Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mhudumu wa Wakati Wote Asiyejiweza Kwa miaka mingi ambayo imepita makala nyingi zimegusa moyo wangu—lakini hakuna iliyougusa kwa kina kama jambo lililoonwa la Gloria Williams, “Risasi Ilibadili Maisha Yangu.” (Oktoba 22, 1995) Matatizo yangu yawa madogo sana yakilinganishwa na yake! Asanteni kwa kutupatia chakula cha kiroho chenye thamani jinsi hiyo na kitia-moyo.
E. L., Kanada
Ono hili lilinikumbusha kwamba haidhuru twajipata katika hali gani, hata ziwe mbaya namna gani, twaweza kusali kwa Yehova na kumwomba msaada. Nina wakati mbaya sana shuleni sasa, nami huvunjika moyo. Lakini kusoma makala hii kulinitia moyo sana.
M. S., Japani
Nilipokuwa nikisoma simulizi la Gloria Williams, nilikuwa na machozi machoni mwangu. Lilinitia moyo kuendelea kutoa yaliyo bora kadiri niwezavyo katika utumishi wa shambani, licha ya kuishi katika nyumba iliyogawanyika kidini.
F. C., Italia
Makala hiyo imenitia moyo kuendelea kuvumilia katika mradi wangu wa kuhubiri wakati wote. Ikiwa Gloria Williams aweza kufanya hivyo, basi kwa nini nisiweze—wakati niko na sehemu zote za mwili wangu?
I. O. A., Nigeria
Mbao Nina umri wa miaka 11, nami nilifurahia sana makala “Kwa Nini Kujenga kwa Mbao?” (Oktoba 22, 1995) Ilinisaidia kuthamini nguvu na uwezo wa Yehova. Pia ilinivuta karibu zaidi naye na Mwana wake, Yesu Kristo, kwa sababu natambua jinsi wao walivyo na ujuzi mwingi.
A. B., Marekani
Kwa Nini Ningali Mseja? Asanteni sana kwa makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Kila Mtu Anafunga Ndoa ila Mimi?” (Oktoba 22, 1995) Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanaofunga ndoa wakiwa wachanga mno katika eneo hili. Wengine wana wasiwasi sana kunihusu, kwa kuwa nina umri wa miaka 18 na sina rafiki mvulana. Makala hiyo ilifika kwa wakati ufaao kabisa kunisaidia kudumisha mtazamo uliosawazika.
S. Z., Ujerumani
Nikiwa mseja mwenye umri wa miaka 19, mara nyingi mimi hujiuliza nina mapungukio katika sehemu zipi hivi kwamba hakuna anayeonyesha upendezi kunielekea. Baadhi ya wasioamini wameonyesha upendezi, lakini si aina ya uangalifu ninaotaka. Makala hiyo ilinisaidia kuona kwamba subira yahitajiwa na kwamba lililo la maana zaidi ni kwamba nampendeza Yehova.
J. G., Marekani
Nikiwa mwanamume mseja mwenye umri wa miaka 38, nimepata nikijiuliza swali lililozushwa katika kichwa cha hiyo makala. Nikiwa nimevumilia kukataliwa kusiko na hesabu na akina dada waseja Wakristo, najua vyema sana maumivu yasababishwayo na “kilichotarajiwa kikikawia kuja.” (Mithali 13:12) Ni jambo lenye kutoa uhakikisho kujua kwamba Yehova hufikiria hisia za Wakristo waseja katika hali hizi kuwa halali na kwamba yeye huthamini uvumilivu wetu wenye ushikamanifu.
D. T., Marekani
Msanii Mkuu Kuliko Wote Baada ya kusoma mfululizo “Kumtafuta Msanii Mkuu Kuliko Wote” (Novemba 8, 1995), ninasukumwa kuonyesha uthamini wangu. Nimeona programu nyingi sana za mambo ya asili kwenye televisheni ambazo hukosa kumpa sifa Mbuni Mtukufu. Hata hivyo, Amkeni! kwa kuendelea humpa sifa Mungu wetu mtukufu, Yehova.
E. Z., Marekani
Ni njia mpya nzuri kama nini ya kumfikiria Yehova! Ubora wa sanaa yake kwa kweli hauna kifani, sawa na ulivyo wingi usiolinganika wa kazi yake. Ningependa pia kuongeza pongezi kwa wasanii wengi wenye vipawa wanaofanya Amkeni! livutie ili livute watu kwa Yehova Mungu.
M. Q., Marekani