Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Miaka 50 Iliyopita Nimetoka tu kumaliza kusoma ule mfululizo “1945-1995—Tumejifunza Nini?” (Septemba 8, 1995) Nilipendezwa na jinsi mlivyotia ndani hayo mambo yote ya historia katika nafasi ndogo hivyo. Nilijifunza mengi; ilikuwa bora kuliko kusoma kitabu cha historia.
M. V., Filipino
Sala Mimi sijaajiriwa na naelekea kuhama. Nilikuwa na hangaiko sana—hadi niliposoma makala “Maoni ya Biblia: Fungu Lako Katika Sala Zako.” (Septemba 8, 1995) Asanteni kwa kuchapisha makala hii. Nitajitahidi kuthibitisha kwamba natamani sala zangu zijibiwe kwa kuishi kupatana nazo.
D. C., Marekani
Uchezaji Kamari Hivi majuzi nilisali nipate makala juu ya kamari, kwa kuwa watu wangu wa ukoo wanahitaji msaada sana juu ya jambo hilo. Wako karibu sana kufilisika. Natumaini mfululizo wa “Uchezaji Kamari—Uraibu Unaoongezeka” (Septemba 22, 1995) utawasaidia. Wao huteseka sana kwa sababu ya uraibu wao. Tulikuwa tukicheza mchezo wa karata uitwao poka tukiwa familia kwa muda wa saa 6 hadi 12 kwa wakati mmoja! Sasa nafurahi kwamba niko na Yehova katika maisha yangu.
L. D., Marekani
Mlifafanua miaka 20 ya ndoa kama yangu kwa mume aliye na uraibu wa kucheza kamari. Nimepata kitia-moyo kingi sana kutoka magazeti haya wakati uliopita, lakini wakati huu nimepata kitu ambacho nimekuwa nikitamani kwa miaka 20!
F. E., Japani
Mbinu za Kujikinga Nilithamini ile makala “Vijana Huuliza . . . Je, Nijifunze Mbinu za Kujikinga?” (Septemba 22, 1995) Hapa Ukrainia sisi hupata toleo moja tu la Amkeni! kila mwezi, na “Vijana Huuliza . . .” hukosekana. Kwa kuwa mimi husoma Kiingereza, niliweza kusoma makala hiyo. Ilinisaidia kujua maoni ya Mungu.
V. L., Ukrainia
Nina umri wa miaka 12, na nataka kuwashukuru kwa makala mnazochapisha. Nilipata ile makala kuhusu kujikinga kuwa yenye msaada hasa. Ilinisaidia kuelewa vizuri jinsi ya kujiendesha wakati wanashule wenzangu wanaponinyanyasa.
D. C., Italia
Shule ya Kiafrika Mimi ni Mwakan ambaye amenufaika sana na shule ya kidesturi ya Kiafrika na shule za Magharibi, na nilifurahia makala yenu “Ile Shule ya Kiafrika—Ilifunza Nini?” (Septemba 22, 1995) Nilivutiwa na staha na adhama mliyoipa ile shule ya Kiafrika. Kuna wale ambao hufikiri kwamba dini yenu hudharau desturi ya Kiafrika. Makala hii yaonyesha kwamba sivyo.
S. N., Ghana
Simulizi la Maisha Nawashukuru sana kwa kuchapisha simulizi la Karen Malone, “Pigano Langu Gumu na Lililo Refu la Kutafuta Dini ya Kweli.” (Septemba 22, 1995) Lilifanya nilie machozi ya shangwe.
J. S., Jamhuri ya Cheki
Mimi ndiye mtoto mkubwa zaidi katika familia. Nilikuwa nikikosa furaha kwa sababu sikuweza kuwa na vitu vingi nilivyotaka. Wakati mwingine hatukuwa na pesa za kutosha za kununua chakula. Lakini kwa sababu ya Karen, sasa natambua kwamba utumishi wetu kwa Mungu ni wa maana zaidi kuliko vitu vya kimwili.
T. T., Ugiriki
Kufikia sasa nimesoma makala hiyo mara nne, na kila wakati nimechochewa mpaka kutoa machozi. Niliweza kuelewa azimio lake la kutumikia Yehova kwa kukabiliana na upinzani wa familia na magumu. Hivi karibuni, natumaini kuanza kutumikia nikiwa painia wa kawaida, mweneza-evanjeli wa wakati wote, na makala hii imenitia moyo kwelikweli.
D. F., Australia