwa ana watoto—wastani wa saa 7 na dakika 18 kwa kazi ya nyumbani, ikilinganishwa na saa 1 na dakika 48 za mwenzi wake. Jambo lisilo la kawaida ni kwamba, akina mama wasio na waume yaonekana wanafanya vema, wakipanga mambo ili waweze kutoa saa mbili chini ya zile 7 kwa kazi ya nyumbani kila siku. “Tangu miaka ya uchanga, akina mama ‘hupangia kimbele’ visichana vyao kufanya kazi ndogo-ndogo za nyumbani,” laongeza La Repubblica.
Kushindwa Lile Pigano la Kifua Kikuu
Katika vita dhidi ya maradhi, pigano dhidi ya kifua kikuu limekuwa “kushindwa kamili katika kiwango cha ulimwenguni pote,” kulingana na Profesa Jacques Grosset, msimamizi wa idara ya taaluma ya bakteria na virusi ya Hospitali ya La Pitié-Salpétrière katika Paris. Wagonjwa wasipotibiwa, kiwango cha kifo kutokana na kifua kikuu ni asilimia 50 hivi. Ingawa uyakinisho na utibabu haupatikani kwa yapata nusu ya wagonjwa wa kifua kikuu ulimwenguni pote, Profesa Grosset alitaja, msiba hasa ni kwamba katika nchi zilizositawi kitekinolojia, ambapo viuavijasumu hupatikana kwa urahisi, ni nusu tu ya wale walio na ugonjwa huo huendelea na utibabu wao hadi kupona kabisa. “Ile nusu nyingine hawatumii utibabu wao, au hawatumii kwa ukawaida, jambo ambalo husababisha kiwango cha juu zaidi cha kifo (asilimia 25 ya wale watibiwao) na pia hutokeza namna nyingine ya tubercle bacillus ambayo hukinza viuavijasumu.”
Venezuela na UKIMWI
Venezuela ni ya tatu katika kuongoza kwa visa vya UKIMWI katika Amerika ya Kilatini, baada ya Brazili na Mexico, lasema El Universal la Caracas, Venezuela. Dakt. Arellano Médici akadiria kwamba kuna watu 350,000 katika hiyo nchi ambao wameambukizwa hiyo virusi yenye kufisha, ingawaje Wizara ya Afya itakubali 3,000 tu kuwa ndio kweli. Uhakika wa kwamba kwa kila mtu aliyeambukizwa, yaelekea kuna mia moja zaidi ambao wameambukizwa lakini hawajui washirikishwa na, kulingana na Médici, “uovyo-ovyo wa kingono wenye kutokeza katika jamii yetu.” Médici ataja kwamba watu walioambukizwa wapaswa kuishi maisha yaliyo safi kiadili, si kwa sababu ya hatari ya kuambukiza wengine tu bali kwa sababu ya kuwapo kwa virusi mbalimbali vya UKIMWI. Wanaweza kwa urahisi kuambukizwa na virusi tofauti, hiyo ikifanya tatizo lao lililopo la afya kuwa baya zaidi. Chanzo kimoja hukadiria kwamba kufikia mwaka 2000, kila familia katika ulimwengu itakuwa na mshiriki aliye na UKIMWI.