Utafutaji wa Majibu wa Mwanamume Kijana
JUA la asubuhi liliangaza kwa wangavu, likipenya kupitia miti hadi kwa mvulana aliyekuwa amepiga magoti akisali kwa bidii. Joseph mwenye umri wa miaka 14 alikuwa amevurugika kwa mchafuko wa kidini wa wakati wake. Makanisa ya kidesturi yalikuwa yamepatwa na mgawanyiko. Mafarakano mapya yalikuwa kila mahali. Ajiunge na kikundi kipi? Akiwa amepiga magoti yeye aliomba hivi: “Ni kipi kati ya vikundi vyote hivi kilicho cha kweli; au, vyote viko katika kosa? Ikiwa kimoja chavyo ni cha kweli, ni kipi, na nitakijuaje?”
Hivyo ndivyo Joseph Smith alifafanua tatizo lake la mapema la kiroho. Si ajabu kwamba alikuwa amevurugika. Hii ilikuwa sehemu ya mashambani ya kaskazini-mashariki mwa Marekani mapema katika karne ya 19, sehemu iliyokuwa na bidii nyingi ya kidini.a Tumaini lilihitajika mno. Wakulima wengi waling’ang’ana na maisha magumu kama ule udongo wenye mawe waliokuwa wakiulima. Wakitamani kitu bora, walikuwa wakitamanishwa bure kwa hekaya za hazina ya Wenyeji wa Marekani iliyozikwa. Kwa hiyo walitafuta sana milimani, wakiwa wamejihami kwa mawe ya waaguzi, maneno ya kunuizia uchawi, na fimbo za uaguzi. Hekaya za mahali hapo zilieleza juu ya ustaarabu mkubwa wa Wenyeji wa Marekani ulioishia katika pigano baya mahali fulani katika Jimbo la New York.
Wahubiri mashuhuri wa wakati huo walichochea moto wa makisio, wakisema kwamba Wenyeji wa Marekani walikuwa wazao kutoka makabila kumi ya Israeli yaliyopotea. Kwa kielelezo, katika 1823, Ethan Smith aliandika kitabu View of the Hebrews; or the Tribes of Israel in America.
Mabamba ya Dhahabu na Nabii
Joseph Smith alilelewa katika mazingira haya yenye rutuba ya kitamaduni na bidii ya kidini yenye kuwaka. Familia yake pia ilijihusisha na msisimko huu. Mama ya Joseph aliandika juu ya kupata kwao maponyo, miujiza, na maono. Lakini wakati yeye na baadhi ya watoto wake walipojiunga na kanisa, Joseph alikataa kuwafuata. Baadaye, katika simulizi lake la maisha, aliandika kuhusu sala yake ya kuomba msaada na majibu aliyopata.
Joseph alieleza juu ya ono ambalo kwalo Mungu alimkanya kujiunga na farakano lolote kwa sababu yote yalikuwa katika kosa. Kisha, siku moja wakati wa masika katika 1823, Smith mwenye umri wa miaka 17 aliambia familia yake kwamba malaika aitwaye Moroni alikuwa amemwonyesha seti ya mabamba ya kale ya dhahabu. Miaka minne baadaye alidai kwamba alipewa hayo mabamba na uwezo wa kimungu yeye pekee wa kuyatafsiri, jambo ambalo lilihitaji kutumia jiwe la pekee lililoitwa “jiwe la mwaguzi” na miwani ya fedha ya kimazingaombwe—almasi mbili zenye pembe tatu zilizowekwa katika gilasi. Ilimaanisha kifo cha papo hapo kwa wengine kuona mabamba hayo wakati huo, Smith akaonya.
Smith, ambaye aliweza kusoma lakini kutoandika vizuri, alikariri “utafsiri” wa mabamba hayo kwa waandishi kadhaa. Akiwa ameketi nyuma ya pazia, yeye alisimulia hadithi ambayo ilikusanywa eti na mwanamume Mwebrania aliyeitwa Mormon. Mabamba hayo yalinakiliwa katika maandishi ya “Kimisri kilichorekebishwa,” Smith akaeleza, ambayo yalikuwa na maneno machache sana kuliko Kiebrania. Mormon na mwana wake Moroni walifafanuliwa kuwa miongoni mwa waokokaji wa mwisho wa watu walioitwa taifa la Wanefiti, wazao wa Waebrania wenye ngozi yenye rangi nyangavu wanaosemekana kuwa walihamia Marekani mwaka wa 600 hivi K.W.K. ili kutoroka uharibifu wa Yerusalemu.
Simulizi hilo hueleza kwamba Yesu alikuwa amelitokea taifa hili katika Marekani baada ya kifo chake na ufufuo na akachagua mitume 12 Wanefiti. Walamaniti, watu walio wazao wa Waebrania pia, walikuwa wenye uasi na wa kivita na kwa hiyo walilaaniwa na Mungu kwa kupewa ngozi nyeusi. Simulizi la Mormon hasa liliwekea kumbukumbu mapigano yaliyokuwa yakiendelea kati ya mataifa haya mawili. Wanefiti wakawa waovu na hatimaye wakaangamizwa na Walamaniti, ambao walikuwa mababu wa kale wa Wenyeji wa Marekani.
Kulingana na Smith, mwana wa Mormon, aliye sasa kiumbe-roho Moroni, alimpa rekodi iliyo kwenye mabamba ya dhahabu na utume wa kuongoza hadi kwenye kurejeshwa kwa kanisa la Kristo. Baada ya muda Smith akapata wafuasi. Mwamini mwenye mali nyingi alilipia gharama za kuchapisha hati ya Smith iliyoitwa The Book of Mormon. Ilipatikana katika chapa wakati wa vuli ya 1830. Majuma mawili baadaye, Joseph Smith alitangaza cheo chake kamili: “Mwaguzi, Mtafsiri, Nabii, Mtume wa Yesu Kristo.” Mnamo Aprili 6, 1830, Kanisa la Mormon, au Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku-za-Baadaye, lilizaliwa.b
Smith alikuwa mwenye haiba ambayo ilimpa ujitoaji wa waamini wengi. Lakini dini yake isiyofuata desturi ilitokeza maadui wengi pia. Kanisa hilo jipya lilisumbuliwa sana; washiriki walo walitoroka kutoka New York hadi Ohio na kisha Missouri katika kutafuta Yerusalemu lalo Jipya. Akiwa nabii, Smith alitoa ufunuo baada ya ufunuo, akisimulia mapenzi ya Mungu juu ya mambo kuanzia michango ya kifedha hadi amri ya kimungu ya kuoa wake wengi. Ufunuo huu wa mwisho hasa ulitokeza mnyanyaso mwingi. Wakikabiliwa na mashaka na kupingwa kila mahali, Wamormon walichukua silaha ili kujikinga.
Mipango ya hila na mvurugo uliobainisha miaka ya mapema ya maisha ya Joseph Smith haukuisha kamwe. Miji iliyokuwa mashambani, iliyojawa na kuingia kwa wafuasi wa Smith, ilipinga kwa nguvu. Hawakutaka wala kitabu kingine kitakatifu wala nabii wa kujitangaza. Kisha katika 1839, kwa mshtuko wa watu wa mahali hapo, Wamormon walianzisha milki yenye kusitawi ikiwa na jengo lao wenyewe la kusaga unga, kiwanda, chuo kikuu, na wanamgambo katika Nauvoo, Illinois. Wakati hali mbaya zilipotokea, Smith alishikwa na kufungwa katika Carthage, Illinois. Huko, katika Juni 27, 1844, kikundi cha watu kilishambulia gereza na kumpiga risasi na kumwua.
Kanisa Laendelea Bila Nabii Walo
Simulizi haliishi kwa kifo cha Joseph Smith. Brigham Young, msimamizi wa Baraza la Mitume Kumi na Wawili, mara moja alichukua mamlaka na kuongoza waamini wengi kwenye safari hatari hadi kwenye bonde la Great Salt Lake katika Utah, ambapo makao makuu ya Wamormon yapo hadi leo.c
Kanisa lililoanzishwa na Joseph Smith laendelea kuvutia waamini, likiwa, kulingana na vyanzo vya LDS, na washiriki wapatao milioni tisa ulimwenguni pote. Limeenea mbalimbali kupita pahali palo pa mwanzo katika Jimbo la New York hadi mahali mbali kama vile Italia, Filipino, Uruguay, na Zaire. Japo kupingwa kunakoendelea, Kanisa la Mormon lenye kutazamisha limenawiri. Je, kweli ndilo urejesho wa Ukristo wa kweli ambao watu wa imani wamengojea?
[Maelezo ya Chini]
a Wanahistoria baadaye waliita sehemu hii katika magharibi mwa Jimbo la New York wilaya iliyoteketezwa kwa sababu ya mawimbi ya muda mfupi ya upendezi mpya wa kidini yaliyokumba sehemu hiyo mapema katika miaka ya 1800.
b Likiitwa mwanzoni Kanisa la Kristo, kwenye Aprili 26, 1838, lilikuja kuwa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku-za-Baadaye, au LDS. Ingawa LDS ni utambulisho unaopendelewa na washiriki, jina Mormon (lililotolewa kutoka The Book of Mormon) pia latumiwa katika mfululizo wa makala hizi, kwa kuwa linajulikana sana kwa wasomaji wengi.
c Kuna vikundi kadhaa ambavyo vimejiondoa kutoka LDS, ambavyo hujiita Wamormon. Kikuu miongoni mwavyo ni Kanisa la Yesu Kristo Lililopangwa Upya la Watakatifu wa Siku-za-Baadaye, kilicho na makao yacho katika Independence, Missouri.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Picha: Kwa hisani ya Church of Jesus Christ of Latter-Day Saints/Dictionary of American Portraits/Dover