Vijana Huuliza . . .
Ugoro—Je, Hauwezi Kudhuru?
‘CORD mwenye umri wa miaka 13 alipohamia magharibi ya kati mwa Marekani, upesi alitambua kuwa alikosa kitu fulani walichopaswa kuwa nacho vijana wote wa darasa la nane: kikebe cha ugoro, aina ya tumbaku isiyo ya kuvutwa. Wengi wa rafiki zake wapya walikuwa “wachovyaji,” au watumia ugoro, naye Cord alitaka kukubaliwa na wenzake. Hivyo mmoja wa hao vijana alipompa paketi ndogo ya ugoro, aliichukua na kuweka kiasi fulani cha ugoro kati ya mdomo wa chini na ufizi kwa urahisi kama mzoefu.’—Gazeti Listen.
Cord mchanga si wa pekee. Dakt. Christopher A. Squier, profesa wa maradhi ya kinywa, asema kwamba idadi inayoongezeka ya matineja wa kiume yaanza kuutumia. Ingawa mauzo ya ugoro yalikuwa yakipungua mwishoni mwa miaka ya 1980, “matumizi ya ugoro mnyevu,” asema Dakt. Squier, “yaongezeka tena.”a Kwa kielelezo, watafiti waripoti kwamba 1 kati ya wanafunzi wa kiume 5 wa shule ya sekondari katika Marekani na 1 kati ya vijana wa kiume 3 katika Sweden—mamilioni ya vijana—sasa hutumia ugoro. Kwa nini hili lafanyika?
“Ni salama kuliko kuvuta sigareti.” “Hakuna uthibitisho wowote kuwa ni hatari.” “Rafiki zangu huutumia. Hauwadhuru.” “Kiasi fulani mara kwa mara hakitanidhuru.” “Hakuna yeyote amepata kufa kutokana nao.” Kulingana na Sosaiti ya Kansa ya Marekani, hizo ni baadhi ya sababu za kuanza kutumia ugoro watoazo vijana mara nyingi.
Ni nini kimefanya vijana wafikiri kuchovya ni salama kuliko kuvuta sigareti? Je, kweli ndivyo mambo yalivyo?
Kuuitikia Ujumbe
Kwa miaka mingi biashara kubwa ya tumbaku imeshambulia vijana kwa matangazo ya biashara yanayoonyesha kuwa ugoro ulikuwa hauna madhara kama isivyo na madhara peremende ya kutafuna, na kuwa nao ni kwa lazima kama kuwa na viatu vya michezo. Misemo kama vile “Twaa paketi ya ugoro badala ya sigareti,” “Mimi hufurahia tumbaku kwelikweli bila hata kuiwasha,” na “Kiasi kidogo tu chatosha” kwa werevu ilidokeza kuwa ugoro ni bora kuliko sigareti.
Baada ya misemo kama hiyo ya televisheni na redio kupigwa marufuku Marekani, biashara ya tumbaku iliendelea kutangaza kupitia magazeti. Picha zenye kupendeza za watu wenye nguvu wakifurahia uwindaji, kupanda miamba, wanaoshinda katika maporomoko ya maji kwa kutumia chelezo—kikebe cha tumbaku kikiwa kimepachikwa katika mifuko yao ya nyuma kwa njia kiwezacho kuonekana—zilitoa ujumbe wenye kusikika ulio wazi: “Ugoro wapendeza, ni wa asili, na kuutumia ni njia ya kuwa mwanamume!”
Ripoti ya 1994 ya ofisa mkuu wa afya wa Marekani, yenye kichwa Preventing Tobacco Use Among Young People, yasema kwamba vijana wengi sasa waamini kwamba “bidhaa za ugoro ni salama na zakubalika kijamii.” Uchunguzi mmoja kati ya wanafunzi wa shule za sekondari ulionyesha kwamba “asilimia 60 ya watumiaji wa ugoro wa gredi ya 7 hadi 9 na asilimia 40 ya wale wa gredi ya 10 hadi 12 waliamini kwamba hakukuwa na hatari yoyote au hatari kidogo tu katika utumiaji wa ugoro kwa ukawaida.” Hata wanaoutumia katika shule ya sekondari watambuao kuwa ugoro waweza kuwa hatari “hawaoni hatari kuwa kubwa.” Matangazo ya biashara yafaulu kuwasilisha ujumbe wayo. Lakini je, hayo matangazo ya biashara yasema kweli?
Mithali ya Biblia husema: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” Au kama mithali nyingine isemavyo, “kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa.” (Mithali 13:16; 14:15, italiki ni zetu.) Hivyo basi, mambo ya hakika huonyesha nini juu ya ugoro?
Habari Mbaya
Ingawa huenda matangazo ya biashara yakadokeza kwamba kutumia ugoro kutaboresha mtazamo wa wengine kukuelekea na kwamba ni salama kwa mwili wako, mambo ya hakika yaonyesha hali tofauti kabisa. Kwanza, kutumia ugoro hakutakufanya uonekane vizuri zaidi. Ikiwa huamini hilo, tia ulimi wako katikati ya shavu na ufizi na uutazame kwenye kioo. Je, ni “poa”? Sivyo hata kidogo. Na ndivyo uathirivyo sura yako! Yale ugoro hukufanyia kwa ndani ni mabaya hata zaidi.
Kwa kielelezo, wale watafunao au kuchovya ugoro waweza kupasuka midomo, kubadili rangi ya meno, kunuka mdomo, na kupata maumivu ya fizi—hakuna lolote la kufurahiwa. Kwa kuongezea, uwezo wao wa kuonja na kunusa hupungua huku mpigo wa moyo na kanieneo ya damu ikiongezeka—kwa kweli ni habari mbaya. Hata hivyo, habari mbaya kwelikweli ni kwamba uchunguzi mbalimbali uliofanywa Ulaya, India, na Marekani waonyesha kwamba ugoro husababisha kansa kwenye mashavu, fizi, na koo. Ugunduzi huu mbalimbali haushangazi wenye ujuzi. Uchunguzi mmoja ulionyesha: “Ugoro una kiwango cha juu zaidi cha visababishi vya kansa vya bidhaa zozote zinazoingizwa mwilini.” Si ajabu kwamba “watumiaji wa ugoro wa muda mrefu wamo hatarini ya kupata kansa ya midomo kuliko wasioutumia kwa asilimia 50.”
Mtu apatapo kansa ya midomo, matokeo huwa mabaya sana. Si kwamba afya yake huzorota tu bali pia uhai wake hukatizwa. Kichapo kutoka kwa Sosaiti ya Kansa ya Marekani husimulia hadithi hii yenye kuhuzunisha: ‘Sean alianza kutumia ugoro akiwa na umri wa miaka 13. Aliona kuwa ulikuwa salama kuliko kuvuta sigareti. Baada ya miaka mitano ya kuchovya kikebe kizima au zaidi kwa siku, alianza kuwa na maumivu kwenye ulimi wake. Hiyo ilikuwa kansa ya mdomo. Madaktari waliondoa kisehemu cha ulimi wake, lakini hiyo kansa ikaenea hadi kwenye shingo yake. Upasuaji zaidi ulioharibu sura yake ukafanywa lakini bila mafanikio yoyote—alipokuwa na umri wa miaka 19 akafa. Kabla ya kifo chake Sean aliandika ujumbe sahili katika karatasi za kuandikia: “Usichovye ugoro.”’
Kuwa Mraibu!
Baada ya Cord mchanga, aliyetajwa mwanzoni, kusoma masimulizi haya yenye kushtua juu ya Sean, hatimaye akaelewa wazi lililohusika. Akaamua kuacha. Hata hivyo, kujaribu kuacha kulikuwa kugumu. “Nahisi ni lazima niutumie,” Cord akaeleza gazeti Listen. “Hata sasa, miezi kadhaa baada ya kuacha, bado hujikuta nikitafuta kikebe mfukoni mwangu. Mimi hutafuna peremende nyingi. Huko husaidia, lakini hakuondoi ile tamaa.”
Jarida Ca-A Cancer Journal for Clinicians huhakikisha hivi: “Katika kuwachunguza matineja waliojaribu kuacha kutumia ugoro, ni wachache tu waliofaulu.” Hata hivyo, ni nini hufanya iwe vigumu kuacha kutumia ugoro? Ni kile kile kifanyacho iwe vigumu kuacha kuvuta sigareti: nikotini.
Nikotini, dawa ya kulevya ipatikanayo kwenye sigareti na vilevile kwenye ugoro, ina sumu imsisimuayo mtumiaji. Kila dakika 30 hivi, mtumiaji huhitaji kuchovya tena ili kuendeleza hisia hiyo. Nikotini hukufanya uwe mraibu. Baadhi ya watumiaji huwa waraibu sana hivi kwamba wao huweka ugoro kidogo mdomoni mwao mchana na usiku—hata walalapo.
Tofauti na wafikirivyo vijana, kuchovya hakupunguzi kiasi cha nikotini kinachoingia mwilini. Kikebe kimoja cha ugoro kwa siku huingiza nikotini ya kiwango sawa na sigareti 60! “Watumiaji wa ugoro,” ikaonyesha Preventing Tobacco Use Among Young People, ‘huingiza angalau kiasi kilekile cha nikotini kama waingizacho wavutaji wa sigareti—labda hata mara mbili ya hicho kiasi.’ (Italiki ni zetu.) Zaidi ya nikotini, ugoro una visababishi vya kansa vyenye nguvu vilivyo mara kumi kwa wingi kuliko sigareti.
Uwe na Hekima
“Hakuna shaka lolote kuwa hizo ni bidhaa zenye madhara,” akasema Dakt. Roy Sessions, mpasuaji wa kichwa na shingo. “Hizo hutokeza hisia ya kuzitegemea ionwayo na wengi kuwa ngumu kuvunja kuliko kuvuta sigareti.” Mtaalamu wa kansa ya mdomo Dakt. Oscar Guerra alifikia mkataa huu: “Mwili haukubali kitu hicho.” Wastadi ulimwenguni pote hukubali: Kuchovya tumbaku kidogo ni zaidi ya matatizo kidogo. Kwaweza kukuua.
Zaidi ya kuhangaikia afya yao vijana Wakristo wana sababu yenye nguvu hata zaidi ya kuepuka bidhaa za tumbaku—tamaa yao ya kumpendeza Yehova Mungu. Neno lake huamuru: “Na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”—2 Wakorintho 7:1.
Gazeti Aviation, Space, and Environmental Medicine latoa muhtasari mzuri, kwa kusema: “Tumbaku ni mmea uchukizao utumiwao na viumbe wawili tu—buu mdogo wa kijani-kibichi na mwanadamu. Buu mdogo wa kijani-kibichi hana ujuzi alio nao mwanadamu.”
Lakini wewe unao. Hivyo uwe na hekima—usianze kutumia tumbaku.
[Maelezo ya Chini]
a Aina mbili za tumbaku isiyo ya kuvuta hutumiwa na wengi: ugoro na ile ya kutafuna. Kuna ugoro mkavu na mnyevu. Kati ya vijana, ugoro mnyevu—tumbaku iliyokatwa vipande vidogo-vidogo na kuchanganywa na peremende, viungo vyenye ladha na vyenye manukato, katika mkebe au paketi kama ile ya chai—ndiyo aina ya ugoro ipendwayo sana. “Kuchovya” hurejezea kuweka kiasi kidogo cha tumbaku katikati ya mdomo au shavu na ufizi.
[Blabu katika ukurasa wa 27]
‘Kabla ya kufa, Sean aliandika ujumbe sahili: “Usichovye ugoro”’
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kutafuna tumbaku kumeanza kuongezeka kati ya vijana. Je, wewe wapaswa kujaribu?