Wale Nzi Wachukizao—Wenye Faida Kuliko Ufikirivyo?
WENGI wetu huwaona nzi kuwa wasumbufu au hatari ya moja kwa moja kwa jamii. Lakini wanabiolojia wanaendelea kugundua kwamba nzi, licha ya usumbufu wao, wana faida kuliko tuwezavyo kufikiri.
Aina nyingi za nzi hutumia muda mwingi zikitembelea maua, yenye chakula kingi na yanayowatolea wadudu walio wateja wayo asalimaua na chavuo. Baadhi ya nzi wanaoweza kuzidua chakula kutoka kwa chavuo—kwa kufanikiwa—hutegemea chakula hiki kinachotoa nguvu nyingi ili kukuza mayai yao.
Wanapotembelea kila ua, nzi hawawezi kuepuka kuchukua chembe fulani za chavuo zinazonata, ambazo hujishikilia kwenye miili yao. Nzi mmoja aliyechunguzwa kwa uangalifu alikuwa na chembe 1,200 za chavuo katika mwili wake! Kadiri uchunguzi zaidi umefanywa juu ya fungu la nzi katika uchavushaji, ndivyo wanasayansi wamegundua kwamba maua fulani hutegemea nzi hao ili kuendelea kuweko.
Gazeti Natural History hueleza mfululizo wa majaribio yaliyofanywa Colorado, Amerika Kaskazini. Nzi wa kawaida, wanaofanana na wale wa nyumbani, walipakwa rangi zing’aazo ili waonekane kwa urahisi. Baada ya kuchunguza utendaji wao wa siku kwa siku, watafiti walishangaa kugundua kwamba kwa maua fulani ya mwituni nzi walikuwa wachavushaji wenye sehemu ya maana kuliko nyuki nao walikuwa na mweneo mkubwa kushinda ule wa nyuki.
Kazi ya nzi ina umaana kiasi gani? Maua kadhaa yalifunikwa kwa wavu ili yasiweze kutembelewa na wadudu. Maua hayo hayakukuza mbegu zozote—yakitofautiana sana na yale yenye kuzaa sana yaliyo karibu yaliyochavushwa na nzi. Ingawa baadhi ya maua yalichavushwa kwa kiwango kikubwa na nyuki, katika visa vya aina fulani kama vile flaksi-mwitu au jeraniamu, katika mwinuko wa kiasi fulani nzi walifanya zaidi ya asilimia 90 ya kazi hiyo.
Wawili kati ya watafiti hao, Carol Kearns na David Inouye, walifikia mkataa gani? “Kwa ajili ya maua mengi ya mwituni katika Colorado Rockies, basi, nzi huwashinda nyuki, vipepeo, na ndege-wavumi . . . Bila wadudu hawa, ambao watu wengi hawapendezwi nao, mengi ya maua-mwitu ambayo hufanya kutembelea mashamba ya alpine kuwe kwenye kupendeza sana yangeshindwa kutokeza mbegu.” Hakuna shaka juu ya hilo, kwamba nzi ni wenye faida!