Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Wanawake wa India Nilithamini ile makala “Wanawake wa India—Wakisonga Kuingia Katika Karne ya 21.” (Julai 22, 1995) Sikuzote nimeiona India kuwa yenye kuvutia sana, kwa kuwa ina utamaduni ulio tofauti sana na ule wa nchi yangu. Makala yenu ilionyesha kwamba uhuru wa kweli kwa mwanamke wa India utapatikana chini ya Ufalme wa Mungu. Natarajia wakati ambapo wanawake wote watapendwa kikweli na kuthaminiwa na waume wawastahio.
W. S., British Columbia
Akataliwa na Familia Mimi nina umri wa miaka 14, nami naandika ili kuwashukuru kwa ajili ya makala “Familia Iliyonipenda Kikweli.” (Julai 22, 1995) Iliitia nguvu imani yangu kwelikweli. Udom Udoh ni mfano mzuri kwa vijana kotekote. Yeye alionyesha kwamba mtu anaweza kuitetea kweli hata katika umri mchanga sana.
A. M., Marekani
Sawa na Udom, mara tu nilipoanza kujifunza Neno la Mungu, upinzani ukaanza kunipata. Mimi pia nilifukuzwa nyumbani. Baada ya kunyanyaswa sana kwa maneno na kimwili, niliondoka nyumbani. Nilitunzwa kwa fadhili na mzee wa kutaniko na mke wake. Makala yenu ilinitia nguvu sana. Ni furaha kama nini kuwa sehemu ya familia hii ya tufeni kote ya kipekee!
L. J., Marekani
Kuwa Rafiki ya Mungu Asanteni sana kwa ajili ya ile makala “Vijana Huuliza . . . Je, Naweza kwa Kweli Kuwa Rafiki ya Mungu?” (Julai 22, 1995) Ilinitosha machozi. Nina umri wa miaka 13 nami tayari nimefanya mambo kadhaa yaliyo mabaya sana. Wengine walijaribu kunitia moyo, lakini bado ikawa vigumu kwangu kusali kwa Yehova. Nilifikiri hanipendi kamwe kwa sababu ya makosa yangu mengi. Makala hii ilionyesha kwamba Mungu husamehe na kwamba naweza kumwendea kwa sala.
J. D., Ujerumani
Sawa na Doris, aliyenukuliwa katika hiyo makala, nilihisi kwamba sistahili kuwa rafiki ya Mungu. Namshukuru Yehova kwa kuniandalia usaidizi huu. Umenisaidia kuelewa kwamba nikitubu matendo yangu mabaya, yeye yuko tayari kunisamehe na kuwa Rafiki yangu. Ni matumaini yangu kwamba hamtaacha kuchapa makala hizi kwa ajili ya vijana.
B. M. A., Hispania
Komahedhi Sisi tuna kampuni ya madawa na hasa madawa ya magonjwa ya wanawake. Tuliona ile makala juu ya komahedhi yenye kichwa “Kupata Uelewevu Mzuri Zaidi” (Februari 22, 1995) kuwa yenye kupendeza zaidi sana kwetu sisi, nasi twafurahi kwamba mlishughulikia habari hii. Hata hivyo, kile kisanduku “Namna Gani Tiba ya Kurudisha Estrojeni?” chasema kwamba “kuongeza projesteroni kwenye utaratibu wa kurudisha homoni . . . hupinga matokeo yenye manufaa ya estrojeni dhidi ya ugonjwa wa moyo.” Hili si kweli nyakati zote, hasa kuhusu projesteroni za kiasili.
Dakt. T. W. na J. K., Ujerumani
Asanteni kwa kutupa habari za karibuni zaidi. Ingawa vyanzo mbalimbali vya zamani vilionyesha kwamba projesteroni zinaweza kupunguza viwango vya HDL au kolesteroli “njema”, na hivyo zikiongeza hatari ya ugonjwa wa moyo, utafiti wa karibuni zaidi huonyesha tofauti. Uchunguzi wa karibuni ulioripotiwa kwenye toleo la Januari 18, 1995, la “JAMA” hudai kwamba “estrojeni peke yake au ikiwa imechanganywa na projesteroni fulani huboresha [viwango vya kolesteroli “njema”].” Hakuna shaka kwamba utafiti zaidi utafanywa kabla ya athari zote za muda mrefu za matibabu ya homoni hazijaeleweka kikamili.—Mhariri.
Mageuzi Nimemaliza tu kusoma ule mfululizo “Nadharia Ambayo Ilishangaza Ulimwengu—Matokeo Yayo Ni Yapi?” (Agosti 8, 1995) Itikio langu? Nilikuwa zaidi ya kufurahishwa. Nilivutiwa sana! Hiyo makala iliandikwa kwa njia yenye kupendeza sana, na yenye kufahamika sana. Kila nukuu lilionyesha utafiti mkubwa. Zaidi ya yote, ilionyesha wazi matokeo halisi ya fundisho la mageuzi katika akili ya mwanadamu. Sikujua kamwe jambo hilo! Kuna uhitaji mkubwa ulimwenguni wa habari za kusomwa zifaazo, lakini ninyi mmeutosheleza vizuri uhitaji huo.
R. H., Marekani