Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Usawaziko Baada ya kusoma makala “Zawadi ya Mungu ya Usawaziko” (Machi 22, 1996), nilihisi kusukumwa kuwaandikia. Wakati huu mimi najifunza sayansi inayohusika na usikiaji, na hakuna kimoja cha vitabu vyangu vya mafundisho kilicho na habari iliyo kamili na rahisi kufahamu kama hiyo makala ya Amkeni! Ule mchoro wa sikio pia ulikuwa bora kabisa.
J. P. A., Brazili
Tai Asanteni sana kwa ile makala “Ni Nani Aliyevumbua Tai?” (Mei 8, 1996) Nikiwa mhudumu wa Mashahidi wa Yehova, nimekuwa nikivaa tai katika joto la zaidi ya digrii 30 Selsiasi nikiwa katika kazi ya kuhubiri mlango hadi mlango. Mara nyingi nimekuwa nikiwaza kwamba ni lazima tai ilivumbuliwa na mtesi fulani mkatili wa karne ya 13 ambaye ili kufanya mtu aliyeasi mambo ya kidini atubu alimtisha kwa ama kitanua-mwili, kifaa cha kufinya kidole gumba kwa bisibisi, kuchemshwa ndani ya mafuta, au kuvaa tai katika alasiri ya kiangazi.
W. B., Marekani
Huenda wengine wakahisi kwamba kuvaa tai ni mateso katika halihewa yoyote. Ingawa hivyo, ni jambo la kupongezwa kwamba katika tamaduni fulani ambapo kuvaa tai huonwa kuwa pambo lifaalo, Mashahidi wa Yehova kwa kawaida hustahimili hali ngumu ya kuvaa tai wakiwa katika huduma na katika kuhudhuria mikutano ya Kikristo.—Mhariri.
Ugoro Katika darasa letu la afya shuleni, tulikuwa tukijifunza juu ya dawa za kulevya. Nilimwonyesha mwalimu wangu nakala ya toleo la Amkeni! la Aprili 22, 1996 lenye makala “Vijana Huuliza . . . Ugoro—Je, Hauwezi Kudhuru?” Aliniruhusu nifanye nakala 30 za makala hiyo ili aweze kuwapa wanafunzi na kuzisoma pamoja nao. Watoto katika darasa langu waliifurahia, na hata nikawaangushia magazeti machache.
M. C., Marekani
Kusumbuliwa Kingono Asanteni kwa ule mfululizo “Wakati Ambapo Kusumbuliwa Kingono Hakutakuwapo Tena!” (Mei 22, 1996) Katika kuyashiriki magazeti hayo na wengine, nilipata kwamba wanawake wengi walishukuru kwa madokezo juu ya jinsi ya kuepuka kusumbuliwa na jambo la kufanya unaposumbuliwa. Majuma kadhaa baadaye mimi mwenyewe nilisumbuliwa kazini na kuripoti jambo hilo polisi. Nilipongezwa kwa jinsi nilivyoshughulikia hali hiyo.
Jina limebanwa, Ujerumani
Nashukuru sana kwa makala hizo. Sasa niko katika mwaka wangu wa pili wa shule ya sekondari, na nimepata kusumbuliwa, ingawa sijamweleza yeyote kamwe kuhusu hilo. Makala hizi zilinitia moyo kuwaeleza wazazi na walimu wangu. Sasa naweza kuchukua msimamo wangu dhidi ya wasumbuaji.
K. Y., Japani
Mimi ni karani mwenye umri wa miaka 21 na hivi majuzi nilisumbuliwa kingono na mwajiri wangu. Nilipokuwa nikijaribu kutafuta jinsi ya kumfikia na kujieleza hisia zangu, nilipata toleo hilo la Amkeni! Nilimpa mwajiri wangu nakala, ambayo aliisoma. Aliomba radhi na kuahidi kutofanya tena kamwe alichokuwa amenifanyia.
D. N. I., Nigeria
Nathamini kufunua kwenu jambo hili muhimu, lakini kulingana na picha zenu, ni wanaume tu wanaosumbua. Kwa wazi, mnatoa maoni yenye ubaguzi.
H. T., Marekani
Watafiti wengi husema kwamba wanawake hushinda wanaume sana kwa idadi za wanaosumbuliwa. Hata hivyo, makala hizo zilikubali kwamba wanaume pia waweza kusumbuliwa, zikitaja vielelezo hususa.—Mhariri.
Makala nyingi juu ya habari hii hukazia tu kile wanawake wapaswa kufanya ili kujilinda lakini hupuuza kuwafundisha wanaume kustahi wanawake. Kwa vyovyote, ikiwa hakungekuwa na wasumbuaji, hakungekuwa na usumbuaji. Makala yenu ilizungumzia “Mwenendo Uwafaao Wanaume.” Kwa sababu ya hilo, inastahili pongezi.
O. C., Taiwan