Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/8 kur. 3-4
  • Kijiji Kimoja cha Dunia Nzima Lakini Bado Kimegawanyika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kijiji Kimoja cha Dunia Nzima Lakini Bado Kimegawanyika
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Watu Watangamana
  • Sababu Inayofanya Watu Wabaki Wakiwa Wamegawanyika
  • Je, Inafaa Kuwachukia Watu wa Jamii Nyingine?
    Amkeni!—2003
  • Ni Nini Suluhisho la Chuki ya Kijamii?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kushinda Vizuizi vya Mawasiliano
    Amkeni!—1996
  • Je! Ulimwengu Waweza Kuungana?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/8 kur. 3-4

Kijiji Kimoja cha Dunia Nzima Lakini Bado Kimegawanyika

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA

JE, UMEPATA kusikia hadithi za jamii fulani ya watu ambao hawakuwa na vinywa na hivyo hawakuweza kula au kunywa chochote? Ilisemekana kwamba wao waliishi kwa kunusa, hasa kwa kunusa matofaa. Uvundo ungewaua.

Pia kulikuwa na hadithi za watu fulani wa Afrika Magharibi waliokuwa na dhahabu za kufanyia biashara. Nahodha mmoja wa wakati huo wa meli ya Ureno aliripoti hivi: “[Umbali] wa leagues mia mbili ng’ambo ya ufalme wa [Mali], mtu apata nchi yenye wakazi ambao wana vichwa na meno ya mbwa na mikia kama ya mbwa. Hawa ndio Weusi wanaokataa mazungumzo kwa sababu hawataki kuona watu wengine.” Hayo yalikuwa baadhi ya mawazo ya ajabu ambayo yaliaminiwa miaka mingi iliyopita, kabla ya enzi ya usafiri na uvumbuzi.

Watu Watangamana

Hadithi kama hizo zilionwa kuwa za kweli kwa karne nyingi. Lakini wavumbuzi walipovumbua dunia, hawakupata watu wasio na vinywa ambao walinusa matofaa, wala hawakupata watu wenye vichwa vya mbwa. Leo hakuna fumbo lolote kuhusu watu wanaoishi ng’ambo ya mipaka yetu. Ulimwengu umekuwa kijiji kimoja. Televisheni huleta habari kuhusu nchi na watu wa kigeni katika vyumba vyetu. Kusafiri kwa ndege hufanya iwezekane kuzuru nchi hizo za kigeni kwa muda wa saa chache; mamilioni ya watu hufanya hivyo kila mwaka. Wengine huhama kwa sababu za kiuchumi au za kisiasa. Ripoti moja ya Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu yasema hivi: “Kwa kiwango kikubwa zaidi katika historia—na ambacho kwa hakika kitaendelea kuongezeka—watu ulimwenguni pote wanahama na kutafuta maisha bora.” Watu wapatao milioni 100 wanaishi nje ya nchi ambamo walizaliwa.

Kwa kuongezeka kuna utegemeano wa kiuchumi kati ya mataifa. Mfumo wa mawasiliano ya duniani pote, kama mfumo mkuu wa neva, huunganisha kila taifa duniani. Huku mawazo, habari, na tekinolojia zikibadilishanwa, tamaduni huungana na kujipatanisha na nyingine. Ulimwenguni pote watu huvalia kwa karibu njia sawa kuliko wakati mwingine wowote. Majiji ya ulimwengu yana mambo yafananayo—polisi, hoteli za anasa, magari, maduka, benki, uchafuzi. Hivyo, watu wa ulimwengu wajapo pamoja, twaona kile ambacho watu wengine hukiita utamaduni unaojitokeza wa ulimwengu.

Sababu Inayofanya Watu Wabaki Wakiwa Wamegawanyika

Lakini ingawa watu na tamaduni huchangamana, kwa wazi si wote wanaoona wengine kuwa ndugu. “Kila mtu ni mwepesi kumlaumu mgeni,” akaandika mwandikaji mmoja Mgiriki wa tamthilia zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Kwa kusikitisha ndivyo hali ilivyo leo. Uthibitisho waonekana kwa urahisi katika ripoti za magazeti ya habari juu ya ushupavu, chuki kwa wageni, “utakasaji wa kikabila,” mashindano ya kijamii, fujo za kidini, machinjo ya raia, mauaji ya kiholela, kambi za kulala wanawake kinguvu, mateso, au maangamizi ya jamii nzima-nzima.

Bila shaka, wengi wetu hawawezi kufanya lolote ili kubadili mwendo wa mapambano ya kikabila. Hata huenda hatuathiriwi nayo moja kwa moja. Hata hivyo, kwa wengi wetu matatizo hutokea kwa sababu ya kutowasiliana na wageni tunaokutana nao—majirani, wafanyakazi wenzetu, au wanashule wenzetu.

Je, haionekani kuwa ajabu sana kwamba watu wa kabila tofauti-tofauti mara nyingi hupata ugumu wa kuaminiana na kuthaminiana? Dunia ina vitu vyenye kutofautiana sana, vya aina nyingi sana. Wengi wetu huthamini wingi wa aina ya vyakula, muziki na rangi mbalimbali na vilevile aina mbalimbali za mimea, ndege, na wanyama. Lakini kwa njia fulani uthamini wetu kwa vitu tofauti-tofauti mara nyingi hauhusishi watu ambao hawafikiri na kutenda kama sisi.

Badala ya kutazama uzuri wa tofauti zilizoko miongoni mwa watu, watu wengi huelekea kukazia tofauti za watu na kuzifanya msingi wa mabishano. Kwa nini? Kuna manufaa gani katika kujaribu kushirikiana na watu ambao utamaduni wao hutofautiana na wetu? Tunaweza kushindaje vizuizi vya mawasiliano na kuziba pengo la mawasiliano? Makala ifuatayo itajaribu kujibu maswali hayo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki