Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 3/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matetemeko ya Dunia Hayawezi Kutabiriwa
  • Kuokoka Kuzama Kwenye Maji Baridi
  • Michezo na Maisha Marefu
  • Hakuna Lazima ya Kusema Kweli
  • Viwango Vipya
  • Mwongo Usio na Matokeo
  • Unyang’anyi Wenye Ujasiri
  • Habari za Mamba
  • Mkazo Unaoongezeka
  • Pengo la Afya
  • Jihadhari na ‘Macho ya Mtoni’!
    Amkeni!—1996
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Kumtazama Mamba kwa Ukaribu Zaidi
    Amkeni!—1995
  • Matetemeko ya Ardhi Ni Ishara ya Ule Mwisho?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 3/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Matetemeko ya Dunia Hayawezi Kutabiriwa

Kwa miaka mingi wanasayansi walihisi kwamba yawezekana kutabiri matetemeko ya dunia. Walichunguza sehemu za juu za ardhi zilizojaa maji, miendo ya pole ya uso wa dunia, gesi ya radoni inayoponyoka kutoka kwa visima, na ishara nyinginezo. “Wengi wa wataalamu mashuhuri wa matetemeko ya dunia wa hilo taifa sasa wanafikiri kuwa matetemeko ya dunia hayawezi kutabiriwa sikuzote,” yaonelea makala katika The New York Times. “Wanasema kwamba kule kuwaonya watu siku, saa, au dakika kadhaa kabla ya tetemeko la dunia kwaonekana ni bure. . . . Ingawa utafiti wa karibuni hudokeza kwamba matetemeko kadhaa ya dunia yaweza kutokeza ishara za kimbele zinazohusu kusonga kwa uso wa dunia, ishara hizi ni ndogo sana, dhaifu na zilizofichika hivi kwamba kuzitambua kwa matokeo huenda kusiwezekane.” Watu fulani sasa wanaiomba serikali ichukue fedha za utafiti wa matetemeko ya dunia na kuzitumia kwa kupunguza madhara yatokeayo. Hata hivyo, wanasayansi wanakubali kwamba ujuzi zaidi wa jinsi ardhi inavyosonga na jinsi majengo huitikia matetemeko ya dunia wahitajiwa.

Kuokoka Kuzama Kwenye Maji Baridi

Wanasayansi wanaochunguza ni kwa nini watu wanaotumbukia kwenye maji ya baridi sana wanakufa haraka sana wamegundua kwamba kiasili mwili unaposhtuka kwa sababu ya baridi huo huongeza kiwango cha kupumua. “Kule kuvuta pumzi ndani kwa ghafula hufuatwa na kumeza maji kwa wingi—na kuzama,” lasema gazeti New Scientist. Kupumua huko hakuwezi kuzuiwa. Kwa hivyo kuokoka hutegemea kuweka kichwa juu ya maji mpaka kule kuvuta hewa upesi-upesi kupungue, kwa kawaida baada ya dakika mbili au tatu hivi.

Michezo na Maisha Marefu

Wajerumani hutumia kiasi cha pesa sawa na dola bilioni 25 katika michezo kila mwaka, au zaidi ya dola 300 kwa kila mtu. Pesa hizi hulipia “mavazi, vifaa, mazoezi, kukodisha viwanja vya michezo, na ada za vilabu,” laripoti Nassauische Neue Presse. Zaidi ya watu milioni tatu hujizoeza kwenye majumba ya mazoezi, na mamilioni zaidi hukimbia. Je, yawezekana kwamba wanaopenda michezo huishi kwa muda mrefu au huishi maisha mazuri zaidi kuliko wanaokaa nyumbani? Si lazima. Kitabu Physiologie des Menschen (Fisiolojia ya Kibinadamu) hutaarifu: “Kusema tu kwa ujumla kwamba michezo ndiyo dawa iliyo bora kwa hakika si sahihi.” Kwa nini? Kwa kuwa zaidi ya Wajerumani milioni 1.5 wanakwenda kwa daktari kila mwaka kwa sababu ya madhara yanayohusiana na michezo yaliyopatikana wakati wa tafrija kwenye miisho-juma na likizoni. Kitabu hicho hushauri kwamba mazoezi na michezo ni mizuri kwa afya ikiwa tu “maendeleo ya afya hayaharibiwi na aksidenti au madhara ya muda mrefu ya michezo.”

Hakuna Lazima ya Kusema Kweli

Kesi za mahakamani za karibuni za Marekani zimevuta uangalifu wa umma ulimwenguni pote na kuwashangaza watazamaji. “Ingawa mawakili wa mashtaka wanalazimika kusema ukweli, mawakili wa watetezi wana makusudio yaliyo tofauti kabisa,” lasema The New York Times. “Kazi ya wakili wa mtetezi ni kumfanya mshtakiwa aachiliwe, kutofikiwa kwa uamuzi (kwa kutia mashaka akilini mwa hata mmoja wa wazee wa mahakama) au kuhukumiwa mashtaka yasiyo na uzito sana.” “Hawalazimiki kuhakikisha kwamba hukumu ya ondoleo la hatia ni sahihi,” anasema Stephen Gillers, mwalimu wa maadili ya kisheria katika shule ya sheria ya Chuo Kikuu cha New York. “Tunawaambia wazee wa mahakama kwamba kesi hiyo ni ya kutafuta kweli, nasi hatuwaambii kwamba mawakili wa watetezi wanalazimika kuwahadaa.” Wakati ambapo “wanakabiliwa na mambo ya hakika yanayoonyesha wazi kwamba mshtakiwa ana hatia lawama, mara nyingi mawakili lazima watunge hadithi ili wazee wa mahakama wafikiri upya na kupuuza mambo ya hakika na wapigie kura kuachiliwa kwa mshtakiwa,” lataarifu Times. Inakuwaje basi wakati mawakili wanajua kwamba mshtakiwa wanayemtetea ana hatia lakini bado anasisitiza kupeleka kesi yake mbele ya wazee wa mahakama? “Ndipo mawakili wanaingia mahakamani wakiwa na unyenyekevu bandia, na kutangaza imani yao ya kina kwa ukweli wa hadithi ya mshtakiwa wakati ule ule wakijua kuwa ni uwongo mtupu,” asema Gillers.

Viwango Vipya

Vijana wa Kirusi pamoja na jamii ya Kirusi kwa ujumla wanakabili tatizo la viwango. Uchunguzi wa karibuni uliofanywa katika St. Petersburg, Urusi, uligundua kwamba mwelekeo wa vijana hutolea mkazo “viwango vya kawaida vya wanadamu—yaani, afya, uhai, familia, na upendo pamoja na viwango vya kibinafsi, kama vile mafanikio, kazi-maisha, starehe, na vitu vingi vya kimwili,” laripoti gazeti la Kirusi Sankt-Peterburgskiye Vyedomosti. Viwango vingine vikuu vinahusu wazazi, fedha, hali njema, furaha, urafiki, na ujuzi. Kwa kushangaza, kuwa na sifa njema na kufurahia uhuru mbalimbali wa kibinafsi kunachukua sehemu mbili kati ya zile za mwisho akilini mwa vijana. Ni nini kilicho katika sehemu ya mwisho? Ufuatiaji wa haki. Ripoti hiyo yamalizia hivi: “Ikiwa kudanganya kunawazingira, basi katika akili ya kizazi kinachokua [ufuatiaji wa haki] hauna thamani yoyote.”

Mwongo Usio na Matokeo

Makanisa ya Uingereza yaliutangaza huo kuwa “Mwongo wa Evanjeli.” Sasa, kufikia nusu yao, ni nini kimetimizwa? Katika Church Times msemaji Michael Green asema: “Hata hatujaanza kubadili gospeli ili ijibu maswali ambayo watu wa kawaida wanauliza. Sioni dalili yoyote ya makanisa kutoka na zile habari njema yakizipelekea jamii za watu. . . . Hata hatujaanza kuwa na matokeo kwa vijana wa kisasa wasiokwenda kanisani, nao hufanyiza asilimia 86 ya vijana wote katika nchi yetu.” Kwa nini hakuna matokeo? “Tunajilazimisha kuamini kwamba mtindo-maisha wetu utafanya hilo bila ya kusema lolote. Twaogopa kumchokoza yeyote,” asema Green.

Unyang’anyi Wenye Ujasiri

Katika Kanada, benki 1 kati ya kila benki 7 ilishambuliwa na wezi katika 1994—mashambulio mengi kwa matawi ya benki kuliko katika nchi nyingine yoyote. Hata hivyo, katika Italia, ambapo ofisi za matawi ya benki 1 kati ya 13 ilishambuliwa, wanyang’anyi walionekana kuwa wajasiri kuliko kwingineko kokote. Ni wachache tu kati ya wezi wa mabenki ya Italia waliojali kufunika sura zao au hata kutumia silaha. Wengine waliwatisha tu wenye kutoa pesa kwenye benki nao wakapewa pesa. Wanyang’anyi kadhaa hata waligeukia kutumia njia ya kupumbaza akili, laripoti The Economist. Wevi wa mabenki katika Italia ni wadumifu: matawi ya benki 165 yalivamiwa mara mbili, 27 mara tatu, na 9 mara nne mwakani. Wastani wa fedha zilizoibiwa katika 1994 ulikuwa nini? Lire milioni 61 (dola 37,803, za Marekani), kiwango kilicho cha chini zaidi tangu 1987.

Habari za Mamba

Baki la mataya ya mamba wa zamani lililofukuliwa karibuni “huenda lawakilisha mshiriki wa kwanza anayejulikana alaye mimea” wa familia ya mamba, laripoti gazeti Nature. Badala ya yale meno marefu yenye ncha ya mamba wa kisasa, anayeogopwa sana na wanadamu leo, babu huyu wa kale alikuwa na meno laini yanayoripotiwa kuwa yalifaa zaidi utafunaji wa nyasi. Yaonekana kwamba kiumbe huyu—aliyegunduliwa na watafiti Wachina na Wakanada katika Mkoa wa Hupeh huko China kwenye kilima karibu na ukingo wa kusini wa Mto Yangtze—pia aliishi kwenye nchi kavu, si majini tu. Ukubwa wake? Alikuwa na urefu wa karibu meta moja.

Mkazo Unaoongezeka

Uchunguzi wa karibuni katika Rio de Janeiro, Brazili, uligundua kwamba zaidi ya asilimia 35 ya watu wanaoenda kutibiwa walikuwa wanaugua na aina mbalimbali za matatizo ya akili, laripoti Veja. Gazeti hilo lilimuuliza Dakt. Jorge Alberto Costa e Silva, mkurugenzi wa afya ya akili wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO): “Tarakimu hizi zaweza kuelezwa jinsi gani? Je, ulimwengu umekuwa mbaya zaidi au watu wamekuwa dhaifu zaidi kiakili?” Jibu lake: “Tunaishi katika wakati wa mabadiliko ya haraka sana, ambayo mwishowe husababisha mahangaiko na mkazo kwa viwango ambavyo havijapata kamwe kufikiwa katika historia ya wanadamu.” Chanzo kimoja cha kawaida cha mkazo, yeye anadai, ni ujeuri ulioongezeka sana katika Rio de Janeiro. Huo mara nyingi huongoza kwenye mkazo wa kurudia-rudia baada ya kisa fulani, ambao, yeye aeleza, “huathiri watu ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa katika visa vyenye kuhatarisha uhai. Wakati wa mchana wana wasiwasi juu ya kila kitu. Wakati wa usiku wanapata ndoto mbaya ambamo kile kisa kilichohatarisha uhai wao chaonekana tena.”

Pengo la Afya

Lile pengo la afya kati ya mataifa tajiri na yale maskini linazidi kupanuka. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakadiria kwamba wastani wa tazamio la urefu wa maisha wa watu wanaoishi katika nchi zilizositawi na waliozaliwa huko ni miaka 76—ikilinganishwa na miaka 54 kwa wale walioko katika nchi ambazo hazijasitawi sana. Katika 1950, vifo vya watoto wachanga katika nchi maskini vilikuwa mara tatu zaidi ya vile vya nchi tajiri; sasa ni mara 15 zaidi. Kufikia mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1980, katika nchi maskini kiwango cha vifo kwa sababu ya matatizo wakati wa kuzaa kilikuwa mara 100 zaidi ya kile katika mataifa tajiri. Kinachochangia tatizo hilo, lataarifu WHO, ni uhakika wa kwamba, nusu ya watu wanaoishi katika nchi maskini wanaweza kupata maji safi na hali safi za kuondoa takataka. Kulingana na Umoja wa Mataifa, idadi ya “nchi zenye usitawi wa chini zaidi” iliongezeka kutoka 27 katika 1975 kufikia 48 katika 1995. Ulimwenguni pote kuna maskini bilioni 1.3, na idadi yao inaongezeka.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki