Uhuru wa Kusema Nyumbani—Je, Ni Hali Itishayo Kutokeza Matatizo?
MTU anapopaaza sauti “Moto!” isivyo kweli katika jumba la maonyesho lililosongamana watu na baadhi yao wakanyagwe-kanyagwe hadi kifo katika makimbizi ya hofu ili kutoroka, je, si ni lazima mpaazaji-sauti huyo alaumike kwa kusababisha vifo na aksidenti? Mtu asemapo, “Sikubaliani na unalosema, lakini nitatetea haki yako ya kulisema,” je, unapewa uwezo wote wa kuamua, uhuru usio na mipaka, kusema lolote utakalo hadharani, haidhuru matokeo ni nini? Kuna wale wanaofikiria hivyo.
Kwa kielelezo, katika Ufaransa, wakati wanamuziki wa rapu walipopendekeza uuaji wa polisi na polisi wakauawa na watu fulani waliosikia huo muziki, je, wanamuziki hao wa rapu wangetozwa hesabu kwa kuchochea jeuri? Au wanapaswa kulindwa chini ya mswada wa haki? Wakati watangazaji wa redio na televisheni wanapofanya mandhari zenye jeuri za wazi na ponografia zipatikane kwa watoto, baadhi yao wakiigiza mandhari hizi na kujiumiza au kuumiza wengine, je, watokezaji wa mambo hayo wapaswa kushiriki lawama?
Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kisaikolojia la Marekani “hukadiria kwamba mtoto wa kawaida, mwenye kutazama televisheni kwa muda wa saa 27 kwa juma, ataona mauaji ya kimakusudi 8,000 na vitendo vya jeuri 100,000 tangu umri wa miaka 3 hadi 12,” likaripoti gazeti U.S.News & World Report. Je, wazazi wanaweza kihalali kudai kwamba hilo halina uvutano wowote kwa watoto wao? Au huenda likahusisha “hatari ya wazi na iliyopo”? Je, ni hapa ambapo kizuizi chapasa kuwekwa au mpaka kuwekwa kwa usemi huru?
Uchunguzi mmoja uliofanywa na wanasaikolojia wa chuo kikuu ulifunua kwamba wakati katuni za “mashujaa walio tayari kupigana sikuzote” zilipoonyeshwa kwa kikundi kimoja cha watoto wenye umri wa miaka minne na “katuni tulivu, zisizosisimua” kuonyeshwa kwa kikundi kingine, wale walioona mashujaa wa vituko walielekea sana kupiga na kutupa vitu baadaye. Wala athari za jeuri ya televisheni haififii baada ya utoto. Uchunguzi mwingine wa chuo kikuu, baada ya kufuatia watoto 650 tangu 1960 hadi 1995 na kuchunguza mazoea yayo ya utazamaji televisheni na mwenendo, ulipata kwamba wale waliotazama televisheni zenye jeuri mno wakiwa vijana walikua na kujihusisha katika mwenendo wenye ukali zaidi wakiwa watu wazima, kutia ndani kutendea vibaya wenzi wao wa ndoa na kuendesha gari wakiwa wamelewa.
Ingawa huenda watoto fulani wasikubali athari ambazo televisheni na sinema huwa nazo kwao, wengine huikubali. Katika 1995, Children Now, kikundi cha utegemezaji cha California, kilihoji watoto 750, wenye umri wa miaka 10 hadi 16. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba 6 kati ya 10, walisema kwamba ngono katika televisheni huchochea watoto kufanya ngono wakiwa wenye umri mchanga mno.
Huenda wengine wakasababu kwamba jeuri ya televisheni na sinema huenda isichukuliwe kihalisi na watoto na kwamba sinema zote hizo zenye kuogofya hazina athari yoyote kwao. “Ikiwa ni hivyo,” likasema gazeti moja la habari la Uingereza, “kwa nini shirika moja la shule katika magharibi-kati ya Marekani lililazimika kuyaambia maelfu ya watoto kwamba hakukuwa na Kasa-Vigeuko Matineja wa Kininja katika mabomba ya maji machafu ya mahali hapo? Mashabiki hao wachanga wa Kasa walikuwa wakitambaa kuingia ndani ya mabomba hayo ili kuwatafuta, hiyo ndiyo sababu.”
Leo, mjadala moto-moto unaendelea juu ya kile watu fulani hukiona kuwa tofauti ndogo kati ya usemi huru na jeuri isababishwayo na mazungumzo ya kupinga utoaji-mimba katika mahali pengi Marekani. Watu wapingao utoaji-mimba hulalamika kwamba madaktari na wafanyakazi wa kliniki ambao hufanya utoaji-mimba ni wauaji-kimakusudi na wao wenyewe hawana haki ya kuishi. Wachache wenye bidii wamedai madaktari hao na wasaidizi wao wauawe. Wapelelezi wamewekwa ili kupata nambari za leseni za magari ya madaktari hao, na majina na anwani zao hutolewa. Likiwa tokeo, madaktari na wafanyakazi wa kliniki wamepigwa risasi na kuuawa.
“Hili si suala ya usemi huru,” akapaaza sauti rais wa Planned Parenthood Federation of America. “Hili ni sawa na kupaaza sauti, ‘Moto!’ katika jumba la maonyesho lililosongamana watu. Hali hii yalinganika na jumba la maonyesho lililosongamana watu; tazama tu furiko la mauaji kwenye kliniki kwa miaka michache iliyopita.” Wale wanaounga mkono jeuri hii husababu kwamba wanadhihirisha tu haki yao kama inavyothibitishwa katika Marekebisho ya Kwanza ya Marekani—uhuru wa kusema. Na kusababu huko kunaendelea. Mapigano ya haki hii yataendelea kupiganwa katika mikutano ya hadharani, na mahakama zitahitaji kusuluhisha suala hilo, kwa ubaya, si kwa utoshelezo wa kila mtu.
Kile Wawezacho Kufanya Wazazi
Nyumbani kwapasa kuwa mahali salama kwa watoto, si mahali ambapo wanaweza kuwa windo rahisi kwa wale ambao wangewatumia kwa faida yao au vibaya, au mahali ambapo nyutu tulivu zaweza kuchochewa kudhihirisha hali za moyoni zenye jeuri. “Huenda ukahisi uhakikisho kwamba mtoto wako hatakuwa mwenye jeuri kamwe licha ya jeuri ya wakati wote ya televisheni,” akasema profesa wa chuo kimoja kikuu cha Marekani akiwahutubia wazazi. “Lakini huwezi kuwa na uhakikisho kwamba mtoto wako hatauawa kimakusudi au kulemazwa na mtoto wa mtu mwingine, aliyelelewa akitazama jeuri.” Kisha akasihi: “Kuwekewa mipaka utazamaji wa jeuri ya televisheni wa watoto kwapasa kuwa sehemu ya ajenda ya afya ya umma, pamoja na viti vya usalama, kofia za baiskeli, chanjo, na lishe bora.”
Ikiwa hungeruhusu mtu usiyemjua aje nyumbani kwako na kutumia lugha yenye matukano na kuzungumza kwa maneno machafu na mtoto wako kuhusu ngono na jeuri, basi usiruhusu redio na televisheni ziwe mtu huyo usiyemjua. Jua wakati wa kuizima au kubadili stesheni. Jua kile atazamacho mtoto wako, kwenye televisheni na kwenye kompyuta, hata katika usiri wa chumba chake. Ikiwa ajua kutumia kompyuta na kufikia mifumo ipatikanayo kwake, huenda ukashtuka kujua kile yeye huingiza akilini kila jioni. Ikiwa hukubali kile anachotazama mtoto wako, sema tu la na ueleze kwa nini. Hatakufa akizuiwa.
Mwishowe, funza watoto wako kuishi kulingana na kanuni za kimungu wala si kwa mazoea ya mfumo huu mwovu wa mambo—wenye usemi na vitendo vichafu na vyenye jeuri. (Mithali 22:6; Waefeso 6:4) Mtume Paulo alipatia Wakristo shauri la wakati ufaao ambalo sote twapaswa kuishi kulingana nalo. “Uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.”—Waefeso 5:3, 4.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Programu fulani za televisheni zaweza kuongoza kwenye uhalifu na ukosefu wa adili