Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 12/8 kur. 16-18
  • Pulatipasi wa Kifumbo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pulatipasi wa Kifumbo
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Acheni Tumtembelee Pulatipasi
  • Mdomo Ule Unaoshangaza
  • Jihadhari na Zile Kucha!
  • Wakati wa Kutaga Mayai
  • Viumbe wa Ajabu Katika Pori la Tasmania
    Amkeni!—2012
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Kuutetea Ukweli Katika Ulimwengu Unaomkana Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Kushinda Vipingamizi kwa Kuweka Miradi
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 12/8 kur. 16-18

Pulatipasi wa Kifumbo

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

WANASAYANSI walipomwona pulatipasi kwa mara ya kwanza, hawakujua jinsi ya kumwainisha. Huyo pulatipasi alitokeza kitendawili, akiwa na uzito wa kilo moja au mbili na mwenye hali za kutatanisha ambazo zilihangaisha itikadi za wanasayansi. Twakukaribisha kukutana na kiumbe hiki kidogo cha kipekee cha Australia—kizuri, chenye haya na chenye kupendeza. Hata hivyo, kwanza, acha turudi nyuma hadi mwaka 1799 na tuone mvurugo aliosababisha wakati ngozi ya kwanza ya pulatipasi ilipochunguzwa na wanasayansi wa Uingereza.

“Hakuweza kuamini [macho yake] kamwe,” yasema ensaiklopedia moja kuhusu Dakt. Shaw, mtunzaji msaidizi katika sehemu ya Historia ya Asili ya Jumba la Kuhifadhi Vitu vya Kale la Uingereza. Alishuku kwamba “mtu fulani alikuwa amepachika mdomo wa bata kwenye [mnyama wa miguu minne]. Alijaribu [kuutoa] mdomo huo, na leo alama za mkasi wake bado zaweza kuonekana katika ngozi ya awali.”

“Hata baada ya ngozi hiyo kuonekana kuwa ni halisi, wanasayansi walishangazwa. Pulatipasi—ambaye jina lake lamaanisha “miguu bapa”—ana mfumo wa uzazi unaofanana sana na wa ndege lakini pia ana matiti. Hili lionekanalo kuwa fumbo lilitokeza swali: Je, kiumbe hiki chenye kutokeza mashaka hutaga mayai, au hatagi?

Baada ya miaka mingi ya mabishano, ilipatikana kwamba ni kweli pulatipasi hutaga mayai. Lakini ilionekana kwamba kila uvumbuzi ulizidisha tu lile fumbo. Utakiainishaje kiumbe ambacho (1) hutaga mayai lakini kina matiti; (2) kina manyoya ya mnyama lakini mdomo wa bata; (3) kina mfumo wa mifupa inayofanana na ya wanyama-watambazi wenye damu baridi lakini mwenyewe ana damu-joto?

Baadaye, wanasayansi walikubaliana kwamba pulatipasi alikuwa mamalia ya oda Monotremata. Mnyama aina ya Monotreme, kama ilivyo na mnyama-mtambazi, ana tundu moja ya kupitishia mayai, mbegu ya kiume, kinyesi, na mkojo. Monotreme mwingine pekee anayeishi ni echidna. Jina la kisayansi alilopewa pulatipasi ni Ornithorhynchus anatinus, ambalo humaanisha “mnyama kama bata mwenye pua ya ndege.”

Acheni Tumtembelee Pulatipasi

Tungeweza kwenda kwenye makao ya wanyama, lakini hakuna ono zuri kama kumwona pulatipasi msiri porini—kitu ambacho hata Waaustralia wachache hawajapata kufanya. Uchunguzi wetu waanzia mashariki mwa Australia, katika Blue Mountains magharibi ya Sydney, ingawa mito, vijito, na maziwa mengi ya maji matamu yaliyoko upande wa mashariki mwa Australia yangeweza kuwa maeneo ya kumwona pulatipasi.

Kabla ya mapambazuko tuliwasili katika daraja la zamani la mbao lililo juu ya mto wenye maji yenye kung’aa na kingo za miti ya eucalyptus. Kwa subira na kwa ukimya, twaangalia maji ili kuona umbo jeusi la sehemu ya mbele ya mdomo wake, utosi, mgongo na mkia. Mara twathawabishwa. Karibu mita 50 kwenye upande wa juu wa mto, umbo latokea, likija upande wetu. Ni lazima tusimame tuli.

Viwimbi vingi vinavyotokezwa na mdomo wake vyathibitisha kwamba ni pulatipasi. Viwimbi hivyo vyenye kuonekana hutokea wakati pulatipasi anapotafuna chakula alichokikusanya katika mifuko ya mashavu yake alipokuwa anatafuta chakula chini ya mto. Ingawa chakula chake hubadilika kwa kutegemea msimu, mara nyingi yeye hula nyungunyungu, mabuu, na uduvi.

Je, umbo dogo la pulatipasi lakushangaza? Huwashangaza wengi. Wengi hufikiri kuwa yeye ni mkubwa kama beaver au fisi-maji. Lakini kama uwezavyo kuona, yeye ni mdogo kuliko hata paka wa kawaida wa nyumbani. Madume huwa kati ya sentimeta 45 hadi 60 na huwa na uzito wa kilo moja hadi mbili na nusu. Majike ni wadogo kidogo.

Akisukumwa na mapigo yenye kubadilishana ya miguu yake ya mbele yenye utando, yeye apiga mbizi kwa ukimya na kubaki chini ya maji kwa dakika moja au mbili anapopita chini ya daraja. Miguu yake ya nyuma yenye utando mdogo haitumiwi kwa kujisukuma lakini yatumika kama usukani na hufanya kazi pamoja na mkia wake aogeleapo. Pia hutegemeza mwili wake kwa uthabiti achimbapo shimo.

Akisumbuliwa, pulatipasi hupiga mbizi kwa kishindo cha kusikika na hiyo yamaanisha kwaheri! Kwa hiyo twaongea wakati tu amezama. “Hiki kiumbe kidogo huhifadhi joto namna gani,” wanong’oneza, “hasa katika maji baridi kama barafu ya kipupwe?” Kwa kawaida pulatipasi hufaulu kwa sababu ya misaada miwili: uyeyushaji wa chakula ambao hutokeza nishati kwa haraka na hivyo kumpasha joto kwa ndani, na ngozi nzito ambayo huhifadhi joto.

Mdomo Ule Unaoshangaza

Mdomo wa pulatipasi ambao ni kama mpira na ni laini ni tata sana. Umefunikwa kwa nywele fupi zinazotambua mguso na utendaji wa umeme. Akiwa chini ya mto, pulatipasi apeleka mdomo wake kwa taratibu huku na huku wakati achunguzapo, akigundua hata uga hafifu wa umeme utokezwao na mpindano wa misuli ya windo lake. Pulatipasi azamapo, mdomo wake ndio njia ya pekee ya kuwasiliana na ulimwengu, kwani macho, masikio na pua hufungwa kabisa.

Jihadhari na Zile Kucha!

Ikiwa rafiki yetu mdogo ni dume, miguu yake ya nyuma ina silaha ya kucha mbili kwenye kifundo, ambazo zimeunganishwa na mishipa yenye kuelekea matezi mawili ya sumu katika eneo la mapaja. Yeye hupiga kwa nguvu kucha zote mbili katika nyama ya mshambulizi kwa njia inayofanana kidogo na mpanda farasi aendeshaye farasi. Mara baada ya mshtuko wa awali, mhasiriwa hupatwa na maumivu makali na majeraha huvimba.

Lakini utekwani, pulatipasi aweza kuwa mpole kama mbwa mdogo. Hifadhi ya Healesville, katika Victoria, imewatunza wanyama hawa kwa miongo kadhaa na huripoti kwamba pulatipasi mmoja wa awali “alikuwa akiwatumbuiza watu wenye kuzuru kwa muda wa saa nyingi, akijiviringisha tena na tena ili tumbo lake likunwe . . . Maelfu ya wageni walifurika kumwona mnyama huyu mdogo wa ajabu.”

Yule pulatipasi tuliyekuwa tunamwangalia apiga mbizi ya mwisho kwa siku hiyo mara tu jua la asubuhi lichomozapo juu ya safu za milima kuelekea mashariki. Usiku huo amekula chakula kinachozidi sehemu moja kwa tano ya uzito wake. Aibukapo nje ya maji, utando katika mguu wake wa mbele hurudi ndani, ukiacha nje kucha zenye nguvu. Sasa anaelekea mojawapo ya mashimo yake mengi, ambayo yamechimbwa kwa hekima katikati ya mizizi ya miti ili yalindwe dhidi ya mmomonyoko na poromoko. Mashimo ya kutagia mayai kwa kawaida yana urefu wa karibu meta nane, lakini mashimo mengine yaweza kuwa kati ya meta 1 na karibu meta 30 kwa urefu nayo yanaweza kuwa na matawi mengi ya kandokando. Pia mashimo huandaa ulinzi dhidi ya joto kali au baridi kali, ikiyafanya kuwa makazi yenye kufaa kwa majike kutunza watoto wao.

Wakati wa Kutaga Mayai

Katika masika jike huenda katika chumba chenye majani kandokando katika mojawapo vijumba vya ndani naye hutaga kati ya yai moja hadi mayai matatu (kwa kawaida mawili) yenye ukubwa wa ukucha wa kidole gumba. Yeye huyaatamia mayai kwa kuyafunika kwa mwili wake na mkia wake wenye mafuta. Kwa muda wa karibu siku kumi, watoto hutoka katika magamba yaliyo kama ngozi na hujilisha maziwa yaandaliwayo na matiti mawili ya mama. Hata hivyo, pulatipasi jike hutunza watoto wake akiwa peke yake; mamalia hawa hawatoi uthibitisho wa kuwa na kifungo cha muda-mrefu kati ya dume na jike.

Karibu Februari, baada ya miezi mitatu na nusu ya ukuzi wa haraka, wachanga hao wako tayari kwenda majini. Kwa vile maji yaweza kutegemeza wachache tu, hatimaye hao wachanga hutafuta maji yasiyo na pulatipasi wengi, hata kwa kuvuka maeneo ya bara yenye hatari ili kuyapata.

Katika utekwa, pulatipasi wameishi kwa miaka 20 au zaidi, lakini porini hawaishi muda mrefu namna hiyo. Ukame na mafuriko huwaangamiza na vilevile kenge, mbweha, ndege wakubwa wawindaji, na, kaskazini zaidi katika Queensland, pia mamba. Walakini, mwanadamu ndiyo tisho kubwa zaidi kwa pulatipasi, siyo kwa kuwaua kimakusudi (uuaji wa pulatipasi umepigwa marufuku kisheria), bali kwa kuendelea kuingilia mazingira yao.

Ukipata kutembelea Australia, waweza kujionea mwenyewe pulatipasi wetu mdogo wa kipekee katika mazingira yake ya asili, kwani hutamwona porini sehemu nyingine yoyote ulimwenguni. Kupitia pulatipasi, utajionea upande mwingine wa ubuni usio na mipaka wa Muumba—na ucheshi pia.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Pulatipasi hujisukuma kwa kutumia miguu yenye utando

[Hisani]

Kwa hisani ya Taronga Zoo

[Picha katika ukurasa wa 17]

Akiwa mdogo kuliko paka wa kawaida wa nyumbani, pulatipasi ana uzito wa kilo moja hadi mbili na nusu

[Hisani]

Kwa hisani ya Dr. Tom Grant

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mdomo wake wenye hisia za hali ya juu hupata windo chini ya maji. (Pulatipasi huyu yuko katika Hifadhi ya Healesville)

[Hisani]

Kwa hisani ya Healesville Sanctuary

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Picha: Kwa hisani ya Dr. Tom Grant

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki