Kuutazama Ulimwengu
Ndoa Zaathiriwa Sana
Wake wengi katika eneo la Kobe, Japani, wameudhika kwa sababu ya mwenendo wa waume zao wakati na baada ya tetemeko la dunia ambalo liliharibu eneo hilo mapema katika 1995. “Mianya imetokea si katika nyumba yetu tu bali pia katika uhusiano wetu kwa kuwa sasa natambua kwamba siwezi kumtumaini mume wangu,” akasema mke mmoja ambaye alinukuliwa katika Asahi Evening News. Waume wanalaumiwa kwa kutokuwa na huruma, kutotoa faraja wakati ilihitajiwa, na zaidi ya yote, kwa kujaribu kujiokoa peke yao. Mke mmoja “alishtuka kwamba mume wake alikula vitumbua vyote walivyopewa [vikiwa ugavi wa kutuliza], bila kumwachia chochote,” charipoti Hyogo Prefecture Women’s Center. Mke mwingine aliambia kitovu hicho hivi: “Nilipoteza tumaini lote katika mume wangu baada ya yeye kuita majina ya watoto wetu bila kutaja langu.” Hata hivyo, kitovu hicho kiliongeza kwamba karibu idadi iyo hiyo wasema kwamba mahusiano yao yaliimarishwa na tetemeko hilo.
Kurudi kwa Waliokaribia Kutoweka
“Muujiza wa Italia”—kulingana na gazeti la habari la Milan Corriere della Sera, ndivyo watu fulani wanavyofafanua jinsi aina kadhaa za wanyama zimerudi kutoka ukingo wa utoweko. Sababu hasa ikiwa maeneo yaliyolindwa katika Alps na Apennines, wanyama kama vile paa, chamoisi, paa aina ya fallow, na paa aina ya roe wanaongezeka Italia. Mbwamwitu wa Apennines, ambaye idadi yake inaongezeka sana, sasa anaenea kutoka Italia kuingia French Maritime Alps. Hata hivyo, bado kuna aina zilizo hatarini, kama vile fisi-maji, na sili-mtawa, lakini wataalamu wanasadiki kwamba programu zinazochukuliwa kwa uzito za uhifadhi “haziwezi kukosa kuleta matokeo mazuri, ya kweli na yenye kudumu,” lasema Corriere della Sera.
Koti Murua la Wakati wa Kipupwe
Wanasayansi wanaojaribu kutazama dubu wa barafuni kutoka kwenye ndege wanapata magumu sana—si kwa sababu tu iliyo wazi kwamba dubu hao ni weupe na hukaa kwenye ncha za barafu. Kulingana na Popular Science, wanasayansi walikuwa na kile kilichoonekana kuwa suluhisho la werevu kwa tatizo hilo: walitumia ukanda mnyetivu wa filamu wa mialekundu isiyoonekana, wakisababu kwamba ingekuwa rahisi kutambua joto la mwili linalotoka kwenye wanyama hawa wakubwa mno. Lakini ukanda huo wa filamu ulitokea ukiwa bila chochote! Yaonekana kwamba koti la dubu wa barafuni ni kihami chenye matokeo sana hivi kwamba hakuna joto linalotoka kwa mnyama huyo. Gazeti hilo laonelea pia kwamba manyoya ya koti hilo yaonekana ni mazuri kwa kupitisha miale kiukaurujuani ya jua, zikiivuta ndani kwa kile kiwezacho kuitwa “seli-jua” ndani ya dubu ambazo kwa njia fulani huweza kubadili nuru hiyo kuwa joto.
Mashabiki Wanaozimia
Kwa nini mashabiki wengi mno huzimia kwenye maonyesho ya roki? Mwananurolojia kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu katika Berlin, Ujerumani, alichunguza jambo hilo hivi majuzi. Kwenye wonyesho mmoja wa roki huko Berlin uliohudhuriwa hasa na wanawake wachanga, wapatao 400 hivi walizimia wakati wa wonyesho huo. Kulingana na gazeti Discover, mwananurolojia huyo alipata kwamba asilimia 90 ya waliozimia walikuwa wamesimama katika safu za mbele. Ili kupata viti katika safu za mbele, wasichana hao walingoja kwa saa nyingi katika milolongo mirefu, na wengi hawakuwa wamekula au kulala usiku uliotangulia. Sababu nyinginezo—kupiga yowe kwao wenyewe na kusukumwa na umati kutoka nyuma—kuliweka msongo kifuani, jambo ambalo lilipunguza kanieneo ya damu. Hilo lilinyima ubongo ugavi wao wa damu. Kuzimia kukafuata. Ingawa mwananurolojia huyo alidokeza kwamba mashabiki wa roki wale na kulala kimbele, kubaki wakiwa wameketi, na kubaki kimya na mbali kutoka kwa umati wakati wa maonyesho, yeye alikubali kwamba ni mashabiki matineja wachache ambao yaelekea wangekubali kufanya hivyo.
Uyaya Usio na Malipo?
Wazazi wa mitaani wenye matatizo wamepata suluhisho la kufanya watu wengine waangalie watoto wao ili wawe huru kufanya ununuzi. Wao huacha watoto wao katika duka la kuuza vichezeo au duka lenye makompyuta mengi. Watoto, ambao huvutiwa na mashine hizo za tekinolojia ya hali ya juu, hucheza na violezo vya maonyesho hadi wazazi wao wanaporudi. Ingawa hivyo, haishangazi kwamba wauzaji hawafurahishwi na tabia hiyo, laripoti gazeti Newsweek. Wanalalamika kwamba watoto huzuia watu wawezao kuwa wateja kuona violezo vya maonyesho; na vibaya zaidi, huvivunja. Wengine wamepata kwamba wazazi fulani hurudi na kulalamika ikiwa hakuna mtu aliyeangalia watoto wao au kuwapeleka chooni! Hivyo, maduka fulani yanapigana na tabia hiyo—ama kwa kuweka mbali kompyuta za maonyesho ama kwa kuita walinzi wakipata watoto ambao hawana mtu wa kuwaangalia.
Vilima vya Mchanga Hatarini
“Israeli inaishiwa na mchanga.” Ndivyo lilivyoripoti gazeti New Scientist hivi majuzi. Kwa nini upungufu huo ambao usiopaswa kutukia? Naam, mchanga ni kichanganyiko kikuu cha saruji, ambacho biashara yenye kusitawi ya ujenzi ya nchi hiyo inahitaji sana. Kwa hiyo, kwa miaka 30 iliyopita, kukiwa na usimamizi mdogo sana wa serikali, wajenzi wamekuwa wakisomba mchanga kwa malori kutoka fungu kubwa kupita yote ya mchanga katika Israeli, ambalo wakati mmoja lilienea kutoka Jaffa hadi Gaza. Na wevi huiba mamilioni ya tani za mchanga kila mwaka ili kuyauza kwenye biashara isiyo halali. Wanaekolojia wana wasiwasi kwamba mazingira yanayopungua na yaliyo rahisi kuharibika ya vilima vya mchanga, ambavyo kwavyo aina chache za mimea na wanyama hutegemea ili kusalimika, yanaharibiwa. Na wajenzi wanaanza kushangaa mahali ambapo mchanga wao utatoka wakati ugavi wa Israeli utakapokwisha.
Afya ya Wajapani Yapatwa na Uvutano wa Magharibi
Watu wa Japani wana muda wa kuishi mrefu zaidi kupita wote ulimwenguni, lakini uvutano wa mitindo-maisha ya Magharibi huenda ukawa unazorotesha hali hiyo. New Scientist liliripoti hivi majuzi kwamba kati ya watu milioni 2.1 waliofanyiwa uchunguzi wa mwili katika 1994, ni asilimia 18 pekee waliopatikana kuwa na afya nzuri. Miaka kumi mapema, tarakimu hiyo ilikuwa asilimia 30. Kulingana na mmoja wa watungaji wa ripoti fulani ya Japan Hospital Association, kisababishi ni kiwango cha juu cha mafuta na kolesteroli katika vyakula vya Kimagharibi, pamoja na ongezeko katika uvutaji sigareti na utumizi wa alkoholi. Upungufu mkubwa zaidi wa afya ulionekana katika maeneo yaliyoendelea sana kiviwanda, kama vile eneo la Osaka na Kobe. Kwa kutofautisha, maeneo yenye afya zaidi ni kaskazini, katika sehemu za mashambani za kisiwa cha Hokkaido.
Mahali Unakoenda Wakati
Wakati umeenda wapi? Wengi huuliza swali hilo bila kutazamia jibu, lakini uchunguzi hivi majuzi ulijaribu kulijibu kisayansi. Shirika la utafiti katika Illinois, Marekani, lilifanya uchunguzi wa miaka mitatu wa utendaji wa kila siku wa watu wapatao 3,000 ambao waliombwa waweke rekodi zenye kuendelea za jinsi walivyotumia wakati wao. Kikundi hicho kilikuwa kuanzia umri wa miaka 18 hadi 90 na kutoka malezi tofauti-tofauti. Mtumizi mkuu wa wakati alikuwa usingizi. Huo ulifuatiwa na kazi, ambayo ilichukua wastani wa dakika 184 kwa siku. Kutazama televisheni na vidio kukafuata, kukiwa na dakika 154. Kazi ndogo-ndogo za nyumbani zilichukua dakika 66, kusafiri 51, kujipamba 49, na utunzaji wa watoto na wanyama-rafiki 25. Karibu na chini ya orodha hiyo kulikuwa ibada, ambayo ilichukua wastani wa dakika 15 kwa siku.
Makanisa Zaidi Yauzwa
Waweka rasilimali wanakimbilia kupata majengo ya kanisa yatumiwayo mara chache sana katika jimbo kuu la kaskazini mwa Australia la Brisbane katika Queensland, kulingana na maajenti wa mashamba. Mambo mawili yanasemwa kuwa yenye kusababisha hilo: uhudhuriaji wa kanisani wenye kupungua na tamaa ya waweka rasilimali ya kununua “kitu fulani cha kipekee.” Gazeti la habari The Courier-Mail laripoti kwamba kwa wakati huu makanisa 12 yanatolewa ili kuuzwa na kwamba mengine tayari yamegeuzwa kuwa nyumba na ofisi katika Brisbane. Gazeti hilo la habari lilimnukuu mkurugenzi wa mauzo akisema: “[Makanisa] machache kadiri fulani yametumiwa kuwa mikahawa, majumba ya maonyesho ya vitu vya sanaa, stoo za kuwekea vitu vya kale, maofisi, au makao.” Ajenti wa mashamba alisema: “Natamani ningekuwa na mengine zaidi ya kuuza.”
Kufanywa Kuwa ya Kilimwengu Kabisa
Jimbo la Ujerumani la Bavaria ni lenye kufuata kwa imara Ukatoliki wa Kiroma. Kwa hakika, maagizo ya shule ya Bavaria hufanya liwe jambo la lazima kwamba kisalaba kiwekwe katika kila darasa katika shule zote za serikali. Hata hivyo, Mahakama ya Kikatiba ya Serikali sasa imetangaza kwamba agizo hilo halifai kwa sababu halipatani na Sheria ya Msingi ya Ujerumani, ambayo huhakikisha uhuru wa dini, laripoti Süddeutsche Zeitung, gazeti la habari la Ujerumani. “Siku yenye kuhuzunisha katika historia ya watu wetu,” akahuzunika Askofu mkuu Meisner wa Cologne, kulingana na Westfälische Allgemeine Zeitung. Watu wengine walishangazwa zaidi na utofautiano huo kuliko na uamuzi wenyewe. Kwa vyovyote, jamii ya Ujerumani “imefanywa kuwa ya kilimwengu kabisa,” likaandika gazeti la Hamburg Die Zeit, nayo “hutoa kicho kwa ufuatiaji wa vitu vya kimwili, ukuzaji wa mapendezi ya watumizi, na utambuzi kamili wa kibinafsi.”