Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kifua Kikuu—“Dharura ya Duniani Pote”
  • Kuchimba ili Kupata Sodoma na Gomora
  • Hatari ya Muziki Wenye Sauti ya Juu
  • Ongezeko la Mwenendo Usiofaa Miongoni mwa Wanawake
  • Baadhi ya Wasiokwenda Kanisani Bado Husali Kibinafsi
  • “Biashara” ya Pili kwa Ukubwa Ulimwenguni
  • Ubatizo Wauzwa
  • Kuwa Mama Kabla ya Kukomaa
  • Viwango vya Televisheni Vyashuka
  • Askofu Atilia Shaka Hekima ya Biblia
  • Shangwe ya Ushindi na Huzuni
    Amkeni!—1997
  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
    Amkeni!—1999
  • Kifua Kikuu Charudi kwa Pigo!
    Amkeni!—1996
  • Muungano Hatari
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kifua Kikuu—“Dharura ya Duniani Pote”

Kila mwaka kifua kikuu (TB) huua watu wazima wengi zaidi kuliko UKIMWI, malaria, na maradhi ya kitropiki yakijumlishwa pamoja, lataarifu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Kila sekunde, mtu fulani mahali fulani anaambukizwa kifua kikuu. Ile bacillus ya kifua kikuu yaweza kupitishwa kwa kukohoa au kupiga chafya. WHO latarajia kwamba katika kipindi cha miaka kumi ijayo, watu milioni 300 wataambukizwa kifua kikuu na watu milioni 30 watakufa kutokana nayo. Vibaya hata zaidi, kuzuka kwa aina za kifua kikuu zenye kukinza dawa hutisha kufanya maradhi hayo yawe yasiyotibika. Kulingana na WHO, “ni asilimia 5-10 ya watu ambao wanaambukizwa kifua kikuu ambao huwa wagonjwa au kuweza kuambukiza wengine, kwa sababu mfumo wa kinga ‘huwekea ukuta’ vijiumbe vya kifua kikuu.” Hata hivyo, mweneo huo ni mbaya sana hivi kwamba WHO liliutangaza kuwa “dharura ya duniani pote”—tangazo la kwanza la aina hiyo katika historia ya WHO.

Kuchimba ili Kupata Sodoma na Gomora

Waakiolojia Wasweden wadai kwamba wamepata Sodoma na Gomora ya kale. Kwa kushirikiana pamoja na Amman Department of Antiquities, wanasayansi hao walifanya ugunduzi wao El Lisan, mashariki ya Bahari Iliyokufa, katika Yordani. Gazeti la habari la Sweden Östgöta-Correspondenten hueleza kwamba kupata mabaki ya majengo yaliyoharibiwa miaka ipatayo 1,900 kabla ya Kristo kwashangaza. Waakiolojia hao wanasadiki kwamba wamepata Sodoma na Gomora. Baada ya kuchanganua vyombo vya udongo, kuta, makaburi, na mawe ya bunduki, mkataa wao ulikuwa kwamba majiji hayo yaliharibiwa na msiba wa asili. Hata hivyo, Biblia huonyesha kwamba Mungu mwenyewe alileta uharibifu huo kwa sababu ya ukosefu wa adili mbaya sana wa majiji hayo.

Hatari ya Muziki Wenye Sauti ya Juu

Maonyesho ya roki yaweza kusababisha kupoteza kusikia kabisa, laripoti gazeti New Scientist. Mtaalamu wa usikiaji Mfaransa Christian Meyer-Bisch alichunguza watu 1,364 kati ya umri wa miaka 14 na 40 na kugundua kwamba asilimia kubwa ya waenda-maonyeshoni kwa kawaida walipatwa na uziwi wa muda. Meyer-Bisch aonya kwamba kwa sababu ya kupendwa sana kwa maonyesho ya roki, athari hizi zenye kudhuru “si tatizo tena kwa mtu mmoja bali kwa afya ya umma.”

Ongezeko la Mwenendo Usiofaa Miongoni mwa Wanawake

• Gazeti Sunday Mail la Brisbane laripoti kwamba wanawake wachanga katika Australia wanatumia lugha mbaya kwa idadi zenye kuongezeka. Profesa Max Brandle, mkurugenzi wa Taasisi ya Australia ya Lugha za Kisasa, aeleza: “Unapata kwamba wanawake sasa hunywa zaidi, huvuta sigareti zaidi kuliko zamani wakilinganishwa na wanaume. Pia wanazidi kutumia lugha chafu. Kwa kuhuzunisha, tokeo moja ni kwamba baadhi ya adabu za kidesturi kati ya wanawake na wanaume zimekwisha. Jinsia zote mbili zitumiapo lugha chafu, hali ya kimahaba ya wakati uliopita yatoweka haraka. Lugha ya mahaba iliyotumiwa na vizazi vya mapema haimo katika jamii wakati huu. Napata kwamba lugha chafu ni ya kawaida sana miongoni mwa vijana leo.”

• Katika Brazili kiwango cha uhalifu unaofanywa na wanawake kilirudufika katika 1995. Kulingana na ofisa wa polisi Francisco Basile, wanawake wengi zaidi wanahusika katika kutendea watu vibaya, unyang’anyi, na hata ulanguzi wa dawa za kulevya, laripoti gazeti la habari O Estado de S. Paulo. Wanawake wengi wanaanza maisha yao ya uhalifu kwa kuvuta kraki kwenye karamu ambazo walanguzi wa dawa za kulevya wanaandaa kraki. Wanawake hao hawakuzi kutegemea dawa za kulevya tu bali pia mara nyingi wanakuwa walanguzi wenyewe. Kulingana na gazeti hilo la habari, mkuu wa polisi Antônio Vilela aeleza: “Inashangaza jinsi idadi ya wanawake wanaouza dawa za kulevya imeongezeka . . . , na hakuna mipaka hususa ya umri.” Wengi ni wanawake wachanga katika miaka yao ya 20, lakini wengine wako katika miaka yao ya 50.

Baadhi ya Wasiokwenda Kanisani Bado Husali Kibinafsi

Kulingana na The Sydney Morning Herald, Australia huonwa kwa ujumla kuwa jamii ya kilimwengu huku hudhurio la kanisa likishuka mwaka baada ya mwaka hadi chini mno. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi majuzi ulifunua kwamba baadhi ya Waaustralia bado husali kwa ukawaida. Uchunguzi huo waonyesha kwamba mtu mzima 1 kati ya 5 husali angalau mara moja kwa siku na, zaidi, kwamba asilimia 11 husali angalau mara moja kwa juma. Katika ripoti yalo juu ya dini katika miaka ya 1990 Shirika la Utafiti wa Ukristo laeleza kwamba ingawa hudhurio la kanisa linashuka kwa kushangaza, “watu wengi wanaendelea kuwa na hali za kiroho katika maisha yao,” lasema The Herald.

“Biashara” ya Pili kwa Ukubwa Ulimwenguni

Biashara isiyo halali ya dawa za kulevya inasitawi ikiwa na mapato yapitayo dola bilioni 400 (za Marekani) kila mwaka, lataarifu World Health, gazeti la Shirika la Afya Ulimwenguni. Hili laifanya iwe “biashara” yenye kukua haraka zaidi ulimwenguni. Pia ni biashara ya pili kwa ukubwa ulimwenguni—ikifuata biashara ya silaha lakini ikiwa mbele ya biashara ya mafuta. Kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita, kupatikana kwa dawa za kulevya zisizo halali kumeongezeka mara sita. Kutumiwa vibaya kwa vitu vilivyo halali, kama vile vimumunyishaji, dawa zilizoagizwa na daktari, na alkoholi, kunaongezeka kwa kiwango hicho hicho.

Ubatizo Wauzwa

Kwa zaidi ya miaka 300 kanisa la Kilutheri la Sweden limefurahia uhusiano wa Kanisa na Serikali. Hata hivyo, hivi majuzi, maofisa wa kanisa walitangaza kwamba kufikia Januari 1, 2000, uhusiano huu wa Kanisa na Serikali utakomeshwa. Kwa karne nyingi Wasweden wamefanywa kuwa washiriki wa hilo kanisa moja kwa moja wakati wa kuzaliwa. Hata hivyo, tangu mwanzo wa 1996, ushiriki wa kanisa umetegemea ubatizo. Gazeti la habari Dagens Industri laripoti kwamba askofu mkuu anatangaza programu ngumu ya mauzo, ambayo itatia ndani kuzuru nyumba kutakakofanywa na makasisi ‘wakiuza ubatizo.’ Kasisi mmoja mwanamke katika Stockholm anaripotiwa kuendeleza “kampeni yenye bidii ya mauzo” ambayo kwayo “moja ya viuzwaji-bora zaidi ni ubatizo.” Gazeti Må Bra laripoti kwamba parishi moja itapatia kila mtoto anayeletwa kwa ajili ya ubatizo kitabu cha benki chenye akiba ya kronor 100 za Kisweden (dola 15 za Marekani).

Kuwa Mama Kabla ya Kukomaa

Katika Brazili katika 1994, kulingana na Taasisi ya Brazili ya Jiografia na Takwimu, wasichana 11,457 chini ya umri wa miaka 15 walizaa. Kuzaa huko kabla ya kukomaa kumeongezeka kwa asilimia 391 kwa miaka 18 iliyopita, huku idadi ya watu ikiwa imeongezeka kwa asilimia 42.5 tu kwa kipindi hichohicho. Idadi ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19 ambao walizaa iliongezeka kwa asilimia 60. Dakt. Ricardo Rego Barros wa Chuo Kikuu cha Serikali cha Rio de Janeiro aeleza kwamba “hali ya ngono kabla ya ukomavu inachochewa na mazingira, televisheni, vitabu, na magazeti,” lasema gazeti Veja. Mtaalamu mwingine alisema kwamba wazazi na shule huona ikiwa vigumu kuwaelimisha watoto juu ya mambo hayo.

Viwango vya Televisheni Vyashuka

Watazamaji wa televisheni hupendelea zaidi ngono na mandhari za televisheni zenye kuonyesha uchi kuliko walivyokuwa miaka kumi iliyopita, laripoti gazeti la habari la London Independent. Kulingana na uchunguzi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, uvumilivu wa wanawake wa makamo kwa ngono na mandhari za televisheni zenye kuonyesha uchi umeongezeka. Asilimia 41 hivi ya wanawake wazee zaidi pia huona aina hii ya programu ya televisheni kuwa si mbaya. Miongoni mwa vijana, asilimia 75 hivi huruhusu lugha chafu ikilinganishwa na asilimia 69 mwongo mmoja uliopita. Badiliko kubwa zaidi katika mtazamo limekuwa kuelekea ugoni-jinsia-moja. Asilimia 40 ya wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 55, na asilimia 56 ya wanaume wenye umri wa miaka 35 hadi 55, na asilimia 70 ya wanaume vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 34 sasa huona maonyesho ya mtindo-maisha wa ugoni-jinsia-moja kwenye televisheni kuwa usioudhi—ongezeko la asilimia 20 katika miaka kumi iliyopita.

Askofu Atilia Shaka Hekima ya Biblia

Akizungumza katika semina moja katika India juu ya “Sheria Ziongozazo Ndoa na Talaka Miongoni mwa Wakristo,” askofu Mnestoria Poulose Mar Poulose alitaarifu kwamba mtu hawezi kuiendea Biblia kuwa kanuni ya maadili. Kama ilivyoripotiwa katika Indian Express, yeye alisema kwamba kusisitiza kwamba fundisho la Kibiblia juu ya talaka haliwezi kubatilishwa ni kukataa maendeleo ambayo mwanadamu wa kisasa amefanya katika uelewevu wake wa uhusiano kati ya mume na mke. Kulingana na Express, askofu huyo alimnukuu msomi wa dini ya Hindu akisema kwamba kila andiko lina pande mbili zenye kutofautiana, mmoja wa muda na usiodumu, ambao ni wa mawazo ya watu wa kipindi na nchi ambayo yaliandikwa, na ule mwingine ni wa milele, wenye kudumu na wenye kutumika kwa mihula yote na nchi zote. “Katika Biblia,” akasema askofu huyo, “ni lazima tutofautishe kiini na mambo ya juu-juu. Twapaswa kupambanua kweli yenye kudumu na upendeleo wa kitamaduni . . . na kuamua mwelekeo wa maisha yetu wenyewe.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki