Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 5/8 kur. 26-27
  • Je, Yafaa Wakristo Kucheza Dansi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Yafaa Wakristo Kucheza Dansi?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kucheza Dansi Ni Uwasiliano
  • Kucheza Dansi—Kufaako na Kusikofaa
  • Kucheza Dansi Kunakofaa au Kusikofaa—Jinsi ya Kupambanua
  • Vipi Kwenda Disko?
    Amkeni!—2004
  • Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare
    Amkeni!—1998
  • Nyimbo na Ngoma Unazochagua Kucheza
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
  • Ninaweza Kujifurahisha Jinsi Gani?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 5/8 kur. 26-27

Maoni ya Biblia

Je, Yafaa Wakristo Kucheza Dansi?

“SIWEZI kutazama hili. Ni lazima niondoke,” mwanamume mmoja kijana akamnong’oneza mke wake huku akiinuka kutoka kiti chake na kuondoka katika chumba ili kutembea-tembea katika hewa yenye ubaridi ya usiku. Yeye alikuwa ameaibika.

Yeye na mkeye walikuwa wamealikwa na marafiki kwa kusanyiko la kirafiki. Waalikaji walikuwa wameamua kuandaa maonyesho ambayo yalitia ndani wanawake watatu wakicheza dansi. Yaelekea watazamaji wale wengine hawakusumbuka. Je, alikuwa mwenye hisia nyepesi kupita kiasi? Je, wacheza-dansi hawakuwa wakidhihirisha tu hisia-moyo zao za ndani na kufurahia uhuru wa dansi? Ebu tujaribu kuelewa dansi kutokana na maoni ya Kikristo.

Kucheza Dansi Ni Uwasiliano

Njia moja ambayo kwayo binadamu huwasiliana ni kwa njia ya ishara na misogeo. Kwa kielelezo, wakiwa katika nchi za kigeni, wageni wengi wameshangazwa kujua kwamba msogeo waliouona kuwa usioweza kuudhi una maana tofauti huko—labda isiyotamanika. Mmoja aliyekuwa mishonari huko Visiwa vya Solomon, Malasia, na Papua New Guinea alisema hivi: “Katika maeneo fulani madokezo ya kingono yanahusianishwa na misogeo fulani ya mwili. Kwa mfano, wakati mwanamke ameketi sakafuni, huonwa kuwa jambo lisilofaa kwa mwanamume kutembea kuvuka miguu yake. Vivyohivyo, ni jambo lisilo la busara kwa mwanamke kutembea mbele ya mwanamume aliyeketi sakafuni. Katika visa vyote viwili mawazo ya kingono huja akilini.” Iwe twatambua au sivyo, misogeo yetu ya mwili hunena. Basi hatupaswi kushangazwa kwamba katika historia yote kucheza dansi kumetumiwa kuwa njia ya uwasiliano.

Hisia-moyo zote zaweza kudhihirishwa katika dansi—kuanzia shangwe na mchachao wa sherehe hadi uzito wa desturi ya kidini na pokeo. (2 Samweli 6:14-17; Zaburi 149:1, 3) The New Encyclopædia Britannica hutaarifu hivi: “Mcheza-dansi huwasiliana na watazamaji kwa njia mbili tofauti, ama kupitia umwagaji wa hisia-moyo kupitia mwili na vilevile uso au kwa lugha tata ya uigizaji na ishara za mwili.” Katika dansi fulani huenda uwasiliano ukawa rahisi zaidi kueleweka. Katika namna fulani za dansi, huenda lugha ieleweke na wachache tu walio na ujuzi. Kwa kielelezo, katika dansi aina ya classical ballet mkono juu ya moyo huonyesha upendo, ilhali kuelekeza kwenye kidole cha nne cha mkono wa kushoto humaanisha ndoa. Katika opera ya Kichina kutembea kimviringo huonyesha safari, hali kuzunguka jukwaa huku ukishikilia mjeledi uliolala humaanisha kuendesha farasi; bendera nyeusi iliyopitishwa kuvuka jukwaa ni dhoruba, hali bendera ya buluu hafifu humaanisha upepo mwanana. Hivyo kwa misogeo na ishara za mwili za dansi, mwili huwasiliana. Lakini je, sikuzote ujumbe ni ufaao?

Kucheza Dansi—Kufaako na Kusikofaa

Kucheza dansi kwaweza kuwa namna yenye kufurahisha ya kitumbuizo na mazoezi ya mwili. Huenda ukawa wonyesho safi kiadili na mnyoofu, ukionyesha itikio lenye shangwe la kimwili kwa raha tupu ya kuishi au uthamini kwa wema wa Yehova. (Kutoka 15:20; Waamuzi 11:34) Dansi fulani za vikundi na za kitamaduni zaweza kuwa zenye kufurahisha. Yesu, katika kielezi chake cha mwana mpotevu, hata alirejezea kikundi cha wacheza-dansi, bila shaka kikundi cha kucheza dansi kilichokodiwa, kikiwa sehemu ya msherehekeo. (Luka 15:25) Kwa hivyo, kwa wazi, Biblia yenyewe haishutumu kucheza dansi kwa ujumla. Hata hivyo, hiyo huonya dhidi ya uchocheaji wa mawazo na tamaa mbaya. Ni kuhusiana na hili kwamba namna fulani za kucheza dansi huenda zisifae, hata zaweza kuwa hatari kwa hali ya kiroho ya mtu. (Wakolosai 3:5) Tangu nyakati za kale katika pindi nyingi kucheza dansi kumekuwa kwa kiashiki na kumetumiwa kwa makusudi yenye kudhuru.—Linganisha Mathayo 14:3-11.

Mpinzani wetu, Shetani Ibilisi, ajua kwamba muunganisho wa misogeo ya dansi na mawazo yasiyofaa ni silaha yenye nguvu sana mikononi mwake. (Linganisha Yakobo 1:14, 15.) Yeye anafahamu vyema sana juu ya uvutio wa ashiki wa mwili unaosogea-sogea na jinsi unavyoweza kuchochea mawazo yenye ashiki. Mtume Paulo alionya kwamba Shetani ameazimia kutushawishi ili ‘aharibu fikira zetu, tukauache unyofu na usafi kwa Kristo.’ (2 Wakorintho 11:3) Wazia jinsi ambavyo Ibilisi angefurahi ikiwa kwa kutazama au kushiriki katika kucheza dansi kusikofaa tungeruhusu akili zetu zinaswe na mawazo yasiyo ya adili. Yeye angefurahi hata zaidi ikiwa tamaa zetu zisizodhibitiwa zingeachiliwa nasi tungenaswa katika matokeo yenye maumivu ya mwenendo usiofaa. Yeye amepata kutumia misogeo na dansi akiwa na lengo hilo wakati uliopita.—Linganisha Kutoka 32:6, 17-19.

Kucheza Dansi Kunakofaa au Kusikofaa—Jinsi ya Kupambanua

Vivyohivyo, iwe dansi yachezwa na vikundi, na watu wawili-wawili, au na mtu mmoja pekee, ikiwa misogeo inazusha mawazo yasiyo safi ndani yako, basi dansi hiyo ni mbaya kwako, hata ingawa huenda isiwe mbaya kwa wengine.

Wengine wametaja kwamba katika dansi nyingi za kisasa wenzi hata hawagusani. Hata hivyo, je, suala hasa ni kugusana? Ensaiklopidia Britannica hufikia mkataa kwa kusema kwamba “matokeo ya mwisho ni yaleyale—raha ya kimwili katika kucheza dansi na utambuzi wa kingono wa mwenzi, iwe anakumbatiwa au anatazamwa kwa nusu utambuzi.” Je, “utambuzi wa kingono wa mwenzi” ni wa kihekima nje ya vifungo vya ndoa? Si kulingana na taarifa ya Yesu kwamba “Kila mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”—Mathayo 5:28.

Iwe utaamua kucheza dansi au la ni chaguo lako. Kufikiria maswali yafuatayo huenda kukakusaidia kuamua kwa hekima. Kusudi la hiyo dansi ni nini? Ina sifa gani? Misogeo ya dansi hukazia nini? Inachochea mawazo na hisia-moyo gani ndani yangu? Inachochea tamaa gani katika mwenzangu au katika wale wanaotazama? Kwa hakika, mtu anapaswa kuitikia kulingana na dhamiri yake, kama alivyofanya yule mume mchanga katika utangulizi wetu, haidhuru kile wanachofanya wengine.

Biblia huonyesha kwamba Muumba hutaka tufurahie zawadi za urembo, mwendo wa muziki, na madaha. Ndiyo, zifurahie—lakini kumbuka kwamba unapocheza dansi, mwili wako huwasiliana. Kumbuka miongozo ya Paulo kwenye Wafilipi 4:8: “Mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Picture Fund/Kwa hisani ya, Museum of Fine Arts, Boston

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki