Ripoti ya Jessica
JESSICA, msichana mwenye umri wa miaka 13 kutoka Marekani, alipewa mgawo pamoja na wanadarasa wenzake kutoa hotuba juu ya kichwa “Mungu, Bendera, na Nchi.” Akijua kwamba wanafunzi wenzake walikuwa wakitaka sana kujua kwa nini yeye akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova hakusalimu bendera, kwa ujasiri Jessica alitumia fursa hii kwa faida ili kueleza itikadi zake. Yafuatayo ni madondoo kutoka ripoti yake.
“Mwanzoni mwa kila siku ya shule, wanafunzi huombwa kusema uapo wa utii, lakini kwa sababu ya itikadi zangu na dini yangu, mimi sifanyi hivyo. Watu wengi hujiuliza kwa nini. Sasa, nitawaambieni.
“Maneno ya kwanza ya kusalimu bendera ni: ‘Naapa kuitii bendera.’ Utii ni nini? Ni wajibu wa uungaji-mkono, uaminifu-mshikamanifu, na ujitoaji. Kwa kuwa tayari nimeshaapa kumtii Mungu, siwezi na sitaapa kuitii bendera. Ingawa hivyo, kwamba siapi kuitii bendera haimaanishi kwamba siistahi.
“Mungu ndiye wa maana sana katika maisha yangu. Najaribu kadiri niwezavyo kufuata amri zake kama zilivyoandikwa katika Biblia. Kila siku mimi humwomba, na pia husali nihitajipo msaada wa ziada au kitia-moyo. Sikuzote mimi hupata msaada na kitia-moyo hicho kwa wakati ufaao. Nimepata kwamba ninapomweka Mungu mahali pa kwanza na ninapofanya mambo ambayo ametuamuru tufanye, ninakuwa na furaha zaidi.
“Kwa hiyo ingawa siisalimu bendera, naistahi na singeivunjia heshima kwa njia yoyote ile. Lakini utii wangu ni kwa Mungu, na ni hivyo kwa kufaa, kwa sababu yeye aliniumba nami nawiwa naye utii huo.”
Wanafunzi katika darasa la Jessica waliombwa wachanganue ripoti walizosikiliza. Jessica alifurahi kama nini kwamba likiwa tokeo la jitihada yake, wanadarasa wenzake walisema kwamba walikuwa wamepata kuzielewa vizuri zaidi itikadi zake. La maana zaidi, vijana wanenao kwa ujasiri kwa kutetea kanuni za Biblia hufanya moyo wa Yehova Mungu ushangilie!—Mithali 27:11.