Jinsi Uhalifu Uliopangwa Unavyokuathiri
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAPANI
Kiongozi wa genge moja la Mafia adunga kidole cha mshiriki mpya wa genge hilo. Damu yadondoka kwenye picha ya “mtakatifu” fulani. Kisha, picha hiyo yachomwa moto. ‘Ukithubutu kutoa siri yoyote ya genge hili, nafsi yako itachomeka kama mtakatifu huyu,’ kiongozi huyo amwambia kijana huyo.
HIYO kanuni ya ukimya—inayoitwa omertà kwa Kiitalia—ilifanya uhalifu uliopangwa usijulikane sana kwa miaka mingi. Hata hivyo, leo, magenge ya uhalifu hutangazwa sana katika vyombo vya habari kotekote kwa kuwa majambazi wengine wamegeuka na kuwa wasaliti. Mtu mashuhuri zaidi ambaye amepata kushtakiwa na wasaliti wa Mafia, ni Giulio Andreotti, ambaye alikuwa waziri mkuu wa Italia mara saba na ambaye sasa anachunguzwa kisheria kwa ajili ya uhusiano wake na Mafia.
Magenge ya uhalifu yameenea katika kila tabaka ya maisha: Mafia katika Italia na Marekani, ambako pia waitwa Cosa Nostra; magenge ya kulangua dawa za kulevya katika Amerika Kusini; magenge ya Utatu ya China; na yakuza katika Japani. Matendo yao maovu yanatuathiri sisi sote na kufanya maisha yagharimu zaidi.
Inasemwa kwamba katika Marekani, Mafia wamegawanya jiji la New York miongoni mwa magenge matano, wakizoa faida za mabilioni ya dola kupitia unyang’anyi, hila za kutoa ulinzi, kutoa mikopo kwa riba za juu, kamari, ulanguzi wa dawa za kulevya, na ukahaba. Inasemekana kwamba magenge ya Mafia yameshika sana vyama vya wafanyakazi na biashara za kuondoa takataka, biashara za usafirishaji, ujenzi, usafirishaji wa vyakula, na biashara za nguo. Kwa kuwa wana uwezo sana juu ya vyama vya wafanyakazi, wao wanaweza kusuluhisha mizozo ya wafanyakazi au wanaweza kudhoofisha mradi wa ujenzi. Kwa mfano, penye ujenzi siku moja tingatinga kubwa ya kulainisha ardhi itaharibika, siku nyingine breki za mashine ya kuchimba hazitafanya kazi, na waendeshaji “wagoma”—visa kama hivyo na vingine vingi huendelea mpaka mjenzi akubali kutimiza matakwa ya genge hilo, yawe ni hongo au kandarasi za kufanya kazi. Kwa hakika, “kulipa Genge kwaweza kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanatimiziwa haja zao haraka, kuna amani miongoni mwa wafanyakazi na uwezo wa kutumia wafanyakazi kwa mshahara mdogo,” laripoti gazeti Time.
Katika Kolombia magenge mawili ya kulangua dawa za kulevya yalishindana mpaka Pablo Escobar, mkuu wa genge la Medellín, alipopigwa risasi katika 1993. Baadaye, genge la Cali lilidhibiti mauzo ya kokeni ulimwenguni. Likizoa jumla ya dola bilioni 7 katika Marekani pekee katika 1994, huenda hilo genge la uhalifu lilikuwa ndilo kubwa zaidi ulimwenguni pote. Lakini kushikwa katika 1995 kwa kiongozi walo, José Santacruz Londoño kukawa pigo kubwa kwa genge hilo. Lakini sikuzote kuna mwandamani aliye tayari kabisa kuwa kiongozi mpya.
Kwa kuanguka pu kwa Ukomunisti, Mafia wa Urusi nao wakaibuka. Tokeo likawa kwamba, “kila biashara katika Urusi ni lazima ishughulike na mafia,” asema mfanyakazi mmoja wa benki aliyenukuliwa katika Newsweek. Hata katika Brighton Beach, New York, Mafia wa Urusi wanasemekana wanazoa faida kutokana na hila za ulaghai zilizo tata zinazohusisha petroli. Wenye magari huishia kulipa zaidi kwa ajili ya petroli, na serikali inapoteza mapato ya kodi. Magenge ya Urusi pia huendesha ukahaba katika Ulaya Mashariki. Mara nyingi hawakamatwi kwa uhalifu wao. Kwani ni nani awezaye kukabiliana na watu ambao zamani walikuwa wanariadha na mashujaa wa vita ya Afghanistan?
Ndivyo hali ilivyo katika Mashariki pia. Katika Japani, wale walio katika biashara ya utumbuizaji ni lazima watarajie matatizo ila tu waheshimu kikundi cha hapo cha yakuza na kukilipa. Katika Japani pia, mabaa na hata watembeaji wa mitaani hudaiwa pesa za kupewa ulinzi. Kwa kuongezea, yakuza wamejipenyeza ndani katika uchumi wa Japani kwa kufanyiza makampuni yao wenyewe, wakinyang’anya biashara kubwa-kubwa pesa, na kuungana na magenge mengine ya uhalifu yaliyo ng’ambo.
Magenge ya uhalifu yenye makao makuu huko Hong Kong na Taiwan pia yanaeneza mifumo yao ulimwenguni kote. Mbali na jina layo Utatu, mengi hayajulikani kuhusu jinsi ambavyo yamepangwa. Historia yao yarudi nyuma hadi karne ya 17, wakati ambapo watawa wa China walijiunga pamoja ili kupinga Wamanchuria walioteka China. Ingawa wana washiriki wapatao makumi ya maelfu, yasemekana kwamba Utatu wa Hong Kong hufanyiza magenge ya muda tu kwa ajili ya uhalifu mmoja hususa au uhalifu kadhaa, jambo linalofanya iwe vigumu kwa polisi kuwapeleleza. Wao huchuma mabilioni ya dola kwa kulangua heroini nao wamegeuza Hong Kong kuwa kitovu cha kufanyiza kadi bandia za mkopo.
Katika kitabu chake The New Ethnic Mobs, William Kleinknecht aandika kuhusu uhalifu Marekani: “Miongoni mwa magenge mapya ya uhalifu uliopangwa, hakuna majambazi wa jamii moja ambao wana wakati ujao ulio murua kama wale Wachina. . . . Magenge ya uhalifu ya Wachina yanapata uwezo haraka sana katika majiji ya nchi hiyo. . . . Wao wanashindwa na Mafia wa New York pekee.”
Kuhusu aina nyingine ya biashara haramu inayotoka Hong Kong, Ofisa mmoja wa Idara ya Sheria ya Marekani asema: “Kuingiza wageni nchini kiharamu ni wonyesho mmoja wa uhalifu uliopangwa.” Maofisa wengine wakadiria kwamba Wachina 100,000 huingia Marekani isivyo halali kila mwaka. Mhamiaji wa kawaida aliyeingizwa nchini humo isivyo halali ni lazima alipe angalau dola 15,000 kwa sababu ya kupelekwa nchi tajiri, akilipa kiasi kingi cha fedha hizo baada ya kufika aendako. Hivyo, kwa wahamiaji wengi maisha katika nchi walizotamani sana hugeuka kuwa maogofyo ya kazi ngumu ya kulazimishwa katika viwanda vya malipo duni na madanguro.
Kwa sababu huhusiki na utendaji wa uhalifu, huenda ukahisi kwamba wewe huathiriwi na uhalifu uliopangwa. Lakini, kweli ndivyo ilivyo? Waraibu wengi wa dawa za kulevya, wakiishi katika kontinenti kadhaa, hugeukia uhalifu ili waweze kupata pesa za dawa zinazoletwa na magenge ya dawa za kulevya ya Amerika Kusini. Uhalifu uliopangwa huhakikisha kwamba mikataba ya utumishi wa umma hupewa kampuni zinazoshirikiana nao; tokeo likiwa kwamba wananchi hulipa zaidi. Tume ya Rais juu ya Uhalifu Uliopangwa pindi moja ilisema kwamba katika Marekani, “uhalifu uliopangwa hubadili gharama za vitu kupitia wizi, unyang’anyi, hongo, kudhibiti bei za vitu na kufanya hila za kuzuia upinzani wa kibiashara” na kwamba wanunuzi hulazimika kulipa “fedha za ziada” kwa Mafia. Kwa hiyo, hakuna mtu asiyeathiriwa na uhalifu. Sote tunalipia uhalifu.
Lakini ni kwa nini uhalifu uliopangwa unasitawi leo?
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Mafia—Chanzo Chayo
“Mafia iliibuka katika Sicily katika Enzi za Kati, ambako yawezekana ilianza ikiwa kikundi cha kisiri kilichotaka kupindua utawala wa mamlaka kadhaa za kigeni juu ya kisiwa hicho—kwa mfano, Wasaraken, Wanorman, na Wahispania. Mafia ilianzishwa na kupata washiriki kutoka kwa majeshi mengi ya watu binafsi, au mafie, ambayo yalikodiwa na mabwanyenye ambao hawakuwapo ili majeshi hayo yalinde mashamba yao dhidi ya majangili katika hali zilizoenea sana wakati huo za ukosefu wa sheria Sicily katika karne zilizopita. Katika karne za 18 na 19, majambazi hao wakakamavu katika majeshi hayo ya watu binafsi yalijipanga na kuwa yenye nguvu sana hivi kwamba hao nao wakawageuka mabwanyenye wa mashamba na kuwa sheria ya pekee katika mashamba mengi, wakiwatoza mabwanyenye fedha kwa vitisho kwa sababu ya kuwalindia hao mabwanyenye mazao yao.” (The New Encyclopædia Britannica) Kutoza fedha kwa vitisho ili kutoa ulinzi ukawa ndio mbinu yao. Walipeleka hizo mbinu Marekani, ambako walijihusisha na kamari, hila za wafanyakazi, mikopo ya riba za juu, ulanguzi wa dawa za kulevya, na ukahaba.