Kuutazama Ulimwengu
Wakatoliki Wapeleka Maombi kwa Papa
Mwishoni mwa 1995, Wakatoliki wa Ujerumani walitayarisha maombi yanayodai marekebisho yafanywe katika kanisa, laripoti Süddeutsche Zeitung. Hayo maombi, yaliyotiwa sahihi na watu wapatao milioni 1.6, yaliomba kanisa liruhusu makasisi kufunga ndoa, kuruhusu wanawake wawe makasisi, na kanisa kubadili msimamo walo juu ya mambo ya ngono na kupanga uzazi. “Mtu tunayemwendea hasa ni papa,” aeleza Christian Weisner, mwanzilishi wa maombi hayo. Gazeti hilo lilisema kwamba Karl Lehmann, msimamizi wa Baraza la Maaskofu wa Ujerumani alikataa kabisa maombi hayo, akidai kwamba hilo lingetokeza mgawanyiko kati ya Wakatoliki wenye kufuata desturi na wale wenye kupendelea marekebisho. Hata hivyo, Lehmann alisafiri Vatikani na kupeleka hayo maombi mbele ya papa.
“Sekunde ya Ziada” Yaongezwa kwa 1995
Yaonekana kwamba mzunguko wa dunia si njia bora zaidi ya kupima wakati. Kulingana na The New York Times, wanasayansi wana njia iliyo sahihi zaidi ya kupima wakati—atomi ya sizi. Ikitumiwa ikiwa mtambo wa kuendesha saa ya atomi, atomi ya sizi hutikisika mara 9,192,631,770 barabara kwa sekunde moja. Kwa kiwango hicho, saa hiyo ya atomi yaweza “kukosea kwa karibu sekunde moja kwa miaka 370,000.” Kwa kulinganisha, mzunguko wa dunia si sahihi kwa karibu mara milioni moja, na hiyo ndiyo sababu “sekunde ya ziada” ni lazima iongezwe mara kwa mara. Shirika moja la kimataifa la watunza-wakati liliamua kuongeza “sekunde ya ziada” kama hiyo mwishoni mwa 1995. Hilo liliruhusu “mzunguko wa sayari yetu na mwendo wa wakati” upatane. Hata hivyo, wanasayansi hawastahili kupata sifa kwa ugunduzi huu. Kwani, “miendo ya vipande vilivyo ndani ya saa ya atomi huiga, kwa kiwango kidogo, utaratibu mkuu wa mifumo ya sayari,” lasema Times.
Vitoto na Tekinolojia
“Watoto wengi zaidi na zaidi wanapata kujua kompyuta kabla ya wao kujua kusoma na kuandika,” laripoti The Globe and Mail la Kanada. Vitoto vingine ambavyo havijajifunza kutembea au kusema tayari vinatumia kompyuta. Hata vitoto ambavyo haviwezi kukaa vyenyewe vinafundishwa stadi za tekinolojia vinapoketi katika mapaja ya wazazi wavyo. Hiyo mbio ya kufundisha vitoto kompyuta mara nyingi hutoka kwa wazazi wanaotamani watoto wao wafanye vizuri shuleni. Kwa kuongezea, kampuni nyingi za kutengeneza programu za kompyuta hutangaza bidhaa zao kuwa njia za kujifunza kwa watoto. Hata hivyo, wazazi fulani wanatilia shaka mkazo uwekwao juu ya kuwasiliana na mashine badala ya kuwasiliana na watu, katika umri huo mchanga. Mama mmoja alisema: “Hatusitawishi uhusiano wowote pamoja na kompyuta, au angalau sifikiri twapaswa kufanya hivyo.”
Suluhisho Rahisi
Katika Japani hesabu ya maiti zinazotolewa kwa ajili ya utafiti wa kitiba imeongezeka katika miaka ya majuzi. Kulingana na The Daily Yomiuri, Wizara ya Elimu yasema kwamba “mwili mmoja wahitajika kwa kila wanafunzi wawili wa kitiba na [mmoja] kwa kila wanafunzi wanne wa meno, jambo linalofanya idadi ya miili inayohitajika nchini kote kuwa 4,500 kila mwaka.” Lakini kwa nini kuna watu wengi zaidi wanaotoa miili yao kuliko idadi ya miili inayohitajika hasa? Ukosefu wa ardhi kwa ajili ya makaburi na kudhoofika kwa vifungo vya familia ni miongoni mwa sababu zilizodokezwa.
UKIMWI Wapita Visa 500,000 Marekani
Kwa mara ya kwanza, kufikia Oktoba 31, 1995, jumla ya idadi ya visa vilivyoripotiwa vya UKIMWI Marekani imepita nusu-milioni, lasema jarida The Journal of the American Medical Association. Kwa idadi hiyo, watu 311,381—asilimia 62—tayari walikuwa wamekufa kutokana na maradhi hayo. Jambo jingine baya lenye kutukia ni ukuzi wenye kuendelea wa UKIMWI kupitia ngono ya jinsia tofauti. Hilo jarida lilionyesha kwamba tangu 1981 hadi 1987, uwiano wa visa vya UKIMWI miongoni mwa wanawake ulikuwa asilimia 8 pekee, lakini tokea 1993 hadi 1995, hesabu hiyo ilikuwa imepanda ikawa asilimia 18.
Waraibu wa Mfumo wa Kompyuta
Zoea la kuunganisha mifumo ya kompyuta na simu (Internet) limetokeza ugonjwa mpya uitwao “Kasoro ya Uraibu wa Internet.” Kulingana na New Scientist, “wale wanaougua tatizo hilo linalofanana na uraibu wa alkoholi wanatafuta msaada kwa wingi zaidi kwa vikundi vyenye kutoa msaada na tiba ili kutibu uraibu wao.” Dakt. Ivan Goldberg, mtaalamu wa matatizo ya akili wa New York, ameanzisha Kikundi Chenye Kutegemeza Waraibu wa Internet ili kusaidia wale “wanaojitahidi kuuacha” mfumo huo wa habari. Ishara za kasoro hiyo zatia ndani “uhitaji wa kutumia wakati mwingi zaidi na zaidi katika Internet ili kuridhika, na kupata fantasia au ndoto juu ya Internet.” Gazeti hilo lasema Goldberg amepokea “itikio kutoka kwa zaidi ya watu 20 wasemao kwamba Internet imeharibu maisha yao.”
Nuru ya Jua Huongeza Motisha
Kuingiza nuru zaidi ya jua katika jengo hutokeza “matokeo ya juu zaidi ya kazi” na “kupoteza siku chache zaidi kwa sababu ya wafanyakazi wachache zaidi kukosa kufika kazini,” laripoti The Wall Street Journal. Ingawa awali ubuni huo wa ujenzi ulitumiwa ukiwa njia ya kuhifadhi nishati, ubuni wa ujenzi ambao unaleta nuru ya jua mahali pa kazi unatokeza manufaa makubwa ya motisha iliyoboreshwa ya wafanyakazi. Kwa kielelezo, wakati kampuni kubwa mno ya ndege, Lockheed Corporation, ilipofungua ofisi mpya katika Sunnyvale, California, ubuni wayo wa kuhifadhi nishati “ulipunguza gharama za nishati kwa nusu.” Lakini Lockheed haikutarajia kwamba wafanyakazi wangependa makao yao mapya hivi kwamba “kukosa kuja kazini kukapungua” kwa asilimia 15. Mafaa ya kuruhusu nuru zaidi ya jua ndani ya jengo hayajakosa kuonwa na wenye maduka ya rejareja. Muuzaji mmoja alipata kwamba mauzo “yalikuwa juu zaidi” katika maduka yatumiayo nuru ya kawaida kuliko yale yatumiayo taa.
Ulimwengu Wenye Kutunza Maji
“Vita vya karne ijayo vitapiganwa kwa sababu ya maji,” aonya Ismail Serageldin, naibu-msimamizi wa Benki ya Ulimwengu. Kulingana na Serageldin, nchi 80 tayari zina upungufu wa maji unaotisha afya na uchumi. Lakini tatizo si kwamba hakuna maji ya kutosha duniani. “Jumla ya maji yote safi kwenye Dunia yazidi mahitaji yote kabisa ya wanadamu,” asema mtaalamu wa maji Robert Ambroggi. Matatizo mengi husababishwa na usimamizi mbaya wa maji. Nusu ya maji ambayo hutumiwa kwa unyunyiziaji ama hupenya chini ama hugeuka hewa. Mifumo ya ugavi ya maji ya majiji huvuja asimilia 30 hadi 50 ya maji yayo, na nyakati nyingine hata zaidi. “Wakati waja,” lasema The Economist, “ambapo ni lazima maji yatunzwe yakiwa mali yenye thamani kubwa, kama mafuta, si kitu cha bure kama hewa.”
Kulala Usingizi Bila Maumivu
Aina fulani za dawa za kununuliwa tu dukani zaweza kuchangia hali ya kukosa usingizi, yaripoti Tufts University Diet & Nutrition Letter. “Hiyo ni kwa sababu baadhi ya dawa mashuhuri za kuondoa maumivu zina kafeni nyingi kufikia, au kuzidi, kikombe kimoja cha kahawa.” Kafeni—kichochezi hafifu—mara nyingi huongezwa kwenye asprini na dawa nyinginezo za kuondoa maumivu ili kuongeza ubora wayo. Hata baadhi ya dawa nyinginezo zijulikanazo sana zina kafeni kufikia miligramu 130 katika tembe mbili za kumezwa pamoja. Hilo “lashinda kwa mbali miligramu 85 ipatikanayo katika kikombe kimoja cha [kahawa] ya kawaida.” Basi karatasi hiyo ya habari yapendekeza kuchunguza kibandiko cha dawa ya kuondoa maumivu ikiwa kina “dawa zenye kutenda” ili kuona ikiwa kuna kafeni.
‘Kifua-Kikuu Changoja Kulipuka’
Aina mpya za kifua-kikuu zenye kukinza dawa nyingi zinaua watu 10,000 India kila juma, laripoti gazeti la habari Indian Express. Kulingana na Kraig Klaudt wa Shirika la Afya Ulimwenguni, India “imekalia kifua-kikuu kinachongoja kulipuka.” Ulimwenguni pote, watu bilioni 1.75 wameambukizwa na bakteria ya kifua-kikuu. Kikundi cha wataalamu, waliokusanywa kutoka nchi 40 kwa ajili ya mkutano uliodhaminiwa na jarida la kitiba la Uingereza The Lancet, chasema kwamba makampuni ya dawa hayataki kutumia pesa zinazohitajika ili kutokeza dawa kwa sababu visa vingi hutukia katika nchi maskini zaidi zinazoendelea.
Wezi Wasioadhibiwa
Kulingana na takwimu za 1994, katika Italia “wale wafanyao unyang’anyi wana uwezekano wa asilimia 94 wa kuepuka adhabu,” na “wale wafanyao unyang’anyi wa kimabavu wana uwezekano wa asilimia 80 wa kuepuka adhabu,” laripoti gazeti la habari la Italia La Repubblica. Tarakimu hizo zilitokana na ripoti ambazo wenye mamlaka za kihukumu walipokea kutoka kwa mashirika ya kutekeleza sheria. Ikiwa wizi mwingi ambao hauripotiwi ungetiwa ndani, asilimia ya uhalifu usioadhibiwa ingekuwa hata juu zaidi.
Familia za Italia Zabadilika
Kulingana na uchunguzi mmoja kuhusu familia za Italia, watu wengi zaidi wasiofunga ndoa wanaishi pamoja na wenzi wengi zaidi waliofunga ndoa wanatengana au kutalikiana, laripoti La Repubblica. Kila mwaka ndoa 18,000 hufunganishwa ambamo angalau mmoja wa wenzi hao anafunga ndoa ya pili. Miungano hiyo mipya ya ndoa mara nyingi hutokeza familia zilizo kubwa ambazo zatia ndani watoto kutoka ndoa za awali. Mwelekeo huo, pamoja na ongezeko la familia za mzazi mmoja, unabadili kwa kasi na kwa njia kubwa muundo wa familia ya kidesturi ya Italia.