Tuliumbwa Tuishi Milele
MWILI wa binadamu umeumbwa kwa njia ya ajabu. Maendeleo yao na ukuzi wao wenyewe ni muujiza tu. Mwandikaji fulani wa kale alipaaza sauti hivi: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.” (Zaburi 139:14) Wakijua vyema sana juu ya ajabu za mwili wa binadamu, wanasayansi fulani wa kisasa wanaona kuzeeka na kifo vikiwa mambo yenye kutatanisha. Wewe huona hivyo?
“Kuzeeka,” akaandika mwanabiolojia wa Chuo Kikuu cha Harvard Steven Austad, “kunatukabili mno sikuzote hivi kwamba nashangaa watu wengi zaidi hawakuoni kuwa fumbo kuu la kibiolojia.” Uhakika wa kwamba kila mtu anazeeka, akaonelea Austad, “hufanya [kuzeeka] kuonekane kuwa hakutatanishi sana.” Ingawa hivyo, unapofikiria sana kuvihusu, je, kuzeeka na kufa kuna maana yoyote?
Mwaka jana, katika kitabu chake How and Why We Age, Dakt. Leonard Hayflick alikubali juu ya ajabu ya uhai na ukuzi wa binadamu na kuandika hivi: “Baada ya kufanya miujiza inayotupata kutoka kutungwa mimba hadi kuzaliwa kisha hadi upevuko wa kingono na utu uzima, hali-asili ilichagua kutounda kile kionekanacho kuwa mfumo wa utendaji ulio sahili zaidi ambao ungedumisha miujiza hiyo milele. Ufahamu huu wenye kina umetatanisha wanabiogerontolojia [wale wanaochunguza sehemu za kibiolojia za kuzeeka] kwa miongo mingi.”
Je, wewe pia unatatanishwa na kuzeeka na kufa? Hali hizo zinatimiza kusudi gani? Hayflick alionelea hivi: “Karibu matukio yote ya kibiolojia kutoka kutungwa mimba hadi upevuko yaonekana yana kusudi, lakini kuzeeka hakuna. Haiko wazi kwa nini kuzeeka kwapasa kutokea. Ingawa tumejifunza mengi kuhusu biolojia ya kuzeeka . . . , bado inatulazimu kukabili matokeo ya kuzeeka kusiko na kusudi kukifuatiwa na kifo.”
Je, inawezekana kwamba hatukukusudiwa tuzeeke na kufa bali tulikusudiwa tuishi milele duniani?
Tamaa ya Kuishi
Ni hakika kwamba unajua karibu kila mtu anachukia kuzeeka na kufa. Kwa hakika, wengi huogopa hilo taraja. Katika kitabu chake How We Die, daktari wa kitiba Sherwin B. Nuland aliandika hivi: “Hakuna yeyote kati yetu ambaye yaonekana anaweza kisaikolojia kukabiliana na wazo la hali yetu wenyewe ya kifo, kukiwa na lile wazo la kukosa fahamu daima ambako hakuna wala utupu wala uwazi—ambako hakuna chochote kabisa.” Je, unajua mtu yeyote ambaye anataka kuzeeka, kuwa mgonjwa, na kufa?
Hata hivyo, ikiwa uzee na kifo ni mambo ya asili na sehemu ya mpango mkuu, je, hatungezikubali? Lakini hatuzikubali. Kwa nini sivyo? Jibu lapatikana katika njia tuliyoumbwa. Biblia husema hivi: “[Mungu] hata ameweka umilele katika akili [zetu].” (Mhubiri 3:11, Byington) Kwa sababu ya hii tamaa ya wakati ujao usio na mwisho, watu wametafuta kwa muda mrefu ile iitwayo eti chemchemi ya ujana. Wanataka kubaki wakiwa vijana milele. Hili lazusha swali, Je, tuna uwezo wa maisha marefu zaidi?
Uliumbwa Ujirekebishe Wenyewe
Akiandika katika gazeti Natural History, mwanabiolojia Austad alitokeza maoni haya ya kawaida: “Sisi huelekea kujifikiria na kufikiria wanyama wengine katika njia ile tunayozifikiria mashine: kuchakaa ni jambo lisiloepukika.” Lakini hili si kweli. “Kimsingi viumbe-hai ni tofauti na mashine,” Austad akasema. “Hujirekebisha vyenyewe: vidonda hupona, mifupa hujitengeneza, ugonjwa hupita.”
Hiyo yatokeza swali lenye kuvuta uangalifu, Kwa nini sisi huzeeka? Kama Austad alivyouliza: “Kwa nini, basi [viumbe-hai] vichakae vilevile kama mashine?” Kwa kuwa tishu mpya za mwili huchukua mahali pa zilizoharibika, je, hazingeweza kufanya hivyo milele?
Katika gazeti Discover, mwanabiolojia wa mageuzi Jared Diamond alizungumzia uwezo wa ajabu wa viumbe vya asili wa kujirekebisha. Yeye aliandika hivi: “Kielelezo kilicho wazi zaidi cha udhibiti wa kuharibika kunakotokea katika miili yetu ni kupona kwa kidonda, ambako sisi hurekebisha uharibifu uliotokea ngozini mwetu. Wanyama wengi wanaweza kupata matokeo yenye kushangaza kuliko sisi: mijusi wanaweza kukuza tena mikia iliyokatwa, kiti-cha-pweza na kaa wanaweza kukuza tena mikono yao, na mibilimbibahari matumbo yao.”
Kuhusu umeaji-tena wa meno, Diamond alitaarifu hivi: “Meno ya binadamu hukua mara mbili, ya tembo mara sita, na ya papa idadi isiyo na mwisho muda wote wa maisha yao.” Kisha akaeleza hivi: “Ubadilishaji wa kawaida pia huendelea katika kiwango kisichoonekana kwa macho matupu. Sisi hubadilisha chembe zilizo ukutani mwa matumbo yetu mara moja baada ya siku chache, zile zilizo ukutani mwa kibofu cha mkojo mara moja baada ya miezi miwili, na chembe zetu nyekundu za damu mara moja kwa miezi minne.
“Katika kiwango cha molekuli, molekuli zetu za protini hupatwa na mabadiliko yenye kuendelea katika kiwango kilicho kawaida ya kila protini hususa; kwa njia hiyo tunaepuka ukusanyaji wa molekuli zilizoharibika. Hivyo ukilinganisha sura ya mpendwa wako leo na ile ya mwezi uliopita, huenda akaonekana vilevile, lakini nyingi za molekuli moja-moja zinazofanyiza mwili huo mpendwa ziko tofauti.”
Chembe nyingi za mwili hubadilishwa baada ya muda fulani na zile zilizofanywa upya. Lakini chembe nyingine, kama vile nuroni za ubongo, huenda zisibadilishwe kamwe. Hata hivyo, Hayflick alieleza hivi: “Ikiwa kila sehemu ya chembe imebadilishwa haiwi chembe ileile ya zamani. Nuroni ulizozaliwa nazo huenda leo zionekane kuwa chembe zilezile, lakini kwa uhalisi nyingi za molekuli zilizozifanyiza ulipozaliwa . . . huenda zilibadilishwa na molekuli mpya. Kwa hiyo chembe zisizoweza kugawanyika huenda zisiwe chembe zilezile ulizozaliwa nazo!” Hii ni kwa sababu vifanyizaji vya hizo chembe vimebadilishwa. Kwa hiyo, kiakili ubadilishaji wa vifanyizaji vya mwili ungeweza kutufanya tuendelee kuishi milele!
Kumbuka kwamba Dakt. Hayflick alizungumzia juu ya “miujiza inayotupata kutoka kutungwa mimba hadi kuzaliwa.” Ni ipi baadhi yayo? Tunapoichunguza kifupi, fikiria uwezekano wa utekelezaji wa kile alichoita ‘mfumo wa utendaji ulio sahili zaidi wa kudumisha miujiza hiyo milele.’
Chembe
Mtu mzima ana chembe trilioni 100, ambazo kila moja yazo ni yenye utata usioweza kufahamika. Ili kutolea kielezi huo utata, gazeti Newsweek lililinganisha chembe na jiji lililozingirwa kwa ukuta. “Vituo vya nguvu za umeme hutokeza nishati za chembe,” gazeti hilo likasema. “Viwanda hutokeza protini, vifanyizo muhimu sana vya mabadilishano ya kemikali. Mifumo tata ya usafirishaji huongoza kemikali hususa kutoka kituo kimoja hadi kingine katika chembe na nje ya chembe. Askari-walinzi kwenye vizuio hudhibiti mauzo ya kupeleka vitu nje na ya kuingiza ndani, na kuchunguza kilicho nje ya chembe kwa ajili ya dalili zozote za hatari. Wanajeshi wa kibiolojia walio na nidhamu husimama wakiwa tayari kumenyana na washambulizi. Serikali ya kijeni iliyowekwa kati hudumisha utengamano.”
Fikiria jinsi wewe—ukiwa chembe trilioni 100—ulivyotokea. Ulianza ukiwa chembe moja ambayo ilibuniwa wakati shahawa kutoka kwa baba yako ilipoungana na chembe ya yai kutoka kwa mama yako. Katika kuungana huko, mpango ulibuniwa ndani ya DNA (kifupi cha asidi kiinidioksiribo) ya chembe hiyo mpya iliyobuniwa ili kutokeza kile kilichokuja hatimaye kuwa wewe—binadamu mpya kabisa na wa kipekee. Maagizo yaliyo katika DNA “yakiandikwa,” inasemekana, “yatajaza vitabu elfu moja kila kimoja kikiwa na kurasa 600.”
Baada ya muda fulani, chembe hiyo ya awali ilianza kugawanyika, ikitokeza chembe mbili, kisha nne, nane, na kuendelea. Hatimaye, baada ya siku 270 hivi—wakati wa kipindi ambacho maelfu ya mamilioni ya chembe aina nyingi tofauti zilikuwa zimekua ndani ya mama yako ili kufanyiza mtoto—WEWE ulizaliwa. Ni kana kwamba chembe hiyo ya kwanza ilikuwa na chumba kikubwa mno kilichojaa vitabu vilivyokuwa na maagizo ya kina ya jinsi ya kukufanyiza. Jambo la ajabu vilevile ni uhakika wa kwamba maagizo haya yenye kutatanisha yalipitishwa kwa kila chembe iliyofuata. Ndiyo, kwa kushangaza, kila chembe katika mwili wako ina habari ileile iliyokuwa katika yai la awali lililotungishwa!
Fikiria hili pia. Kwa kuwa kila chembe ina habari ya kutokeza aina zote za chembe, wakati ulipofika, tuseme, wa kufanyiza chembe za moyo, maagizo ya kufanyiza chembe zile nyingine zote yalikandamizwaje? Yaonekana, ikitenda kama mfanyakazi wa mkataba ikiwa na kabati iliyojaa plani za kufanyiza mtoto, chembe moja iliteua kutoka kabati yayo ya faili plani ya kufanyiza chembe za moyo. Chembe nyingine ziliteua plani tofauti ya kutokeza chembe za neva, na bado nyingine zikachukua plani ya kufanyiza chembe za ini, na kadhalika. Kwa hakika, uwezo huu wa chembe ambao bado haujafahamika vizuri wa kuteua maagizo yanayohitajika ili kutokeza aina hususa ya chembe na kwa wakati uleule kukandamiza maagizo mengine yote ni muujiza mwingine kati ya mingi ya “miujiza inayotupata kutoka kutungwa mimba hadi kuzaliwa.”
Hata hivyo, kuna mengi zaidi yanayohusika. Kwa kielelezo, chembe za moyo huhitaji kuamshwa ili zikunjamane kwa utaratibu fulani. Kwa hiyo, ndani ya moyo mfumo tata ulijengwa ili kutokeza mipwito ya kiumeme ili kusababisha moyo upige kwa kiwango kifaacho cha kutegemeza mwili katika utendaji ambao unajihusisha. Kwelikweli, muujiza wa ubuni! Si ajabu kwamba madaktari wamesema hivi kuhusu moyo: “Unafanya kazi vyema zaidi ya mashine yoyote ya aina yoyote ambayo imepata kubuniwa na mwanadamu.”
Ubongo
Ajabu kubwa hata zaidi ni ukuzi wa ubongo—sehemu ya kifumbo kuliko zote ya muujiza wa binadamu. Majuma matatu baada ya kutungwa mimba, chembe za ubongo huanza kufanyizwa. Hatimaye, chembe za neva ziitwazo nuroni zipatazo bilioni 100—nyingi mno kama nyota zilizo katika Njia ya Kimaziwa—hujaa katika ubongo wa binadamu.
“Kila moja ya hizi hupata habari kutoka nuroni nyingine katika ubongo zipatazo 10,000,” likaripoti gazeti Time, “nazo hupeleka habari kwa maelfu mengine ya nuroni.” Akiona uwezekano wa mchanganyo uelekeao kutokea, mwanasayansi wa nuroni Gerald Edelman alisema hivi: “Sehemu ya ubongo iliyo ndogo kama vile kichwa cha mshale wa kiberiti ina miunganisho bilioni moja hivi ambayo inaweza kuungana katika njia ambazo zinaweza kufafanuliwa tu kuwa nyingi ajabu—nambari kumi ikifuatiwa na mamilioni ya sufuri.”
Hii yapatia ubongo uwezo upi? Mstadi wa nyota Carl Sagan alisema kwamba ubongo wa binadamu waweza kushikilia habari ambayo “yaweza kujaza mabuku milioni ishirini, mengi mno kadiri ya yale yapatikanayo katika maktaba kuu zaidi ulimwenguni.” Mtungaji vitabu George Leonard alieleza zaidi, akishangaa: “Kwa hakika, labda sasa twaweza kutoa wazo la nadhariatete yenye kushangaza mno: Uwezo wote wa ubuni wa ubongo waweza kuwa usio na mwisho kabisa.”
Kwa hiyo, hatupaswi kushangazwa na taarifa zifuatazo: “Ubongo,” akasema mwanabiolojia ya kimolekuli James Watson, aliyesaidia kuvumbua mfanyizo wa kiumbo wa DNA, “ndio kitu tata kuliko vyote ambavyo tumepata kuvumbua katika ulimwengu wetu mzima.” Mstadi wa nuroni Richard Restak, ambaye anachukia kulinganishwa kwa ubongo na kompyuta, alisema hivi: “Hali ya kipekee ya ubongo hutokana na uhakika wa kwamba hakuna mahali popote pajulikanapo katika ulimwengu mzima ujulikanao, ambapo kuna chochote hata kinachokaribia kufanana na ubongo.”
Wanasayansi wa nuroni wanasema kwamba katika muda wetu sasa wa maisha, tunatumia sehemu ndogo tu ya uwezo wetu wa ubongo, 1/10,000 hivi tu au 1/100 ya asilimia moja, kulingana na kadirio moja. Fikiria hilo. Je, ni jambo la kiakili kwamba tungepewa ubongo ulio na uwezekano mbalimbali kama huo wa kimuujiza ikiwa haungetumiwa kikamili kamwe? Je, si jambo la kiakili kwamba binadamu, wakiwa na uwezo wa kujifunza kusiko na mwisho, waliumbwa hasa waishi milele?
Ikiwa hilo ni kweli, kwa nini tunazeeka? Ni nini kilichoenda mrama? Kwa sababu gani, baada ya miaka 70 au 80, tunakufa, hata ingawa miili yetu kwa wazi iliumbwa idumu milele?
[Mchoro katika ukurasa wa 7]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Chembe—Muujiza wa Ubuni
Kiwambochembe
Kifuniko kinachodhibiti kile kinachoingia na kutoka katika chembe
Kiinichembe
Kikiwa ndani ya kifuko chenye kiwambo maradufu, hicho ndicho kitovu cha udhibiti ambacho huelekeza utendaji wa chembe
Ribosomu
Maumbo ambapo asidi amino hutengenezwa kuwa protini
Kromosomu
Zina DNA ya chembe, ambayo ni mpango mkuu wa kijeni
Kijiinichembe
Mahali ambapo ribosomu hutengenezwa
Wavu Utendani
Tabaka za viwambo ambazo huhifadhi au kusafirisha protini zilizofanyizwa na ribosomu zilizoshikanishwa nazo (baadhi ya ribosomu huelea kwa uhuru katika chembe)
Mitokondria
Vitovu vya utokezwaji wa ATP, molekuli zinazotoa nishati kwa ajili ya chembe
Viriba vya Golgi
Kikundi cha viriba vya kiwambo vilivyotandazwa ambavyo hupakia na kusambaza protini zilizofanyizwa na chembe
Sentrioli
Hukaa karibu na kiinichembe na ni muhimu sana katika utokezaji wa chembe