Ustahimilivu—Kutoka Mwisho Mmoja Hadi Ule Mwingine
MANDHARI zenye kuvutia za Bonde la Kashmir zilichochea mwanafalsafa wa karne ya 16 apaaze sauti hivi: “Ikiwa kuna paradiso mahali popote, ni hapa!” Kwa wazi, hakuwa na wazo lolote kuhusu kile ambacho kingetokea baadaye katika sehemu hii ya ulimwengu. Katika kipindi cha miaka mitano ambayo imepita, angalau watu 20,000 wameuawa huko katika vita kati ya vikundi vya kupigania uhuru na Jeshi la India. Gazeti la habari la Ujerumani Süddeutsche Zeitung sasa hufafanua eneo hilo kuwa “bonde la machozi.” Bonde la Kashmir huandaa somo sahili lakini lenye thamani: Ukosefu wa ustahimilivu waweza kuharibu sehemu iwezayo kuwa paradiso.
Yamaanisha nini kuwa mstahimilivu? Kulingana na Collins Cobuild English Language Dictionary, “ikiwa wewe ni mstahimilivu, wewe huruhusu watu wawe na mitazamo na itikadi zao wenyewe, au waenende kwa njia fulani, hata ikiwa wewe hukubali au hupendelei jambo hilo.” Ni sifa nzuri kama nini ya kudhihirisha! Kwa hakika sisi huhisi tukiwa tumestareheka tukiwa na watu ambao hustahi itikadi na mitazamo yetu hata ikiwa inatofautiana na yao.
Kutoka Ustahimilivu Hadi Ushupavu
Kinyume cha ustahimilivu ni ukosefu wa ustahimilivu, ambao huwa na viwango tofauti-tofauti vya mkazo. Ukosefu wa ustahimilivu waweza kuanza na kutokubali kwa akili iliyofungika mwenendo au njia ya mtu mwingine ya kufanya mambo. Kuwa na akili iliyofungika huzuia kufurahia maisha na kufanya akili ya mtu isipate mawazo mapya.
Kwa kielelezo, huenda mtu mgumu akachukizwa na idili nyingi za mtoto. Huenda kijana akachoshwa na njia za kutafakari za mtu mwenye umri mkubwa kupita wake. Mwulize mtu mwenye hadhari afanye kazi bega kwa bega na mtu ambaye hupenda sana kujasiria, na wote watachokozeka. Kwa nini mtu achukizwe, achoshwe, na achokozeke? Kwa sababu, katika kila kisa, mtu huona likiwa jambo gumu kustahimili mtazamo na mwenendo wa yule mwingine.
Mahali ambapo ukosefu wa ustahimilivu husitawi, kuwa na akili iliyofungika kwaweza kuongezeka kufikia ubaguzi, ambao ni kujiepusha na kikundi, jamii, au dini fulani. Ulio mbaya zaidi kuliko ubaguzi ni ushupavu, ambao waweza kujidhihirisha kwa chuki yenye jeuri. Tokeo ni taabu na umwagikaji wa damu. Fikiria kile ambacho ukosefu wa ustahimilivu ulitokeza wakati wa zile Krusedi! Hata leo, ukosefu wa ustahimilivu ni kisababishi kikuu cha mapambano katika Bosnia, Rwanda, na Mashariki ya Kati.
Ustahimilivu huhitaji usawaziko, na kudumisha usawaziko ufaao si jambo rahisi. Tuko kama pinduli ya saa, ikibembea kutoka upande mmoja hadi ule mwingine. Nyakati fulani, sisi huonyesha ustahimilivu mchache sana; nyakati nyingine, ustahimilivu mwingi sana.
Kutoka Ustahimilivu Hadi Ukosefu wa Adili
Je, inawezekana kuwa mstahimilivu kupita kiasi? Mbunge wa Marekani Dan Coats, alipokuwa akizungumza katika 1993, alifafanua “bishano juu ya maana na udhihirishaji wa ustahimilivu.” Alimaanisha nini? Mbunge huyo aliomboleza kwamba kwa kutoa udhuru kwamba ni ustahimilivu, wengine “wameacha itikadi katika ukweli wa adili—katika jema na baya, lililo sawa na lisilo sawa.” Watu kama hao wanahisi kwamba jamii haina haki ya kuhukumu ni upi ulio mwenendo mwema na upi ulio mbaya.
Katika 1990, mwanasiasa Mwingereza Lord Hailsham aliandika kwamba “adui mbaya sana wa maadili si uatheisti, uagnosti, ufuatiaji wa vitu vya kimwili, pupa wala chochote cha visababishi vinginevyo vinavyokubaliwa. Adui wa kweli wa maadili ni unihili, ikisemwa wazi kabisa, kutoitikadi chochote.” Kwa wazi, tusipoitikadi chochote, hatuna viwango vya mwenendo ufaao na kila kitu chaweza kustahimiliwa. Lakini ni jambo linalofaa kustahimili kila namna ya mwenendo?
Mkuu wa shule ya sekondari aliye Mdenmark hakufikiri hivyo. Yeye aliandika makala ya gazeti la habari katika miaka ya mapema ya 1970, akilalamika kuhusu matangazo ya biashara katika vyombo vya habari kwa maonyesho ya kiponografia yenye kuonyesha tendo la ngono kati ya wanyama na wanadamu. Matangazo haya yaliruhusiwa kwa sababu ya “ustahimilivu” wa Denmark.
Kwa wazi, matatizo huzuka si kutokana na kuonyesha tu ustahimilivu mchache bali pia ustahimilivu mwingi kupita kiasi. Kwa nini ni jambo gumu kuepuka kupita kiasi na kubaki katika usawaziko ufaao? Tafadhali soma makala ifuatayo.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Kupinga kupita kiasi makosa ya watoto kwaweza kuwadhuru
[Picha katika ukurasa wa 4]
Kustahimili kila kitu ambacho watoto hufanya hakuwezi kuwatayarisha kwa madaraka ya maisha