Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/22 kur. 24-27
  • Pilikapilika za Kujaa kwa Maji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pilikapilika za Kujaa kwa Maji
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Umuhimu wa Milango-Mto
  • Bamvua
  • Kujaa kwa Maji
  • Pilikapilika Zaanza
  • Mahali pa Kupumzikia
  • Vitwitwi Ndege Wanaotangatanga Kote Ulimwenguni
    Amkeni!—2006
  • Je, Umewahi Kuona Samaki Akitembea?
    Amkeni!—1999
  • Msiba wa Chile Waongoza Kwenye Upendo wa Kikristo
    Amkeni!—1992
  • Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/22 kur. 24-27

Pilikapilika za Kujaa kwa Maji

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Uingereza

NDEGE milioni kumi hivi huenda kaskazini-magharibi mwa Ulaya kila mwaka wakati wa kipupwe. Wao hawatoki tu sehemu zao za kuzaliana za Aktiki bali pia wao hutoka sehemu za mbali kama Kanada na Siberia ya kati. Wakiwa njiani kwenda Afrika, wengine wengi hujikusanya katika Njia ya Angani ya Atlantiki Mashariki, ambayo ni njia ya uhamiaji inayovuka Visiwa vya Uingereza.

Chakula na makao ya kupumzikia huandaliwa na milango-mto mikubwa zaidi ya 30 katika bahari za Uingereza. Kila moja hutumikia zaidi ya ndege 20,000, lakini ule ulio muhimu zaidi ni The Wash, kwenye pwani ya mashariki ya Uingereza, ambao huwa na ndege zaidi ya robo milioni—kutia ndani chekeamwezi, dunlin, godwits, knots, vizamiachaza, viluwiluwi, viguuhina, na geuzamawe. Milango-mto huandaa chakula cha aina gani, na kwa nini milango-mito ni muhimu sana?

Umuhimu wa Milango-Mto

Milango-mto ni hori za maeneo ya pwani ambapo maji ya chumvi huchanganyikana na maji yasiyo ya chumvi. Hapo maji yenye ujoto, yenye kujaa madini na virutubisho vya asili, hutegemeza nusu ya viumbe vyote vilivyopo katika bahari-kuu za ulimwengu. Uduvi, panzimchanga, na aina nyinginezo za viumbe hupatikana katika mchanga, lakini matope ya milango-mto hutegemeza hata viumbe vingi zaidi.

Matope hutofautiana kulingana na ukubwa wa mchanga ambamo yametoka. Kila aina ya matope ina wanyama wayo wa kipekee wa majini, ambao ni chakula cha ndege wa ufuko. Kwa mfano, katika meta moja ya mraba ya aina fulani ya matope, mnaweza kuwa na mamilioni ya konokono wadogo sana wanaopungua milimeta 3 kwa urefu! Kwa kuongezea, matope huwa na moluska, vitambaapole, na marijanitanzu, pamoja na viumbe vingine visivyo na uti wa mgongo.

Bamvua

Hata ingawa kunaweza kuwa na maelfu mengi ya ndege wa ufuko, inaweza kuwa vigumu kuwapata kwa sababu mara nyingi wao wametawanyika katika maeneo makubwa. Hata hivyo, bamvua ifikapo hali hubadilika kwa ghafula. Msukumo wa maji mengi hufanya nyangwa za matope na mchanga kufurika, huo ukilazimisha ndege hao wa ufuko waende katika maeneo ambayo hufurikwa kwa ukawaida na kujaa kwa maji na sehemu nyinginezo zilizoinuka. Ni rahisi zaidi kuwaona wakiwa wamekusanyika, wakipumzika katika kundi kubwa lenye kuchangamana ndege mbalimbali.

Leo, asubuhi nyangavu yenye jua ya Aprili, tunatazamia bamvua. Kuna upepo baridi wa kaskazini-mashariki unaopepea twendapo kwa gari kuelekea mlango-mto mdogo ulio maridadi ambako mto Alde hupinda-pinda kupitia wilaya ya Suffolk ya Uingereza na kuingia katika Bahari ya Kaskazini. Hapo, idadi ya ndege wa ufuko ambao huenda huko wakati wa kipupwe hufikia kilele cha ndege zaidi ya 11,000, na itakuwa rahisi zaidi kuona utendaji wao, kwa kuwa mlango-mto huo una upana wa nusu maili tu.

Vizuizi vingi vya bahari hufuata mkondo wa mto. Kingo nyingine zimejaa matete, nyingine zina nyasi. Zilizobaki zimefunikwa kwa mbao nyeusi na mawe. Upande wa juu kidogo wa mto, katikati ya mkusanyo wa majengo ya enzi ya Victoria, kuna Jumba la Muziki la Snape Maltings, ambalo ni makao ya sherehe ya muziki ya Aldeburgh. Lakini ni lazima tuteremke na mto na kutafuta mahali palipositirika. Sasa upepo ni mkali na wenye kuchoma, na muda si muda macho yetu yaanza kuwasha.

Tunapofika tu kwenye ukingo wa mto (ona picha, mahali A), twasikia mlio mwororo mwangavu wa domojuu wawili. Wako umbali wa meta 40 hivi katika upande wetu wa mlango-mto, wakati huu wakinyosha manyoya yao kwa midomo. Kila ndege anakuna-kuna sehemu ya kando ya kifua chake kwa ncha ya mdomo wake mwembamba uliopinda kuelekea juu. Inafurahisha kutazama hilo, lakini ni lazima tuendelee mbele, kwa kuwa kuna mengi zaidi ya kuona.

Kujaa kwa Maji

Maji yanajaa upesi sasa, kwa hiyo twasonga haraka kwenda mahali tulipochagua pa kutazama. (Ona picha, mahali B.) Njiani kiguuhina—akionyesha kawaida yake ya kuwa mlinzi wa mlango-mto—aruka kutoka kwenye maeneo ambayo hufurikwa kwa ukawaida na kujaa kwa maji, kwa kelele zake za kutahadharisha, “tuhuhu-tuhuhu!” Miguu yake myekundu hutofautiana na ncha nyeupe ya mabawa yake yenye kumetameta katika jua. Tufikapo mahali tulipokuwa tukienda, twatazama haraka-haraka nyangwa za mchanga na matope zinazokwisha upesi.

Kwa umbali makumi ya viguuhina yalikuwa yakila polepole, wakichimba-chimba matope juu-juu, huku wengine wakitafuta chakula katika hori zisizo na upepo. Ndege aina ya dunlin, wenye midomo ambayo kwa kawaida imepinda kuelekea chini, wako pamoja, katika vikundi vidogo-vidogo. Katika mstari wenye kubadilika-badilika, wao wadonoa-donoa matope, wakipendelea kuwa karibu na ukingo wa maji. Chekeamwezi waliotawanyika wapita, wakichunguza kwa uangalifu matope hayo mororo na mepesi. Kuelekea juu mtoni, geuzamawe kadhaa wanatafuta chakula kwa kutumia midomo yao mifupi iliyopinda kidogo kuelekea juu ili kugeuza vitu vinavyoachwa na maji kwenye ukingo wa bahari.

Kwa ghafula, kuna mlio mkali wa kutamani wenye silabi tatu wa “tlee-oo-ee” wa kiluwiluwi-kijivu unaojaza hewa. Arukapo juu, mabawa meusi ya makwapa ya ndege huyo hutofautiana kabisa na tumbo lake la kijivu. Viluwiluwi-dhahabu mia nne, wakiwa karibu-karibu katika umbo la duara, wapumzika wakiwa wamefunika vichwa vyao ndani ya mabawa yao, wote wakikabili upepo. Kuna mizozo ya pindi kwa pindi kati ya viluwiluwi kadhaa na nidhamu hudumishwa. Wengi wao bado wangali wana manyoya yenye madoadoa ya wakati wa kipupwe—sehemu za juu zikiwa za rangi ya dhahabu na nyeusi-nyeusi; rangi ya kijivu kwenye macho, uso, na sehemu za chini; na mdomo mweusi. Tutafutapo kwa darubini zetu, twaona viluwiluwi-mraba pia.

Kundi lenye kuenea la ndoero wapatao 1,000 lafika kwa ghafula. Ndege hao wafika kwa mchachawo sana, wakipeperuka kwa njia ya kipekee. Hao ndoero na viluwiluwi-dhahabu wamekuwa katika mashamba yaliyo sehemu ya magharibi, sehemu ambayo wao hupenda zaidi kwa malisho. Wao huja kwenye mlango-mto si kula tu bali pia kuoga na kunyosha manyoya yao.

Kelele kubwa za kichinichini ni milio ya chekeamwezi iliyo kama bubujiko, miluzi yenye kuridhika zaidi ya viguuhina, na milio ya shakwe kichwa-cheusi. Ndege wawili aina ya bar-tailed godwit wachimba ndani katika matope. Vizamiachaza wachache wanatoa vitambaapole kwa midomo yao mikubwa yenye rangi ya machungwa. Kiluwiluwi mmoja wa kijivu achukua hatua chache za kifahari, atua, atikisa mguu wa kulia, kisha afuata windo lake, na kummeza. Lakini kujaa kwa maji kwawafikia hao wote!

Pilikapilika Zaanza

Kwa ghafula, ndege hao waruka na kufanyiza makundi, hasa ya spishi zao wenyewe. Ni mwono wenye kuvutia sana, kwa kuwa ndege hao wa ufuko waruka wakiwa karibu-karibu. Kwa upande, makundi hayo hubadilika rangi miale ya jua iwaangazapo—toka hudhurungi ya nyeusi-nyeusi hadi rangi ya fedha—pindi moja wakionekana vizuri sana na pindi nyingine, wakilandana na mandhari ya matope-matope ya kujaa kwa maji. Nyeusi hadi fedha, fedha hadi nyeusi, kwa upatano kabisa na, kwa wakati uo huo, wakibadilisha umbo la kuruka—kutoka kwa umbo la mayai hadi la mviringo, kisha la parafujo, na hatimaye kufanyiza mstari ulio wima. Wengi hurudi kwenye nyangwa za matope ambazo hazijafurikwa bado kwa maji.

Punde si punde, nyangwa za matope na mchanga zilizotuzingira zitajaa maji, kwa hiyo twaharakisha kwenda juu, pamoja na ndege wengi wa ufukoni. Wa kwanza kutupita ni vikundi vidogo vya dunlin walio wadogo sana, wakipigapiga mabawa haraka sana, wanaodumisha uwasiliano kwa mbinja fupi iliyo kali. Kisha, viguuhina walio wakubwa zaidi wapita, kundi lao likiwa limeenea vizuri zaidi na kwa fahari. Chekeamwezi wanaotoshana na shakwe wakubwa wapita, wakiimba wimbo wao mtamu ulio kama bubujiko. Domojuu wafuata katika kikundi kimoja kikubwa, rangi zao nyeupe na nyeusi zikibadilikana katika anga la buluu. Wao watua sehemu za juu za mlango-mto, miguu yao mirefu yenye buluu-kijivu ikionekana kidogo tu juu ya maji.

Mahali pa Kupumzikia

Twaharakisha mwendo kufika mahali palipoinuka ambapo mlango-mto ni mwembamba. (Ona picha, mahali C.) Spishi huelekea kukusanyika pamoja, ingawa kwa wazi si lazima. Maji yaendeleapo kujaa haraka, ndege wengi zaidi wajazana. Hilo lasababisha msukumano kwa kuwa inakuwa vigumu zaidi kupata nafasi za kusimamia ukingoni, huku wenye kufika kama wamechelewa wakitaka nafasi zaidi.

Maji yamejaa sasa. Ndoero na viluwiluwi-dhahabu wamerudi kwenye mashamba. Ndege wote wanaobaki wamelazimishwa kuondoka matopeni na kupumzikia katika kingo za mto wa zamani. Kulia daima kwa vizamiachaza hakulingani na idadi yao. Viguuhina na chekeamwezi huongezea kelele za kichinichini, ambazo hupitwa na kipozamataza aimbaye juu—hali nzuri ajabu.

Twaondoka ndege hao wa ufuko wafurahiapo mapumziko ya alasiri wanayostahili sana, wakiepuka bamvua kubwa. Japo uhakika wa kwamba baadhi ya ndege wako sehemu wasizoweza kuona maji, hao watajua wakati wa kurudi kwenye nyangwa za matope au fuko za mchanga. Wakiwa watunza-saa bora na wenye hekima kisilika, wao waelewa kujaa na kupwa kwa maji.

Ndiyo, husisimua sana kutazama pilikapilika za kujaa kwa maji, hasa kwa mara ya kwanza!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

Furahia Hizo Pilikapilika

Ili kufurahia pilikapilika za kujaa kwa maji, kwanza tafuta mlango-mto wenye kufaa. Kisha utahitaji habari fulani kuhusu eneo hilo, kama vile mahali ambapo ndege hao wa ufuko huenda na mahali pa kuwaona. Chunguza saa za bamvua kubwa ambayo hutukia baada tu ya mwezi mpevu na mwezi mwandamo. Kwa kuongezea wakati wa usafiri, uwe na muda wa saa tatu hivi wa kuwatazama vizuri ndege hao, na ufike angalau muda wa saa mbili kabla ya maji kujaa.

Utahitaji vifaa gani? Kama huwafahamu ndege wa ufuko, nenda na kitabu kitakachokuwezesha kuwatambulisha. Darubini zaweza kufaa sana. Upesi utajua kwamba kila spishi ya ndege wa ufuko ina tabia yayo yenyewe nayo hula kwa njia ambayo mdomo wayo umeumbwa. Si lazima kwenda na darubini-upeo—lakini, mavazi yenye joto, yasiyoweza kulowa maji ni muhimu! Jihadhari na hatari. Usiende kwenye nyangwa za matope ila kama unazijua vema. Ni rahisi kunaswa na kujaa upesi kwa maji. Isitoshe, ukungu tu wa bahari waweza kukupoteza. Fikiria upepo vilevile. Pepo kali zaweza kusababisha mawimbi makubwa wakati wa kujaa kwa maji, jambo liwezalo kuhatarisha katika mlango-mto wowote ule.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Milango-Mto Mikuu ya Dunia

Ule Wadden Zee, katika Uholanzi, ndio eneo muhimu zaidi ya kujaa na kupwa kwa maji katika Ulaya na nyakati nyingine huwa na ndege wa ufuko wawezao kufikia milioni nne. Huo huenea kaskazini hadi Jutland ya kusini-magharibi. Sehemu tatu nzuri za kuzuru katika eneo hili kubwa ni daraja la kwenda Rømø, Denmark; Mlango-mto wa Mto Weser, mahali pakubwa pa kupumzikia wakati wa kujaa kwa maji, Ujerumani; na Lauwers Zee karibu na Groningen, Uholanzi. Katika Peninsula ya Iberia, mlango-mto ulio muhimu sana ni ule wa Mto Tagus wa Ureno.

Milango-mto iliyo kandokando ya Pasifiki katika pwani ya Amerika ya Kaskazini na Kusini huandaa chakula kwa wahamaji wa ufuko wapatao milioni sita hadi nane. Miongoni mwa sehemu zilizo kuu ni ghuba za San Francisco na Humboldt, California; lile eneo la kilometa 200 za mraba katika Canada kutoka Vancouver’s Boundary Bay karibu na Kisiwa cha Iona, British Columbia; na mlango-mto wa Alaska’s Stikine, na delta ya Copper River.

Sehemu nzuri zaidi za ndege wa ufuko pia zapatikana katika Bolivar Flat na Galveston, Texas, Marekani; katika Tai-Po, Hong Kong; katika Cairns, kaskazini-mashariki mwa Australia; na karibu na Mombasa, Kenya.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Vizamiachaza watano

[Picha katika ukurasa wa 25]

“Knots” wakitoka kupumzika

[Picha katika ukurasa wa 25]

MLANGO-BAHARI WA ALDE, SUFFOLK

Jumba la Muziki la Snape Maltings

Mahali pa kutazama B

Mahali pa kutazama C

Mahali pa kwanza pa kutazama A

[Hisani]

Snape Maltings Riverside Centre

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Knot”

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kiguuhina

Chekeamwezi

[Picha katika ukurasa wa 27]

Juu: Chekeamwezi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki