Wanawake wa India—Wakisonga Kuingia Katika Karne ya 21
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
Ni warefu, ni wafupi. Ni wembamba, ni wanene. Ni wenye ucheshi, ni wenye kununa. Ni wenye utajiri mno, ni maskini hohehahe. Wameelimika sana, hawajui kusoma na kuandika kabisa. Ni nani hao? Wanawake wa India. Na wanaelekea wapi? Wanasonga kuingia katika karne ya 21.
KWA watu walio wengi wanaoishi nje ya India, sura ya mwanamke wa India ni moja ya madaha, urembo, tabia isiyoelezeka, na uvutio. Wanaume wengi hugeukia India kutafuta wake, kwa sehemu sababu ikiwa maoni ya kwamba wanawake wa India wanaelekea kuwa watiifu zaidi, kupendeza waume zao, kuwa watengeza-nyumba wema kuliko wanawake wenzao wenye roho ya kujitegemea katika nchi za Magharibi. Hata hivyo, ni jambo lenye kupotosha kufafanua mwanamke halisi wa India katika idadi hii kubwa ya hali ya malezi yenye kutofautiana ya kikabila, kidini, na kijamii. Aina zote za wanawake huishi katika bara hili lenye kuvutia.
Historia ya India ni tamaduni nyingi zilizounganishwa ama kwa amani au kwa nguvu. Kuna makisio kuhusu mahali ambako masetla wa mapema, wale Wadravidiani, walikotoka. Chanzo chao yaonekana ni kupitia mchanganyiko wa Waaustralia na watu wa kusini mwa Mediterania, kukiwa na uhusiano hususa na Krete. Waarya na Wamedi walipohamia India kutoka kaskazini-magharibi na Wamongoli kutoka kaskazini-mashariki, Wadravidiani walirudi kuelekea kusini. Kwa hiyo, kwa ujumla twapata kwamba, wanawake wa India kusini ni wenye umbo dogo zaidi na rangi ya ngozi iliyo nyeusi kidogo kuliko wanawake wa kaskazini, ambao huelekea kuwa warefu zaidi na rangi ya ngozi nyepesi lakini bado wakiwa na nywele na macho yenye rangi nyeusi. Watu katika kaskazini-mashariki mara nyingi wana maumbo ya Kimashariki.
Dini imekuwa na fungu kubwa katika kusitawisha cheo cha wanawake katika India. Kwa sababu India ya kisasa ni hali ya kilimwengu, kila jitihada yafanywa ili kubadili maoni ya kidesturi ambayo yamezuia wanawake kutofanya maendeleo. Hatua kubwa zinachukuliwa ili kuongeza fursa za kielimu, si tu kwa wanawake matajiri au wenye uvutano bali kwa wanawake wote. Madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika, mazoezi katika vijiji yaelekezwayo katika kupata kazi, na shule zisizolipiwa kwa wasichana zinaboresha heshima ya hali ya wanawake wa India.
Katika Juni 22, 1994, katika jimbo la Maharashtra, hatua kubwa ya kusonga mbele ilichukuliwa wakati sera ya serikali kuhusu wanawake ilipotolewa. Ikifafanuliwa na makamu wa rais wa India, K. R. Narayanan, kuwa “ya maana” na “ya badiliko la kimsingi,” hiyo ilielekezea fikira matatizo ya msingi ya wanawake, kama vile haki za umiliki wa kishirika, ulezi, manufaa za nyumba na fursa sawa katika kuajiriwa.
Huku wanawake wengi wakihudhuria koleji na kuingia katika kazi inayopatikana, bila kuzuiliwa nyumbani zaidi, swala la mabadiliko katika maadili limekuzwa. Ripoti zinatokea za utumizi mbaya wa dawa za kulevya na maadili yanayoshuka katika koleji. Vyombo vya habari vina fungu kubwa katika kubadilika kwa wanawake wachanga wa India. Wakilinganisha sinema za India za miaka 30 iliyopita na za leo, wengi wanapata kwamba kuonekana kwa wanawake kumebadilika kwa kiwango kikubwa. Mwanamke mmoja wa India alitoa maelezo hivi: “Shujaa wa kike wa sinema aliyekuwa mbeleni mwenye kiasi, mwanana, mwenye kujidhabihu wa wakati nilipokuwa shuleni amemwachia nafasi msichana wa kisasa ambaye, anapokasirika, anamwacha mumeye na wakweze na kupigania haki zake na uhuru wake.”
Lakini licha ya yote hayo, India kwa ujumla, ni yenye kiasi katika mwenendo na mavazi ikilinganishwa na nchi nyingi. Vazi livaliwalo kwa kawaida sana, ile sari maridadi, hufunika kwa kiasi sehemu kubwa ya mwili. Kwa wanawake wachanga, hasa katika magharibi, ile shalwar-kameez, vazi lisilokazwa livaliwalo juu ya aina ya suruali ndefu, linapendwa na wengi. Fashoni za nchi za Magharibi, zionekanazo hasa katika Bombay, Goa, na Calcutta, huwa kwa kawaida za mitindo na urefu wa kiasi.
Nafasi Mpya Katika Uajiri
Ni aina gani ya uajiri ipatikanayo kwa wanawake wa India wasongapo kuingia karne ya 21? Sehemu kubwa ya idadi ya watu wa India huishi katika vijiji, na kazi yao ni ya kilimo. Mamilioni hufanya kazi mashambani. Wanawake hufanya kazi kando-kando ya wanaume wakifanya kazi za shambani za namna zote. Wao pia hubeba maji miendo mirefu kutoka mitoni na visimani na hukusanya kwa bidii kuni kwa ajili ya moto. Wakati wa kazi, watoto hutuliwa nyongani au kulazwa katika susu zilizoning’inizwa kwenye miti.
Tangu kuingia katika karne ya 20, familia za India za mashambani zimemiminika katika maeneo ya mijini kutafuta uajiri. Wanawake wamefanya kazi katika mitambo na viwanda vya kutengeneza nguo. Hata hivyo, kufanywa kwa viwanda kuwa vya kisasa, kuliathiri wafanyakazi wanawake kuliko wanaume. Wanaume walizoezwa kuendesha mashine, lakini wanawake hawakuzoezwa. Hili lilisababisha hali ngumu sana kwa wanawake. Waliwekewa mipaka kubeba vifaa kwenye mahali pa ujenzi, kuvuta mikokoteni iliyoshehenezwa magunia mazito, wakiuza nguo zilizotumiwa, au kufanya kazi nyingine zenye mshahara wa chini.
Warekebishaji wa kijamii walifanya jitihada ya kuboresha hali ya maisha ya wanawake. Harakati kama vile SEWA (Shirika la Wanawake Waliojiajiri) lilizuka kwa ghafula, lengo lalo likiwa kusaidia wanawake wasio na elimu kutunza afya yao ili kwamba waweze kufanya kazi, waweze kusoma na kuandika ifaavyo ili kuepuka kunaswa katika kazi zilizofisidika ili kuboresha stadi zao za kazi, na kujifunza kuweka akiba ya fedha ili kwamba watengeneze mali zilizojumlishwa kuleta pato na kuepuka viwango vya riba vinavyotozwa na wakopeshaji wasio wanyofu. Alipoulizwa kuhusu kutumia usawa wa jinsia kama kifaa cha kijamii, mwanasosholojia mashuhuri Zarina Bhatti alitaarifu hivi: “Katika India usawa wa jinsia humaanisha kusikiliza matatizo ya wanawake, kuwapanga kitengenezo, kujaribu kuwatolea elimu ya kiufundi pamoja na afya na lishe.”
Kwa wakati huo huo, maoni yamekuwa yakibadilika kuhusu hali ya wanawake walio na elimu kutoka familia tajiri walioonwa kuwa katika ngazi ya juu zaidi ya kijamii, na vilevile wanawake kutoka familia za tabaka la katikati. Sasa wanawake kutoka malezi hayo mawili wanaweza kupatikana katika nyanja zote za utendaji, si tu za kufundisha au udaktari. Wana kazi-maisha wakiwa marubani wa ndege, violezo, wafanyakazi wa kike katika ndege, na polisi na wanapatikana katika vyeo vya ngazi za juu. Kwa miaka mingi India ilikuwa na mwanamke akiwa waziri mkuu, aliyechaguliwa katika demokrasia iliyo kubwa kuliko zote ulimwenguni. Wanawake wa India wana vyeo katika jeshi na ni wanasheria na mahakimu wakuu, na maelfu wameingia katika biashara wakiwa wamiliki-biashara.
Mabadiliko Katika Eneo la Ndoa
Kukiwa na mwelekeo huu kuelekea kujiajiri, mwanamke wa kisasa wa India huhisije kuhusu ndoa? Karne za 19 na 20 zilileta mabadiliko makubwa kwa wanawake walioolewa wa India. Desturi ya kale iliyoitwa Suttee, ambayo katika hiyo mjane kwa kujitolea alijichoma kwenye rundo la kuni za kuchomea maiti la maziko ya mumeye, iliondolewa chini ya utawala wa Uingereza. Ndoa za watoto zimepigwa marufuku na sheria ili kwamba sasa msichana aliye chini ya umri wa miaka 18 hawezi kuolewa kihalali. Kudai mahari kutoka familia ya msichana pia kumepigwa marufuku kihalali, lakini zoea hili lenye kudhuru liko bado. Maelfu mengi ya bibi arusi wachanga wameuawa kimakusudi katika njia moja au nyingine, ama kwa sababu familia yao ilishindwa kutoa mahari ya kutosha au kwa sababu fedha zaidi zingeweza kupatikana kutokana na ndoa ya pili.
Pole kwa pole visababishi vikuu vya vifo vya kimahari vinaelekezewa fikira. Kidesturi, wakati wa kuolewa msichana wa India alienda kwa wazazi wa mumeye na kubaki huko hadi kifo chake. Wazazi wake hawangemrudisha nyumbani kwao kamwe. Wakiwa hawana elimu ya msingi, wanawake wengi hawangeweza kuacha waume zao nyumbani na kufanya kazi ili kujitegemeza. Kwa hiyo wanawake wachanga mara nyingi waliteswa na walikuwa na tisho la kifo likiwaotea, na ikiwa wazazi wao wangeweza kutoa fedha zaidi au vitu ili kutosheleza wakwe wenye pupa, mabibi arusi hao kwa wazi walingoja kwa maumivu ya kimya ajali inayowangojea, kwa kawaida aksidenti hatari iliyopangwa ambayo katika hiyo stovu ya kupikia ingelipuka au sari laini ingeshika moto.
Kwa wakati huu sheria, vituo vya wanawake polisi, na mahakama za wanawake na vikundi vya utegemezaji hutolea mwanamke aliyeolewa mahali pa kugeukia kwa ajili ya msaada ahisipo maisha yake yamo hatarini. Kukiwa na elimu zaidi na fursa za kazi zikiwa wazi kwao, wanawake fulani wanachagua kutoolewa au kuolewa baadaye maishani baada ya kujifanyia kazi-maisha. Hivyo, utegemeo kwa wanaume, ambao mara nyingi huongoza kwenye kutawalwa kikatili, si mwingi.
Watoto wa Kike Wapata Uangalifu Zaidi
Tatizo lingine linaloathiri wanawake, na linalobadilika kadiri karne ya 21 ikaribiapo, ni uchu wa kupata watoto wa kiume. Ikitegemea mafundisho ya kale ya kidini, pamoja na ufikirio wa kiuchumi, dhana hii mara nyingi imeongoza kwenye kuuawa kwa vitoto vya kike na kutendewa kwa ukatili kwa wasichana kwa kuwapa chakula, elimu na utunzi wa kiafya kwa kiwango cha chini kuliko kile kinachopewa wavulana.
Katika nyakati za hivi majuzi utumizi wa amniocentesis ili kujua jinsia ya kijusu, mara kwa mara ikiongoza kwenye utoaji-mimba ya watoto wa kike, umeenea sana. Ingawa inasimamiwa na sheria, hiyo taratibu bado ni zoea la kawaida. Jitihada zenye bidii zinafanywa kubadili maoni ya kwamba mtoto wa kiume ndiye anayefaa zaidi.
Falsafa za mwanadamu zimeshusha wanawake katika njia nyingi. Kielelezo ni jinsi wajane wanavyotendewa. Katika India ya kale, kuolewa tena kwa wajane kulikubalika. Lakini kutoka karne ya sita hivi W.K., watoa-sheria walikataa hili, na hali ya maisha ya wajane ikawa ya kusikitikiwa. Wakiwa wamekatazwa kuolewa tena, mara nyingi kunyang’anywa mali za waume zao waliokufa na watu wa ukoo, kutendewa kama laana juu ya familia, wajane wengi walichagua kujiua kidhabihu kwenye rundo la kuni za kuchoma maiti katika maziko ya waume zao badala ya maisha ya kutendwa vibaya na kutoheshimiwa.
Tangu mwishoni mwa karne ya 19, warekebishaji walijaribu kupunguza mzigo wa wanawake kama hao, lakini hisia zilizokazwa kwa kina huchukua muda mrefu kuisha. Katika jamii nyingi hali ya maisha ya mjane, nyakati fulani mwanamke mchanga sana ambaye mume wake mzee amekufa, kwa kweli ni yenye kutaabisha. Asema Dakt. Saharada Jain wa Institute for Development Studies: “Yale maumivu makali ya ujane kwa msingi hutokea kutokana na uhakika wa kwamba wanawake hujirekebisha sana hivi kwamba utu wao wote unafanyizika na kutegemea hadhi ya waume zao.” Jitihada zinafanywa ili kusaidia wajane wasonge kuelekea karne ya 21 wakiheshimiwa.
Tofauti za Mashambani na Mijini
Kuna tofauti kubwa kati ya wanawake wa mijini na wale walio mashambani. Inakadiriwa kwamba asilimia 25 ya wanawake wa mashambani wanajua kusoma na kuandika; katika miji asilimia za juu zaidi hunufaika kutokana na shule na koleji. Ili kusaidia wanawake wa mashambani, wafanyakazi wa kijamii hupanga madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika, mazoezi ya utunzaji-afya, na mipango ya uajiri. Serikali fulani za kimajimbo zimetenga kando asilimia 30 ya nafasi za kazi katika sekta ya umma, mashirika ya muungano, na kujitawala wenyewe kwa wanawake. Harakati za wanawake zatafuta kupunguza maumivu na umaskini ambao ndio hali ya maisha ya mamilioni katika India. Kwa kiwango fulani hizi zimekuwa na mafanikio. Kwa hiyo, twaweza kusema nini kuhusu wakati ujao wa wanawake wa India?
Kusonga Kuingia Katika Karne ya 21!
Je, fungu la mwanamke wa India labadilika asongapo kuingia katika karne ya 21? Ndiyo, na lafanya hivyo kwa haraka. Lakini wanawake wa India wanakabili hali sawa na ile ya wanawake wenzao ulimwenguni pote. Kuna maendeleo, lakini kuna vizuizi. Kuna tumaini, lakini kuna utamausho. Kuna nyumba zenye kuvutia na mitindo-maisha ya raha, lakini kuna makao ya hali ya chini, umaskini mwingi, na njaa nzito. Kwa mamilioni kitu kinachowawezesha kuendelea kuwako tu ndicho wawezacho kupata. Wengine yaonekana wana kila kitu ambacho ulimwengu unatoa. Kwa wengi, wakati ujao haujulikani; wana miradi wanayotamani sana lakini pia wana tashwishi.
Hata hivyo, kwa wengine wakati ujao ni mwangavu kwa ahadi, hasa kwa wale ambao wana tumaini katika dunia Paradiso itakayokuja chini ya utawala wa Ufalme wa Yehova kupitia Kristo Yesu. (Ufunuo 21:1, 4, 5) Hawa wanatazamia wakiwa na uhakika kamili karne ya 21 ambayo katika hiyo wanawake watafurahia maisha kwa ukamili.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kubeba matofali hadi kwenye mahali pa ujenzi
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kuteka maji kwa matumizi ya nyumbani
[Picha katika ukurasa wa 18]
Katika mkutano pamoja na wanaume
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kutendesha kompyuta