Je, Wahindi wa Brazili Wanakabili Hatari ya Kutoweka?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI
MBUGA ya Wanyama ya Xingu iko katika jimbo la Mato Grosso, Brazili. Mbuga hiyo ina ukubwa wa kilomita 27,000 hivi za mraba, eneo linalokaribia kulingana na ukubwa wa nchi ya Burundi. Mbuga hiyo ambayo ina Wahindi wa Brazili 3,600 hivi kutoka makabila 14, ni kisiwa chenye rutuba sana katikati ya kile kinachoonekana kama “meza tambarare iliyofunikwa kitambaa cha kijani” kwenye picha za setilaiti.a Misitu inayozunguka imechomwa ili kuwawezesha wakataji-miti kuifikia miti ambayo hukatwa kwa ajili ya biashara au ili kugeuza misitu hiyo iwe malisho ya ng’ombe wengi.
Katika miaka ya 1960, serikali ya Brazili ilianza kutenga maeneo kwa ajili ya wenyeji hao. Maeneo hayo ambayo yanapatikana hasa katika eneo la Amazoni, yanafanyiza asilimia 12 hivi ya eneo la Brazili. Kutengwa kwa maeneo hayo kumetokeza badiliko lenye kushangaza: Idadi ya Wahindi wa Brazili imeongezeka kwa mara ya kwanza katika miaka 500 iliyopita! Inakadiriwa kwamba kuna wenyeji 300,000 hivi. Hata hivyo, idadi hiyo ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya wenyeji katika mwaka wa 1500. Wakati huo, inakadiriwa kuwa kulikuwa na kati ya wenyeji milioni mbili na milioni sita.
Kama mwandishi mmoja alivyosema, katika miaka 500 iliyopita, “kumekuwa na msiba mkubwa sana wa kupunguka kwa idadi ya [Wahindi].” Kwa nini Wahindi hao walipunguka hivyo? Je, kuongezeka kwa idadi yao katika miaka ya karibuni kunaonyesha kwamba Wahindi wa Brazili hawatatoweka?
Jinsi Ukoloni Ulivyoanza
Katika miaka ya kwanza 30 baada ya Ureno kuimiliki Brazili mnamo 1500, wakoloni hao walipendezwa hasa na brazilwood, mti ambao hupasuliwa mbao ngumu ambayo hutokeza rangi nyekundu. Nchi ya Brazili ilipewa jina lake kutokana na mti huo. Mbao zake zilikuwa na bei ghali sana huko Ulaya, na Wazungu walipata mbao hizo kwa kuwapa wenyeji vitu vyenye thamani ndogo.
Hata hivyo, iligunduliwa kwamba hali ya hewa nchini Brazili inafaa kwa kilimo cha miwa. Lakini kulikuwa na tatizo. Haikuwa rahisi kupanda miwa na wafanyakazi wengi walihitajika. Na wahamiaji hawakuhitaji kuwatafuta mbali! Kulikuwa na wafanyakazi wengi wenyeji.
Utumwa Ulianzaje?
Wahindi wa Brazili walikuwa wamezoea kulima ili tu kupata mahitaji ya lazima. Wanaume waliwinda na kuvua samaki. Wao ndio waliofyeka misitu kwa ajili ya kilimo. Wanawake walipanda, wakavuna, na kutayarisha chakula. Wazungu walioelimika waliwasifu kwa kuwa hawakupenda mali wala hawakuwa wenye pupa. Kwa upande mwingine, wahamiaji wengi waliwaona wenyeji hao kuwa wavivu.
Wenyeji wenye urafiki walitiwa moyo wahamie karibu na makazi ya Wareno ili kuwafanyia kazi na kuwalinda. Mara nyingi Wajesuti na watu wa dini nyingine walihusika sana katika jambo hilo. Hawakutambua jinsi ambavyo kukaribiana huko kungewaathiri sana wenyeji hao. Ingawa sheria ilihakikisha kwamba wenyeji hao hawangenyang’anywa nchi na uhuru wao, walilazimishwa kuwafanyia wahamiaji kazi. Ni mara chache tu walilipwa au kuruhusiwa kulima mashamba yao.
Jitihada za Milki ya Ureno kupiga marufuku utumwa hazikufua dafu. Kwa kawaida, wahamiaji walipata njia za kuhepa sheria za kupinga utumwa. Ilionekana kuwa sawa kuwafanya watumwa au hata kuwauza wenyeji waliosemekana kuwa maadui waliokamatwa katika vita vilivyodaiwa kuwa vya haki. Pia wenyeji walioshikwa mateka na makabila mengine wangeweza kununuliwa na kufanywa kuwa watumwa.
Mwishowe, biashara ya sukari ndiyo iliyoleta faida nyingi kutoka kwa koloni hilo. Na wakati huo biashara ya sukari haingeweza kufanikiwa bila watumwa. Hivyo, mara nyingi Milki ya Ureno ililazimika kufumba macho ili kupata faida.
Wakoloni Washindana —Wareno Dhidi ya Wafaransa na Waholanzi
Wenyeji ndio walioumia zaidi wakoloni waliposhindana. Wafaransa na Waholanzi walijaribu kuichukua Brazili kutoka chini ya udhibiti wa Wareno. Walishindana na Wareno ili kupata utegemezo wa wenyeji. Wenyeji hao hawakutambua kwamba sababu kuu ya wakoloni hao ilikuwa kuchukua nchi yao. Badala yake waliona vita hivyo kuwa nafasi ya kulipiza kisasi dhidi ya maadui wao wa makabila tofauti ya wenyeji na hivyo walikuwa tayari kujihusisha katika mapambano ya nchi za kigeni.
Kwa mfano, Novemba 10, 1555, (10/11/1555) Nicholas de Villegaignon, Mfaransa maarufu alifika kwenye Ghuba ya Guanabara (ambayo leo ni Rio de Janeiro) na kujenga ngome. Alifanya mapatano na Wahindi wa Brazili wa kabila la Tamoio. Wareno walikuja na Wahindi wa kabila la Tupinamba kutoka Bahia na mnamo Machi (Mwezi wa 3) 1560, wakavamia ngome iliyoonekana kuwa haiwezi kushindwa. Wafaransa walikimbia lakini wakaendelea kufanya biashara na Watamoio na kuwachochea wawavamie Wareno. Baada ya kupigana mara kadhaa, Watamoio walishindwa. Inaripotiwa kwamba katika pigano moja tu, watu 10,000 kati yao waliuawa na 20,000 wakafanywa kuwa watumwa.
Magonjwa Yenye Kuchukiza Kutoka Ulaya
Wenyeji ambao Wareno waliwaona kwa mara ya kwanza walionekana kuwa na afya nzuri. Wagunduzi wa mapema walisema kwamba wenyeji wenye umri mkubwa walikuwa na zaidi ya miaka mia. Lakini wenyeji hao hawakuwa na kinga dhidi ya magonjwa kutoka Ulaya na Afrika. Huenda magonjwa hayo yaliwaangamiza wenyeji wengi kuliko kitu kingine chochote.
Rekodi za Wareno zinaonyesha ripoti mbaya sana za magonjwa ambayo yalipunguza sana idadi ya wenyeji. Mnamo 1561, ugonjwa wa ndui ulitokea huko Ureno na ukaenea hadi kwenye koloni lao. Matokeo yalikuwa mabaya sana. Mei 12, 1563 (12/5/1563), Mjesuti Leonardo do Vale aliandika barua iliyoeleza matatizo ya magonjwa nchini Brazili: “Hiyo ilikuwa aina yenye kuchukiza sana ya ndui na yenye uvundo mbaya hivi kwamba hakuna mtu angeweza kustahimili harufu ambayo [wagonjwa] walitoa. Kwa sababu hiyo watu wengi walikufa kwa sababu ya kutotunzwa, huku wakiliwa na minyoo mingi iliyokua katika vidonda vya miili yao na iliyokuwa na ukubwa wa kutisha hivi kwamba yeyote aliyeiona alishangazwa.”
Wajesuti Washangazwa na Ndoa za Watu wa Rangi Tofauti
Ndoa za watu wa rangi tofauti zilifanya makabila mengi yatoweke. “Wareno na Wahindi wa Brazili hawakushangazwa na ndoa za watu wa rangi tofauti,” kinasema kitabu Red Gold—The Conquest of the Brazilian Indians. Wahindi wa Brazili waliona kuwapa wageni wanawake wao kuwa njia ya kuwakaribisha wageni, na mara nyingi walitoa binti zao. Wajesuti wa kwanza walipofika Brazili mnamo 1549, walishangazwa na kile walichoona. “[Viongozi wa kidini] waliwaambia wanaume waziwazi kwamba ilikuwa sawa kuishi katika dhambi na wanawake wao wenyeji,” akalalamika Mjesuti Manoel da Nóbrega, akiongeza hivi: “Wahamiaji waliwatumia wanawake wote [watumwa] wenyeji kama masuria.” Mfalme wa Ureno aliambiwa kwamba mhamiaji mmoja Mreno ‘alikuwa na watoto, wajukuu, vitukuu, na wazao wengine wengi sana hivi kwamba [msemaji huyo akasema] siwezi kuthubutu kukuambia Mfalme walikuwa wangapi.’
Kufikia katikati ya karne ya 17, wenyeji wa nyanda za pwani za Brazili walikuwa ama wameuawa, wamefanywa kuwa watumwa, ama wametoweka kwa sababu ya kuoana na watu wa rangi tofauti. Baada ya muda jambo hilohilo lilitukia katika makabila mengine ya eneo la Amazoni.
Kuwasili kwa Wareno huko Amazoni kulifuatwa na kipindi cha kuwaua kwa wingi wenyeji wa eneo la chini la Amazoni. Kasisi mkuu wa Maranhão, Manoel Teixeira, anasema kwamba kwa muda wa miaka michache tu, Wareno waliwaua wenyeji milioni mbili hivi wa Maranhão na Pará! Ingawa labda kadirio hilo lilitiwa chumvi, bado maangamizi na mateso yalikuwa yameenea kote. Baadaye, maeneo ya Amazoni ya juu pia yalikuwa katika hali hiyohiyo. Kufikia katikati ya karne ya 18, eneo la Amazoni, isipokuwa maeneo machache ya mbali, lilikuwa limepoteza idadi kubwa ya wenyeji.
Maendeleo ya maeneo ya mbali ya Amazoni katika karne za 19 na 20 yalifanya wazungu wakutane na wenyeji wa mbali waliokuwa wamebaki. Ugunduzi wa mpira uliofanywa mnamo 1839 na Charles Goodyear na utengenezaji wa magurudumu ya mpira uliofuata, uliwafanya watu wamininike huko. Wafanyabiashara walimiminika kwenye eneo la Amazoni, kwani ni huko tu ambako mpira ulipatikana. Katika kipindi hicho, wenyeji walitendewa kwa jeuri na hilo lilifanya wapungue sana.
Karne ya 20 Imewaathirije Wahindi wa Brazili?
Mnamo 1970, serikali ya Brazili iliamua kujenga barabara kuu za kuunganisha sehemu za mbali za Amazoni. Njia nyingi kati ya hizo zilipitia maeneo ya wenyeji na hivyo kufanya iwe rahisi kwao kushambuliwa na watu waliokuwa wakitafuta mpira na vilevile kupatwa na magonjwa hatari.
Kwa mfano, fikiria kilichowapata watu wa kabila la Panarás. Kabila hilo lilipungua kwa sababu ya vita na utumwa kwenye karne ya 18 na 19. Watu wachache waliobaki walikimbilia upande wa kaskazini, ndani sana ya msitu wa kaskazini mwa Mato Grosso. Kisha barabara kuu ya Cuiabá-Santarém ilijengwa kupitia katikati ya eneo lao.
Kwa wengi kukutana na watu kutoka Ulaya kulikuwa jambo la hatari. Mnamo 1975, ni watu 80 tu wa kabila hilo waliosalia. Watu wa kabila la Panarás walihamishiwa kwenye Mbuga ya Taifa ya Xingu. Walijaribu kutafuta eneo ndani ya mbuga hiyo ambalo lingefanana na msitu wao wa asili lakini hawakufanikiwa. Kisha kabila hilo la Panarás likaamua kurudi kwenye eneo lao la asili. Novemba 1, 1996 (1/11/1996) waziri wa sheria wa Brazili alitangaza kwamba eneo lenye ukubwa wa hekta 495,000 ni “mali ya kudumu ya Wahindi wa Brazili.” Hatimaye kabila la Panarás likawa limeokolewa ili lisitoweke.
Je, Wanaweza Kutarajia Hali Nzuri?
Je, hifadhi hizo zinaweza kuwasaidia Wahindi wa Brazili waliobaki wasitoweke? Kwa sasa haionekani kwamba wenyeji hao wa Brazili watatoweka. Hata hivyo, maeneo yao yana madini na maliasili. Inakadiriwa kwamba madini yenye thamani ya karibu dola trilioni moja, kama vile dhahabu, platinamu, almasi, chuma, na risasi yanapatikana katika eneo ambalo linajulikana kama Legal Amazonia, ambalo linachukua majimbo tisa kaskazini na magharibi ya kati ya Brazili. Karibu asilimia 98 ya Wahindi wa Brazili wanapatikana katika eneo hilo. Tayari maeneo fulani ya wenyeji yameanza kuchimbwa kwa njia isiyo halali.
Historia inaonyesha kwamba Wahindi wa Brazili wamepata hasara kila mara wanaposhughulika na wazungu. Walibadilishana dhahabu na vioo, wakabadilishana mbao za brazilwood na vitu vyenye thamani ndogo, na walilazimika kukimbilia maeneo ya ndani sana ya misitu ili wasifanywe kuwa watumwa. Je, historia itajirudia?
Wahindi wa Brazili wamejifunza kutumia vifaa vya kisasa vya kiteknolojia kama vile, ndege, mashua zenye mota, na simu za mkononi. Lakini wakati tu ndio utakaoonyesha ikiwa wanaweza kukabiliana na hali ngumu za karne ya 21.
[Maelezo ya Chini]
a Wahindi wa Brazili wanaotajwa katika makala hii wanarejezea Wenyeji wa Asili wa Amerika wanaoishi Brazili.
[Ramani katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
■ Mbuga ya Taifa ya Xingu
□ Hifadhi ya Wahindi wa Brazili
BRAZILI
BRASÍLIA
Rio de Janeiro
GUIANA YA UFARANSA
SURINAME
GUYANA
VENEZUELA
KOLOMBIA
EKUADO
PERU
BOLIVIA
PARAGUAI
URUGUAI
[Picha katika ukurasa wa 15]
Wafanyabiashara waliwatumia Wahindi wa Brazili kama watumwa katika mashamba yao ya mpira
[Hisani]
© Jacques Jangoux/Peter Arnold, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Line drawing and design: From the book Brazil and the Brazilians, 1857