Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/8 kur. 11-14
  • Kushinda Fadhaiko la Dyslexia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kushinda Fadhaiko la Dyslexia
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Dyslexia Ni Nini?
  • Ni Nini Ambacho Husababisha Dyslexia?
  • Msaada wa Wazazi
  • Msaada wa Walimu
  • Jinsi ya Kujisaidia
  • Dyslexia Haijanizuia Kufikia Miradi Yangu
    Amkeni!—2009
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Kuwasaidia Watoto Wenye Matatizo ya Kujifunza
    Amkeni!—2009
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2009
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/8 kur. 11-14

Kushinda Fadhaiko la Dyslexia

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

“NAMBARI yako ya simu ni gani?” Julie auliza. Mpiga-simu ajibu. Lakini nambari ambazo Julie anaziandika hazifanani hata kidogo na nambari anazopewa.

‘Mwalimu wangu alirarua picha niliyochora,’ alalamika Vanessa, akiongezea, ‘Hata sikuweza kamwe kukumbuka kile alichokuwa akisema.’

David, aliye katika miaka ya 70, hung’ang’ana kusoma maneno rahisi ambayo alikuwa amejua vizuri sana zaidi ya miongo sita ambayo imepita.

Julie, Vanessa, na David wana tatizo la kujifunza—lenye kufadhaisha. Linaitwa dyslexia. Ni nini ambacho husababisha tatizo hili? Wale wanaougua dyslexia waweza kushindaje fadhaiko ambalo tatizo hilo hutokeza?

Dyslexia Ni Nini?

Kamusi moja yafafanua dyslexia kuwa “kasoro ya uwezo wa kusoma.” Ingawa dyslexia huonwa kuwa tatizo la usomaji hiyo yaweza kutia ndani mengi zaidi.a

Asili ya neno la Kiingereza yatokana na Kigiriki dys, linalomaanisha “ugumu na,” na lexis, “neno.” Tatizo la Dyslexia latia ndani kupata magumu na maneno au lugha. Lahusisha pia matatizo ya kutoweza kuweka vitu kwa mfuatano ufaao, kama vile siku za juma na herufi katika neno. Kulingana na Dakt. H. T. Chasty, wa Taasisi ya Dyslexia ya Uingereza, dyslexia “ni kutoweza kuratibu kunakoathiri uwezo wa kukumbuka mambo yaliyotokea hivi punde, ufahamu na stadi za mkono.” Si ajabu kwamba wale wenye dyslexia hufadhaika sana!

Fikiria hali ya David. Ilikuwaje kwamba huyu mtu ambaye zamani alipenda sana kusoma na ambaye alikuwa msomaji mzuri sana akaja kuhitaji msaada wa mke wake wa kujifunza tena kusoma? Mshtuko wa akili uliharibu eneo fulani la ubongo wa David ambalo lilihusika na matumizi ya lugha, na jambo hilo lilifanya maendeleo yake ya kusoma kuwa polepole sana. Lakini, maneno marefu hayakumsumbua kama yale mafupi. Japo dyslexia aliyopata, uwezo wa David wa kuzungumza na akili yake timamu haikuathiriwa. Ubongo wa mwanadamu ni tata sana hivi kwamba watafiti hawajafahamu yote yanayohusika unaposhughulikia sauti na ishara za macho unazopokea.

Kwa upande mwingine Julie na Vanessa walikuwa na dyslexia ya kukua, ambayo ilikuja kuonekana wazi walipokuwa wakikua. Kwa ujumla watafiti hukubali kwamba watoto ambao kufikia umri wa miaka saba au nane na ambao wana akili za kawaida lakini wanapata magumu fulani ya kusoma, kuandika, na kuendeleza maneno huenda wakawa na dyslexia. Mara nyingi, vijana wenye dyslexia huziandika kinyume herufi wanazojaribu kunakili. Ebu wazia fadhaiko la Julie na Vanessa wakati walimu shuleni kwa makosa waliwaambia wao ni wajinga, wazito wa kujifunza, na wavivu!

Katika Uingereza, mtu 1 kwa watu 10 ana dyslexia. Hali ya wengine kukosa kutambua matatizo wanayokabili huongezea tu fadhaiko lao.—Ona sanduku kwenye ukurasa 14.

Ni Nini Ambacho Husababisha Dyslexia?

Kutoona vizuri mara nyingi hutokeza magumu ya kujifunza. Suluhisha tatizo hilo, na dyslexia hupotea. Idadi ndogo ya wale ambao wanapata ugumu wa kusoma wanaona kwamba wao waweza kukazia maneno kwa njia bora zaidi wanapoweka plastiki nyembamba yenye rangi fulani juu ya kile wanachosoma. Lakini hilo halisaidii wengine.

Wengine, wakiona kwamba tatizo hilo linapata familia nzima, husema hilo ni tatizo la urithi. Kwa kweli, gazeti New Scientist liliripoti hivi majuzi juu ya utafiti “uliochunguza ule ushirikiano ujulikanao kuwa kati ya chembe za urithi zinazohusika na maradhi yatokanayo na fingo za mwili kama vile kuumwa kichwa kwa kurudia-rudia na ugonjwa wa pumu, na zile chembe za urithi zinazosababisha dyslexia.” Kwa sababu wale wenye dyslexia na watu wao wa ukoo huelekea zaidi kuugua maradhi yatokanayo na fingo zao, wanasayansi wanaamini kwamba chembe za urithi za dyslexia ziko katika eneo fulani la jenomu lenye chembe za urithi za kusababisha maradhi. Lakini kama asemavyo mwanasayansi wa tabia Robert Plomin, watafiti “wametambua tu eneo la kromosomu, bali si chembe yenyewe inayosababisha kutoweza kusoma.”

Sehemu ya ubongo inayodhibiti mkao, usawaziko, na upatano wa mwili inaitwa ubongo-kati. Wanasayansi fulani hudai kwamba hiyo hutimiza pia fungu fulani katika kushughulikia mawazo yetu na lugha. Kwa kupendeza, watafiti katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza wameanzisha kupimwa kwa dyslexia kunakohusisha usawaziko na upatano wa mwili. Wao husababu kwamba makosa yaliyo katika ubongo-kati huchochea maeneo yasiyo na kasoro katika ubongo kusaidia. Kwa kawaida watoto hawana tatizo la kudumisha usawaziko wao wanapoambiwa wasimame tuli, mguu mmoja ukiwa mbele ya mwingine huku mikono ikiwa imenyoshwa kando. Lakini uwafunge macho, na watoto wenye tatizo la dyslexia watayumba-yumba zaidi, kwa kuwa wao hutegemea sana macho ili wadumishe usawaziko wao.

Na watafiti wengine bado wasema kwamba bongo za watoto wenye dyslexia huwa na muundo tofauti. Kwa kawaida, upande wa kushoto wa sehemu ya mwisho ya ubongo ni mkubwa kidogo kuliko upande wa kulia, lakini katika bongo za wenye dyslexia, pande za kushoto na kulia huonekana kana kwamba zinatoshana. Na wengine hudai kwamba wamegundua hitilafu fulani katika mpangilio wa chembe za neva katika sehemu za ubongo zinazohusika na lugha.

Lakini hata dyslexia iwe inasababishwa na nini, wale wenye tatizo hilo wanaweza kusaidiwaje kwa njia bora zaidi?

Msaada wa Wazazi

Wengine ambao ni wazazi wa watoto wenye dyslexia huhisi hatia na kujilaumu kwa tatizo la mtoto wao. Ukihisi hivyo, ondosha huzuni kwa kutambua kwamba hakuna mtu kati yetu aliyekamilika na sisi sote ni tofauti. Anza kwa kutambua kwamba kama vile mtoto asiyeweza kupambanua rangi mbalimbali ahitajivyo msaada wa kuishi na tatizo lake, ndivyo mtoto wako mwenye dyslexia ahitajivyo msaada. Wewe ukiwa mzazi una fungu hususa la kutimiza katika kuelimisha mtoto wako.

Ingawa kwa sasa dyslexia haiwezi kuzuiwa au kuponywa, hiyo inaweza kupunguzwa. Kwa njia gani? Profesa T. R. Miles, mtungaji wa kitabu Understanding Dyslexia, hushauri wazazi kwanza watambue ni nini hasa ambacho mtoto wao anapata ugumu nacho. Kisha wao wataweza kuchanganua kihalisi upungufu wa mtoto wao na kile wawezacho kumtarajia atimize. “Mtoto huyo apaswa kuambiwa afanye kadiri awezavyo,” lashauri Reading and the Dyslexic Child, “lakini si kupita hapo.” Kwa kuwa mwenye hisia-mwenzi na mwenye kutia moyo, na hasa kwa kupanga mafundisho yamfaayo mtoto, wazazi waweza kupunguza athari za dyslexia na, kwa wakati uo huo, kupunguza mkazo wa mtoto mwenye dyslexia.

Msaada wa Walimu

Kumbuka kwamba dyslexia ni tatizo la kujifunza. Hivyo, walimu wanahitaji kutumia wakati pamoja na watoto wenye dyslexia katika masomo yao na kujaribu kuwasaidia. Punguza fadhaiko la watoto kwa kutazamia watimize yale tu unayojua wao waweza kutimiza. Kwani, mtoto mwenye dyslexia aweza kuja kuwa mtu mzima ambaye bado ana matatizo ya kusoma kwa sauti.

Usivunjike moyo. Badala ya hivyo, uwapongeze watoto kwa maendeleo yoyote wanayofanya—na kwa hakika kwa jitihada zao zote. Kisha pia, epuka kusifu mno. Profesa Miles apendekeza kwamba walimu wanapoona maendeleo fulani, wawaambie hivi wanafunzi wenye dyslexia: “Ndiyo, nakubali kwamba umefanya makosa kidogo. Lakini bado umefanya vyema; ni maendeleo kwa kulinganisha na ile ya juma lililopita na, kwa sababu ya tatizo lako, hayo ni matokeo mazuri.” Lakini kama hakuna maendeleo, yeye ashauri akisema: “Ndiyo, inaonekana hili na hili bado linakutatiza; ebu tuone ikiwa tunaweza kujaribu njia nyinginezo za kukusaidia.”

Jihadhari usiseme maneno ya kuvunja heshima juu ya usomaji wa mtoto mwenye dyslexia. Jaribu kufanya vitabu na usomaji uwe wenye kumfurahisha. Kwa njia gani? Wazazi na walimu waweza kupendekeza kwamba mtoto ashikilie kitu, labda rula ndogo, chini ya mstari ambao anasoma, kwa kuwa msomaji wa polepole mara nyingi hushindwa kuwa makini. Tatizo likitokea katika kusoma herufi za maneno kwa mfuatano mbaya, kwa fadhili umuulize, “Ni ipi herufi ya kwanza?”

Ebu wazia jinsi inavyomvunja moyo mtoto mwenye dyslexia akiambiwa kila mara na mwalimu wake wa hesabu kwamba majibu yake si sahihi. Ni afadhali kama nini kumpa hesabu zilizo rahisi kidogo ili fadhaiko la kuanguka hesabu libadilishwe na uradhi wa kuwa amepata majibu ya hesabu.

“Ufunguo kwa wenye dyslexia ni,” kulingana na mwalimu mmoja stadi “kujifunza kwa kutumia hisi zote.” Changanya mwono, kusikia, na mguso ili kusaidia mtoto huyo asome na kuendeleza maneno kwa usahihi. “Mtoto ahitaji kutazama kwa uangalifu, kusikiliza kwa makini, kuwa makini kwa miendo ya mikono yake aandikapo, na kutoa uangalifu kwa miendo ya midomo yake asemapo,” Aeleza Profesa Miles. Kwa kufanya hivyo, mtoto mwenye dyslexia atalinganisha umbo la herufi iliyoandikwa na jinsi sauti itamkwavyo na miendo ya mkono afanyayo anapoiandika. Ili kusaidia mtoto kupambanua kati ya herufi zinazomchanganyisha akili, mfunze aanze kuandika herufi hizo kwa sehemu tofauti za herufi hiyo. “Kwa kufaa,” chapendekeza Reading and the Dyslexic Child, “kila mtoto [mwenye dyslexia] apaswa kuwa na muda wa saa moja kila siku wa kufundishwa akiwa yeye tu na mwalimu.” Kwa kuhuzunisha, ni nadra hali ziruhusu hilo. Hata hivyo, wenye dyslexia wanaweza kujisaidia.

Jinsi ya Kujisaidia

Ukiwa mwenye dyslexia, jaribu kusoma sana wakati wewe ni timamu zaidi. Watafiti wameona kwamba wanafunzi wenye dyslexia hupata matokeo mazuri wakiendelea kusoma kwa muda wa saa moja na nusu na baada ya muda huo kazi yao hudhoofika. “Funzo la kawaida la kila siku lakini la muda mfupi-mfupi laelekea kuwa yenye manufaa zaidi kuliko kusoma siku fulani pekee kwa bidii nyingi sana,” chasema Dyslexia at College. Ni kweli kwamba itakuchukua muda mrefu zaidi kusoma na kuendeleza maneno vema. Lakini vumilia.

Tumia taipureta yenye kubebeka au, hata bora zaidi, yenye kichanganua-maneno ya programu ya kompyuta inayokusaidia kuchunguza mwendelezo wa maneno unayoandika. Pamoja na hayo, jifunze jinsi ya kupanga na kutumia habari.—Ona sanduku kwenye ukurasa 13.

Furahia kusoma vitabu kwa kusikiliza vile vilivyorekodiwa kwenye kaseti. Kwa kweli, gazeti hili na jenzile, Mnara wa Mlinzi, sasa hutokea kwa ukawaida katika kaseti katika lugha nyingi, kama ilivyo na Biblia nzima.

Ikiwa unaona wewe ni mwenye dyslexia baada ya kusoma lile sanduku, usifiche tatizo hilo. Likubali, na ulifikirie. Kwa kielelezo, unaweza kuwa unajitayarishia mahoji ya kupata kazi. Kama ilivyo na watu wengi, unaweza kupata kwamba ule msongo wa hali hiyo unafanya iwe vigumu kujieleza kwa wazi na kwa ufupi. Mbona usijaribu kufanya mazoezi ya mahoji kabla ya kwenda?

Magumu yaletwayo na dyslexia hayawezi kutatuliwa kwa urahisi. Lakini, ubongo ukiwa kiungo cha ajabu sana, husawazisha hilo tatizo. Basi, haielekei kwamba utakosa furaha kabisa. Julie, Vanessa, na David wote wamefanya bidii ili kushinda fadhaiko lao. Wewe pia unaweza. Tambua kwamba tatizo lako hususa halipaswi kukukomesha usijifunze. Vumilia ukijaribu kusoma, kuandika, na kuendeleza maneno ifaavyo. Kufanya hivyo kutakusaidia kushinda fadhaiko la dyslexia.

[Maelezo ya Chini]

a Watu fulani wenye mamlaka hutumia neno “dysgraphia” kufafanua magumu ya kujifunza yanayohusiana na kuandika na pia “dyscalculia” kwa matatizo yahusikayo na hesabu.

[Sanduku katika ukurasa wa13]

Madokezo ya Kujiratibia

Tumia yafuatayo:

• ubao wako mwenyewe wa kuandikia

• kalenda ya kuandikia mambo unayotaka kutimiza

• trei ya mambo unayotaka kushughulikia

• faili ya kibinafsi

• kitabu cha mambo utakayofanya kwa siku

• kitabu cha anwani

[Sanduku katika ukurasa wa14]

Jinsi ya Kutambua Dyslexia Katika Watoto

Ukijibu ndiyo kwa maswali matatu au manne yaliyo chini kwa kila rika, inawezekana kwamba watoto wanaohusika wana dyslexia kwa kadiri fulani.

Watoto wenye umri wa miaka 8 au chini:

Je, walikawia kujifunza kusema?

Je, wao wangali wana tatizo hasa katika kusoma au kuendeleza maneno? Jambo hilo lakushangaza?

Je, unafikiri kwamba kwa mambo yasiyohusu kusoma na mwendelezo, wao ni timamu na wenye akili?

Je, wao huandika herufi na tarakimu kwa kinyume?

Wanapofanya hesabu, je, wao wamehitaji msaada wa vitu, vidole, au alama katika karatasi kwa muda mrefu zaidi kuliko wengine wa umri wao? Je, wao wana tatizo lisilo la kawaida la kukumbuka jedwali la kuzidisha hesabu?

Je, wana tatizo la kupambanua kati ya kushoto na kulia?

Je, wao ni wazembe kupita kiasi? (Si watoto wote wenye dyslexia walio wazembe.)

Watoto wenye umri wa miaka 8 hadi 12:

Je, wao hufanya makosa yasiyo ya kawaida ya mwendelezo wa maneno? Je, nyakati nyingine wao huruka herufi fulani katika maneno au kuziweka katika mfuatano mbaya?

Je, wao hufanya makosa yanayoonekana kuwa ya kizembe wanaposoma?

Je, uwezo wao wa kuelewa kile wanachosoma ni wa polepole kuliko watoto wengine wa umri wao?

Je, wanapata ugumu wa kunakili kutoka kwenye ubao wakiwa shuleni?

Wanaposoma kwa sauti, je, wao huruka maneno au mistari, au wao husoma mstari mara mbili? Je, hawapendi kusoma kwa sauti?

Je, wao bado hupata ugumu wa kukumbuka jedwali la kuzidisha hesabu?

Je, wao hawafahamu vizuri kushoto na kulia?

Je, wao wanakosa kujitumaini na kujishusha heshima?

[Hisani]

—Awareness Information, kilichotangazwa na Shirika la Uingereza la Dyslexia, na Dyslexia, kilichotangazwa na Broadcasting Support Services, Channel 4 Television, London, Uingereza.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Ili kusaidia kukaza akili, shikilia kitu chini ya mstari unaosoma

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki