Uasilishaji—Je, Unakufaa?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
“UASILISHAJI (tendo la kumchukua mtoto aliyeachwa na kumkubali kwenye familia yako kama mtoto halisi wa kumzaa) ni mpango wa kunufaisha watoto, si mpango wa kuwapatia kitoto mume na mke wasio na watoto,” asisitiza mfanyakazi mmoja wa kijamii wa Uingereza. Hata ikiwa hivyo, kwa kawaida mtoto ana mamlaka gani katika kuasilishwa kwake?
Je, unafikiria kuasilisha mtoto? Basi unakabili uamuzi ambao si wa kihisia-moyo tu bali pia ule usioweza kuvunjwa. Mtoto huyo atajichangamanisha katika familia yako kwa kadiri gani?
Ikiwa wewe ni mtoto aliyeasilishwa, je, unajua ni nani walio wazazi wako wa asili? Ikiwa sivyo, wafikiri kungekuwa na tofauti gani ikiwa ungewajua?
Je, wewe ni mama ambaye anafikiria kuacha mtoto wake aasilishwe? Je, kuacha mtoto wako aasilishwe ndilo suluhisho pekee na ambalo litamnufaisha mtoto wako?
Katika 1995, zaidi ya watoto 50,000 waliasilishwa katika Marekani, na 8,000 hivi kati yao walizaliwa katika nchi za kigeni. Kwa kuendelea, watu wanaasilisha watoto kutoka nchi za kigeni. Kulingana na gazeti Time, katika miaka 25 iliyopita familia katika Marekani zimeasilisha watoto zaidi ya 140,000 waliozaliwa katika nchi za kigeni. Tarakimu za Ulaya za kulinganishwa ni Sweden 32,000, Uholanzi 18,000, Ujerumani 15,000, na Denmark 11,000.
Je, hali hii inakuhusu kwa njia fulani? Kuasilisha mtoto humaanisha kwamba maisha yako—si maisha ya huyo mtoto tu—hayatakuwa yaleyale tena kamwe. Wazazi walioasilisha watoto wana sababu halali ya kutarajia furaha nyingi, lakini lazima wajitayarishe kwa ajili ya matatizo na utamausho mwingi. Vivyo hivyo, maumivu ya moyoni anayopata mama kwa kumwacha mtoto wake aasilishwe huenda yasipone kabisa.
Kila kisa chatokeza magumu ya kujenga au kujenga upya maisha machanga kwa upendo. Makala zifuatazo zitawasilisha baadhi ya shangwe—na magumu—ya uasilishaji.