“Si Kosa Langu”
NI MARA nyingi kadiri gani leo usikiapo mtu akisema, ‘Nasikitika. Lilikuwa kosa langu. Napaswa kulaumika kabisa!’? Ni nadra sana ufuatiaji wa haki ulio sahili hivyo kusikiwa tena. Kwa hakika, katika visa vingi, hata wakati kosa lakiriwa, kila jitihada inafanywa ili kumwekea mtu fulani lawama au kulaumu hali zenye kupunguza ukubwa wa kosa ambazo mkosaji adai hakuweza kuzidhibiti.
Wengine hata hulaumu jeni zao! Lakini je, hili laweza kuaminika? Kitabu Exploding the Gene Myth hutilia shaka malengo na matokeo ya sehemu fulani za utafiti wa jeni. Mwandikaji wa habari wa Australia aitwaye Bill Deane, katika pitio lake la kitabu hicho, afikia mkataa huu wa kusababu kiakili: “Watu waaminio kwamba kila kitu kinaamuliwa na hali zilizopo yaonekana hivi karibuni wameanza kuamini kwamba wamepata uthibitisho unaoelekea kutokuwa na kasoro ili kutegemeza falsafa yao kwamba hakuna mtu apaswaye kutozwa hesabu kwa matendo yake: ‘Hakuweza kujizuia asikate koo la mhasiriwa wake, Mheshimiwa—aliongozwa na maumbile yake ya kijeni.’”
Kwa Kweli Si Mwelekeo Mpya
Kizazi hiki kinapositawi na kuwa kile ambacho mwandikaji mmoja akiita kizazi cha “si-mimi,” mwelekeo huu huenda ukaonekana kuwa unaongezeka. Hata hivyo, historia iliyorekodiwa hufunua kwamba kulaumu wengine, kwa kutoa udhuru kwamba “kwa kweli si mimi nipaswaye kulaumika,” kumekuwapo tangu mwanzo wa mwanadamu. Itikio la Adamu na Hawa baada ya dhambi yao ya kwanza, kula tunda lililokatazwa na Mungu, lilikuwa kielelezo halisi cha kulaumu wengine. Simulizi la Mwanzo huripoti mazungumzo yaliyokuwapo, Mungu akisema kwanza: “Je! umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.”—Mwanzo 3:11-13.
Tangu wakati huo, wanadamu wamevumbua njia tofauti-tofauti za itikadi na wametafuta udhuru usio wa kawaida ambao utawaondolea wajibu wowote wa kweli wa kutozwa hesabu kwa matendo yao. Wenye kutokeza kati ya udhuru huo ni ile itikadi ya kale katika ajali. Mwanamke Mbuddha ambaye aliamini kwa unyoofu katika Karma alisema: “Nilifikiri kwamba lilikuwa jambo lisiloeleweka kuteseka kwa kitu nilichozaliwa nacho na ambacho sikujua chochote kukihusu. Nililazimika kukikubali kuwa kitu nilichopangiwa kimbele.” Ikisitawishwa na fundisho la kuamuliwa kimbele yatakayokupata lililofundishwa na John Calvin, itikadi katika ajali pia ni jambo la kawaida katika Jumuiya ya Wakristo. Mara nyingi makasisi huambia watu wa ukoo wenye kuomboleza kwamba aksidenti fulani ilikuwa mapenzi ya Mungu. Kisha, pia, Wakristo fulani wenye nia nzuri humlaumu Shetani kwa kila kitu kinachokwenda vibaya maishani mwao.
Sasa, twaanza kushuhudia mwenendo usiotozwa hesabu ambao unakubaliwa kisheria na kijamii. Twaishi katika muhula wa haki zenye kuongezeka na madaraka yenye kupungua ya watu mmoja-mmoja.
Utafiti kuhusu mwenendo wa kibinadamu umetokeza eti uthibitisho wa kisayansi ambao watu wengine wanahisi waweza kuruhusu kabisa mwenendo kuanzia ukosefu wa adili hadi uuaji-kimakusudi. Hilo laonyesha hamu ya jamii kulaumu chochote kile, au yeyote yule, isipokuwa mtu anayehusika.
Twahitaji majibu kwa maswali kama haya: Sayansi imegundua nini hasa? Je, mwenendo wa binadamu unaamuliwa na jeni hasa? Au kani za ndani na za nje hudhibiti mwenendo wetu? Uthibitisho waonyesha nini kikweli?