Ni Nani Aliyevumbua Tai?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI
WANAUME wapatao milioni 600 huvaa tai kwa ukawaida ulimwenguni pote. Katika Ujerumani mwanamume wa kawaida ana tai 20 hivi. Wanaume wengi, huku wakivaa tai zao wamejiuliza kwa udhiko, ‘Lakini, hili lilikuwa wazo la nani?’ Tai zilitoka wapi?
Steenkerke, mji mmoja katika Ubelgiji, husisitiza kupewa heshima ya “kuvumbua” tai. Katika 1692, majeshi ya Uingereza yalishambulia ghafula majeshi ya Ufaransa yaliyokuwako huko. Kulingana na gazeti la habari la Ujerumani Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung, “maofisa [Wafaransa] hawakuwa na wakati wa kuvalia ifaavyo. Lakini kwa haraka, walifunga skafu za yunifomu zao kuzunguka shingo zikiwa na kifundo kilicholegea kisha wakatia miisho ya skafu kupitia matundu ya vifungo vya makoti yao. Voilà (kumbe), huo ukawa mwanzo wa tai katika hali yayo ya awali.”
Hata hivyo, fashoni hiyo mpya ya majeshi hao haikuwa isiyo na kifani. Wataalamu wa historia ya tai hutaja kwamba karne nyingi mapema, mashujaa wa vita wa maliki Mchina Cheng (Shih Huang Ti) walivalia kitambaa kilichofanana na skafu kilichokunjwa kuzunguka shingo, kuonyesha cheo chao.
Ingawa hivyo, labda zijulikanazo kupita zote zilikuwa skafu zilizovaliwa na Wakroatia waliompigania Mfalme Louis 14 wa Ufaransa. Wakati wa gwaride la ushindi katika Paris, Wafaransa walivutiwa sana na skafu za Wakroatia hivi kwamba wakaziita cravates, kutokana na Cravate, Mkroatia, kisha pia wao wakaanza kuvalia skafu hizo. “Tangu wakati huo na kuendelea,” laandika gazeti la habari lililotangulia kutajwa, “fashoni za tai zikaendelea kuenea, ingawa ni majeshi katika Steenkerke waliokuwa wa kwanza kufanya skafu kuwa tai yenye kifundo.”
Wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa (1789-1799), mwanamume alionyesha mwelekeo wake wa kisiasa kwa rangi ya “croat,” au skafu, kuzunguka shingo yake. Katika karne ya 19, jamii ya Ulaya ya mitindo “iligundua” aina hii ya mavazi. Ilikuwa wakati huo ambapo cravat ilikwezwa kutoka mandhari ya kijeshi na ya kisiasa na kuingia kwenye makabati ya kuwekea mavazi ya wanaume kwa ujumla. Leo tai haikubaliwi tu katika jamii nyingi ulimwenguni pote bali katika vikao fulani, hata ni jambo la lazima.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Mavazi ya Kihistoria Pichani/Dover Publications, Inc., New York