Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 1/22 kur. 5-7
  • Usawaziko Ufaao Waweza Kufanya Maisha Yako Yapendeze

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Usawaziko Ufaao Waweza Kufanya Maisha Yako Yapendeze
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wenye Uwezekano wa Kuwa Wadadisi
  • “Hisi Yenye Kina ya Kukosa Uhakika”
  • Epuka Mtego wa Ubaridi
  • Kulinda Uhuru—Jinsi Gani?
    Amkeni!—1999
  • Ustahimilivu—Kutoka Mwisho Mmoja Hadi Ule Mwingine
    Amkeni!—1997
  • Wenye Kubadilikana, Hata Hivyo Wenye Wajibu Kuelekea Viwango vya Kimungu
    Amkeni!—1997
  • Uvumilivu
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 1/22 kur. 5-7

Usawaziko Ufaao Waweza Kufanya Maisha Yako Yapendeze

USTAHIMILIVU ni kama sukari katika kikombe cha chai. Kiwango kifaacho chaweza kuongeza utamu katika maisha. Lakini ingawa twaweza kuwa wakarimu na sukari, mara nyingi hatuwi wakarimu na ustahimilivu. Kwa nini?

“Wanadamu hawataki kuwa wastahimilivu,” akaandika Arthur M. Melzer, profesa mshiriki kwenye Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan. “Wanadamu wana mwelekeo wa asili wa kuonyesha . . . ubaguzi.” Kwa hiyo ukosefu wa ustahimilivu si tu kasoro ya utu ambayo hupata wachache tu; kuwa wenye akili iliyofungika hutupata sote kiasili kwa kuwa wanadamu wote si wakamilifu.—Linganisha Waroma 5:12.

Wenye Uwezekano wa Kuwa Wadadisi

Katika 1991, gazeti Time liliripoti juu ya hali inayoendelea kuongezeka ya akili iliyofungika Marekani. Makala hiyo ilifafanua “mtindo-maisha wa wadadisi,” watu ambao hujaribu kulazimisha kila mtu afuate viwango vyao wenyewe. Wasiokubaliana wamehasiriwa. Kwa mfano, mwanamke mmoja katika Boston alifutwa kazi kwa sababu ya kukataa kutumia virembeshi. Mwanamume mmoja katika Los Angeles alifutwa kazi kwa sababu ya kuwa mnene kupita kiasi. Kwa nini jitihada hiyo yote ya kufanya wengine wakubaliane?

Watu wenye akili iliyofungika hawakubali sababu, ni wenye ubinafsi, wenye shingo ngumu, na wenye kutaka watu wafuate maoni yao tu. Lakini je, watu wengi si ni wenye kukosa kukubali sababu, wenye ubinafsi, wenye shingo ngumu, au wenye kutaka maoni yao tu yafuatwe kwa kiwango fulani? Tabia hizi zikipata mizizi mizuri katika utu wetu, tutakuwa watu wenye akili iliyofungika.

Namna gani wewe? Je, wewe hudhihirisha hali ya kutokubali kwa habari ya ladha ya mtu mwingine ya chakula? Katika mazungumzo, je, kwa kawaida wewe hutaka kuwa mwenye neno la mwisho? Unapofanya kazi mkiwa kikundi, je, wewe hutarajia wengine wafuate njia yako ya kufikiri? Ikiwa ndivyo, lingekuwa jambo zuri kuongeza sukari kidogo katika chai yako!

Lakini, kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, ukosefu wa ustahimilivu waweza kuja katika namna ya ubaguzi wenye uhasama. Jambo moja liwezalo kufanya ukosefu wa ustahimilivu uongezeke ni hangaiko baya.

“Hisi Yenye Kina ya Kukosa Uhakika”

Wataalamu wa jamii na asili za wanadamu wamechunguza wakati uliopita wa mwanadamu ili wajue ni wakati gani na mahali gani ambapo ubaguzi wa jamii ulikuwa wazi. Walipata kwamba aina hii ya ukosefu wa ustahimilivu haiwi wazi wakati wote, wala haijidhihirishi katika kila nchi kwa kiwango kilekile. Gazeti la Ujerumani la sayansi ya asili GEO huripoti kwamba mikwaruzano ya kijamii hujitokeza katika wakati wa tatizo wakati ambapo “watu wana hisi yenye kina ya kukosa uhakika na kuhisi kwamba utambulisho wao umo hatarini.”

Je, hiyo “hisi yenye kina ya kukosa uhakika” imeenea sana leo? Bila shaka. Zaidi ya wakati mwingineo wote, wanadamu wanasumbuliwa na tatizo moja baada ya jingine. Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, kupanda kwa gharama ya maisha, idadi ya watu yenye kupita kiasi, kupungua kwa tabaka la ozoni, uhalifu majijini, uchafuzi wa maji ya kunywa, kuongezeka kwa joto tufeni pote—hofu yenye kusumbua ya lolote la mambo hayo huongeza hangaiko. Matatizo husababisha hangaiko, na hangaiko lisilofaa huongoza kwenye ukosefu wa ustahimilivu.

Ukosefu huo wa ustahimilivu hujidhihirisha, kwa mfano, mahali ambapo vikundi vya kikabila na tamaduni tofauti huchangamana, kama ilivyo katika nchi fulani za Ulaya. Kulingana na ripoti moja iliyotolewa na National Geographic katika 1993, nchi za Ulaya Magharibi wakati huo zilikuwa na wahamiaji zaidi ya milioni 22 kutoka nchi nyinginezo. Watu wengi wa ulaya “walihisi wamelemezwa na kuja kwa wingi wa wageni” wa lugha, tamaduni, au dini tofauti. Kumekuwa na ongezeko la maoni yaliyo dhidi ya wageni katika Austria, Hispania, Italia, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani.

Namna gani viongozi wa ulimwengu? Katika kipindi cha miaka ya 1930 na 1940, Hitler alifanya ukosefu wa ustahimilivu uwe sera ya serikali. Kwa kuhuzunisha, viongozi fulani wa kisiasa na wa kidini leo hutumia ukosefu wa ustahimilivu ili kupata malengo yao. Ndivyo imekuwa katika mahali kama vile Austria, Ireland, Marekani, Rwanda, Ufaransa, na Urusi.

Epuka Mtego wa Ubaridi

Kukiwa na sukari chache sana katika chai yetu twahisi kwamba kuna kitu kinachokosekana; kukiwa na sukari nyingi mno twahisi ladha ya utamu isiyofurahisha kinywani mwetu. Ndivyo ilivyo na ustahimilivu. Fikiria ono la mwanamume mmoja afundishaye katika chuo fulani Marekani.

Miaka kadhaa iliyopita David R. Carlin, Jr., alipata njia rahisi lakini yenye matokeo ya kufanya mazungumzo ya darasani yawe yenye kusisimua. Alikuwa akitokeza taarifa iliyokusudiwa kutoa wito wa ushindani kwa maoni ya wanafunzi wake, akijua kwamba wangepinga. Matokeo yalikuwa kwamba kulikuwa na mazungumzo moto-moto. Hata hivyo, katika 1989, Carlin aliandika kwamba njia iyo hiyo haikuwa na matokeo tena. Kwa nini? Ingawa wanafunzi bado hawakukubaliana na kile alichosema, hawakushughulika kubishana. Carlin alieleza kwamba walikuwa wamekuwa na “mtazamo wa mtu mwenye kushuku na kuachilia mambo”—mtazamo wa kutojali kabisa.

Je, mtazamo wa kutojali ni sawa na ustahimilivu? Ikiwa hakuna mtu anayejali kile ambacho mtu mwingine hufikiri au kufanya, hakuna viwango kabisa. Ukosefu wa viwango ni ubaridi—ukosefu kamili wa upendezi. Hali kama hiyo yaweza kutokeaje?

Kulingana na Profesa Melzer, ubaridi waweza kuenea katika jamii ambayo hukubali viwango vingi tofauti vya mwenendo. Watu huja kuamini kwamba aina yote ya mwenendo inakubalika na kwamba kila kitu ni jambo tu la uchaguzi wa kibinafsi. Badala ya kujifunza kufikiri na kutilia shaka kinachokubalika na kisichokubalika, watu “mara nyingi hujifunza kutofikiri kabisa.” Wanakosa nguvu ya maadili inayomsukuma mtu kukinza kwa ujasiri ukosefu wa ustahimilivu wa wengine.

Namna gani wewe? Je, wewe hujipata ukiwa na mtazamo wa kutojali? Je, wewe hucheka vichekesho visivyo safi au vya ubaguzi wa jamii? Je, wewe huruhusu mwana au binti yako tineja atazame vidio ambazo huchochea pupa na ukosefu wa adili? Je, wahisi kwamba ni sawa watoto wako wakicheza michezo yenye jeuri ya kompyuta?

Kukiwa na ustahimilivu wa kupita kiasi, familia au jamii itavuna maumivu makali, kwa kuwa hakuna mtu anayejua—au anayejali—kilicho sawa na kisicho sawa. Mbunge wa Marekani Dan Coats alionya kuhusu “mtego wa kuunga mkono ustahimilivu kumbe ni ubaridi.” Ustahimilivu waweza kuongoza kwenye kuwa mtu mwenye akili iliyofunguka; ustahimilivu wa kupita kiasi waweza kuongoza kwenye—ubaridi—kuwa na kichwa kitupu.

Kwa hiyo, tustahimili nini na tukatae nini? Ni nini iliyo siri ya kupata usawaziko ufaao? Hiyo ndiyo itakayokuwa habari ya makala ifuatayo.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Jitahidi kuwa na maitikio yaliyosawazika kuelekea hali mbalimbali

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki