Kuutzama Ulimwengu
Viwango vya Kifo Vyapanda kwa Wanawake Wavutao Sigareti
Uchunguzi wa hivi majuzi uliotangazwa katika The Canadian Journal of Public Health wapata kwamba vifo vinavyohusiana na uvutaji wa sigareti miongoni mwa wanawake Wakanada viliongezeka kutoka 9,009 katika 1985 hadi 13,541 katika 1991. Uchunguzi huo hukadiria kwamba wanawake zaidi kuliko wanaume watakufa likiwa tokeo la uvutaji kufikia mwaka 2010 ikiwa mielekeo ya sasa itaendelea. Katika 1991, kulikuwa na vifo vinavyokadiriwa kuwa 41,408 vilivyosababishwa na uvutaji wa sigareti (wanaume 27,867 na wanawake 13,541), kulingana na gazeti The Toronto Star. Katika Marekani, vifo vya kansa ya mapafu miongoni mwa wanawake wavutao sigareti vimeongezeka mara sita kati ya miaka ya 1960 na 1980, asema Dakt. Michael Thun wa Shirika la Kansa la Marekani. Watafiti wafikia mkataa kwamba “uvutaji wa sigareti wabaki ukiwa kisababishi kikuu zaidi kiwezacho kuzuiwa cha kifo cha mapema katika Marekani,” laripoti gazeti The Globe and Mail la Toronto, Kanada.
Dawa za Kulevya Katika Shule za Ujerumani
Uchunguzi miongoni mwa zaidi ya wanafunzi 3,000 katika kaskazini mwa Ujerumani wafunua utumizi ulioenea sana wa vitu vyenye kuraibisha shuleni. Kulingana na gazeti la habari la kila juma Focus, karibu nusu ya wanafunzi wenye umri wa miaka 17 wametumia wenyewe dawa zisizo halali, na zaidi ya thuluthi wanatumia wakati huu. Profesa Peter Struck alieleza kwamba “kwenye shule nyingi za sekondari katika Hamburg, unapata wanafunzi wa shule wenye umri wa miaka 16 au 17 ambao hubadilishana daima kati ya kutumia visisimuaji na vitulizaji.” Lakini kwa nini utumizi wa dawa za kulevya umeenea sana? Profesa Klaus Hurrelmann alitoa sababu tatu za utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana: Kuchoshwa na maisha, hisia ya kutotambuliwa kwa matimizo ya kibinafsi, na msongo wa marika.
Wasafiri Wenye Kutazamisha
Ndege aina ya alibatrosi alipuruka kilometa 26,000 kwa siku 72, na sili-kijivu aliogelea kilometa 5,000 kwa miezi mitatu. Wanasayansi wa kuhifadhi waligundua uvumilivu huu wenye kushangaza baada ya kuweka transmita ndogo mno za redio kwa alibatrosi na sili walioteuliwa ili kufuatia mwendo wao kwa satelaiti. Katika pindi moja alibatrosi alipuruka kwa karibu kilometa 3,000 kwa siku nne kuvuka Bahari kuu ya Pasifiki ya Kusini. Sili aliogelea kwa hadi kilometa 100 kwa siku moja kati ya Scotland na Visiwa vya Faeroe akionyesha uwezo wenye kushangaza wa kujielekeza kuvuka bahari wazi, laonelea gazeti The Times la London. Ni nini kilichochochea safari hizo ndefu? Utafutaji wa chakula, yasema hiyo ripoti.
“Shirika la Ulimwengu Lisilo na Utu wa Kutosha”
“Kwa siku tatu juma lililopita, viongozi kutoka kila kontinenti walikutana kwenye karamu ya mwaka wa 50 wa kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ili kutoa hotuba zenye fahari kuhusu hali ya ulimwengu,” likaripoti The New York Times Oktoba uliopita. Hata hivyo, kwa wazi, kichanganyiko kimoja cha maana kilikosekana katika ‘hotuba kadhaa zenye fahari’—moyo wa kufuatia haki. “Sawa na wanasiasa kila mahali,” likasema Times, “walitoa ahadi ambazo hawatatimiza na kumlaumu mtu mwingine kwa mapungukio yao.” Baada ya kunukuu viongozi wa kitaifa wanane ambao maneno yao yalipingana na matendo ya nchi zao, gazeti hilo la habari lilimalizia ujumbe wao wenye kupita kiasi kuwa: “Ulimwengu; sahau ninachotenda, sikiliza ninachosema.” Si ajabu kwamba jarida U.S.News & World Report liliita Umoja wa Mataifa “shirika la ulimwengu lisilo na utu wa kutosha.”
Nyuki-Asali Wenye Halijoto ya Juu
Nyuki-asali wa Japani hujilinda dhidi ya shambulizi kutokana na nyigu-jitu kwa kumwua kwa joto la mwili wao, laripoti Science News. Baada ya kugundua kuwapo kwa nyigu, nyuki-asali hao humshawishi adui huyo kuingia ndani ya kiota, ambamo mamia ya wafanyakazi humzingira na kumfunika. Kisha, “nyuki hao huvuma na kupandisha halijoto ya kikundi hicho hadi kufikia digrii zenye kufisha 47 Selsiasi kwa muda wa dakika 20 hivi,” laonelea gazeti hilo. Kwa kuwa nyuki-asali wa Japani wanaweza kuvumilia joto hadi digrii 50 Selsiasi, mbinu hii haiwadhuru. Hata hivyo, si manyigu wote hunaswa na nyuki-asali. “Kwa kuwa manyigu 20 hadi 30 wanaweza kuua milki ya nyuki 30,000 kwa muda wa saa tatu,” manyigu-jitu wanaweza kushinda nyuki-asali kwa kuwashambulia wakiwa wengi. “Katika visa hivi,” lasema News, “wao huteka kiota na kukusanya mabuu na viluwiluwi vya nyuki.”
Msalaba —Kifananisho cha Jeuri?
Wanatheolojia fulani wanatilia shaka kufaa kwa msalaba kuwa kifananisho cha Ukristo kwa sababu ya ushirika wao wenye jeuri, laripoti The Dallas Morning News. Wanatheolojia hao wanatia moyo utumizi wa mifano inayoonyesha uhai wa Yesu badala ya kifo chake. Msalaba “huchochea ibada ya kifo,” akasema mwanatheolojia Catherine Keller wa Shule ya Theolojia ya Chuo Kikuu cha Drew katika Madison, New Jersey, Marekani. “Hakuna mtu angetaka kiti cha umeme cha kunyongea, au kitanzi kuwa ishara ya imani, lakini hicho ndicho tungekuwa tukitumia ikiwa Yesu angeuawa na serikali leo.”
Viroboto-Maji Watoa Msaada
Kiroboto-maji aliye duni aweza kutoa suluhisho kwa tatizo la vipito vya majini vya barani vyenye uchafuzi, laripoti gazeti la habari la London Independent. Hilo laonyeshwa na mradi wa urudishaji unaoendelea. Kwanza, wanabiolojia walitoa tani 9.5 za samaki walao viroboto-maji kutoka mto mkubwa wa Ormesby katika Norfolk, Uingereza. Hilo liliruhusu viroboto hao waongezeke na kumeza mwani uliokuwa ukichafua ziwa hilo. Kisha mimea mingine ikachipuka chini ya maji kutoka mbegu zilizokuwa bwete, na ndege, kama vile kuti na bata-wakuu, wakarudi. Hatimaye, samaki watarudishwa, na yakadiriwa kwamba mazingira yote yatarudia hali ya kawaida kwa kipindi cha miaka mitano. Wahifadhi katika Ulaya wanatazama matokeo ya mradi huu kwa upendezi.
Kuepuka Suala la Dhambi
“Nini kilichopata dhambi?” lauliza gazeti Newsweek. “Hisi muhimu ya dhambi ya kibinafsi karibu imepotea katika mtindo wa sasa wa kutazamia mazuri katika dini za Marekani.” Wanaparishi “hawataki kusikia mahubiri ambayo huudhi hali yao ya kujiheshimu,” na miongoni mwa Wakatoliki “kuungama kwa kawaida mbele ya kasisi kumekuwa kawaida ya wakati uliopita.” Makasisi wanaojitahidi kudumisha vyeo wanaogopa kutenganisha makundi yao. Wengi “kwa kawaida hushutumu maovu ya ‘kawaida’ ya kijamii kama vile ubaguzi wa kijamii na wa kijinsia,” makala hiyo yataarifu. “Lakini hawatoi sauti kuhusu habari zinazoathiri watu kibinafsi—kama vile talaka, kiburi, pupa, na kujitakia makuu kwa umbelembele.”
“Alama za Vidole” za Vito
Wanawake wa Uingereza wana vito vya almasi milioni 39 vinavyogharimu dola bilioni 17.5, na kila mwaka vitu vinavyogharimu dola milioni 450 huibwa. Vito vingi vinavyopotea kwa njia hii haviwezi kufuatilika. Metali ambapo almasi huwekwa huyeyushwa mara moja. Kisha vito hivyo huundwa upya. Hata hivyo, sasa wakifanya kazi kupitia kompyuta kuu, wauza vito wataweza kuingiza katika kumbukumbu la kompyuta kasoro za kipekee za kila kito. Hizi “alama za vidole” hutambuliwa na mwangaza wa leza wa nuru ya chini ambao husoma kasoro za kila jiwe—hakuna mawe mawili yanayofanana. Njia pekee ya wezi kushinda mfumo huo wa usalama ingekuwa kukata upya mawe, taratibu ghali mno, ambayo hupunguza thamani yayo, laripoti The Sunday Times la London.
Onyo la Fataki
Maofisa waripoti kwamba “watu wapatao 12,000 hutibiwa kila mwaka katika vyumba vya dharura vya Marekani kwa sababu ya majeraha yanayohusiana na fataki,” yataarifu Morbidity and Mortality Weekly Report (MMWR). Ripoti hiyo, iliyokusanywa na Tume ya Usalama wa Bidhaa za Watumizi kwa miaka ya 1990-1994, yakadiria kwamba asilimia 20 ya majeraha yote yenye kutokana na fataki yalikuwa ya macho. Haya, yasema MMWR, “mara nyingi ni mabaya mno na yaweza kusababisha mwono uliopunguzwa daima au upofu.” Yapasa kuonwa pia kwamba, kwa wazi wasimama-kando wengi walipata majeraha kuliko wenye kulipua fataki.
‘Liwezalo Kuwa Bomu Lililopimiwa Wakati’
Asimilia 45 hivi ya idadi ya watu ulimwenguni kwa sasa huishi majijini, laripoti gazeti Focus, na kufikia mwaka 2000, yakadiriwa kwamba nusu ya idadi ya watu itakuwa wakazi wa jijini. Sehemu kubwa ya Ulaya kaskazini, Italia, na mashariki mwa Marekani zina idadi zilizosongamana kwa kiasi fulani, na sehemu za Afrika Kusini, China, India, na Misri, zina majiji yaliyosongamana katikati ya sehemu za mashambani. Hata hivyo, picha za satelaiti sasa zafunua kwamba ni kuanzia asilimia 3 hadi 4 ya dunia ambayo imefanywa kuwa ya kisasa. Lakini huku watu milioni 61 wakihamia majijini kila mwaka, hasa katika nchi zinazositawi, msongamano katika maeneo haya ya majijini huongezeka kwa sababu “majiji hayawezi kukua haraka kama idadi yayo ya watu,” laonelea Focus, likiongeza: “Hiyo ni hali iwezayo kuwa bomu lililopimiwa wakati.”