Wakati Maneno Yanapokuwa Silaha
“Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga.”—MITHALI 12:18.
“MNAMO majuma machache baada ya arusi, mambo yakaanza,” asema Elaine.a “Maneno yasiyo na fadhili, maneno yenye kushusha, na jitihada za kunifedhehesha. Sikuweza kushindana na mume wangu. Akili yake yenye kufahamu mambo upesi na ulimi wake wa haraka vingeweza kugeuza na kupotosha kila kitu nilichosema.”
Katika ndoa yake yote Elaine amekuwa chini ya aina ya udhia wenye athari inayoongezeka ambayo haiachi makovu na ambayo haionewi huruma. Kwa kuhuzunisha, hali yake haijaboreka kadiri wakati upitavyo. “Tumeoana kwa zaidi ya miaka 12 sasa,” yeye asema. “Hakuna siku ipitayo bila yeye kuwa mwenye kunichambua na mwenye kunikejeli, akitumia usemi wenye kudhulumu, ulio mchafu.”
Biblia haitii chumvi inaposema kwamba ulimi waweza kuwa “kitu kisichotawalika chenye ubaya, . . . umejaa sumu yenye kuleta kifo.” (Yakobo 3:8, NW; linganisha Zaburi 140:3.) Hili ni kweli hasa katika ndoa. “Yeyote yule aliyesema ‘vijiti na mawe vyaweza kuvunja mifupa yangu lakini maneno hayawezi kamwe kuniumiza’ alikosea vibaya sana,” asema mke mmoja aitwaye Lisa.—Mithali 15:4.
Waume pia waweza kuwa shabaha ya ukatili wa maneno. “Je, unajua jinsi ilivyo kuishi na mwanamke ambaye daima hukuita mwongo, mjinga au maneno mabaya hata zaidi?” auliza Mike, ambaye ndoa yake ya miaka minne pamoja na Tracy yaelekea kwenye talaka. “Siwezi hata kurudia mambo aniambiayo mbele ya waandamani wenye kuheshimika. Hiyo ndiyo sababu siwezi kuzungumza naye na inayofanya nibaki kazini hadi kuchelewa mno. Kuna amani nyingi zaidi kazini kuliko kuja nyumbani.”—Mithali 27:15.
Akiwa na sababu yenye msingi mzuri, mtume Paulo alionya Wakristo hivi: “Acheni . . . kupiga kelele na usemi wenye kuudhi viondolewe mbali kutoka kwenu.” (Waefeso 4:31, NW) Lakini “usemi wenye kuudhi” ni nini? Paulo autofautisha na “kupiga kelele” (Kigiriki, krau·geʹ), ambako humaanisha kupaaza sauti tu. “Usemi wenye kuudhi” (Kigiriki, bla·sphe·miʹa) hurejezea zaidi yaliyo katika ujumbe. Ikiwa huo ni wa kukandamiza, wenye nia ya kudhuru, wenye kuharibia heshima, au wenye kutukana, basi huo ni usemi wenye kuudhi—iwe waja kwa njia ya mpaazo wa sauti au kwa mnong’ono.
Majeraha ya Maneno
Tabia ya usemi mkali yaweza kudhoofisha ndoa, kama tu vile mawimbi ya bahari yamomonyoavyo mwamba mgumu. “Kadiri yanavyozidi kuwa mazito na yenye kuendelea,” aandika Dakt. Daniel Goleman, “ndivyo hatari iwavyo kubwa. . . . Mazoea ya kuchambua na kudharau au kuchukizwa ni ishara za hatari kwa sababu huonyesha kwamba mume au mke kwa ukimya tayari amemhukumu mwenzi kuwa mbaya.” Upendo unapopungua, mume na mke wanakuwa, kama kitabu kimoja kisemavyo, “wameoana kisheria, bali si kihisia-moyo.” Baada ya muda, ndoa yao haitaendelea tena.
Hata hivyo, usemi wenye kukemea-kemea waweza kuathiri mtu hata kuliko kuathiri ndoa yenyewe. Mithali ya Biblia husema: “Kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.” (Mithali 15:13) Mkazo unaotokana na mashambulio ya daima ya maneno yenye kuumiza waweza kuharibu sana afya ya mtu. Kwa kielelezo, uchunguzi mmoja uliofanywa na Chuo Kikuu cha Washington (Marekani) ulifunua kwamba mwanamke ambaye hutukanwa-tukanwa anaweza kupatwa zaidi na homa, matatizo ya kibofu cha mkojo, maambukizo ya Candidiasis (ambayo huathiri uke), na matatizo ya tumbo.
Wake wengi ambao wamevumilia kutendwa vibaya kwa maneno na kupigwa kimwili husema kwamba maneno yanaweza kuumiza zaidi kuliko ngumi. “Michubuo itokanayo na makofi itapona na kwisha hatimaye,” asema Beverly, “lakini sitasahau kamwe mambo mabaya aliyosema kuhusu sura yangu, jinsi ninavyopika, jinsi ninavyotunza watoto.” Julia ahisi vivyohivyo. “Najua inasikika kama kichaa,” yeye asema, “lakini afadhali anipige na mambo yaishe kuliko kuendelea kuteswa kiakili.”
Lakini kwa nini watu wengine huchambua na kukemea-kemea yule ambaye walidai kumpenda? Makala ifuatayo itashughulikia swali hili.
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina katika mfululizo huu wa makala yamebadilishwa.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Afadhali anipige na mambo yaishe kuliko kuendelea kuteswa kiakili”
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Je, unajua jinsi ilivyo kuishi na mwanamke ambaye daima hukuita mwongo, mjinga, au maneno mabaya hata zaidi?”