Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/8 kur. 20-21
  • “Kuna Fedha Potosí!”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Kuna Fedha Potosí!”
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kufanywa Watumwa
  • Babiloni
  • Hazina Iliyotumiwa Vibaya
  • Baraka ya Yehova Imenitajirisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Jinsi Wainka Walivyopoteza Milki Yao Yenye Fahari
    Amkeni!—1998
  • Je, Wahindi wa Brazili Wanakabili Hatari ya Kutoweka?
    Amkeni!—2007
  • Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari Zake
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/8 kur. 20-21

“Kuna Fedha Potosí!”

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BOLIVIA

Ulikuwa mwaka wa 1545, miaka 12 tu baada ya Francisco Pizarro kuishinda Milki ya Inca iliyoenea sana. Wahispania walimgundua kijana fulani Mhindi akizidua mtapo wa fedha kisiri kutoka mahali pa siri katika Milima ya Andes ambayo sasa ni Bolivia. Mahali hapo pakaitwa Potosí. Kwa ghafula, habari ilienea: “Kuna fedha Potosí!” Japo kipupwe kilichokuwa kikikaribia, watu walifanya haraka kupata umiliki wa shamba katika eneo hilo. Mtapo huo ulikuwa na thamani ya juu sana—asilimia 50 fedha safi! Baada ya kipindi cha miezi 18 watu 14,000 walikuwa wakiishi Potosí.

MTAPO huo ulikuwa upande wa mlima fulani wenye kimo cha meta 4,688 juu ya usawa wa bahari. Hapakuwa mahali pazuri, kulikuwa na mimea michache sana, na kupita sana kimo cha ukuzi wa miti. Mtapo huo wenye thamani nyingi mno uliyeyushwa katika majiko ya kuokea yenye kuchukulika yaliyotumia upepo ili kuchochea makaa kuwaka kufikia halijoto ifaayo. Msimulizi mmoja wa wakati huo alisema kwamba aliona majiko ya kuokea 15,000 yakitenda kazi kwa wakati mmoja. Usiku yalionekana kama galaksi ya nyota.

Mji ulioko upande wa chini wa mlima ulijengwa bila utaratibu ukiwa na barabara nyembamba, zenye kupinda ili kuandaa ulinzi kutokana na pepo zenye kugandisha. Mwanahistoria R. C. Padden aliandika hivi: “Hakukuwa wala plani wala sheria, hasa, yafikiriwa ni kwa sababu fedha hiyo haikutarajiwa kudumu.” Lakini ilidumu. Huo mlima, uitwao Cerro Rico (Mlima Wenye Utajiri), ulikuja kuwa na fedha nyingi zaidi kuliko iliyowahi kupatikana wakati wowote.

Kufanywa Watumwa

Wahispania walivumilia hali ngumu sana zisizostarehesha katika utafutaji wao wa fedha. Mara nyingi, chakula kilikuwa kichache, maji yalikuwa yamechafuliwa, na machimbo yalikuwa hatari. Halihewa yenye baridi mno ilitokeza tatizo zito. Wale waliojaribu kujitia joto kwa makaa nyakati fulani walisumishwa kwa kaboni monoksidi.

Muda si muda Wahispania wakapata njia ya kupunguza hali yao mbaya. Wakiwa washindi, waliwalazimisha Wahindi wenyeji kuwa watumwa. Gazeti Bolivian Times la La Paz lilitaarifu: “Yasemekana kwamba watumwa Wahindi milioni nane waliangamia,” walikufa, katika machimbo ya Potosí wakati wa kipindi cha ukoloni. Ukatili, kufanyishwa kazi kupita kiasi, na maradhi yalisababisha kupungua kwenye kuogofya kwa idadi ya watu. Si ajabu kwamba katika 1550 msimulizi aliita Potosí “kinywa cha helo”!

Babiloni

Kufikia 1572, Potosí ulikuwa mkubwa zaidi ya jiji lolote katika Hispania. Kufikia 1611, ulisemekana kuwa na wakazi 160,000 na kuwa na ukubwa sawa na Paris na London. Ulikuwa pia mmoja wa miji tajiri zaidi ulimwenguni. Mtindo ulikuwa kuvaa vazi la hariri lililorembwa kwa nguo nyembamba ya dhahabu na fedha. Ilionekana kwamba anasa yoyote, ingeweza kupatikana ikiwa ungeweza kuigharimia: hariri kutoka China, kofia kutoka Uingereza, fulana kutoka Naples, marhamu kutoka Arabia. Wakazi walipamba nyumba zao kwa mazulia kutoka Uajemi, vitu vya mbao kutoka Flanders, michoro kutoka Italia, kioo kutoka Venice.

Lakini Potosí ulikuwa na jeuri sawa tu na ulivyokuwa na utajiri. Mapigano yenye umwagaji-damu yalikuwa tamasha ya kila siku kwenye baraza za mji. Nyumba za kamari na madanguro yalijaa. Potosí ukaja kuitwa Babiloni.

Mojapo malengo makuu ya washindi Wahispania lilikuwa kuanzisha dini ya Katoliki katika Amerika. Ingawa hivyo, watu hawa wenye kudai kuwa Wakristo waliteteaje kupata kwao faida nyingi kutokana na utumwa? Ingawa watu fulani wa kanisa walisema kwa ujasiri dhidi ya ukosefu huo wa haki, wengine walitetea utumwa kwa kudai kwamba utawala mkatili wa Wahispania haukuwa mbaya sana kama utawala mkatili wa Inca. Walidai kwamba Wahindi walikuwa wa hali ya chini na kiasili walielekea kutenda mabaya—hivyo, ilikuwa vyema wafanye kazi kwenye machimbo. Na bado wengine walidai kwamba kuleta Wahindi wafanye kazi machimboni kulikuwa hatua iliyohitajika ili kuwageuza imani wawe Wakatoliki.

Hata hivyo, historia yaonyesha kwamba, makasisi walikuwa miongoni mwa watu matajiri mno katika Potosí. Mwanahistoria Mariano Baptista asema: “Kanisa likiwa shirika, na wawakilishi walo mmoja-mmoja, walifanyiza sehemu iliyopendelewa ya wanyonyaji” wa Wahindi. Mwanahistoria huyu amnukuu gavana mmoja ambaye katika 1591 alilalamika kwamba makasisi “hunyonya Wahindi kwa pupa zaidi na kwa tamaa nyingi kuliko watu wa kawaida.”

Hazina Iliyotumiwa Vibaya

Hispania ilikuwa nchi maskini, lakini kwa miongo michache, utajiri wayo uliifanya kuwa kuu zaidi katika uwezo duniani. Lakini cheo hicho kilichopendelewa hakikudumu. Kikitoa maelezo juu ya kwa nini utajiri ulikosa kupatia Hispania faida zenye kudumu, kitabu Imperial Spain—1469-1716, kilichoandikwa na J. H. Elliott, chasema: “Machimbo ya Potosí yaliletea nchi hiyo utajiri mwingi sana; ikiwa fedha hazingetosha leo, zingekuwa nyingi tena kesho wakati meli za hazina zilipofika Seville. Kwa nini kupangia mambo, kwa nini kuweka akiba, kwa nini kufanya kazi?”

Hazina ya Potosí ilitumiwa vibaya; kipindi hicho kilipatwa na ufilisi wa jamii ya kifalme mara kwa mara. Kulingana na msemo wa wakati huo, kufika kwa meli zenye hazina kulikuwa kama mvua fupi za kiangazi ambazo hulowesha vigae vya paa kwa muda mfupi kisha hukauka mara. Kwa kufaa, mchunguzi wa karne ya 17 alisema hivi kuhusu kuanguka kwa Hispania: “Kwa sababu Hispania ilipata utajiri mwingi hivyo, iliutumia vibaya.”

Katika karne ya 18, Potosí ulipoteza utajiri wakati fedha ilipokwisha, lakini ukapata nguvu tena wakati bati lilipokuwa na umaana. Sasa, bati si maarufu sana, ingawa bado Potosí ni kitovu cha viwanda kwa ajili ya utengenezaji na uchimbaji. Lakini watalii wengi huzuru Potosí ili kufurahia uzuri wao wa ukoloni. Huenda pia wakaona makanisa yao ya kimadoido sana, mengi yayo yakiwa matupu yakitoa uthibitisho wa upendezi wenye kupungua wa Ukatoliki.

Leo Potosí ni kikumbusha chenye kuhuzunisha cha kuteseka kwingi kwa kibinadamu kulikosababishwa na pupa, hila ya kisiasa, na upotovu wa kidini, kikumbusha cha sehemu ya maana sana katika historia ya Bolivia ambayo ilianza kwa mwito: “Kuna fedha Potosí!”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki