Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/8 kur. 6-8
  • Kwa Nini Uhalifu Uliopangwa Unasitawi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kwa Nini Uhalifu Uliopangwa Unasitawi?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mfumo Bandia wa Familia
  • Malaika wa Nuru
  • Ulimwengu Usio na Uhalifu Utapatikanaje?
    Amkeni!—1997
  • Naacha Uhalifu Uliopangwa—“Nilikuwa Yakuza”
    Amkeni!—1997
  • Jinsi Uhalifu Uliopangwa Unavyokuathiri
    Amkeni!—1997
  • Kwa Nini Uhalifu Ni Mwingi Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/8 kur. 6-8

Kwa Nini Uhalifu Uliopangwa Unasitawi?

AL CAPONE, lile jambazi lenye sifa mbaya katika ule wakati wa Sheria ya Kuharamisha Unywaji wa Vileo Marekani (1920-1933), alidai kwamba yeye alikuwa mfanyabiashara tu aliyekuwa akitekeleza sheria—sheria ya kuuza kwa sababu ya mahitaji. Wakili mmoja wa genge kubwa zaidi la yakuza katika Japani alisema: “Huwezi kukana kwamba kuna mahitaji makubwa ya [ngono, dawa, na kamari].” Mahitaji hayo hukuza uhalifu uliopangwa. Ingawa hakuna mtu anayetaka kupatwa na uhalifu, wengine waweza kugeukia magenge ya uhalifu na kupata msaada wao.

Kwa mfano, fikiria hila za ulinzi ambazo magenge katika nchi nyingi hutumia ili kupata fedha. Ingawa nyakati nyingine wao hulenga wenye maduka walio wanyoofu, mara nyingi wao hutumia wale wanaoendesha biashara zenye kutilika shaka. Mwenye kasino moja katika Shinjuku, Tokyo, ambaye ameficha biashara yake halisi kwa kuendesha mkahawa wa michezo ya vidio, alisema: “Karani mmoja alidungwa kisu, na kunyang’anywa [yen] milioni 2 [dola 20,000 za Marekani]. Lakini hatukuthubutu kuita polisi.” Kwa nini? “Kwa kuwa tunaendesha biashara haramu (kamari), hatutaki kamwe kuhusika na polisi. Mteja akileta fujo, tunawaita yakuza.” Huyo mwenye kasino hulipa dola 4,000 kila mwezi kwa yakuza, pesa kidogo kwa kulinganisha na faida ya dola 300,000 ambazo yeye huchuma kupitia biashara yake haramu katika kipindi hicho. Pesa hizo zinatoka wapi? Mifukoni mwa watu ambao hufurahia kamari haramu.

Ndivyo ilivyo na biashara zenye kuheshimika ambazo hazitaki matatizo. Ofisi ya mkuu wa sheria wa New York ilikadiria kwamba mtu mmoja aliyechukua kandarasi ya kupaka rangi ambayo ingemletea dola milioni 15 kwa mwaka aliokoa dola milioni 3.8 kwa kuwalipa majambazi. Hilo liliruhusu mtu huyo kutumia watu wenye mshahara wa chini na kuepuka mzozo na chama cha wafanyakazi kinachoongozwa na magenge. Katika Japani, wakati wa ufanisi wa kiuchumi, wafanyabiashara wa kifedha waliweka pesa zao kwa wingi katika mashamba na majengo na kuharibu nyumba na maduka ya kale ili majengo makubwa yajengwe. Wakazi walipokataa kuhama au kuuza shamba lao, hao waweka-rasilimali waliita jiageya, ambayo mara nyingi ni kampuni zinazohusika na yakuza, ili kuwahamisha.

Wakati yakuza walipoona jinsi ilivyo rahisi kukopa na kuchuma pesa katika miaka ya 80, wao walianzisha kampuni nyingi na kujitosa katika biashara za nyumba na za kukisia-kisia hisa za biashara. Mashirika ya benki na ya kifedha yalitumia fedha nyingi katika kampuni hizo, bila shaka yakinuia kupata faida. Lakini uchumi ulipozorota, benki hizo zilipata ugumu sana wa kurudisha fedha zao. Akizungumzia uchumi unaozorota katika Japani, aliyekuwa ofisa wa polisi alisema, katika Newsweek: “Sababu yenyewe inayofanya matatizo ya kutolipa mkopo kwa wakati yasisuluhishwe haraka ni kwamba sehemu kubwa ya mikopo hiyo imehusika na uhalifu uliopangwa.”

Kwa kweli, uhalifu uliopangwa husitawi na kunawiri mahali ambapo watu wanataka kuridhisha tamaa zao kwa vyovyote vile. Pupa ya raha, ngono, na pesa huandaa ukuzi wa ulanguzi wa dawa za kulevya, ukahaba, kucheza kamari, na kutoa mikopo ya riba ya juu. Kujihusisha na matendo kama hayo mara nyingi humaanisha kutajirisha magenge ya uhalifu. Ni kweli kama nini kwamba uhalifu uliopangwa hushughulikia matakwa ya wale ambao wameazimia kuridhisha tamaa zao wenyewe za kimwili!

Mfumo Bandia wa Familia

Kwa kuongezea mahitaji ya utendaji haramu, kuna mahitaji mengine leo ambayo husitawisha uhalifu uliopangwa. Kiongozi mmoja aliyekufa majuzi wa mojawapo ya magenge makubwa zaidi ya yakuza katika Japani alisisitiza kwamba yeye alikuwa akiwachukua wahalifu na kuwatunza na hivyo akiwafanya wasiwe wabaya zaidi. Alidai kwamba yeye alikuwa baba ya washiriki wa genge hilo. Magenge mengi ya uhalifu, hata yawe ya taifa gani, hujenga magenge yao kwenye uhusiano bandia wa familia.

Chukua mfano wa Chi Sun,a aliyetoka katika familia maskini katika Hong Kong. Mara nyingi baba yake alimpiga sana kwa visababu vidogo-vidogo. Chi Sun mchanga akawa mwasi akajiunga na ule Utatu mashuhuri akiwa na umri wa miaka 12. Katika genge la uhalifu, alipata mahali ambapo alihisi “amestarehe.” Kwa sababu ya ujasiri wake katika mapigano ya silaha, upesi alipandishwa cheo na kusimamia watu kadhaa. Hatimaye alipokuwa na umri wa miaka 17 tu, alifungwa gerezani.

Wengi kama Chi Sun hugeukia magenge ya uhalifu ili kupata upendo wa familia ambao walikosa nyumbani. Washiriki hudai kuwa wanajali, lakini mara nyingi wachanga hutamauka wapatapo kwamba kila mshiriki hasa anajipenda mwenyewe.

Malaika wa Nuru

Wakati genge kubwa zaidi la uhalifu katika Japani lilipotajwa kuwa kikundi chenye jeuri chini ya sheria mpya dhidi ya magenge katika 1992, mmojawapo viongozi walo alidai kwamba kikundi hicho kilijiona kuwa chenye “kuheshimika,” kikipambana na maovu. Lile tetemeko kali la dunia lilipopiga Kobe katika 1995, genge hilohilo liligawanya chakula, maji, na bidhaa nyinginezo za dharura kwa majirani wao. “Ukarimu kama huo,” likaripoti Asahi Evening News, “bila shaka utaimarisha mwonekano wa yakuza kuwa wahalifu wenye kuheshimika.”

Viongozi wa magenge ya uhalifu mara nyingi wamejaribu kuonekana kuwa wakarimu. Kwa wakazi wa mitaa ya mabanda katika jiji alikoishi, Pablo Escobar, yule kiongozi sugu wa genge la ulanguzi wa dawa za kulevya la Medellín la Kolombia, alionekana kuwa “mtu wa kiajabu—kama Mesiya, kama Robin Hood, kama Mfadhili katika maana halisi ya kuwa bwana-mkubwa, kiongozi,” akaandika Ana Carrigan katika Newsweek. Alijenga mahali pa watoto kuchezea na nyumba nzuri kwa maskini, akawapa kazi watoto wanaorandaranda bila makao. Yeye alikuwa shujaa kwa wale walionufaika na msaada wake.

Hata hivyo, wahalifu ambao huonekana wanajisetiri kabisa na magenge yao, ni mabaradhuli tu wa mhalifu mkuu zaidi ulimwenguni pote. Biblia yafunua huyo ni nani. “Shetani mwenyewe hufuliza kujigeuza umbo mwenyewe kuwa malaika wa nuru. Kwa hiyo si jambo kubwa ikiwa wahudumu wake pia wafuliza kujigeuza umbo wenyewe kuwa wahudumu wa uadilifu. Lakini mwisho wao utakuwa kulingana na kazi zao.” (2 Wakorintho 11:14, 15) Leo, watu wengi hawaamini kwamba Shetani ni mtu halisi. Mwanashairi mmoja wa Ufaransa wa karne ya 19 alisema: “Mbinu ya Ibilisi ya ujanja zaidi ni kukushawishi kwamba hayuko.” Yeye huchochea na kutumia yale yanayoendelea, si kwa magenge ya uhalifu tu bali ulimwenguni pote. “Ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu,” yaeleza Biblia. Yesu alimfafanua Shetani kuwa “muua-binadamu kikatili wakati alipoanza, . . . mwongo na ndiye baba ya uwongo.”—1 Yohana 5:19; Yohana 8:44.

Unabii wa Biblia wafunua kwamba Shetani Ibilisi amekuwa mtendaji hasa tangu 1914. Tokea mwaka huo na kuendelea, amekuwa akikusanya makundi yake katika vita kubwa dhidi ya watu wa Mungu. Yeye anavuta wanadamu waingie katika mvurugo. Yeye ndiye msababishi mkubwa zaidi afanyaye uhalifu na magenge ya uhalifu kuenea leo.—Ufunuo 12:9-12.

Je, huyu mchocheaji wa magenge ya uhalifu ya dunia atapata kuondolewa? Je, wanadamu watapata kuwa na amani na utengamano? Je, wewe waweza kuachana na milki mbovu ambayo Shetani amejenga duniani leo?

[Maelezo ya Chini]

a Majina fulani yamebadilishwa kwa ajili ya usalama wa wale ambao wamehusika.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Jinsi ya Kulinda Familia Yako

UKOSEFU wa uchangamfu na muungano katika familia waweza kufanya vijana wanaswe kwa urahisi na magenge ya uhalifu. Inaripotiwa kwamba katika Marekani wengi wa vijana ambao huhusika na uuaji wa kimakusudi unaofanywa na magenge wanatoka katika familia ambazo ni maskini au familia zilizovunjika. “Kwa kuwa maskini,” asema ofisa mmoja wa kitovu cha kizuizi katika North Carolina, “wao huvutwa kwa urahisi na upendo wenye nguvu uliopo kati ya kiongozi na wahuni wake na hisia ya umoja akiwa mshiriki wa genge fulani, ambayo wao hupata kwa mara ya kwanza maishani mwao.”

Kwa njia hiyohiyo, katika sehemu za Mashariki yakuza mmoja mchanga ambaye yuko tayari kuwa ngao kwa mkubwa wake asema: “Nyumbani nilikuwa peke yangu pindi zote. Ingawa tulikuwa familia, sikuhisi kamwe kwamba tungeweza kuzungumza kutoka moyoni. . . . Lakini sasa naweza kuzungumza kutoka moyoni na watu hawa.” Vijana wapweke huwashukuru sana washiriki wa genge la uhalifu ambao huwaingiza katika mfumo ulio kama wa familia.

“Watu wa yakuza ni wenye kujali sana, sana,” asema kiongozi wa kikundi cha waendesha-pikipiki wasichana katika Okinawa. “Labda huo ndio ujanja wao; lakini, kwa kuwa hatujapata kutendewa kwa ungwana, jambo hilo hutuvutia.” Mkuu mmoja wa makao ya wasichana wahalifu athibitisha kwamba majambazi “wanajua sana kunasa mioyo ya wasichana.” Wasichana wapweke wawaitapo usiku wa manane, majambazi hao huenda upesi kuwasaidia na kusikiliza yote watakayosema, bila kujaribu kuwatongoza.

Mtazamo wao wa kujali hudumu mpaka wawe wamenasa kabisa vijana ambao wanataka. Mara vijana wanaswapo, wanatumiwa vibaya—wasichana katika ukahaba na wavulana katika uhalifu.

Unaweza Kuwalindaje Wapendwa Wako?

“Nyinyi akina baba, msiwe mkichochea watoto wenu wakasirike, ili wasishuke moyo,” yaonya Biblia kwa upole. (Wakolosai 3:21) Huko si kuwatia moyo wazazi kuwa waendekevu. Mithali ya Biblia yasema: “Mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.” (Mithali 29:15) Badala ya hivyo, Biblia inatia moyo akina Baba—na mama pia—kuwa wenye kusababu katika kushughulika na watoto wao, kuwasikiliza, na kuwasiliana nao. Ndipo, watoto watachochewa kuzungumza kwa usiri na wazazi wao wanapojikuta wana matatizo.

Kwa kuongezea kuwasiliana, wazazi wanahitaji kuwapa watoto viwango vyao vya maisha. Baba aweza kupata wapi mwongozo kama huo? Biblia yasema: “Nanyi, akina baba, msiwe mkiwasumbua watoto wenu, bali endeleeni kuwalea katika nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova.” (Waefeso 6:4) Chukua muda wa kusoma Biblia pamoja na watoto wako kwa njia ya vipindi vya familia vya kujifunza Biblia. Na ukazie mioyoni mwao hofu ifaayo ya Yehova ili kwamba sikuzote watafuata mwongozo wa Yehova kwa faida yao wenyewe.—Isaya 48:17.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki