Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/8 kur. 4-6
  • Sababu Inayofanya Spishi Ziwe Hatarini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sababu Inayofanya Spishi Ziwe Hatarini
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uharibifu wa Makao ya Wanyama
  • Mashambulio ya Moja kwa Moja
  • Mfumo Tata wa Viumbe
    Amkeni!—2001
  • Spishi Zilizo Hatarini mwa Kutoweka—Mweneo wa Hilo Tatizo
    Amkeni!—1996
  • Uhifadhi Dhidi ya Utoweko
    Amkeni!—1996
  • Manufaa za Misitu ya Mvua
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/8 kur. 4-6

Sababu Inayofanya Spishi Ziwe Hatarini

SPISHI hutoweka kutokana na visababishi kadhaa. Fikiria visababishi vitatu vikubwa. Wanadamu wanahusika na visababishi viwili kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kuhusika na kisababishi kingine kwa njia ya moja kwa moja.

Uharibifu wa Makao ya Wanyama

Uharibifu wa makao ya wanyama huhusika sana na upungufu wa spishi za wanyama. Kitabu The Atlas of Endangered Species chataja huo kuwa “tisho kubwa zaidi” na vilevile “lililo gumu zaidi kuzuia.” Idadi ya watu ulimwenguni inayozidi kuongezeka hulazimisha wanadamu kuingilia zaidi na zaidi ardhi ambayo zamani ilikuwa makao ya wanyama wa pori. Kielelezo bora ni kile cha misitu ya mvua ya ulimwengu.

‘Kwa miaka 40 ijayo hakutakuwa na misitu ya mvua’ ndilo kadirio lenye kuhuzunisha ambalo linaelekeza fikira kwenye kile ambacho wengi huona kuwa hali yenye kusikitisha ya kupoteza mali asili. Hakika, karibu robo za dawa zote zijulikanazo katika ulimwengu wa Magharibi zimetoka kwenye mimea ya misitu ya mvua. Ingawa misitu ya mvua hufunika asilimia 7 tu ya uso wa dunia, hiyo ni makao ya sehemu nne kwa tano za mimea ya nchi kavu.

Ukataji wa miti na njia za kubadilika-badilika za kilimo hunyang’anya misitu ya Afrika Magharibi miti mingi. Kukatwa kwa miti katika kontinenti ndogo ya India hata kumebadili halihewa, ukipunguza mvua katika maeneo mengine na kusababisha mafuriko katika maeneo mengine tofauti.

Mwanadamu akatapo miti ili alime, mimea, wanyama, ndege, wanyama-watambazi, na wadudu hutoweka mmoja-mmoja. Profesa wa Harvard Edward Wilson akadiria kwamba misitu hupunguka kwa asilimia 1 kila mwaka, na kupunguka huko hudhuru maelfu ya spishi ambayo hutoweka hatimaye. Inahofiwa kwamba spishi nyingi zitapotea hata kabla ya kupewa majina ya kisayansi.

Hivyo ndivyo hali ilivyo katika mabwawa ya ulimwengu, ambayo ni makao mengine yaliyo hatarini. Wasitawishaji huondoa maji ili waweze kujenga nyumba, au wakulima huyabadili kuwa mashamba ya kulima. Katika miaka 100 ambayo imepita, asilimia 90 ya mbuga za Ulaya zimetwaliwa kwa ajili ya kilimo. Kupotezwa kwa malisho katika Uingereza katika miaka 20 ambayo imepita kumetokeza upungufu wa asilimia 64 wa ndege aina ya mkesha-waimbaji.

Ingawa gazeti Time huita kisiwa cha Madagaska “Safina ya Noa ya kijiolojia,” aina zayo nyingi za wanyama wa pori zimo hatarini. Idadi ya watu iongezekapo na deni kwa mataifa mengine ziongezekapo, mkazo nao huongezeka kwa wakazi wa kisiwa hicho kugeuza misitu kuwa mashamba ya mipunga. Kwa sababu ya robo tatu za makao ya mnyama golden bamboo lemur kupotea katika miaka 20 ambayo imepita, ni 400 tu ya wanyama hao wanaobaki.

Badiliko kubwa la jinsi ambavyo wanadamu hutumia ardhi limedhoofisha wanyama wa pori katika maeneo yao. Kwa kielelezo kingine, fikiria Wapolinesia, waliofika Hawaii miaka 1,600 iliyopita. Tokeo la utendaji wao ni kwamba spishi 35 za ndege zilitoweka.

Masetla wa mapema waliokuja Australia na New Zealand walileta paka, ambao baadhi yao wakawa paka-mwitu. Kulingana na gazeti New Scientist, paka hao wa mwitu sasa hula spishi 64 za wanyama wa Australia. Pamoja na mbweha-wekundu wa Ulaya walioletwa, wao hushambulia idadi ndogo zilizobaki za spishi ambazo zimo hatarini mwa kutoweka.

Mashambulio ya Moja kwa Moja

Uwindaji si jambo jipya. Masimulizi ya Biblia katika Mwanzo yanafafanua yule Nimrodi mwasi kuwa mwindaji aliyeishi zaidi ya miaka 4,000 iliyopita. Ingawa haitajwi kwamba aliangamiza spishi nzima-nzima za wanyama, hata hivyo yeye alikuwa mwindaji hodari sana.—Mwanzo 10:9.

Katika karne ambazo zimepita wawindaji wamemaliza simba katika Ugiriki na Mesopotamia, viboko katika Nubia, tembo katika Afrika Kaskazini, dubu na beaver katika Uingereza, na ng’ombe wa mwitu katika Ulaya Mashariki. “Katika miaka ya 1870 na 1880, wawindaji waliua tembo robo milioni katika Afrika Mashariki pekee,” laripoti gazeti la kutangaza vipindi vya BBC, Radio Times. “Kwa nusu karne, Afrika ilijawa na mifyatuo ya bunduki za watu mashuhuri, wenye kutafuta mali, na wenye vyeo, wakiwapiga risasi tembo, vifaru, twiga, jamii ya paka wakubwa na kingine chochote ambacho wangeona. . . . Kile kinachoonekana kuwa chenye kushtua sana leo zamani kilikubalika kabisa.”

Ebu fikiria tena hali ya simbamarara mwenye fahari. Hesabu zilizofanywa katika miaka ya 1980 zilionyesha kwamba jitihada za uhifadhi zilikuwa zimefanikiwa. “Lakini, mambo hayakuwa hivyo,” chasema 1995 Britannica Book of the Year. “Hesabu zilizofanywa kwa uangalifu zaidi zilifunua kwamba hesabu za awali zilikuwa zimeongezwa na maofisa ambao ama walikuwa wakishirikiana na wawindaji-haramu ama waliotaka tu kupendeza wakubwa wao. . . . Ile biashara haramu ya viungo vya simbamarara ilisitawi sana huku kukosekana kwa viungo hivyo kukifanya ziwe ghali mno.” Hivyo, katika 1995, kadirio la thamani ya simbamarara wa Siberia lilikuwa kati ya dola 9,400 hadi 24,000 za Marekani—si tu kwa ajili ya ngozi yake yenye thamani sana bali pia kwa ajili ya mifupa, macho, masharubu, meno, viungo vya ndani, viungo vyake vya ngono, zote zikiwa na thamani sana katika dawa za kienyeji za Mashariki.

Biashara ya pembe za tembo, pembe za kifaru, ngozi za simbamarara, na viungo vinginevyo vya wanyama sasa ni biashara haramu yenye kuchuma mabilioni ya dola, ikiwa ya pili tu kwa ulanguzi wa dawa za kulevya, lasema Time. Na biashara hiyo haihusu wanyama wakubwa pekee. Katika 1994 dawa za kienyeji za Wachina zilitumia idadi ya kustaajabisha ya samaki aitwaye farasimaji milioni 20, jambo lililofanya uvuvi wao upunguke kwa asilimia 60 kwa miaka miwili katika maeneo fulani ya Asia ya Kusini-Mashariki.

Si vigumu kutambua ni nani anayepaswa kulaumika wakati spishi za viumbe zinapowindwa na kutoweka. Kisha, vipi wale wakusanyaji? Kasuku-mkia mmoja ambaye yumo hatarini mwa kutoweka, golden conure, huuzwa kwa dola 500 za Marekani na wafanya biashara haramu Brazili. Lakini anapomuuza nje ya nchi, yeye hupata zaidi ya mara tatu na nusu ya fedha hizo.

Vita na matokeo yayo, umati unaozidi kuongezeka wa wakimbizi, pamoja na kiwango chenye kuongezeka sana cha uzazi, uchafuzi wenye kuongezeka, na hata utalii, hutisha spishi zilizo hatarini mwa kutoweka. Wapendao kutazama mandhari wakiwa katika motaboti hudhuru dolfini ambao wao huja kuona, na kelele zilizo chini ya maji kutoka kwa boti hizo zaweza kuhitilafiana na mfumo dhaifu wa dolfini wa kuwasiliana.

Baada ya orodha hii yenye kuhuzunisha ya uharibifu wa mwanadamu, huenda ukajiuliza, ‘Wahifadhi wanafanya nini ili kuhifadhi spishi zilizo hatarini, nao wanafanikiwaje?’

[Picha katika ukurasa wa 6]

Mimea, wanyama, ndege, wanyama-watambazi, na wadudu hutoweka mmoja-mmoja mwanadamu akatapo miti

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki