Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 5/8 kur. 4-8
  • Uasilishaji—Kwa Nini na Jinsi Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uasilishaji—Kwa Nini na Jinsi Gani?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuasilisha au Kutoasilisha?
  • Ukiamua Kuasilisha . . .
  • Kutoka Jamii Nyingine?
  • Kutoka Ng’ambo?
  • Uasilishaji—Je, Unakufaa?
    Amkeni!—1996
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Uasilishaji—Napaswa Kuuonaje?
    Amkeni!—1996
  • Kuzaliwa Upya—Kunatimiza Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 5/8 kur. 4-8

Uasilishaji—Kwa Nini na Jinsi Gani?

KWA nini idadi ya watoto walioasilishwa katika Uingereza imeshuka kwa njia ya kutazamisha katika miaka 20 iliyopita? Sababu mbili zimedokezwa—kupatikana kwa utoaji-mimba wa kihalali na ukubali unaoongezeka wa mama kumlea mtoto wake bila mume. Kuwa familia ya mzazi mmoja sasa kwaonwa kuwa tatizo linaloweza kukabiliwa kwa mafanikio katika jamii ya kisasa.

Hata hivyo, zaidi tu ya miaka 100 iliyopita mambo yalikuwa tofauti. Wakati Polly, mama ya Edgar Wallace, mwandikaji Mwingereza wa riwaya za uhalifu, alipotungwa mimba na mwana wa mwajiri wake, alienda zake na kuzaa kisiri. Edgar alikuwa na umri wa siku tisa wakati mkunga alipanga atunzwe na mke wa George Freeman, mpagazi kwenye soko la samaki la Billingsgate la London. Akina Freeman tayari walikuwa na watoto wao wenyewe kumi, naye Edgar akakua akiitwa Dick Freeman. Polly alitoa malipo ya kawaida ya kusaidia kumtegemeza mtoto wake, na baba yake hakupata kujua kamwe kuhusu kuwapo kwa mwana wake.

Leo wakati watoto hawatakikani, mamlaka za serikali mara nyingi huchukua daraka la kuwatunza. Watoto wengi hutunzwa na mamlaka za serikali kwa sababu wanahitaji ulinzi kutokana na kutendwa vibaya au kwa sababu wana ulemavu wa kimwili au kiakili. Wale waliofanywa mayatima kwa sababu ya maogofyo ya vita na watoto wanaotokea kwa sababu ya ulalwaji kinguvu huongezeka daima kwa watoto wanaohitaji sana shauku na ulinzi wa kimzazi—katika neno moja, uasilishaji.

Kuasilisha au Kutoasilisha?

Kumwasilisha mtoto si rahisi kamwe, na si jambo la hekima kamwe kufanya uamuzi wa ghafula unapotafakari jambo hilo. Ikiwa mtoto wako amekufa, huenda likawa jambo jema zaidi kungoja hadi mshtuko au huzuni iishe kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu kuasilisha. Hilo ni kweli pia kwa mume na mke wanaoambiwa kwamba hawawezi kuzaa.

Kila mtoto hurithi tabia za kipekee za kijeni. Wazazi mara nyingi hushangazwa na mielekeo ya watoto wao wenyewe, lakini ni vigumu kupima uwezo wa mtoto wa kiakili na kihisia-moyo ikiwa wazazi wake hawajulikani.

Je, unaweka thamani ya juu kwenye matimizo ya kielimu? Ikiwa ndivyo, utahisije ikiwa mtoto unayemwasilisha hafikii matarajio yako? Je, utaona mtoto aliye punguani au mlemavu kimwili kuwa tatizo ambalo unaweza kulikabili?

Wafanyakazi waliozoezwa kwenye ofisi za uasilishaji watoto au wafanyakazi wa kijamii wa serikali watakuuliza maswali kama hayo kabla hujafanya uamuzi wa mwisho. Hangaiko lao la kwanza lazima liwe kwa usalama na furaha ya huyo mtoto.

Ukiamua Kuasilisha . . .

Kila nchi ina sheria zayo na maagizo yayo yenyewe ya uasilishaji ambayo yapaswa kuchunguzwa. Katika Uingereza kuna mamia ya mashirika ya uasilishaji, nayo kwa kawaida hushirikiana na mamlaka za serikali za mahali. Mashirika yote yana sheria zayo yenyewe.

Zilizo mashuhuri hasa katika Uingereza ni tafrija za uasilishaji, ambapo idadi kadhaa ya wanaotazamiwa kuwa wazazi wanaweza kuchangamana na watoto wanaopatikana kwa ajili ya kuasilishwa, bila mkazo wowote wa kihisia-moyo ambao huwa katika kukutana na mtoto mmoja-mmoja. Hali hiyo iliyotulia hufanya iwe rahisi kwa wanaotazamiwa kuwa wazazi kukataa mtoto fulani nalo hufanya isiwe rahisi kwa watoto kutamauka, kwa kuwa hakuna mtoto fulani hususa ambaye hutengwa kuelekezewa fikira.

Kwa kawaida viwango vya mwisho vya umri huwekwa kwa wale wanaoasilisha, labda umri wa miaka 35 au 40 hivi—ingawa hili mara nyingi hutumika kwa kuasilisha vitoto, sanasana si watoto wenye umri mkubwa zaidi. Mashirika ya uasilishaji husema kwamba kiwango cha mwisho cha umri hufikiria pia muda wa kuishi unaotarajiwa wa wanaotazamiwa kuwa wazazi. Hata hivyo, wanatambua kwamba uzoefu huja na umri.

Miaka mingi iliyopita uasilishaji ulipangiwa mume na mke tu. Leo, waseja wanaweza kutoa maombi na kufanikiwa kuasilisha watoto fulani. Pia, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa na ulemavu si lazima ziwe sababu za wanaotazamiwa kuwa wazazi kukataliwa. Swali la msingi ni, Mpango huo utamwandalia mtoto nini?

Hata wakati taratibu za uasilishaji zinapomalizwa hatimaye, huenda wazazi wakachunguzwa ili kuhakikisha kwamba mambo yanaenda sawasawa.

Kutoka Jamii Nyingine?

Miaka 30 iliyopita ilikuwa vigumu kwa watoto weusi katika Uingereza kuchukuliwa na familia za weusi, tokeo likiwa kwamba wengi walienda kwa wazazi weupe. Tangu 1989 imekuwa sera ya kitaifa katika Uingereza kuweka watoto kwa wazazi-walezi walio na malezi yaleyale ya kikabila. Inahisiwa kwamba kwa njia hii mtoto atajipatanisha kwa utayari zaidi na jamii na utamaduni wake. Hata hivyo, hilo liliongoza kwenye hali zenye kupingana.

Hivi majuzi The Sunday Times liliripoti kwamba wazazi fulani weupe “wamejiainisha upya kuwa ‘weusi’” ili kuwawezesha kumwasilisha mtoto mweusi. Ni jambo la kawaida kwa wazazi weupe kutunza mtoto mweusi, jambo linalomaanisha wanamtunza kwa muda tu. Lakini baadaye wakinyimwa haki ya kumwasilisha huyo mtoto daima, tokeo ni hali mbaya ya kihisia-moyo kwa mtoto na wazazi.

Mume na mke kutoka Scotland, ambao walitunza watoto wawili Wahindi kwa miaka sita, hivi majuzi walikabili tatizo linalofanana na hilo la uasilishaji wa jamii mchanganyiko. Mahakama iliruhusu uasilishaji kwa kufahamu kwamba wazazi hao “watumie jitihada zao bora zaidi kuhakikisha kwamba hao watoto watajulishwa utambulisho wao [wa kikabila] na kulelewa wakiwa na uelewevu wa vyanzo vyao vya kikabila na desturi,” laripoti The Times. Katika kisa hiki wazazi-walezi walikuwa tayari wakifanya hivyo. Watoto hao walikuwa wakifundishwa Kipunjabi, na nyakati fulani walikuwa wakivishwa mavazi ya kienyeji.

Wengi watakubaliana na maoni ya msemaji mwanamke wa huduma za kijamii wa Uingereza ambaye alisema kwamba uasilishaji wa jamii mchanganyiko wapaswa kuruhusiwa kwa uhuru zaidi. “Twaishi katika jamii ya tamaduni nyingi,” yeye akasema, “na kutunza mtoto asiye wako na uasilishaji wapaswa kuonyesha hilo.”

Kutoka Ng’ambo?

Uasilishaji wa watoto wa kutoka nchi za kigeni ni ‘biashara inayositawi,’ kulingana na gazeti la habari The Independent. Ingawa ripoti zinaonyesha kwamba shughuli fulani huenda zisiwe halali, Ulaya Mashariki ndiyo chanzo kikuu cha ugavi kwa Uingereza.

Kwa kielelezo, baadhi ya watoto waliozaliwa kwa sababu ya ulalwaji kinguvu wakati wa kuvunjika kwa iliyokuwa Yugoslavia wameachwa. Inadaiwa kwamba wengine wangetolewa kama si mwingilio wa “wakala wa watoto,” ambaye aliahidi uasilishaji wa mtoto ikiwa alizaliwa baada ya miezi tisa. Hata hivyo, serikali za nchi za Magharibi, zinahangaikia malipo yanayofanywa ili kupata uasilishaji huu.

Kisababishi cha hangaiko kuu huhusiana na madai ya udanganyaji wa hati unaofanywa na madaktari wakati wa watoto kuzaliwa. Gazeti la habari The European liliripoti madai kwamba akina mama fulani katika Ukrainia waliambiwa kwamba vitoto vyao vilizaliwa vikiwa vimekufa. Ilidaiwa pia kwamba vitoto hivi viliuzwa hatimaye. Akina mama wengine huenda walikuwa wamejulishwa kwamba watoto wao walikuwa mapunguani. Chini ya msongo kama huo, akina mama wenye wasiwasi wanahimizwa kwa urahisi kutia sahihi watoto wao waasilishwe. Hata hivyo watoto wengine huenda hawakufika kwenye makao ya kutunzia watoto ambapo walikuwa wakipelekwa badala ya hivyo huenda waliishia katika nchi za kigeni.

Chuki hutokea katika nchi zinazositawi. Hizo hudai kwamba Magharibi yenye utajiri yapaswa kusaidia familia za kienyeji kutunza watoto wazo katika mazingira ya nyumbani badala ya kuwachukua kwa ajili ya kuwaasilisha katika utamaduni wa kigeni.

Nchi za Magharibi lazima zifahamu pia desturi ya kale sana ya familia zilizoenea, ambazo ndizo utegemezo wa jamii katika tamaduni nyingi. Kwa kawaida mtoto hatanyimwa utunzi anapoishi katika vikundi vya kikabila, hata wazazi wake wakifa. Kando na washiriki wa karibu wa familia, kama vile wazazi-wakuu, familia iliyoenea ya shangazi na wajomba zitamwona huyo mtoto kuwa wazo, na toleo lolote la uasilishaji kutoka nje laweza kueleweka vibaya na kuonwa kuwa mwingilio usiokubaliwa.a

Kupanga uasilishaji si rahisi, na hata wakati ambapo taratibu hiyo imemalizwa, kazi ngumu inahitajika ili kuufanikisha. Lakini kama tutakavyoona, pia kuna shangwe nyingi.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa mazungumzo kamili ya zoea la kupatia washiriki wengine wa familia watoto, ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1988, kurasa 28-30, lililotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku katika ukurasa wa5]

Je, Mwana Wangu Atanitafuta?

WAZAZI wangu walitalikiana nilipokuwa na umri wa miaka 11. Nilitamani sana upendo. Nilipokuwa chuoni, nilijihusisha katika uhusiano wa kimahaba; ilikuwa njia yangu ya kupata shauku. Kisha, kwa fadhaiko, nikapata kwamba nilikuwa mja-mzito. Lilikuwa upuuzi sana. Mwanafunzi mwenzangu nami tulikuwa wachanga sana. Sikuwa nimepata kutumia dawa za kulevya, alkoholi, au tumbaku, lakini mvulana-rafiki wangu alikuwa ameharibiwa sana kutokana na siku alizokuwa akitumia LSD.

Nilishauriwa nitoe mimba, lakini baba yangu akanihimiza nisifanye hivyo. Sikutaka kuwa mja-mzito, lakini pia sikutaka kuharibu uhai. Mwana wangu alipozaliwa 1978, niliamua kutoweka jina la baba yake katika cheti chake cha kuzaliwa ili kuhakikisha kwamba baba yake hangeweza kumfikia. Kwa hakika, nilikubali mtoto huyo aasilishwe tangu kuzaliwa kwake; kwa hiyo alichukuliwa mara moja na kuwekwa kwa utunzi wa muda. Hata sikumwona. Kisha nikabadili mawazo yangu. Nilimtoa mtoto wangu kwenye utunzi na kujaribu sana kumlea peke yangu. Lakini sikuweza, kidogo nipate tatizo la kiakili.

Mwana wangu alikuwa na umri wa miezi sita hivi wakati agizo la uasilishaji lilipokubaliwa nikahitajiwa kumwacha achukuliwe. Nakumbuka nikihisi kana kwamba mtu fulani alikuwa amenidunga kisu. Nilikufa kihisia-moyo. Ni tangu nipate ushauri wa kitaalamu kwa miaka miwili iliyopita ndipo nimeweza kujenga mahusiano yenye maana. Singeweza kuomboleza—mwana wangu hakuwa amekufa. Lakini singeweza kumfikiria—nilikataa kujiruhusu kufanya hivyo. Ilikuwa vibaya mno.

Linaloumiza sana ni kusikia watu wakisema: “Ukimwacha mtoto wako aasilishwe, humpendi mtoto wako.” Lakini hilo halikuwa kweli katika kisa changu! Ilikuwa kwa sababu nilimpenda mwana wangu kwamba nilimwacha achukuliwe! Hadi dakika ya mwisho, nilikuwa nikijiuliza: ‘Nitafanya nini jamani? Naweza kufanya nini?’ Hakukuwa na njia ya badala. Nilijua kwamba singeweza kushinda hili tatizo na kwamba kitoto changu kingeteseka ikiwa ningejaribu kukaa nacho.

Katika Uingereza, jamii sasa yakubali familia za mzazi mmoja—lakini si wakati nilipozaa. Laiti ningaliweza kumlea mwana wangu ifaavyo. Ushauri ambao nimekuwa nikipata hivi majuzi nafikiri ungalisaidia, lakini ni kuchelewa mno sasa. Je, mwana wangu yuko hai bado? Amekua na kuwa mvulana wa aina gani? Wanapofikia umri wa miaka 18 watoto walioasilishwa huruhusiwa kisheria kutafuta wazazi wao. Mara nyingi mimi hujiuliza kama mwana wangu atanitafuta.—Imechangwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Tulifanikiwa

TUKIWA na wavulana wetu wawili matineja, tulikuwa familia ya Waingereza iliyoridhika na iliyoungana. Wazo la kuwa na binti—wa jamii tofauti—halikuwa jambo lililotujia akilini. Kisha Cathy akaja katika maisha zetu. Cathy alizaliwa London, Uingereza. Alilelewa akiwa Mkatoliki wa Kiroma, lakini akiwa mtoto mchanga, alihudhuria mikutano michache pamoja na mama yake kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, alipokuwa na umri wa miaka 10, alipelekwa katika makao ya kutunzia watoto.

Ingawa mambo yalikuwa magumu kwake huko, alifaulu kuhudhuria mikutano peke yake kwenye Jumba la Ufalme, ambapo tulikutana naye. Cathy alikuwa msichana mwenye kufikiri. Mke wangu nami tulipomtembelea kwenye makao ya kutunzia watoto, tuligundua kwamba ukuta kando ya kitanda chake ulikuwa umefunikwa kwa picha za wanyama na mandhari za mashambani, tofauti na vibandiko vya watu mashuhuri wa muziki ambavyo wale wasichana wengine walikuwa wamebandika.

Wakati fulani baadaye Cathy alilazimika kutokea mbele ya halmashauri ya ukaguzi, ambayo ilimuuliza ikiwa angependa kuondoka kwenye makao hayo na kuishi pamoja na familia. “Ni pamoja na familia ya Mashahidi wa Yehova tu!” akajibu. Cathy alipotuambia kuhusu hilo na alichokuwa amesema, hilo likatupatia jambo la kufikiria. Tulikuwa na chumba cha ziada. Je, tungeweza kuchukua daraka hilo? Tukiwa familia, tulilizungumzia na kusali kulihusu. Ilikuwa baadaye sana ambapo tuligundua kwamba mfikio huu—kumuuliza mtoto maoni—ulikuwa jaribio jipya kwa upande wa huduma za kijamii, jaribio lililokuwa likithibitishwa.

Huduma za kijamii zilichunguza hali yetu ya maisha kutoka kwa polisi na daktari wetu na kupata marejezo ya kibinafsi. Upesi mkataba ukafanywa. Tukaambiwa kwamba tungempata Cathy kwa kipindi cha jaribio na kwamba tungemrudisha ikiwa hatukumpenda! Hilo lilituogofya, nasi tulikuwa thabiti kabisa katika kusema kwamba hatungefanya hivyo kamwe. Cathy alikuwa na umri wa miaka 13 tulipomchukua kirasmi nyumbani kwetu.

Kile kifungo cha kipekee cha upendo kati yetu sote huendelea kuimarika. Cathy sasa ni painia wa kawaida (mweneza-evanjeli wa wakati wote) katika kutaniko la Kifaransa la Mashahidi wa Yehova katika kaskazini mwa London. Mwaka alioondoka nyumbani kwenda kupainia, alituandikia barua ndogo yenye kugusa moyo: “Kuna msemo usemao ‘huwezi kuchagua familia yako.’ Hata hivyo, ningependa kuwashukuru kutoka moyoni kwa kunichagua.”

Tunashukuru sana kwamba Cathy alijiunga nasi. Kumfanya sehemu ya familia yetu kuliboresha maisha zetu. Tulifanikiwa!—Imechangwa.

[Picha]

Cathy pamoja na wazazi waliomwasilisha na ndugu zake

[Picha katika ukurasa wa 7]

Watoto wengi huhitaji sana shauku na ulinzi wa kimzazi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki