Kuutazama Ulimwengu
Makosa ya Usahihishaji Katika Biblia
“Ilikuwa kawaida kupata makosa ya uchapishaji katika Biblia katika karne ya 17 na 18,” lasema gazeti Bible Review, “lakini hiyo haimaanishi kwamba makosa hayo yaliachiliwa tu.” Kwa mfano, ile iliyoitwa Biblia Pumbavu ilitolewa wakati wa utawala wa Charles wa Kwanza. Katika Zaburi 14, wachapishaji waligeuza neno kimakosa. Basi mstari wa kwanza ukasema: “Mpumbavu amesema moyoni, kuna Mungu.” Kosa hilo lilifanya wapigwe faini ya pauni 3,000. Kampuni nyingine, Barker and Lucas, ilipigwa faini ya pauni 300 mwaka wa 1631 kwa kuacha neno moja katika ile iliyoitwa Biblia ya Uzinzi. Faini hiyo iliwafilisisha. Tafsiri yao ilisema: “Ufanye Uzinzi.” Vilevile kulikuwa na ile iliyoitwa Biblia ya Endelea Kufanya Dhambi, ya mwaka wa 1716. Mahali ambapo Yesu alimwambia mtu aliyeponywa ‘asiendelee kufanya dhambi,’ Biblia hiyo inamtaja akisema “endelea kufanya dhambi.” Pia hatuwezi kusahau Biblia ya Siki, iliyochapishwa mwaka wa 1717. Kichwa cha Luka sura ya 20 chasema, “Mfano wa Siki,” badala ya kusema, “Mfano wa Shamba la Mizabibu.”
Polisi Wenye Viatu Vyenye Magurudumu
Ili wafaane zaidi na watu katika maeneo yao, polisi wengine kule Amerika Kaskazini wanavaa viatu vyenye magurudumu. Vilevile kushika doria kwa miguu, kwa farasi, na kwenye baiskeli kunaanza kuongezeka, laripoti The Toronto Star. Polisi wanatumia viatu vyenye magurudumu katika majiji makubwa kama Chicago, Miami, na Montreal. Mmojawapo wa polisi wa kwanza kutumia viatu vyenye magurudumu, Sajini Bill Johnston wa kikosi cha polisi cha Fort Lauderdale, asema: “Ilikubaliwa sana na polisi tangu mwanzoni kabisa. Ukivaa viatu vyenye magurudumu, kwa njia fulani unafaana zaidi na watu, na kuwa mwenye kufikiwa kwa urahisi.” Gazeti The Toronto Star lasema kwamba “kuna manufaa ya kuvaa viatu vyenye magurudumu—kama vile kuwafumania wezi wa magari kwenye maegesho.”
Dira ya Samaki
Samaki aina ya rainbow trout hujuaje wanakokwenda? Wanabiolojia wa New Zealand wamepata kwamba samaki hao wana “dira yenye sumaku kwenye pua zao,” laripoti gazeti New Scientist. Ndege wengi na reptilia wengi na baadhi ya mamalia pia wanaweza kujua wanakokwenda kwa kuongozwa na nguvu za sumaku ya dunia. Lakini wanasayansi hawakuwa wamepata kamwe kugundua chembe zinazotambua kaskazini ambazo zinaaminiwa kuwa zina madini yaitwayo maginetiti yenye sumaku. Katika samaki hao, watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Auckland waligundua uzi wa neva uliokuwa kwenye uso wa samaki huyo ambao huchochewa unapohisi sumaku. Kuchunguza uzi huo kuliwapeleka hadi sehemu ya nyuma ya pua ya samaki huyo, ambako walipata chembe za neva zenye maginetiti.
Ujeuri wa Kandanda
Ushindani mkali baina ya timu zilizokuwa zikipambana katika mchuano wa kandanda wa Kombe la Dunia mwaka uliopita ulikuwa ukianzisha sherehe ambazo mara nyingi zilisababisha ghasia. Nchini Mexico, zaidi ya polisi 1,500 waliitwa kuwadhibiti mashabiki wa timu ya Mexico. Zaidi ya watu 200 walizuiliwa na polisi, laripoti gazeti la Mexico El Universal. Fataki moja iliyorushwa wakati wa ghasia hizo ililipuka kwenye uso wa shabiki mmoja mchanga ikaharibu sehemu ya fuvu lake. Nchini Argentina, Ubelgiji, na Brazili, sherehe vilevile ziligeuka zikawa mbaya, zikisababisha majeraha na kukamatwa kwa watu. Nchini Ufaransa, laripoti gazeti Excelsior la Mexico City, watu wapatao 1,000 walikamatwa kuhusiana na mechi za Kombe la Dunia, na 1,586 walipigwa marufuku kurudi nchi hiyo.
Mikono Yako na Afya
“Mtu anapopiga chafya na kufunika mdomo wake kwa mikono au akipenga makamasi, anahitaji kunawa mikono kabla hajashika simu wala vitasa vya mlango,” lasema The Medical Post la Kanada. Gazeti The Post lilinukuu Shirika la Marekani la Wataalamu wa Kudhibiti Maambukizo na Mweneo wa Magonjwa, ambalo linasema kwamba “asilimia 80 ya magonjwa ya kawaida huenezwa hasa kwa mikono na kugusana, wala si kupitia hewa.” Dakt. Audrey Karlinsky wa Chuo Kikuu cha Toronto apendekeza kunawa mara kwa mara na kusugua mikono kwa kutumia sabuni “kwa angalau sekunde 10 hadi 15, ukihakikisha kwamba umeondoa uchafu ulio katikati ya vidole na chini ya kucha.” Apendekeza kwamba baada ya kunawa hivyo, unapaswa kusuuza mikono kwa maji moto na kutumia karatasi kufunga mfereji. Unaweza kuwafanyaje watoto wako wanawe mikono kwa muda wa kutosha? Uwafanye waseme alfabeti yote wanaposugua mikono wakitumia sabuni, apendekeza Dakt. Karlinsky.
Kirusi Kipya cha Damu
Kufuatia kugunduliwa kwa kirusi kipya katika damu ya watoa-damu kule Ulaya, maofisa wa afya nchini Ufaransa wameamua kuweka “kikundi cha kudumu cha wanasayansi wa uchunguzi,” laripoti gazeti Le Monde la Ufaransa. Kijidudu hicho, kinachoitwa kirusi kinachoambukizwa kupitia damu (TTV), kilitambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Japani mwaka wa 1997, ambako asilimia 10 ya watoa-damu wana kirusi hicho. Bado madaktari hawajajua athari hasa za kirusi hicho, lakini uchunguzi nchini Uingereza uligundua kwamba kirusi cha TTV kilipatikana miongoni mwa asilimia 25 ya kikundi cha wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa mbaya wa ini ambao haujulikani. Kwa wakati huu, hakuna mbinu sanifu ya kuchuja kirusi hicho, lasema Le Monde.
‘Tetemeko la Jua’ la Kwanza Kupimwa
Watafiti Valentina Zharkova wa Chuo Kikuu cha Glasgow cha Scotland na Alexander Kosovichev wa Chuo Kikuu cha Stanford, California, wamegundua ‘tetemeko la jua’ kwa mara ya kwanza walipokuwa wakichunguza picha zilizopigwa na chombo cha angani kiitwacho Soho cha Shirika la Anga la Ulaya. “Tetemeko hilo lilitokea baada ya mwako wa kadiri—ambao ulikuwa mlipuko wa hidrojeni na heli juu ya uso wa Jua—kugunduliwa mwezi wa Julai 1996,” laripoti The Daily Telegraph la London. Tetemeko hilo lilifikia kiwango cha 11.3 na kusababisha mitikiso iliyofikia kimo cha kilometa tatu na vijiwimbi vinavyofanana na vile vinavyotokea kwenye kidimbwi jiwe liangushwapo ndani yake. Vijiwimbi hivyo vilisafiri hadi kilometa 120,000 kwenye uso wa jua, vikifikia mwendo wa kilometa 400,000 kwa saa moja. ‘Tetemeko hilo la jua’ lilitoa nishati inayotoshana na ile Marekani hutumia kwa miaka 20 na lilikuwa na nguvu mara 40,000 kuliko tetemeko la dunia la San Francisco la 1906, lililofikia kiwango cha 8.3 kwenye kipimo cha Richter.
Shangwe Tele-Kazi Nyingi Zaidi
“Wenzi wengi wa ndoa walio wachanga hawajui vizuri kazi za ziada zinazotokea wanapopata mtoto. Jambo hilo mara nyingi hutokeza ubishi baina ya wenzi baada ya kuzaliwa kwa mtoto,” laandika Nassauische Neue Presse la Ujerumani. Uchunguzi uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Groningen, nchini Uholanzi, ulionyesha kwamba akina mama wachanga mara nyingi hawaridhiki kwa sababu ya mabadiliko makubwa yaletwayo na kuzaliwa kwa mtoto. Kwa wastani, akina mama wanahitaji muda wa saa 40 zaidi kwa juma moja kwa ajili ya mtoto—na kati ya hizo muda wa saa 6 hutumiwa kufanya usafi wa ziada, kufua, na kupika kunakohitajiwa na muda wa saa 34 hutumiwa kumlea mtoto moja kwa moja. Kwa akina baba, muda wa saa 17 unaotumiwa moja kwa moja na mtoto ndio utendaji wa ziada tu ambao wanao. Kulingana na ripoti hiyo, mkazo katika ndoa “hauhusu hasa masuala kama vile ni nani anayembadilishia mtoto nepi au anayeamka usiku kumpa chupa ya maziwa, bali wahusu kugawa kazi za nyumbani.”
Televisheni na Aksidenti
Watoto wanaotumia muda mwingi wakitazama televisheni huenda wakawa na mielekeo ya kujaribu kuiga michezo hatari wanayotazama. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na mtafiti Mhispania Dakt. José Umberos Fernández, uwezekano wa mtoto kujeruhiwa huongezeka kwa kila muda wa saa anaotumia kutazama televisheni. Fernández apendekeza kwamba hilo hutukia kwa sababu televisheni hupotoa uhalisi wa mambo. Wazazi wanaweza kufanya nini ili kuondoa tatizo hilo? Kulingana na gazeti la Kigiriki To Vima, wazazi wanapaswa kushiriki kuchagua programu ambazo watoto wao hutazama na kuwasaidia “kutazama [vipindi] kwa umakini sana,” badala ya kukubali kila kitu wanachoona kuwa halisi.
Watoto na Kafeini
Hata kama watoto hawanywi kahawa wala chai, wengi hupata kafeini nyingi katika vinywaji vyenye kaboni na chokoleti hivi kwamba wanaweza kupatwa na madhara ya kuacha kafeini wanapoacha kunywa vinywaji hivyo, laripoti gazeti The New York Times. Kikundi cha wataalamu wa akili wakiongozwa na Dakt. Gail A. Bernstein, wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Minnesota, kilitilia maanani jinsi kafeini inavyoathiri umakini wa watoto wapatao 30 wenye umri wa kwenda shule. Watoto hao waliongeza kafeini mwilini kwa kadiri inayolingana na kunywa mikebe mitatu ya cola kila siku. Baada ya juma moja watoto hao waliacha kafeini kwa siku moja. Siku hiyo na juma lote lililofuata, umakini wa watoto hao ulipunguka kwa ghafula. “Njia bora ya kuzuia tukio hili,” wakasema watafiti hao, “ni kuwazuia watoto wasinywe vinywaji vingi vyenye kafeini.”