Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 2/8 kur. 23-24
  • Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mavazi ya Mashetani Wacheza-Dansi
  • Kushika Njia Hadi Kwenye Kanisa
  • Baraka ya Kikasisi
  • Si kwa Mashahidi wa Yehova
  • Je, Yafaa Wakristo Kucheza Dansi?
    Amkeni!—1996
  • Vipi Kwenda Disko?
    Amkeni!—2004
  • Utamaduni wa Wenyeji na Kanuni za Kikristo—Je, Zapatana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Nyimbo na Ngoma Unazochagua Kucheza
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 2/8 kur. 23-24

Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare

ILIKUWA ni katikati tu ya asubuhi, lakini tayari kulikuwa na joto sana. Tulipokuwa tukitazama kikundi cha wanaume waliovalia mavazi ya kitamaduni, tulistaajabu jinsi ambavyo wangeweza kustahimili lile joto lenye kuunguza! Tulikuwa tunazuru mji mdogo wa kilimo wa San Francisco de Yare, Venezuela. Wanaume waliokuwa na mavazi walikuwa ni wale Diablos Danzantes de Yare, wenye sifa, Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare.

Watu wengi katika Venezuela ni Wakatoliki na huungama kuitikadi Biblia. Hata hivyo, kwa vizazi kadhaa dansi za kidesturi ambazo hukazia kwa kutokeza taswira ya roho waovu zimetimiza sehemu muhimu katika utamaduni wa hapo. Kanisa Katoliki haliruhusu tu dansi hizo bali kwa kweli huziendeleza. Hili ni kweli kuhusu Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare.

Baada ya kuwasili Yare, tulishangaa kuona kwamba makao makuu ya Udugu wa Sakramenti Iliyo Takatifu Zaidi, shirika la Kikatoliki, yalikuwa pia makao makuu ya mashetani wacheza-dansi. Jengo hilo hujulikana kuwa Casa de Los Diablos (Nyumba ya Mashetani). Ilikuwa Jumatano, siku kabla ya sherehe ya Wakatoliki ya Corpus Christi, na kulikuwa na wapiga-picha wataalamu kadhaa waliokuwa wamekaa upande wa nje wa jengo. Kwa ghafula, kulikuwa na mlio mkuu wa ngoma, na wanaume kadhaa waliovalia kama mashetani wakaanza kucheza dansi.

Mavazi ya Mashetani Wacheza-Dansi

Kila mcheza-dansi alivalia shati nyekundu, suruali nyekundu, soksi nyekundu, na makubazi. Kila mmoja alivalia rozari, msalaba, na nishani kubwa ya Kikatoliki kuzunguka shingo yake. Msalaba mwingine ulifungwa kwenye mavazi yake. Katika mkono mmoja kila mmoja alishika kayamba iliyokuwa na sura ya kishetani na katika ule mwingine, mjeledi mfupi. Lakini vyenye kutokeza zaidi vilikuwa vile visetiri-uso vikubwa, vya ajabu na vyenye rangi nyingi, na pembe, macho yaliyotokeza na, mara nyingi, meno yaliyokenuliwa. Kila kizuizui kiliambatanishwa na kifuniko kirefu, cha nguo nyekundu.

Tulipata habari kwamba kulikuwako namna tofauti za wacheza-dansi. Capataz mkuu, au mwangalizi, hujulikana pia kuwa diablo mayor, au shetani mkuu. Kizuizui chake kina pembe nne. Kwa ujumla yeye huchaguliwa kwa sababu ya ukuu wake. Mwangalizi-msaidizi, au segundo capataz, ana pembe tatu, na wacheza-dansi wa kawaida wasio na daraja lolote wana mbili pekee. Baadhi ya wacheza-dansi ni promeseros, watu wawekao ahadi ya kucheza dansi mara moja kwa mwaka kwa idadi fulani ya miaka, au labda kwa muda wote wa maisha yao. Ahadi hii, au nadhiri, kwa kawaida hufanywa na watu ambao huamini kwamba Mungu amewapa ombi la pekee.

Kushika Njia Hadi Kwenye Kanisa

Ifikapo adhuhuri, wacheza-dansi huondoka kwenye makao yao makuu na kuelekea kwenye kanisa la mahali hapo ili kupata idhini ya kasisi kwa mwandamano wao unaobakia. Mashetani wacheza-dansi hukutana na kasisi nje ya kanisa. Hapo wao hupiga magoti ili kupokea baraka yake. Kisha wao hucheza dansi kupitia barabara za mjini, nyakati nyingine kutoka mlango hadi mlango. Mara nyingi wenye nyumba husalimu mashetani wacheza-dansi kwa peremende, vinywaji, na vyakula vinginevyo. Mwandamano huu huendelea bila kukoma alasiri yote.

Asubuhi ifuatayo Misa ianzapo kanisani, wacheza-dansi hukutana tena kwenye Casa de Los Diablos. Wakitikisa kayamba zao kwa umoja, kutoka huko wanacheza dansi wakielekea makaburini, kwa wizani wa ngoma. Madhabahu imesimamishwa makaburini, na mbele yake huwaheshimu marafiki waliokufa. Wakati wa sherehe hii wizani wa ngoma huwa wa polepole. Kisha, kwa hofu ya kishirikina, wanatoka makaburini kwa kutembea wakirudi nyuma, wakihakikisha kwamba hawageuzi migongo yao kuelekea madhabahu. Kutoka huko wao huenda mpaka kanisani na kungojea Misa imalizike.

Baraka ya Kikasisi

Mwishoni mwa Misa, kasisi huja na kuwabariki wacheza-dansi, ambao hupiga magoti vichwa vyao vikiwa vimeinamishwa, vizuizui vyao vikining’inia kutoka kwenye vifuniko, vikifananisha ushindi wa wema dhidi ya uovu. Kasisi huyo huketi kando ya shetani mkuu. Hao wawili husikiliza nadhiri za promesero wapya, ambao hueleza kwa nini wanaahidi kucheza dansi na watafanya hivyo kwa miaka mingapi.

Wacheza-ngoma huanza kupiga ngoma zao haraka zaidi, na mashetani wacheza-dansi hufuata kwa kutikisa kwa nguvu miili na kayamba zao kwa kufuatisha mwendo wa wizani ulioongezeka. Wanawake hucheza dansi pia lakini si wakiwa na mavazi ya kishetani. Wao huvalia skati nyekundu, blauzi nyeupe, na vitambaa vya mkono vyeupe au vyekundu vichwani mwao. Katika sehemu ya mwandamano wao, baadhi ya mashetani wacheza-dansi hubeba sanamu ya mtakatifu mfadhili wao kwenye mabega yao. Wacheza-dansi humalizia mwandamano wao kwa kufanya gwaride mbele ya kanisa, baada ya kuupa heshima msalaba mashuhuri wa mjini.

Si kwa Mashahidi wa Yehova

Hili lilithibitika kuwa jambo lenye kutupendeza tukiwa watalii. Wakati wa kuzuru kwetu ule mji mdogo wa Yare, hatungeweza kuepuka kuona matukio ya waziwazi yaliyotokezwa na mashetani wacheza-dansi. Na bado, sisi tukiwa Wakristo, kama Mashahidi wa Yehova wengineo zaidi ya 70,000 katika Venezuela, hatuungi mkono sherehe ya Mashetani Wacheza-Dansi wa Yare au miandamano inayofanana na hiyo.

Kwa sababu gani? Kwa sababu tunasikiza maneno ya mtume Paulo: “Sitaki nyinyi mwe washiriki pamoja na roho waovu. Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na pia kikombe cha roho waovu. Hamwezi kuishiriki meza ya Bwana na vilevile meza ya roho waovu.” (1 Wakorintho 10:20, 21, New American Bible)—Imechangwa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki