Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 5/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matatizo ya Kiakili Yaongezeka
  • Hoja ya Mwafaka
  • Kutojali Uhifadhi
  • “Biblia Haipaswi Kuchujwa”
  • Kuepusha Msiba wa Tabia-Nchi
  • “Kubadilisha Muundo wa Familia”
  • Watoto wa Kafeni
  • Kikumbusha kwa Wapenda-Wanyama
  • Ahadi Zisizotimizwa
  • Kukabiliana na Elki
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 5/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Matatizo ya Kiakili Yaongezeka

Kikundi cha wataalamu wa afya wa duniani pote kimeonya juu ya “kiwango chenye kutisha cha matatizo ya afya ya kiakili katika mataifa yanayositawi,” lataarifu jarida First Call for Children. Watafiti katika Shule ya Kitiba ya Harvard walithibitisha idadi kubwa ya magonjwa ya kiakili ambayo “yalisababishwa na vita, misiba ya asili, kutendewa vibaya na kuuawa kimakusudi kwa wanawake na watoto, na mabadiliko katika idadi za watu, siasa na uchumi.” Kwa kuongezea, viwango vya udumavu wa kiakili na kifafa vilipatwa kuwa vimeongezeka kutoka mara tatu hadi tano katika jamii zenye mapato ya chini, na ujiuaji kimakusudi ukawa ndio kisababishi kikuu cha kifo miongoni mwa vijana. Kulingana na Dakt. Arthur Kleinman, ambaye aliongoza kikundi hicho, ni lazima afya ya kiakili ipewe uangalifu wa kimataifa. “Mataifa maskini na vilevile tajiri yamekosa kuweka rasilimali ihitajikayo ili kurudisha na kuhifadhi afya ya kiakili,” akasema.

Hoja ya Mwafaka

“Viongozi wa dini ya Othodoksi ya Urusi na wa Uislamu kutoka jamhuri nne za kiislamu hasa ambazo ni za uliokuwa Muungano wa Sovieti—Kazakhstan, Tajikistan, Turkmenistan, na Uzbekistan—wamefikia mwafaka usio na kifani wa kujumlisha dini mbalimbali ili kuzuia dini na vikundi vya kidini vyenye kuacha njia ifaayo ambavyo vinakuwa na uvutano katika Asia ya kati,” lataja gazeti Christianity Today. Wakikutana katika Tashkent, jiji kuu la Uzbekistan, viongozi hao wa kidini “waliazimia kushirikiana katika kukomesha uvutano wa Wakristo wa kievanjeli, Wabaptisti, Wamormon, na Mashahidi wa Yehova,” yasema hiyo ripoti.

Kutojali Uhifadhi

Phalarope mwenye shingo nyekundu, ndege aliye nadra kupatikana, alionekana kwenye hifadhi ya maji katika Leicestershire, Uingereza, kisha watazama-ndege kutoka kotekote Uingereza wakasafiri ili kumwona. Lakini walitazama kwa ogofyo huku samaki mwenye futi nne aitwaye pike akimmeza ndege huyo mhamaji kwa umo moja tu. “Ilikuwa kama mandhari kutoka sinema Jaws,” akasema mtazama-ndege mmoja. “Kwa sekunde moja ndege huyo alikuwa akiogelea—sekunde iliyofuata kulikuwa na mpasuko na kurushwa kwa maji naye akatoweka.” “Ni manyoya machache tu yaliyobaki kuthibitisha kwamba ndege huyo wa kigeni wa majini alikuwa amezuru hifadhi ya maji ya Leicestershire,” ikasema ripoti ya shirika la habari la Reuters.

“Biblia Haipaswi Kuchujwa”

Chini ya kichwa hicho, uhariri mmoja katika gazeti la habari The Weekend Australian ulishutumu “majaribio ya kufasili tena na kurekebisha sehemu za Biblia ili kuipatanisha na mahitaji ya kisasa.” Ingawa tafsiri nyingi mpya “zimekuwa kazi za usomi, zikifaidika na uvumbuzi mpya wa maandiko ya kale na utafiti wa kihistoria,” uhariri huo ulionya dhidi ya “kuchanganya kazi ya utafsiri na ya ufasili.” Masuala ya kubishaniwa yalikuwa miongozo ya makasisi na walimu iliyotangazwa na Baraza la Wakristo na Wayahudi katika jitihada ya kuepuka mtazamo wowote wa kupinga Wayahudi. Maneno kama vile “Wayahudi,” yanayotumiwa kuhusiana na kesi na kifo cha Yesu, yatabadilishwa kuwa “wakazi fulani wa Yerusalemu,” na maneno “Mafarisayo,” kuwa “viongozi fulani wa kidini.” Uhariri huo uliongeza hivi: “Hati za Agano Jipya si maelezo ya maoni. . . . Kuvuruga maneno na kubadili maandiko kwaweza kwa urahisi kushindwa kudhibitiwa na kutokeza utoaji usio wa kweli wa matukio ya maisha ya Kristo. Muktadha wa kijamii wa maisha yake ni lazima upatane na wakati alioishi.”

Kuepusha Msiba wa Tabia-Nchi

Tabia-nchi ya dunia itakabili msiba miaka 25 hadi 30 ijayo hatua isipochukuliwa karibuni, laonya Baraza la Ushauri wa Kisayansi la Ujerumani. “Wataalamu wanasisitiza upunguzo wa duniani kote wa mitokezo ya kaboni dioksidi (CO2) yenye kuleta mabadiliko mabaya kwa tabia-nchi kwa angalau asilimia 1 kwa mwaka,” laripoti gazeti la habari Süddeutsche Zeitung. “Ongezeko katika halijoto halipasi kuruhusiwa kupita digrii 0.2 Selsiasi kwa mwongo.” Wakosaji wakuu, wenye kuchangia asilimia 80 ya uharibifu wa tabia-nchi ya ulimwengu, ni nchi za ulimwengu uliovuvumuka kiviwanda. Kwa kielelezo, mwananchi katika Ujerumani hutokeza, kwa wastani, kaboni dioksidi mara 20 kuliko mwananchi katika India. Matatizo mengine makubwa ya kimazingira yasababishwayo na mwanadamu yalisemwa kuwa mmomonyoko wa udongo, uhaba wa maji safi, na kumalizwa kwa aina fulani za mimea na wanyama.

“Kubadilisha Muundo wa Familia”

Kupuuza watoto na jeuri kuwaelekea kwaongezeka, laripoti gazeti la habari la Brazili O Estado de S. Paulo. Ingawa huenda matatizo ya kijamii na kiuchumi yakawa kisababishi, kutendea watoto vibaya hakutukii katika sehemu zenye umaskini tu. Kulingana na Lia Junqueira, mratibu wa Kitovu cha Ushauri wa Watoto na Wabalehe, ‘hakuna tofauti yoyote kati ya matajiri na maskini—isipokuwa kwamba katika nyumba za mabanda na zilizosongamana, kila mtu husikia watoto wakilia; huku katika majumba makubwa, kuta huzima vilio hivyo.’ Paulo Victor Sapienza, mkurugenzi wa shirika la SOS Child, ahisi kwamba kuimarisha vifungo vya familia ndiko njia bora zaidi ya kupambana na tatizo hilo. “Kumweka mtoto katika shirika la utunzaji ambako hatapata upendo na shauku hakutimizi chochote,” yeye akasema. “Ni jambo la muhimu kusaidia kubadili muundo wa familia ili kwamba watoto wapate shauku na upendo nyumbani.”

Watoto wa Kafeni

Watoto wasiomakinika, wenye kusumbua-sumbua, wenye kukengeushwa kwa urahisi, na wenye kutenda kulingana na misukumo huenda wakawa wanadhuriwa na kunywa kafeni nyingi,” yasema Tufts University Diet & Nutrition Letter. Kwa mtoto mwenye uzito wa kilo 18, “mkebe mmoja wa kinywaji cha cola kuongezea nusu kikombe tu cha chai iliyobarafushwa ni sawa na vikombe vitatu vya kahawa” kwa mtu mzima. Makala hiyo ilirejezea utafiti uliofanywa na Mitchell Schare, profesa wa saikolojia kwenye Chuo Kikuu cha Hofstra, ambao ulionyesha kwamba “dalili nyingi za kunywa kafeni nyingi katika watoto hufanana na dalili za hali kama vile kasoro ya upungufu wa makini na utendaji wa kupita kiasi.” “Kabla ya kuamua mtoto wako asiyetulia mwenye kurukaruka ana hilo tatizo,” hiyo ikaongeza “huenda ukapata suluhisho kwa usumbufu huo kuwa kupunguza tu unywaji wa cola na chai.”

Kikumbusha kwa Wapenda-Wanyama

Je, wewe ni mpenda-wanyama? Ikiwa ndivyo, basi yaelekea sana mbwa mwenye urafiki ameramba uso wako au mikono yako. Hata hivyo, kulingana na Lane Graham, mtaalamu wa vimelea katika Chuo Kikuu cha Manitoba, kuna uwezekano kwamba waweza kuchukua mabuu ya vimelea au minyookuru. “Ni bora zaidi kutoruhusu mdomo wa mbwa wako kukaribia mdomo wako,” laripoti Winnipeg Free Press. Mbwa hutumia ndimi zao kujisafisha; na kwa kuwa ndimi zao ni kama ubao wa kusugulia nguo, hizo huchukua vitu vingi sana, kutia ndani uchafuzi wa kinyesi. Vijibwa “vyajulikana sana kwa kuwa wanyama waliojaa vijidudu,” gazeti hilo likataja. Ingawa hatari za kuwa mgonjwa ni chache, shauri ni “kuosha mikono na uso wako, na ule wa watoto wadogo, baada ya vipindi virefu vya kurambwa na mbwa, kwa sababu tu za usalama.”

Ahadi Zisizotimizwa

“Sawa na maendeleo yote ya kitiba yaliyoitangulia, uwanja wa tiba ya jeni ulianza kwa tumaini la wakati ujao mwangavu,” laonelea gazeti Time. “Watafiti waliahidi kutibu matatizo ya kurithiwa kama vile cystic fibrosis, kuzorota kwa misuli na sickle-cell anemia, si kwa dawa za kawaida bali kwa mazingaombwe ya badiliko la taratibu ya kijeni, kubadili jeni zenye kasoro na kuweka nyingine zisizo na kasoro.” Lakini sasa, zaidi ya miaka mitano baada ya majaribio ya kwanza ya binadamu kuidhinishwa na watu 600 kuandikishwa katika majaribio 100 ya kitiba, hakujakuwa na matokeo mazuri. “Baada ya majaribio yote na kutangazwa kupita kiasi, bado hakuna uthibitisho usiotiliwa shaka kwamba tiba ya kijeni imetibu—au hata—kusaidia mgonjwa mmoja,” lasema Time. Kwa hakika, watafiti bado hawajui njia bora zaidi ya kufikisha jeni ndani ya chembe zenye kasoro au jinsi ya kufanya mfumo wa kinga wa mwili usizikatae. “Wakati ambapo hakuna ithibati kwamba kitu kinafanya kazi,” asema mtaalamu wa jeni kwenye Chuo Kikuu cha Arizona Robert Erickson, “tiba ya kijeni haina tofauti kubwa na michanganyiko yenye kuuzwa bila kujali kama ina thamani ya kitiba.”

Kukabiliana na Elki

“Katika Sweden, nusu ya aksidenti zote za barabarani ziripotiwazo polisi, huhusisha mgongano na wanyama wa porini,” laripoti gazeti New Scientist. Kati ya Wasweden 12 na 15 hufa kila mwaka likiwa tokeo la migongano hiyo. Hasa wenye kuleta hangaiko ni elki wa Ulaya, ambao waweza kukua hadi kilo 800 na hawahofu magari kisilika. Katika Finland iliyo jirani, elki ni ‘kisababishi cha pili cha aksidenti za barabarani, baada ya alkoholi,’ lasema gazeti Newsweek. Ili kusaidia kukabiliana na tatizo la elki, kampuni ya Sweden ya magari, Saab, hufanya majaribio ya migongano, ikitumia elki bandia, ili kutahini usalama wa magari yayo. Na maofisa katika Finland wametenga dola milioni 22 kwa ujenzi wa mahandaki ya kutumiwa na elki chini ya barabara zenye magari mengi. ‘Mahandaki hayo yatajengwa ili elki waone upeo-macho mwishoni mwa handaki, nayo yatapandwa mimea ambayo elki hupenda sana,’ lasema Newsweek. “Wakati wa kipindi cha uzazi, elki hawatazami kulia wala kushoto kabla ya kuvuka barabara.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki